KIYAMA: HEBU TUSAWIRISHE PAMOJA MANDHARI HII YA KUTISHA

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-hebu sote kwa pamoja tusawirishe na tuitie akilini na fikrani mwetu mandhari ya kutisha na kuogofya, kisha tuzingatie. Hebu tuyaone hayo ndio makaburi yanapasuka kila upande wa ulimwengu na hao ndio watu wanatoka humo makaburini baada ya kulala humo kwa kipindi kirefu. Makaburi yaliyo sheheni upweke na utisho kwa makafiri na watenda maasi wakati yale ya watenda twaa na walio mpwekesha Allah katika maisha yao ya dunia yakianikiza nuru. Kila mtu akitoka kaburini mwake huku akikung’uta mchanga mwilini mwake ilhali akikodolea macho upande mmoja kwa yule mtangazaji (Malaika Mtukufu) ambaye anawaswaga watu kwenda kwenye uwanja wa makutano ili kusimamishwa mbele ya Allah na kuhisabiwa kwa matendo yao.

 

 

Allah Mtukufu anasema: “Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani Mwingi wa rehema. Basi husikii ila mchakato na mnong’ono. Siku hiyo uombezi haufai kitu, ila aliye mruhusu Arrahmani Mwingi wa rehema na akamridhia kusema. Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo. Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye hai milele, Mwangalizi mkuu. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma. Na anaye tenda mema, naye ni muumini, basi hatakhofu kudhulumiwa wala kupunjwa”. Twaaha [20]:108-112

 

Eeeh! Enyi mifupa iliyo chakafuka! Enyi miili iliyo utupu (uchi)! Enyi watu! Haya sasa umesha fika ule wakati wa kusimama mbele ya Allah aliye Mtukufu!

 

Eeeh! Huo hapo ulimwengu mzima unaelekea kwenye uwanja wa makutano ili kusimama kwenye uwanja huo kungojea kuanza kuhisabiwa na kisha kulipwa jazaa sawiya!

 

Watu wote wamefufuliwa kutoka makaburini mwao wakiwa uchi pasina kukhitaniwa kama linavyo tajwa hilo na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika Hadithi iliyo pokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi: “Hakika nyinyi mtafufuliwa mkiwa watupu na msio khitaniwa”. Kisha akasoma (neno lake Mola): {Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao} [Al-Anbiyaa 21:104]Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

 

Na imepokewa katika baadhi ya nassi (nukuu za Hadithi) ya kwamba kila mtu atafufuliwa akiwa amevaa ile nguo yake aliyo kufa akiwa nayo. Imepokewa kutoka kwa Abu Saeid Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-ya kwamba alipo karibia kufa aliomba aletewe nguo mpya, akaivaa kisha akasema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Hakika maiti atafufuliwa akiwa amevaa ile nguo yake aliyo kufa akiwa ameivaa”. Abu Dawoud & Al-Haakim-Allah awarehemu.

 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-punde tu tumenukuu hadithi mbili ambazo moja inasema watu watafufuliwa wakiwa hawana nguo na nyingine inasema watakuwa wamevaa nguo walizofia nazo. Kwa akili zetu sisi waandazi wa jukwaa na wewe mdau wa jukwaa, tunaona pana mgongano baina ya hadithi hizi. Imamu Al-Baihaqiy-Allah amrehemu-aliliona na kulitambua hilo kitambo, akatuondoshea mushkeli huo kwa kuzioanisha hadithi hizo kwa njia tatu zifuatazo:

 

  1. Kwamba watu watakapo toka makaburini mwao baada ya kufufuliwa nguo zao zitakuwa zimeoza kabisa na zimechanganyika na udongo, kwa hivyo watafika kwenye uwanja wa hisabu wakiwa uchi. Kisha ndipo watavishwa nguo za peponi.

  2. Kwamba watakapo vikwa nguo Mitume, wakifuatiwa na Sidikiina (wale watu wakweli katika imani, kauli na matendo yao), kisha wakafuatiwa na watu wengine kulingana na daraja zao. Hapo nguo ya kila mtu itakuwa katika jinsi/namna aliyofia nayo, kisha watakapo ingia peponi watavikwa nguo za peponi.

  3. Kwamba muradi/mapendeleo ya nguo hapa ni zile amali zao (matendo yao); yaani likusudiwalo kusemwa ni kwamba mtu atafufuliwa katika matendo yake aliyo kufa akiyatenda, yawe ya kheri au ya shari. Allah aliye Mtukufu amesema: “… Na nguo za uchaMngu ndio bora…”. Al-A’raaf [07]:26

 

Na akasema: “Na nguo zako, zitakase”. Al-Muddathir [74]:04

 

Imamu Al-Baihaqiy-Allah amrehemu-akaitolea ushahidi hii njia ya tatu kwa hadithi iliyo pokewa na A’amash kutoka kwa Abu Sufyaan, naye akipokea kutoka kwa Jaabir-Allah awawiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kila mja atafufuliwa kwa lile alilo fia nalo”. AN-NIHAAYAH ya Ibn Kathiir-Allah amrehemu.

 

Na hadithi hii ya Jaabir ameipokea Imamu Muslim katika SAHIH yake (04/2206), na wala haifahamishi ya kwamba mtu atafufuliwa akiwa amevaa nguo zake zile alizo kafiniwa nazo (sanda) au zile alizokufa akiwa amezivaa. Na hakika si vinginevyo, atafufuliwa akiwa katika ile hali ambayo alikufa akiwa nayo; yaani akiwa katika imani au kufru, yakini au shaka, kama ambavyo atakavyo fufuliwa akiwa katika amali ambayo alikuwa akiitenda wakati wa kufa kwake. Hili linafahamishwa na hadithi aliyo ipokea Imamu Muslim katika SAHIH yake kutoka kwa Abdillah bin Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Allah atakapo watakia watu kufikwa na adhabu, itawasibu adhabu hiyo wote (wema na waovu), kisha ndio watafufuliwa kwa mujibu wa amali zao”. SAHIH MUSLIM [02/2206]

 

Kwa mantiki hiyo basi, yule aliye kufa akiwa amehirimia Hija, atafufuliwa akiwa analeta Talbiya; anasema Labbaikal-laahumma labbaika… Kwani imepokewa Hadithi katika Sahih Bukhaariy, Muslim na Musnad ya Imamu Ahmad kutoka kwa Abdillah bin Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Hakika mtu mmoja alikuwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaangushwa na ngamia wake akavunjika shingo naye akiwa amehirimia Hija, akafa. Mtume wa Allah akasema: “Mkosheni kwa maji na mkunazi na mkafinini katika nguo zake (za Ihramu) na wala msimtie manukato na msikifunike kichwa chake, kwani hakika yeye atafufuliwa siku ya Kiyama akiwa analeta Talbiya”.

 

Na shahidi atafufuliwa siku ya Kiyama na ilhali jeraha lake likitona damu, rangi ya damu lakini harufu yake ni harufu ya miski.

 

Ni kwa ajili/sababu hiyo basi, pakapendelewa kulakiniwa (kutamshwa) maiti kalima ya Laa Ilaaha illal-laah huenda naye akaitamka na akawa amekufa katika Tauhidi, kisha siku ya Kiyama akafufuliwa ilhali akiitamka kalima hiyo tukufu. [AL-QIYAAMATUL-KUBRAA 59:61]

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *