Chimbuko na msingi wa somo/mada hii ni kauli tukufu ya mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya kitabu chake kitukufu allipomwambia Mtume wake;
“… NA UFUNGAPO NIA MTEGEMEE ALLAH (tu ufanye uliloazimia) HAKIKA ANAWAPENDA WAMTEGEMEAO.” (3:159)
Tutafahamu kutokana na kauli hii ya Mwenyezi Mungu kwamba “azma” ni nguvu fulani ya utendaji ambayo huwa ndani ya nafsi ya kila mtu, ni nguvu hii ambayo humsukuma mtu kulitenda lile alitakalo, liwe ni jema au baya.
Bila ya kuwa na nguvu hii ya utendaji “azma” binadamu hawezi kutenda/kufanya jambo lolote lile liwalo, la shari au la kheri. Kwa mantiki hii tunaruhusika kabisa kuigawa azma katika makundi mawili:
- Azma njema (ya kheri)
- Azma mbaya (ya shari)
Azma njema, ambayo ndio somo letu na ambayo ndio iliyotajwa ndani ya aya hapo juu ni ile inayompelekea mtu kuwa na subira, kuridhia kukabiliana na vikwazo na magumu yote atakayokutana nayo katika safari ya utekelezaji wa maazimio yake mema.
Azma hii njema itamfanya mtu kuwa thabiti asiyeyumbishwa na yeyote/lolte katika kutekeleza amali zake njema mpaka ayahakikishe matakwa yake.
Katika kuyafanya yote hayo, mtu mwenye azma hii njema humtegemea sana mola muumba wake katika kufikia ufanisi na matokeo bora ya azma yake.
Huamini kuwa hakuna yeyote au nguvu yoyote kutoka kwa yeyote inayoweza kumsaidia katika hayo aliyoyaazimia ila kwa nguvu, matakwa na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Bwana Mlezi wa viumbe wote.
Azma yaani nguvu/msukumo wa utendaji una athari kubwa sana katika maisha ya kila siku ya binadamu katika ulimwengu huu aishimo hivhi sasa na ule ujao. Azma huathiri kwa kiwango kikubwa maeneo yafuatayo:-
- Akili
- Tabia
- Itikadi
1. Akili:- Hebu tujaribu kuangalia ni kwa kiasi gani azma inavyoweza kuliathiri eneo hili mama katika mwili wa binadamu.
Azma ndio kichocheo kikubwa katika kuamsha ari na kumuhamasisha mtu kujikomboa kutoka hali duni aliyomo kwenda katika hali bora zaidi.
Azma inapoungana na neema ya akili aliyozawadiwa mwanadamu na mola wake, hapo ndipo utamuona mwanadamu anaweza kugundua vitu na zana mbalimbali ambazo zinamsaidia kuyaboresha na kuyarahisisha maisha yake na kuyaongezea utamu na ladha maisha haya.
Hapo ndipo binadamu huutumia ukhalifu wake kwa kuyatawala mazingira yake na kuzitumia rasilimali zilizomo duniani kwa ajili ya manufaaa ya vizazi vya wanadamu.
“YEYE NDIYE ALIYEKUUMBIENI VYOTE VILIVYOMO KATIKA ARDHI (kabla hajakuumbeni ili mkute kila kitu tayari)…” (2:29)
Azma kwa kushirikiana na akili humsukuma binadamu kuwa mdadisi, udadisi huu humsukuma kuwa mtafiti.
Utafiti ambao humfikisha katika pwani ya ugunduzi. Ugunduzi huu ndio humfanya binadamu kupiga hatua mbele katika maendeleo. Kutumia akili, kutafiti na hatimae kugundua ni jambo jema ambalo uislamu unalihimiza sana, tusome kwa mazingatio:
“AMBAO HUMKUMBUKA ALLAH WAKIWA WIMA NA WAKIKAA NA WAKILALA NA HUFIKIRI UMBO LA MBINGU NA ARDHI (pia namna gani Allah alivyoumba wakasema:)” MOLA WETU!HUKUVIUMBA HIVI BURE. UTUKUFU NI WAKO BASI TUEPUSHE NA ADHABU YA MOTO” (3:191) Tuzidi kusoma: “………NAMNA HIVI ALLAH ANAKUBAINISHIENI AYA(zake) MPATE KUFIKIRI (mfikiri) KATIKA (mambo ya ) DUNIA NA (mambo ya ) AKHERA.” (2:219 – 220)
Ni azma pia kwa msaada wa akili ambayo humsukuma binadamu kukaa chini, kutafakari na hatimaye kuibuka na jawabu na ufumbuzi wa matatizo yanyomkabili kutokana na ujinga, maradhi, umasikini na itikadi potofu.
Hapo ndipo binadamu huweza kugundua dawa anuwai za kumtibu maradhi mbalimbali yanayomsumbua na kuvuruga utendaji wake. Akagundua zana stadi zitakazomsaidia kuutokomeza umasikini.
2. Tabia: Tabia ya mtu pia kwa kiasi kikubwa huathiriwa na kutawaliwa na azma.
Hii ni kwa sababu tabia ya mtu haiwezi kabisa kujulikana na watu wengine ila kwa kupitia nguvu hii ya utendaji iliyomo ndani yake.
Mtu anapoimiliki nguvu hii na ikamuelekeza kutenda matendo yayokubalika kiutu, kimaadili na kiitikadi matendo haya yanapokuwa dhahiri mbele ya wanajamii wamzungukao, hapo ndipo jamii husika humtia mtu huyo katika daftari la watu wenye tabia njema, watu wakubalikao katika jamii.
Ama yule ambaye hushindwa kuimiliki azma yake, azma hii ikampelekea kutenda matashi ya nafsi yake bila ya kuangalia madhara au manufaa yua matendo hayo kwake na kwa jamii ni dhahiri kuwa utendaji wake utakuwa ni mbaya mbele ya hadhira (jamii).
Hapo ndipo jamii humhukumu kupitia utendaji wake huo kuwa ni mtu mbaya mwenye tabia na athari mbaya kwa jamii.
Kwa ujumla tunasema kwamba azma ndio huidhirihirisha nje tabia ya mtu, iwe ni nzuri inayokubalika au ile mbaya isiyokubalika.
3. Itikadi: Itikadi au Imani hili pia ni eneo ambalo huathiriwa sana na azma.
Nguvu hii ya utendaji azma ndio humsukuma mwanaitikadi au muumini wa imani fulani kutenda na kuishi kwa mujibu wa imani yake.
Humfinyanga kuitetea imani yake kwa gharama yoyote ile hata ikibidi rorho yake. Humuandaa kusubiri na kuvumilia misukosuko na matatizo mbalimbali ya kimaisha. Tusome pamoja na tutafakari:-
“MTAPATA MISUKOSUKO KATIKA MALI ZENU NA NAFSI ZENU, NA MTASIKIA UDHIA MWINGI KWA WALE WALIOPEWA KITABU KABLA YENU NA KWA MUSHRIKINA. NA KAMA MKISUBURI NA KUJILINDA NA ALIYOYAKATAZA ALLAH (mtakuwa mmefanya jambo zuri) KWANI MAMBO HAYA NI KATIKA MAMBO MAKUBWA YA KUAZIMIA MTU KUYAFANYA.”(3:186)
Hii ndio azma na namna iinavyotawala na kuathiri akili, tabia na itikadi ya binadamu. Kutokana na umuhimu huu, tunaweza kusema kuwa uislamu wa mtu haukamiliki ila pale atakapojipamba na tabia/hali hii ya “azma”.
Muislamu ni lazima awe mtu mwenye azma, na sio azma tu bali azma njema.
Hii ni kwa sababu mtu anapoikosa nguvu hii ya utendaji “azma” jepesi huliona gumu, dogo huliona kubwa na liwezekanalo huwa kwake ni muhali na hivyo kumfanya abakie nyuma kimaendeleo.
Akili yake itadumaa, haitoweza kudadisi kutafiti wala kugundua, vipi utamtazamia mtu kama huyo kuwa na maendeleo?!