KUZOEANA NA WATU

Kimaumbile mwanadamu ni kiumbe mwenye tabia ya kuchanganyika kimaisha na wenziwe.

Maumbile ya mwanadamu hayakubaliani kabisa na upweke bali kuchanganyika mwanadamu na wanadamu wenziwe katika maisha ya kijamii ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu huyu ambayo hawezi kuyaepuka wala kuyabadilisha.

Mwanadamu hajitegemei kimaisha peke yake, bali ili aweze kuishi na kuyafurahia maisha hana budi kuchanganyika na watu wa rika, jinsia na tabia tofauti.

Hapa sasa katika kuchanganyika na jamii kimaisha ndipo linapojitokeza suala zima la tabia hii muhimu ya kuzoeana na watu, tabia ambayo kila muumini anapaswa kujipamba nayo kwani ni moja wapo ya vigezo vya imani ya mja kama anavyolibainisha hilo mkweli Muaminifu – Rehema na Amani zimshukie:

“Muumini anayechanganyika na watu na kustahimilia maudhi (kero) yao ni bora zaidi kuliko yule muumini ambaye hachanganyiki na watu na wala hastahamilii maudhi yao.” Ahmad, Bukhariy, Tirmidhy na Ibn Maajah.

Tayari tumekwisha kuona umuhimu, nafasi na mchango wa tabia ya kuzoeana na watu katika maisha yetu ya kila siku kama wanadamu.

Hebu sasa tujue tunakusudia na kumaanisha nini tunapozungumzia suala hili la kuzoweana na watu ?

Tunapozungumzia kuzoeana na watu huwa hatumaanishi kingine zaidi ya ile hali ya mwanadamu kuliwazika, kufarijika kuwa karibu na jamii inayomzunguka na kufurahika nayo. Hali au tabia hii huchochewa na mambo kadhaa, miongoni mwa mambo hayo ni yafuatayo:

1.      Dini. Hii ndiyo chachu kuu inayoziathiri nyoyo za watu kuzoeanan na hivyo kuwafanya waungane na kuwa ndugu moja chini ya Imani moja na hapo ndipo hupatikana ikamilifu wa imani. Tusome:

“NA (Allah) AKAZIUNGA NYOYO ZAO (wakapendana wote hao Masahaba zake) HATA KAMA UNGALITOA VYOTE VILIVYOMO ARDHINI USINGALIWEZA KUZIUNGA NYOYO ZAO, LAKINI ALLAH NDIYE ALIYEWAUNGANISHA …………..” (8:63).

2.      Nasabu (Ukoo). Hiki ndicho chanzo cha pili kinachoweza kuziathiri nyoyo mpaka watu wakaweza kuzoeana.

Katika hali ya kawaida udugu/ujamaa utokanao na nasabu huwafanya wana nasabu husika kuoneana huruma na kupendana wao kwa wao.

Hivyo ndivyo tunavyoelewa kutokana na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani ziimshukie: “Hakika udugu (wa nasabu) utakapogusana (ndugu hao) huonekana huruma.”

3.      Ukwe. Ukwe ni matokeo ya mtu kuoa kwa watu wengine au yeye kuwaozesha wao.

Jambo hili ni kichocheo kikubwa cha kuziunganisha familia mbili husika; familia ya binti na ile ya kujana wa kiume.

Watu wa familia mbili hizi huzoeana, wakajihisi ndugu na hivyo kuwafanya kuungana pamoja katika furaha na huzuni.

Khalid Ibn Yaziyd mjukuu wa Muawiyahn anasimulia kuonyesha ni jinisi gani ukwe unavyoziathiri nyoyo za watu zikazoeanan na kupendana, anasema:

Kulikuwa hakuna watu ninaowachukia kama watu w ukoo wa Zubeyr mpaka pale nilipowaolea, wakawa wanapendeza zaidi kwangu”.

Haya yote hutokana na yale maumbile yaliyomo ndani ya mtu, maumbile haya ambayo mwanadamu hayatawali ndiyo humsukuma mtu anapompenda mkewe kuwapenda na ndugu/jamaa wa mwanamke huyo.

4.      Wema: Wema wa kuwafanyia hisani watu huchangia kwa kiasi kikubwa zoezi la watu kuzoeana na hatimaye huwaunganisha pamoja na wakapendana.

Hili linatokana na maumbile kwa sababu nyoyo za wanadamu zimeumbwa katika maumbile ya kumpenda mwenye kuzitendea wema na kumchukia mwenye kuzitendeauovu/ubaya. Mshairi wa Kiarabu analizungumzia hili katika beti zake, anasema :

Wafanyie ihsani watu tazitia utumwani nyoyo zao. Mja ni mtumwa wa Ihsani.

Haya ndio baadhi ya mambo ambayo huchangia sana watu kujenga tabia ya kuzoea na matunda ya hali/tabia hii ni pamoja na mtu.

    1. Kufaidika na jamii yake na yeye kuifidisha katika kuchangia maendeleo yao
    2. Kushirikiana na kusaidiana katika wema na kumcha Mwenyezi Mungu mtukufu
    3. Kuchangia kwa kiasi kikubwa kuleta hali ya maelewano na masikilizano baina ya wana jamii

 

Ni kwa kuyazingatia matunda haya ndipo Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie akatuambia : “ Muumini huzoea (watu) na wala hazoeleki”.Ahmad na Al-Haakim.

KUUNGA / KUFANYA UDUGU

“MUHAMMAD NI MTUME WA ALLAH NA WALIO PAMOJA NAYE NI WENYE NYOYO THABIT MBELE YA MAKAFIRI NA WENYE KUHURUMIANA WAO KWA WAO …..” (48:29)

Hii ndio siri kubwa ya mafanikio na ushindi wa waislamu wale wachache kiidadi wakiongozwa na Bwna Mtume – Rehema na Amani zimshukie – dhidi ya makafiri wengi wa idadi na wenye zana bora za vita.

Hili halikutokea kwa sadfa au bahati tu bali haya ndiyo matunda ya kazi nzuri ya Bwana mtume. Haya yalitokana na kazi aliyoifanya mtume mara tu baada ya kufika Madinah akitokea Makkah.

 Kazi hii si nyingine bali ni ule mkakati wa kuunga undugu wa kweli, udugu wa Imani. Bwna Mtume aliunga udugu huu halisi baina ya Muhajiri na (watu wa Makkah) na Ansaari, ( wenyeji wa Madinah) alikuwa akiwaambia kila, watu wawili:

 “ kuweni ndugu wawili wawili kwa ajili ya Allah”.

Athari ya udugu huu ikawa kama anavyotuelezea Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya Qur-ani

“ NA WALE WALIOFANYA MASKANI YAO HAPA (yaani Madinah) NA WAKAUTAKASA UISLAMU WAO KABLA YA (kuja Muhajiri huko Madinah) NA WAKAWAPENDA HAO WALIOHAMIA KWAO, WALA HAWAONI DHIKI NYOYONI MWAO KWA HAYO WALIOPEWA (hao Muhajiri) NA WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI NDOGO….” (59:9)

Huu ndio udugu wa Kiislamu na hayo ndio matunda yake. Huko ndiko kuunga udugu, sifa ambayo anatakiwa muislamu ajipambe nayo ili kujenga mapenzi na mshikamano imara ili kuupa nguvu Uislaamu na waislamu.

Naam, sasa tujiulize udugu au kuunga udugu ambalo ndilo somo letu ndio kufanya nini?

 Tunalolikusudia katika udugu huu tuliotangulia kuueleza ni yale mafungamano ya nyoyo na maungano ya kiroho yanayotakiwa kuwepo baina ya waislamu.

Udugu huu unapomea, ukastawi, na ukakita mizizi yake hapo ndipo huanza kutoa matunda mazuri na matamu. Miongoni mwa matunda hayo ni :

1.      Ndugu humsaidia nduguye kwa mali yake, humpa ushauri nasaha, na huwa karibu naye kwa hali zote . Hii ni kwa sababu anatambua na kuamini kuwa

“ KWA HAKIKA WAISLAMU WOTE NI NDUGU……”(49:10)

Na pia hili linatokana na uekelezaji wake kivitendo kauli na agizo la Mola wake

” …………..NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA TAQWA WALA MSISAIDIANE KATIKA DHAMBI NA UADUI …………. (5:2)

2.      Ndugu hufurahi kwa furaha na neema ya nduguye kama ambayo huhuzunika kwa msiba, janga na taabu ya nduguye.

Hili linachimbuka kutoka na kauli ya Mjumbe wa mwenyezi Mungu – Rehema na amani zimshukie “ “ Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao ni mfano wa kiwiliwili, kitapoumwa kiungo kimoja (tu) katika huo ( mwili), mwili mzima hushirikiana nacho katika homa na kukesha.”

3.      Undugu huu, huondosha uadui, chuki, husuda na kila aina ya shari na ubaya baina ya ndugu na nduguye. Hivyo ndivyo tunavyojifunza na kuelewa kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu ndani ya Qur-ani tukufu:

“……NA KUMBUKENI NEEMA YA ALLAH ILIYO JUU YENU (zamani ) MLIKUWA MAADUI, NAYE AKAZIUNGANISHA NYOYO ZENU; HIVYO KWA NEEMA YAKE MKAWA NDUGU ………” (3:103)

4.      Udugu huu utampelekea ndugu kutomdharau nduguye na yeye kujiona ni bora zaidi kuliko nduguye. Haya ndiyo matunda ya mfinyango wa udugu huu yatokanayo na msingi sahihi ya Qur-ani Tukufu, tusome

“ENYI WATU ! KWA HAKIKA TUMEKUUMBENI (nyote) KWA (yule) MWANAMUME (mmoja; adamu) NA (yule yule) MWANAMKE (mmoja; Hanwa) NA TUMEKUFANYENI MATAIFA NA MAKABILA (mbalimbali) ILI MJUANE (tu basi; siyo mkejeliane). HAKIKA AHISHIMIWAYE SANA MIONGONI MWENU MBELE YA ALLAH NI YULE AMCHAYE ALLAH ZAIDI KATIKA NYINYI …” (49:13)

Naye Bwana Mtume – Rehema na amani zimshukie anatuonyesha natija ya udugu huu kwa kusema :

“ Muislamu nduguye ni mwislamu, hamdhulumu, hamdharau, hamtupi (akaacha kumnusuru) na wala hamkadhibishi.”

5.      Ndugu atokanaye na udugu huu ataijali na kuichunga mali ya nduguye, ataheshimu haki yake ya kuishi na hatamvunjia heshima nduguye.

Hii ni kwa sababu ndugu huyu anaiamini kauli ya Bwna Mtume – Rehema na amani zimshukie :

“ Kila muislamu kwa muislamu (mwezie) ni haramu (kuimwaga) damu yake ( kunyang’anya) mali yake na (kuvunja) heshima yake”. Huu ndio udugu tulioukusudia na hao ni baadhi tu ya matunda yake.

 

KUZOEANA NA WATU

Kimaumbile mwanadamu ni kiumbe mwenye tabia ya kuchanganyika kimaisha na wenziwe.

Maumbile ya mwanadamu hayakubaliani kabisa na upweke bali kuchanganyika mwanadamu na wanadamu wenziwe katika maisha ya kijamii ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu huyu ambayo hawezi kuyaepuka wala kuyabadilisha.

Mwanadamu hajitegemei kimaisha peke yake, bali ili aweze kuishi na kuyafurahia maisha hana budi kuchanganyika na watu wa rika, jinsia na tabia tofauti.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *