Makurayshi walihisi khatari inayowanyemelea ikiwa ni natija ya yale maagano ya pili ya Aqabah. Katika maagano haya Answaar (wenyeji wa Madinah) waliagana na Mtume wa Allah yeyote awaye atakayemzuia kuufikisha ujumbe wa Mola wake kwa watu.
Nae Mtume kwa upande wake akaahidi kushirikiana nao bega kwa bega. Kwa hivyo Makurayshi wakatambua kuwa Bwana Mtume tayari sasa ana himaya, ana watu walio tayari kwa lolote katika kuihami na kuitetea imani yao:
“ …………WATAIPIGANIA DINI YA ALLAH, WALA HAWATAOGOPA LAWAMA YA ANAYEWALAUMU……..” (5:54)
Miaka kumi na tatu, ya utume aliyokaa Mtume Madinah, Makurayshi walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuidhibiti da’awah ya Uislamu isitoke nje ya mipaka ya Makkah.
Wakafanya juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa habari za Uislamu haigongi masikio ya waarabu walio nje ya mipaka ya Makkah.
Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini iliyo ya haki alitaka dini yake ienee katika ardhi kinyume na matakwa yao.
“WANATAKA KUIZIMA NURU YA ALLAH KWA VINYWA VYAO, LAKINI ALLAH AMEKATAA ISIPOKUWA KUITIMIZA NURU YAKE, IJAPOKUWA MAKAFIRI WANACHUKIA” (9:32).
Allah akamuandalia Mtume wake kundi hili lenye imani thabiti, isiyoyumbishwa wala kutetereshwa na chochote wala yeyote, kundi la watu wa Madinah.
Kundi hili likamuamini Mtume na kusadiki yote aliyokuja nayo yakiwa yamehodhi uongofu na bayana ya kila kitu. Likamuahidi kumlinda kwa nafsi na mali na wataipigania dini ya Allah kufa kupona”……..WANAPIGANA KATIKA NJIA YA ALLAH, WANAUA NA WANAUAWA…….” (9:111).
Kadhalika Makurayshi walitambua fika ujuzi, uhodari na ushujaa wa vita waliokuwa nao Ausi na Khazraji.
Nguvu yao itarudufika mara mbili zaidi Waislamu wa makkah wakihamia kwao, hapo wote watakuwa mkono mmoja, sauti moja dhidi yao.
Pia Makurayshi walifikiri kuwa Mtume amewapangia maswahaba wake mkakati wa kuhamia Madina kwa ndugu zao wa imani ambao
“…..WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI NDOGO……..” (59:9)
Baada ya kupewa idhini ya kuhama na Mtume, maswahaba walianza kuelekea Madina kwa uficho mkubwa.
Walikuwa wakiondoka mmoja mmoja au makundi ya watu wachache.
Walihama wao wenyewe na imani yao tu, huku wakiwaacha nyuma wake zao, watoto na mali zao.
Nae Mtume akabakia Makkah akisubiri amri na idhini ya Mola wake ya kuhamia Madinah kuungana na maswahaba wake. Makurayshi walipoona kwamba waislamu wanapenya kwa uficho wakifuatana kwenda Madina, waliiona hatari ya uhamiaji huu. Wakafanya kila waliwezalo kuuzuia uhamaji huu, lakini wapi, hawakuweza ila kuwazuia wanyonge tu.
Wanahistoria wa kiislamu wamepokea riwaya nyingi zinazohusiana na hijrayh hii ya masahaba wa Mtume na namna waliyojitolea muhanga.
Miongoni mwa riwaya hizo, wamepokea kwamba Bwana Swuhayb Ibn Sinaah alipotaka kuhama, makafiri wa Makkah walimwambia ulikuja kwetu ukiwa fakiri hohehahe, mtu duni kabisa, ukachuma mali hapa kwetu mpaka ukafikuia hapo ulipo.
Kisha eti leo unataka uondoke wewe na mali hiyo! Wallah, hilo haliwezekani katu! Swuhayb akwaambia: Mnaonaje, nikikuachieni mali yangu, mtaniacha niondoke?
Wakajibu: naam. Akasema: Basi mimi nimekupeni mali yangu yote. Anasema mpokezi Ibn Is-haaq : Khabari ile ikamfikie Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akawa akisema “amepata faida swuhayb! Amepata faida swuhayb!”.
Kuhusiana na kitendo hiki adhimu cha swahba wa Mtume, Bwana Swuhayb ikashuka kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu
“NA KUNA KATIKA WATU, WAUZAO NAFSI ZAO KWA KUTAKA RADHI YA ALLAH, NA ALLAH NI MPOLE KWA WAJA WAKE” (2:207).
Alipofika Madinah alipokelewa kwa shangwe na maswahaba wenzake huku wakimpa bishara njema hiyo.
Ama Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi– yeye hakuhama kwa uficho, bali alitangaza wazi kuhama kwake kama alivyotangaza kusilimu kwaka.
Imepokelewa riwaya kutoka kwa Imam Aliy. Ibn Twaalib – Allah amuwiye radhi – kwamba yeye amesema.
Muhajirina wote walihama kwa uficho isipokuwa umar tu peke yake. Yeye alipotaka kuhama, alichukua upanga, upinde, mishale na shoka yake ndogo aliyoivaa kiunoni.
Akatoka akaenda kwenye Al–kaaba ambapo wazee wa kikurayshi walikuwa wamekaa, akatufu mara saba.
Kisha akaja Maqaamu Ibrahim kaswali rakaa mbili, halafu akaziendea baraza zile za mabwana wakubwa wa Makkah moja baada ya nyingine akiwaambia, Anayetaka mama yake ampoteze mwanae, au wanawe wawe yatima, au mkewe awe mjane, basi na anifuate nyuma ya jangwa hili. Imam Aliy anasema.
Hakuna hata mmoja aliyethubutu kumfuata, nae akashika njia kuungana na wenziwe Madinah.
Hivi ndivyo Waislamu walivyouacha mji wao wa Makkah, mahala walipozaliwa, kukulia na kupazoea.
Hawakubeba chochote zaidi ya imani yao, wanakwenda ugenini Madinah kuanza maisha upya. Waislamu wakamiminika Madinah mpaka hawakusalia Makkah ila Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie Abuu Bakri, Aliy na baadhi ya wanyonge ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu anawataja ndani ya Qur-ani Tukufu:
“ISIPOKUWA WALE WALIOKUWA MADHAIFU KWELI, KATIKA WANAUME NA WANAWAKE NA WATOTO WASIO NA UWEZA WA HILA YOYOTE, WALA HAWAWEZI KUONGOZA NJIA (kwenda Madinah) BASI HAO HUENDA ALLAH AKAWASAMEHE,. ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUGHUFURIA”. (4:-99)
Hapo Madinah, Muhajirina hawa wakapokelewa na ndugu zao wa Imani Answaar kwa mapenzi yaliyochanganyika na udugu kwa Imani ya kweli. Wakawapa makazi, wakagawana nao mali na majumba yao na wakawapendelea kuliko nafsi zao. Kuhusiana na udugu huu tunasoma.
“HAKIKA WALE WALIOAMINI NA WAKAHAMA NA WAKAIPIGANIA DINI YA ALLAH KWA MALI ZAO NA NAFSI ZAO (nao ni wale Muhajiria – Waislamu wa Makkah) NA WALE WALIOWAPA (Muhajirina) MAHALA PA KUKAA (Nao ni Answaar) NA WAKAINUSURU (dini ya Allah) HAO NDIO MARAFIKI, WAO KWA WAO……….” (8:72) Ama Mtume yeye aliendelea kubakia Makkah akisubiri idhini ya kuhama kutoka kwa Mola wake.
Sayyidna Abu Bakri kila alipotaka kuhama, Bwana Mtume alimsubirisha na kumwambia.
“Usiwe na haraka, huenda Allah akakupa mtu wa kufuatana nae” Hapo ndipo Abu Bakri alipotambua kwamba Bwana Mtume ana nia ya kuhama lakini tu anaingojea ruhusa ya Mola wake.
Akanunua vipando(wanyama) viwili akaviweka nyumbani kwake tayari kwa safari ya Madinah, yeye na Mtume wa Allah.