Baada ya kujifunza mambo mengi yahusianayo na swala, sasa ni vema tukajifunza namna ya kuswali ili kulitekeleza agizo la Mtume wa Alalh – Rehema na Amani zimshukie – lisemalo:
“Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali” Bukhaariy.
Ni dhahiri kwamba amri na maelekezo haya ya Bwana Mtume yalikuwa yanawagusa moja kwa moja maswahaba wake, kwa kuwa wao ndio walikuwa pamoja nae wakamuona anavyoswali.
Ama sisi amri hiyo nasi inatugusa lakini si kwa njia ya moja kwa moja kama maswahaba.
Sisi hatuwezi kuswali kama alivyoswali Bwana Mtume kwa kuwa hatukuishi nae kwa hiyo hatukupata bahati ya kumuona akiswali kama alivyofundishwa na mwalimu wake Malaika Jibril-Amani ya Allah imshukie kwa amri na maelekezo ya Allah:
“Alinijia Jibril – Amani imshukie mwanzo kabisa mwa wahyi (ufunuo) akanifundisha udhu na swala………………..” Al-haakim, Baihaqiy na Ahmad.
Sisi tunaswali kama maswahaba wa Mtume wa Allah – Allah awawiye radhi, kwani wao ndio waliotufundisha dini ndani yake ikiwemo swala.
Ni kwa kuwafuata wao tu ndio tunaweza kuswali kuwa alivyoswali Mtume wa Allah.
Sasa hebu tufuatane nao kwa makini watufundishe swala ili nasi tuweze kuswali kama alivyokuwa akiswali mwenyewe Bwana Mtume, nae kama alivyofundishwa na Jibril kwa amri ya Allah. Ewe Mola wa haki wee!
Tuongoze na utuwafikishe kuswali, kufunga, kuhiji, kutoa zakkah na baki ya amali nyingine kama alivyofundisha kipenzi chako, Nabu Muhamaad Aamiyn!
Haya na tuswali sasa:
1. Baada ya kujitwaharisha na kuingia wakati wa swala unayotaka kuiswali na kujistiri tupu (uchi) kama tulivyobainisha katika darasa zilizotangulia, simama wima uelekee Qiblah kwa kuitekeleza amri ya Mola wako.
“NA POPOTE UENDAKO GEUZA USO WAKO KWENYE MSIKITI MTAKATIFU.NA POPOTE MLIPO GEUZENI NYUSO ZENU UPANDE ULIKO (msikiti huo)……………………. (2: 150)
Muradi na makusudio ya “msikiti Mtakatifu” hapa ni dhati ya Al-ka’abah”, hivi ndivyo inavyobainishwa na hadhiti kadhaa. Miongoni mwazo ni hii:
Imepokelewa na Ibn Abbaas – Allah awawiye radhi amesema:
Mtume Rehama na Amani zimshukie alipoingia ndani ya Al-ka’abah aliomba dua katika pande zake zote na hakuswali (mle ndani) mpaka alipotoka nje.
Alipotokea nje akaswali rakaa mbili mbele ya Al-kaabah na akasema “Hiki ndio Qiblah”. Bukhaariy na Muslim.
2. Baada ya kusimama na kuelekea Qiblah, ni wajibu utie nia ya swala unayotaka kuswali moyoni. Huko ni kumfuata Mtume kwa kutekeleza kauli yake,
“Hakika si vinginevyo amali zote zimefungamaan na nia na kila mtu atalipwa kwa kadri ya nia yake………” Bukhaariy
Nyanyua vitanga vya mikono mpaka mkabala wa mabega yako hali ya kuleta nia na kisha useme (Allah Akbar) Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar – Allah awawiye radhi – amesema:
“Alikuwa Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anaposimama kuswali, hunyanyua mikono yake (vitanga) mpaka ikawa mkabala na mabega yake kisha akakabiri (akasema Allahu Akbar)………..”Muslim.
3. Halafu funga swala kwa kuiteremsha mikono na kuiweka chini ya kifua, huku ukiushika mgongo wa kitanga cha mkono wa kushoto kwa kile cha kulia. Hivi ndivyo atufundishavyo swahaba Waail Ibn Hijri – Allah amuwiye radhi amesema:
“Nilimuona Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie anapoingia ndani ya swala huushika mkono wake wa kushoto kwa ule wa kulia” Ibn Mundhir, Ibn Khuzaymah na Abuu Dawoud.
4. Kisha fungua swala yako kwa kuleta dua ya ufunguzi wa swala (Iftilaahi). Hili linatokana na kauli ya Imam Aliy-Allah amuwiye radhi amesema:
“Alikuwa Mtume wa Allah- anaposimama kuswali husema.
WAJJAHTU WAJHIYA LILLADHI FATARASWAMAAWATI WAL-ARDHI HANIIFAN WAMAA ANA MINALMUSHRIKIIN, INNA SWALAATIY WA NUSUKII WA MAHYAAYA WA MAMAATIY LILLAHI RABBIL-AALAMIIN LAA SHARIIKA LAHU WABIDHALIKA UMIRTU WA ANAA MINAL-MUSLIMIIN. Muslim na Ibn Hibban.
5. Baada ya kumaliza kusoma dua hiyo ya ufunguzi wa swala, lete “Audhubillah kabla ya kuanza kusoma Al-hamdu. Hayo ndiyo maelekezo ya Mola wako, sikia:
“NA UKITAKA KUSOMA QUR-ANI PIGA AUDHU (Kwanza, jikinge) KWA ALLAH (akulinde) NA SHETANI ALIYEFUKUZWA (Katika rehema ya Allah)” (16: 98)
Kadhalika imepokelewa kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie kamba:
“Alikuwa akisema baada ya Iftitaahi (dua ya ufunguzi) na kabla ya kisomo (cha Al-hamdu).
AUDHU BILLAHI-SSAMI’UL-ALIIM MINAS-SHAITAANI-RRAJIIM. Abuu Daawoud.
6. Halafu soma Suuratil – Faatihah (Al-hamdu) kwa kuanza na Bismillahi kwani hiyo Bismillahi ni aya miongoni mwa aya zake (Al-hamdu).
Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Huray-rah-Allah amuwiye radhi – amesema: Amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie:
“ Mnaposoma Al-hamdulillah” someni BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM kwani hiyo ndiyo Umul-Qur-ani, Umul-Kitaab na Sab-ul-mathaaniy, na BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM ni mojawapo ya aya zake. Daaru qutwniy na Baihaqiy.
7. Unapofikia mwisho wa Al-hamdu WALADHWAAALIIN itikia “Amiyn” Hivi ndivyo ilivyopokelewa na Abuu Hurayrah – Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa Allah – rehema na Amani zimshukie amesema:
“Atakaposema Imamu WALADHWAAALIIN Semeni Aamiyn, kwani itakayewafikiana Aamiyna yake na Aamiyna ya malaika, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia (yaliyopita)” Bukhaairy.
8. Baada ya Kuitikia “Aamiyn”, soma sura nyingine au sehemu ya sura yoyote lakini bora ni kusoma sura kamili.
Hiyo ndiyo swala ya Mtume kama alivyotupokelea Abuu Qataadah-Allah amwie radhi-
“Kwamba Mtume Rehema na Amani zimshukie- alikuwa akisoma katika swala ya Adhuhuri katika rakaa mbili za mwanzo Ummul Kitaab (Al-hamdu) na sura mbili (nyingine) na katika zile rakaa mbili nyingine (za mwisho akisoma) Ummul-Kitaab pekee …” Bukhariy
9. Kisha nyanyua vitanga vyako mpaka mkabala wa mabega na uende rukuu il-hali ukisema ALLAHU AKBAR, na kufanya hivyo ni kuitii kauli ya Mola wako isemayo “MLIYOAAMINI! RUKUUNI NA SUJUDUNI NA MWABUDUNI MOLA WENU NA FANYENI MEMA ILI MPATE KUFAULU” [22:77].
Katika rukuu weka vitanga vyako magotini, nyoosha mgongo wako na utulizane.
Hivi ndivyo alivyosema Mtume wako-Rehema na Amani zimshukie- wakati alipokuwa akimfundisha swala yule mtu aliyekuwa akiswali sivyo, akamwambia :
“…Halafu rukuu mpaka utulizane il-hali umerukuu …” Bukhaariy.
Ama uwekaji wa vitanga magotini, imepokelewa kwa Saalim Al-Barraad Al-kuufiy amesema :
“Tulimwendea Abu Mas-oud, tukamwambia : -Tuhadithie kuhusiana na swala ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie, akasimama mbele yetu akakabbbir, aliporukuu akaweka vitanga vyake juu ya magoti yake na vidole vyake akaviweka chini ya hapo …” Nasaai.
Ukishatulizana katika rukuu ndipo useme mara tatu au zaidi : SUBHAANA RABBIYAL-ADHIIM.
Hii ndiyo swala ya Mtume kama ilivyopokelewa kutoka kwa Hudhayfah Ibn Al-yamaan – Allah amwie radhi – amesema :
“Niliswali pamoja na Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – aliporukuu akawa akisema : SUBHAANA RABBIYAL-ADHIIM …” Muslim na Ibn Hibbaan.
10. Baada ya Kukamilisha rukuu, inuka kutoka rukuu il-hali ukisema SAMIA’-LLAHU LIMAN HAMIDAH na usimame ukiwa umetulizana.
Hayo ndiyo mafundisho ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomfundisha yule mtu aliyekuwa akikosea katika swala yake :
“… Kisha rukuu mpaka utulizane hali ya kurukuu, kisha inuka mpaka utulizane hali ya kusimama …” Ibn Maajah.
Kisha ukilingana sawa hali ya kusimama sema katika itidali hiyo RABBANAA LAKAL-HAMDU.
Haya yote yamepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – :
“… Kisha husema SAMIA’L-LAHU LIMAN HAMIDAH wakati anpounynanyua uti wa mgongo wake kutoka rukuu, kisha husema naye akiwa amesimam : RABBANAA LAKAL-HAMDU …” Bukhaariy
11. Halafu poromoka kwenda kusujudu il-hali ukisema (Allahu Akbar), usujudu kwa viungo saba.
Hakikisha uso, vitanga (viwili) magoti (mawili) na miguu (nyayo mbili) vyote hivi viguse ardhi (busati/mkeka). Kusujudu kunatokana na kauli ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-wakati akifundisha swala :
“..kisha usujudu mpaka utulizane hali ya kusujudu …” Bukhariy na Muslim.
Ama kuhusiana na viungo vinavyohusika na sijida, imepokelewa na Ibn Abbaas – Allah awawiye radhi – kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – amesema :
“Nimeamrishwa kusujudu juu ya viungo saba, juu ya paji la uso, akaiashiria pua yake kwa mkono (kidole) na mikono (miwili) na magoti (mawili) na ncha (za vidole) vya miguu …” Bukhaariy na Muslim.
Ukishatulizana katika sijida sema : SUBHAANA RABBIYAL-A’LA mara tatu au zaidi. Hivyo ndivyo alivyoswali Mtume wa Allah kama anavyotueleza Hudhayfah Ibn Al-yamaan –Allah amuwie radhi –
“Niliswali pamoja na Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie- aliporukuu akawa akisema : SUBHAANA RABBIYAL-ADHIIM kisha akasujudu na akasema : SUB-HAANA RABBIYAL-A’LA ..” Muslim.
Pia imethibiti kwamba wakati mwingine Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akisema katika sijida yake :
SUB-HAANA RABBIYAL-A’LA WA BIHAMDIH na katika rukuu (akisema) SUB-HAANA RABBIYAL-ADHIM WABIHAMDIH. Hivyo ndivyo alivyopokea Daaruqutwniy.
12. Kisha inuka kutoka sijida il-hali ukisema (Allahu Akbar) ukae kitako mkao wa iftiraashi na useme :
ALLAHUMMAGHFIR LII WARHAMNII WA A’AFINIY WAHDINII WARZUQNII Hivyo ndivyo alivyoelekeza Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – :
“…Kisha usujudu mpaka utulizane hali ya kusujudu, halafu inuka mpaka itulizane hali ya kukaa …” Bukhariy na Muslim.
Ama dhikri hiyo ya kitako inatokana na ile hadithi ya Ibn Abbaas – Allah awawie radhi – amesema :
“Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akisema baina ya sijida mbili : ALLAHUMAGHFIR LII WARHAMNII WA A’FINIY WAHDINIY WARZUQNIY” Abu Daawud, Tirmidhiy na Muslim.
Na katika riwaya ya Baihaqiy kuna ziada : WAJBURNIY WARFA’NIY.
Kisha sema Allahu Akbar huku ukienda kusujudu sijida ya pili kama ulivyosujudu ile ya kwanza. Sijida hii ya pili imo katika ile kauli ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“…Kisha sujudu mpaka utulizane hali ya kusujudu (sijida ya kwanza), halafu inuka mpaka utulizane hali ya kukaa (kitako baina ya sijida mbili), kisha sujudu (tena) mpaka utulizane hali ya kusujudu (sijida ya pili) … “ Bukhariy na Muslim.
Kwa kufuata utaratibu huu tulioutaja, mpaka hapo itakuwa imetimia na kukamilika rakaa ya kwanza.
Sasa inuka kutoka kutoka sijida il-hali ukisema Allahu Akbar mpaka usimame wima tayari kuanza rakaa ya pili.
Hii rakaa ya pili utaiswali kama ulivyoiswali ile ya kwanza. Isipokuwa katika hii rakaa ya pili hakuna tena kuleta nia ya Iftitaahi (Dua ya ufunguzi).
Kadhalika rakaa hii ya pili isiwe ndefu kama ile ya kwanza, hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Qatadah – Allah amuwie radhi – :
“…na akiitwawilisha (akirefusha) katika rakaa ya kwanza asivyotwawilisha katika rakaa ya pili …” Bukhaariy.
13. Baada ya kutoka katika sijida ya pili ya rakaa ya pili, kaa kitako usome tashahudi ya kwanza ikiwa swala uiswaliyo ni ya rakaa tatu au au nne kama Magharibi na Isha.
Hivi ndivyo iliyopokelewa katika hadithi ya yule mtu aliyekuwa akiswali sivyo ndivyo, Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akamwambia :
“…utakapokaa kitako katikati ya swala, basi tulizana na (ukae mkao wa Iftiraashi) ulitandike paja lako la kushoto, kisha ulete tashahudi …” Abu Daawoud.
Na tashahudi ni kama ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbaas – Allah awawie radhi – kwamba yeye amesema : Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akitufundisha Tashahudi kama anavotushinda sura ya Qur-ani, alikuwa akisema :
“ATTAHIYYATU ALMUBARAKATU, ASSWAALAWATU ATTAYIBAATU LILLAHI, ASSALAAMU ALAYKA AYYUHANNABII WARAHMATULLAHI WABARAKATUH, ASSALAAMU ALAYNA WA A’LAA IBADILLAHI SSWALIHIIN, ASH-HADU AN LAA ILAHA ILLALLAH, WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN RASULULLAH” Muslim
Baada ya kumaliza kusoma tashahhudi kama ilivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume, sasa inuka huku ukisema Allahu Akbar, uiinue mikono yako mkabala wa mabega, funga swala. Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Humayd As-saaidiy :
“ … Kisha hukabiri anapoinuka kutoka katika rakaa mbili (za mwanzo) na huinyanyua mikono yake mpaka mkabala wa mabega yake …” Abu Daawoud.
Swali rakaa ya tatu na ya nne kama rakaa mbili za mwanzo.
Lakini katika rakaa mbili hizi za mwisho baada ya Al-hamdu husomi sura nyingine wala husomi Al-hamdu kwa sauti ikiwa swala uiswaliyo huswaliwa kwa kutoa sauti.
14. Baada ya sijida ya pili ya rakaa ya tatu ya swala ya Magharibi au sijida ya pili ya rakaa ya nne ya swala za adhuhuri, alasiri, na ishaa., kaa mkao wa tawaruki na usome tashahudi ya mwisho.
Lete tashahudi kama tulivyokwisha itaja, halafu umswalie Bwana Mtume kabla ya kutoa salamu. Kumswalia Bwana Mtume ndani ya swala na kulitekeleza agizo la Allah :
“HAKIKA ALLAH ANAMSWALIA MTUME (anamteremshia rehema) NA MALAIKA WAKE WANAMSWALIA (wanamuombea dua). BASI, ENYI MLIOAMINI MSWALIENI (Mtume, muombeeni rehema) NA MUOMBEENI AMANI” [33:56].
Imepokelewa kutoka kwa Abdulrahman ibn Abiy Laylaa, amesema :
Nilikutana na Ka’bu ibn Ujrah akaniambia : Je, nikupe hidaya (zawadi) niliyoisikia kutoka kwa Mtume –Rehema na Amani zimshukie – ? Nikasema : Kwani, nipe, akasema : Tulimuuliza Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – tukasema : Ewe Mtume wa Allah, tukuswalieni vipi enyi Ahlul-bayti, kwani Allah ametufundisha jinsi ya kukuombeeni amani.
Akasema (Mtume) : “Semeni :
ALLAHUMMA SWALLI ALAA MUHAMMAD WA A’LAA AALI MUHAMMAD KAMAA SWALLAYTA ALAA IBRAHIM WA A’LAA AALI IBRAHIM INNAKA HAMIDUN MAJIID. ALLAHUMMA BAARIK ALAA MUHAMMAD WA A’LAA AALI MUHAMMAD KAMAA BAARAKTA ALAA IBRAHIM WA A’LAA AALI IBRAHIM INNAKA HAMIDUN MAJIID. Bukhaariy, Muslim na Baihaqiy.
15. Kisha toa salamu kwa kusema : ASSALAAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH huku ukigeukia kuliani na toa salamu ya pili huku ukigeukia kushoto. Imepokelewa na Bi Aysha – Allah amwie radhi – amesema :
“Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akiifungua swala kwa Takbiyrah na kuikhitimisha kwa salamu.” Abu Daawoud na Baihaqiy.
Imepokelewa kutoka kwa Sa’d ibn Abiy Waqqaaswi – Allah amuwie radhi- amesema : “Nilikuwa nikimuona Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akitoa salamu kuliani na kushotoni kwake mpaka nikiuona weupe wa kitefute (shavu) chake.” Muslim.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Mas-oud – Allah amwie radhi – amesema :
“Sijasahau mambo, kwani mimi bado sijaisahau utoaji salamu wa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – kuliani na kushotoni kwake :
“ASSALAAMU ALEYKUM WARAHMATULLAH ASSALAAMU ALEYKUM WARAHMATULLAH.” Ibn Hibbaan na wengineo.
Hiyo ndio swala ya Mtume na kwa kuswali hivyo utakuwa umeikubali na kuitekeleza kivitendo kauli na agizo la Mtume :
“Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali” Bukhariy.
HITIMISHO (KIJALIZO):
Huenda wewe msomaji wetu mpenzi ukawa unajiuliza kama wanavojiuliza wengine na kusema : Allah-Subhanahu Wa Ta’ala anasema ndani ya Qur-ani :
“…BILA SHAKA SWALA HUMZUILIYA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU …” [29:45].
Ikiwa ndivyo hivi, mbona tunawaona baadhi ya watu wanaswali kila siku na bado wana mambo machafu na maovu ?! Tabia zao mbaya, maneno yao machafu na mienendo yao miovu !
Jawabu sahihi la swali hili ni kwamba watu hawa hawajaisimamisha swala kwa namna sahihi itakiwayo ambayo iliyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie.
Hawajaswali bado kama alivyoamrisha Mtume na kuwafundisha maswahaba wake watukufu – Allah awawiye radhi.
Hawa wamepuuza kujifunza fiq-hi ya swala na mchanganuo wake sahihi. Wametosheka na kutekeleza matendo (harakati) ya dhahiri (nje) kwa kuwaiga tu watu.
Hawa ndio mithili ya yule mtu ambaye aliyeingia msikitini akaswali na il-hali Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akimuangalia.
Alipomaliza kuswali swala yake hiyo, Mtume akamwambia :
“rejea uswali tena kwani hakika wewe bado hujaswali” Bukhariy na Muslim.
Mtu anaswali na bado Mtume anamwambia mara tatu kaswali tena.
Chini ya kivuli cha kauli hii ya Mtume kuna ufumbulizo wa wazi kwamba kuna baadhi ya watu wanatenda matendo ya swala; wanasimama, wanarukuu, wanaitadili, wanasujudu na kukaa lakini hawaswali.
Hawa hawaswali kwa maana ya kuswali kwa sababu ya kutokuwa na elimu ya kutosha na sahihi juu ya swala.
Elimu na maarifa ambayo yatawapelekea kuswali kama alivyofundisha Bwana Mtume na si kama watakavyo na kupenda wao.
Kwa mantiki hii swala yao inakuwa fasidi (isiyokubalika) na wanahesabika kama hawajaswali, japokuwa wao watajihesabu wameswali. Kama wanadai wameswali, tunawauliza mbona swala zenu hazijakufikisheni katika lengo :
“…BILA SHAKA SWALA HUMZUILIA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU…” Zinduka na utambue kwamba yule atakayeswali kwa kuijua swala, kuanzia nguzo, suna, sharti, karaha na yabatilishayo na baki ya mambo mengine yafungamanayo na swala.
Akayajua yote hayo kupitia elimu sahihi, huyu ndiye ambaye Allah humuumbia kinga ndani ya moyo wake.
Kinga hii ndio humfanya aamrike katika mema na akatazike katika maovu na machafu.
Kinga hii ndio humpendezesha mambo ya twaa na kumchukizishia mambo ya maasi na kuifanya njema tabia yake. Hi ndio falsafa ya amri ya kwanza kumshukia Mtume kuwa ni KUSOMA na sio KUSWALI.
Ataswali vipi bila ya kuijua hiyo swala yenyewe ?!
(ALLAH NDIYE MJUZI MNO)