KWA NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI ?

Haukuwa Uislamu ndiyo dini ya kwanza kuruhusu kuoa wake wengi na wala Uislamu haukuzua utaratibu huu.

Bali Uislamu umekuwa ndiyo dini ya kwanza kuratibisha na kuyawekea utaratibu mzuri masuala ya ndoa. Isitoshe Uislamu ukaliwekea suala la kuoa wake wengi masharti madhubuti na magumu, ambayo Mume analazimika kuyazingatia kabla ya kuongeza mke/wake.

Suala la kuoa wake wengi halikuwa tu ni ada na desturi za waarabu zama za jahiliya, bali pia ilikuwa ni desturi ya mataifa mbalimbali kwa namna moja au nyengine, kama historia inavyokiri ukweli huu.

Historia inaonyesha kuwa hata hapa kwetu Tanzania, watemi (machifu) wa makabila mbali mbali bali watu wa kawaida wenye mali walikuwa na wake wengi, huu ni ukweli usiopingika.

 Utaratibu huu wa kuoa wake wengi ulikuwemo pia katika vitabu vilivyotangulia Qur-ani Tukufu.

Mna ndani ya Taurati maandiko na matukio yanayouthibitisha ukweli huu na wala hamna ndani ya Injili aya/maandiko yanayoharimisha kuoa wake wengi.

Bali kuoa wake wengi kulizuiliwa na kanisa katika karne ya kati {karne ya 10-15 AD} na wakati mwingine waliruhusiwa na kanisa baadhi ya wafalme wakubwa kuoa wake wengi. Rejea vitabu vya historia ya kanisa.

Uislamu umeruhusu kuoa wake wengi kwa sharti

  1. isizidi idadi yao wake wanne
  2. Kufanya uadilifu baina yao.

Tunasoma ndani ya Qur-ani Tukufu juu ya ruhusa hii :

“…. BASI OENI MNAOWAPENDA KATIKA WANAWAKE (maadam mtafanya uadilifu) WAWILI AU WATATU AU WANNE (tu). NA MKIOGOPA KUWA HAMWEZI KUFANYA UADILIFU, BASI (oeni) MMOJA TU, AU (wawekeni masuria) WALE AMBAO MIKONO YENU YA KUUME IMEWAMILIKI. KUFANYA HIVYO NDIKO KUTAPELEKEA KUTOFANYA UJEURI.” [4:3]

Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alimwambia Ghaylan At-thaqafiy, ambaye alisilimu akiwa na wake kumi

“Kaa na wanne (tu) miongoni mwao na waache (wataliki) waliosalia” At-tirmidhiy, An-nisaai na Ibn Maajah. Ni vema ikafahamika kwamba huyu Ghaylan alikuwa ndiye mtemi (mfalme) wa Twaif.

Suala hili la kuoa wake wengi ni suala lililofanywa na mwenyewe Bwana Mtume, maswahaba na waliokuja baada yao na ni suala ambalo umma mzima wa kiislamu umekongamana juu yake. Sheria hii inayomruhusu mwanamume kuoa zaidi ya mke mmoja ina maslahi na manufaa kwa wote wawili; mwanamume na mwanamke. Kwa upande wa mwanamume :

  1. Inawezekana kabisa mkewe akawa hamtoshelezei haja yake ya maumbile. Hili husababishwa na uwezo mkubwa wa mume katika tendo la ndoa na udhaifu wa mke. Mume hataki kumuacha mkewe, sasa ataitosheleza wapi kiu yake ?

Hapo ndipo uislamu ukamruhusu kuoa mke mwingine na yule wa mwanzo kubakia pale pale. Lau uislamu usingemruhusu mume huyu kuongeza mke mwingine ni dhahiri kuwa ili kukidhi haja yake angefanya moja kati ya mawili. Ima angemtaliki huyu aliye naye, asiyekidhi haja na kuoa mwingine au angekuwa na nyumba ndogo (mwanamke wa pembeni/kimada)

 

  1. Kadhalika mwanamke anaweza kuwa tasa; hazai na mume anatamani kupata watoto, ambalo hili la kupata watoto ni mojawapo ya malengo na madhumuni ya ndoa. Lakini mume anampenda mkewe na kwa sababu moja au nyingine hataki kumuacha.

Sasa huyu mume afanyeje ili aweze kupata watoto kuendeleza kizazi cha binadamu ? Akazae nje ya ndoa ? Hapana, hilo ni kosa. Hapa ndipo sheria ikaizingatia haki ya huyu mume kupata watoto na ikamruhusu kuoa mke mwingine ajaribu bahati yake. Huenda Mola wake akamruzuku watoto kwa mke huyu.

Haya ni baadhi tu ya maslahi ya sheria hii ya kuoa zaidi ya mke mmoja kwa upande wa mume. Hebu tuangalie mwanamke naye, ananufaika vipi na sheria hii :

  1. Inawezekana kabisa mke akapatwa na maradhi; yakamsababishia kushindwa kabisa kuitekeleza haki ya unyumba kwa mumewe. Maskini mke huyu mgonjwa, aende wapi na il-hali sasa katika kipindi kigumu cha ugonjwa ndio anahitajia zaidi huruma, mapenzi na liwazo la mumewe.

Mumewe amtaliki ? La, hapana, sheria inambana mume kuwa katika mkataba wa ndoa alichukua ahadi kuishi naye katika raha/shida, uzima/ugonjwa, basi amuuguze mkewe na ili kukidhi haja zake za kimaumbile basi na aoe mke mwingine, Je hapo mwanamke hajanufaika?

  1. Kadhalika kama ambavyo binadamu anavyotofautiana katika sura, akili, tabia na kadhalika. Ni kama hivyo pia tunatofautiana katika uwezo/nguvu ya kujamiiana. Inaweza uwezo wa mume ukawa ni mkubwa sana kuliko mkewe, mume ni tembo na mke ni kondoo, vipi kondoo atahimili vishindo vya tembo ?

Sasa, ili mke huyu asiichukie ndoa na hatimaye kukimbia, uislamu ukamruhusu mume kuongeza mke mwingine. Siku za zamu ya mke mwingine, huyu asiyehimili vishindo atapata kupumzika. Hebu tuwe wakweli, mwanamke huyu kanufaika au la?

Vile vile sheria hii ina maslahi makubwa kwa jamii. Hakuna jamii isiyokuwa na wajane na mayatima; ambao hawa wanataka wapate uangalizi na malezi.

Nani basi atawalea wajane hawa waliofiwa na waume zao na hawa walioachwa na baba zao ? Hapo ndipo Uislamu ukampa ruhusa mwanaume ambaye tayari ana mke, kuongeza mke mwingine. Pengine huyu atakayemuoa ni huyo mjane, mwenye mayatima.

Je hapo mwanamke huyu hajasitirika na wanawe ? Kwani huyu mume atakuwa anawajibika kumhudumia yeye na wanawe. Waswahili husema ukipenda boga penda na maua yake. Je, hapa jamii imenufaika au haikunufaika ?

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake duniani ni kubwa kuliko idadi ya wanaume, kadhalika idadi ya wanyama jike ni kubwa kuliko ya wanyama dume.

Haya ni matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi mbali mbali ulimwenguni kote. Sasa itakuwa tunakubaliana na takwimu hizi na leo vita vimetapakaa duniani kote na wahanga (victims) wa vita hivi, wengi wao ni wanaume kwa kuwa wao ndio askari wanaopigana vita.

Hebu tuchukulie/tukadirie kuwa uwiano wa wanaume na wanawake duniani 1:5 yaani mwanaume mmoja kwa wanawake watano. Sasa ikiwa kila mmoja akioa mke mmoja hawa waliobaki waende wapi, wakaolewe na nani ?

Hawa pia ni binadamu, wanayo haki yao ya msingi ya kupenda na kupendwa katika jamii. Wanayo matakwa yao ya kimaumbile, wakakidhi wapi haja na hamu zao za kimaumbile ? Ni kwa kuzingatia hili ndio uislamu ukamruhusu mwanaume kuoa mke zaidi ya mke mmoja kwa sharti ya kuwa awe muadilifu baina yao.

Ni lazima tukubali kuwa kila sheria aliyotuwekea Mola wetu mtukufu ina faida,maslahi na manufaa kwetu sisi waja wake. Akiamrisha au kukataza ni kwa maslahi na faida yetu sisi wenyewe.

Ni mamoja tumeyajua na kuyaona maslahi na faida za amri au katazo hilo au hapana. Kushindwa kwetu kuyajua maslahi na kuziona faida, hakuziondoshi faida na maslahi hayo na kuyafanya yasiwepo, bali yatabakia pale pale.

Huu ndio ukweli usiopingika. Waislamu tumekuwa tukiwacha mafundisho ya dini yetu na kufuata mafundisho ya shetani yaliyopitia kwa wanaojiita wanamaendeleo. Leo matatizo yanayotukuta yanatokana na kuacha mafundisho ya Uislamu.

Tukodolee macho wakati wa Mtume na masahaba na tuone nia zao katika kuoa wake wengi, jinsi mwanamke wa kiislamu alivyohifadhika, wajane wa vita pia nao hawakutupwa mkono, na Mtume –Rehema na Amani zimshukie – ndiye aliyeanza kuonyesha mfano.

Je, tuna mfano mkubwa kuliko wa Mtume wakati Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuamrisha tumfuate ?

Tunafuata mkumbo wa maadui wa kiislamu unaodai haki za wanawake na kushikilia kuoa mke mmoja, pamoja na kuweka vimada, kumvunjia mwanamke heshima yake kwa kumvua nguo na kumtumia kwenye matangazo ya biashara, madansa, miss world na kadhalika.

Leo mwanamke akiolewa ananyang’anywa hata jina la mzazi wake na kujulikana kwa jina la mumewe, Mrs fulani, sasa ni nani anayemtakia mema mwanamke, Mwenyezi Mungu aliyemuumba au wakazi wa dunia hii wakiongozwa na mwanaume ambaye yuko tayari kufanya lolote kutekeleza matashi ya nafsi yake ???

 

KWA NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI ?

Haukuwa Uislamu ndiyo dini ya kwanza kuruhusu kuoa wake wengi na wala Uislamu haukuzua utaratibu huu.

Bali Uislamu umekuwa ndiyo dini ya kwanza kuratibisha na kuyawekea utaratibu mzuri masuala ya ndoa. Isitoshe Uislamu ukaliwekea suala la kuoa wake wengi masharti madhubuti na magumu, ambayo Mume analazimika kuyazingatia kabla ya kuongeza mke/wake.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *