ADABU NA TARATIBU ZA IJUMAA

Siku ya Ijumaa na swala yake zina adabu na taratibu zilizosuniwa, yatakikana kwa kila muislamu kuzishughulikia na kuzoea kuzifanya, adabu na taratibu hizo ni pamoja na:-

1.Kukoga:

hili ni kwa mujibu wa hadithi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-isemayo: Anapoiendea mmoja wenu Ijumaa basi na akoge”. Bukhaariy (387) & Muslim (844).

Amri hii ya Bwana Mtume hapa inavuliwa kutoka katika hukumu ya uwajibu kwenda katika usuna kwa mujibu wa ile hadithi iliyopokelewa na Imamu Tirmidhiy: “Atakayetawadha siku ya Ijumaa amefuata suna na hiyo ni suna njema na atakayekoga, basi huko kukoga ni bora zaidi”.

 

2. Kuunadhifisha mwili kutokana na taka (uchafu) na harufu mbaya, kupakaza mafuta na kujitia manukato:

Muislamu anatakiwa kuyafanya yote haya ili asiwaudhi na kuwakera watu wangine kutokana na uchafu na harufu yake mbaya.

Na badala yake awe katika hali na mandhari ambayo watu watapenda na kuona raha kukaa karibu yake.

Na umekwishajifunza huko nyuma kwamba miongoni mwa nyudhuru zinazompa mtu rukhsa kutokuhudhuria swala ya jamaa ni kula kitu chenye kutoa harufu mbaya inayowakera watu.

Imepokelewa kutoka kwa Salmaan Al-Faarisiy-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

Mtu hakogi siku ya Ijumaa na kujitwaharisha kiasi awezacho cha twahara na kujipaka mafuta yake au kujitia manukato ya nyumbani kwake. Kisha akatoka (kwenda msikitini), hatenganishi baina ya watu wawili, halafu akaswali alichofaradhiwa. Kisha akakaa kimya Imamu atakapoanza kukhutubu ila atasamehewa madhambi yaliyo baina yake na Ijumaa ijayo”. Bukhaariy (843)-Allah amrehemu.

 

3.Kuvaa nguo nzuri:

Imepokelewa kutoka kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Atakayekoga siku ya Ijumaa, kisha akavaa nguo zake nzuri kabisa na akajitia manukato akiwa nayo. Kisha akaiendea Ijumaa akiwa na utulivu na asimkeuke ye yote na asimfanyie maudhi. Halafu akaswali alichofaradhiwa, kisha akangojea mpaka aondoke Imamu, atasamehewa madhambi yaliyo baina ya Ijumaa mbili”. Ahmad (3/81) & wengineo-Allah awarehemu.

Na ni bora zaidi ikiwa nguo nzuri hizo zitakuwa ni nyeupe, haya ni kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Vaeni zilizo nyeupe katika nguo zenu na wakafinini (wavisheni sanda) maiti zenu katika hizo (nguo nyeupe)”. Tirmidhiy (994) & wengineo-Allah awarehemu.

 

4.Kukata kucha na kutengeneza nywele:

Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikata kucha zake na kupunguza sharubu zake siku ya Ijumaa. Al-Bazaar-Allah amrehemu-katika Musnadi yake.

 

5.Kwenda mapema msikitini:

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Atakayekoga siku ya Ijumaa mithili ya josho la janaba, kisha akaenda mapema (msikitini) huwa kana kwamba katoa sadaka ya ngamia. Na atakayekwenda katika saa ya pili huwa ni kama aliyetoa sadaka ya ng’ombe na atakayekwenda katika saa ya tatu huwa ni kama aliyetoa sadaka ya kondoo mwenye pembe. Na atakayekwenda katika saa ya nne huwa ni kama aliyetoa sadaka ya kuku na atakayekwenda katika saa ya tano huwa ni kama aliyetoa sadaka ya yai. Imamu atakapotoka (atakapopanda mimbarini) huhudhuria malaika kusikiliza dhikri (khutba)”. Bukhaariy (841) & Muslim (850)-Allah awarehemu.

 

6.Kuswali rakaa mbili wakati wa kuingia msikitini:

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakapokuja mmoja wenu siku ya Ijumaa na ilhali Imamu anakhutubu, basi na aswali rakaa mbili na akhafifishe ndani yake (rakaa mbili hizo)”. Muslim (875)-Allah amrehemu.

Hili la kuswali rakaa mbili ni iwapo khatibu hajafikia mwishoni mwishoni mwa khutba.

Na kama atakuwa amefikia mwishoni, basi na asubiri tu kukimiwa kwa swala. Angalia rakaa mbili hizi zitafutu kwa kukaa kwake kitako, kwani akishakaa haitosihi kwake kuswali swala ya suna tena. Bali kutamuwajibikia kuendelea kukaa na kusikiliza khutba na kusubiri swala ikimiwe.

 

7.Kukaa kimya na kusikiliza khutba:

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Utakapo mwambia mwenzako siku ya Ijumaa: Nyamaza, na ilhali Imamu anakhutubu, hakika umefanya porojo”. Bukhaariy (892), Muslim (851) & wengineo-Allah awarehemu.

Na imekuja katika riwaya ya Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi: “Na atakayefanya porojo, hana cho chote katika Ijumaa yake”. Abuu Daawoud (1051)-Allah amrehemu.

 

ADABU NA TARATIBU JUMLA ZA SIKU YA IJUMAA:

 

Siku ya Ijumaa ndio bora ya siku za juma (wiki) na siku hii ina adabu na taratibu maalumu ambazo muislamu anatakiwa kuzijua. Ili aweze kuzitia vitendoni kiasi cha uweza wake na hizi hapa ni baadhi yake:-

a.      Ni suna kusoma Suratil-Kahfi (18) usiku wa kuamkia Ijumaa na mchana mzima wa Ijumaa:

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Atakayesoma Suratil-Kahfi siku ya Ijumaa, itamzagazia  (itamuangazia) nuru katika kipindi kilicho baina ya Ijumaa mbili”. Nasaai-Allah amrehemu.

 

b.      Kumesuniwa kukithirisha kuomba dua usiku na mchana wake:

Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliitaja siku ya Ijumaa, akasema:

Umo ndani yake muda fulani ambao mja muislamu hauwafiki (haupati) na ilhali amesimama akiswali, akamuomba Allah Mtukufu cho chote ila humpa”.- Na Bwana Mtume akaashiria kwa mkono wake akiudogesha; yaani akibainisha kwamba muda huo ni kitambo kifupi. Bukhaariy (893) & Muslim (852)-Allah awarehemu.

 

c.       Ni suna kukithirisha kumswalia Bwana Mtume usiku na mchana wake.

Suna hii ni kwa mujibu wa ile hadithi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-isemayo:

“Hakika miongoni mwa bora ya siku zenu ni siku ya Ijumaa, basi kithirisheni kuniswalia ndani yake. Kwani mimi ninaonyeshwa swala zenu (mnazoniswalia ndani ya siku ya Ijumaa)”.  Abuu Daawoud (1047) & wengineo-Allah awarehemu.

 

TANBIHI:

ü      Ni haramu kuendelea kuuza na kununua baada ya kuadhiniwa kwa ajili ya swala ya Ijumaa, hili ni kufuatia kauli tukufu ya Allah:

“ENYI MLIOAMINI! KUKIADHINIWA KWA AJILI YA SWALA SIKU YA IJUMAA, NENDENI UPESI KUMTAJA ALLAH NA ACHENI BIASHARA…” [62:9]

ü      Ni karaha ilekeayo katika uharamu kukeuka shingo za watu siku ya Ijumaa kwa lengo la kwenda kukaa mbele. Imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Yusri-Allah amuwiye radhi-amesema:

Alikuja mtu mmoja siku ya Ijumaa akizikeuka shingo za watu na ilhali Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akikhutubu. Mtume wa Allah akamwambia:

“Kaa kitako, kwa yakini umewaudhi (watu) na umechelewa”. Abuu Daawoud, Nasaai, Ahmad & Ibn Khuzaymah ameiweka katika daraja ya USAHIHI & wapokezi wengineo-Allah awarehemu.

 

ADABU NA TARATIBU ZA IJUMAA

Siku ya Ijumaa na swala yake zina adabu na taratibu zilizosuniwa, yatakikana kwa kila muislamu kuzishughulikia na kuzoea kuzifanya, adabu na taratibu hizo ni pamoja na:-

1.Kukoga:

hili ni kwa mujibu wa hadithi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-isemayo: Anapoiendea mmoja wenu Ijumaa basi na akoge”. Bukhaariy (387) & Muslim (844).

Amri hii ya Bwana Mtume hapa inavuliwa kutoka katika hukumu ya uwajibu kwenda katika usuna kwa mujibu wa ile hadithi iliyopokelewa na Imamu Tirmidhiy: “Atakayetawadha siku ya Ijumaa amefuata suna na hiyo ni suna njema na atakayekoga, basi huko kukoga ni bora zaidi”.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *