Bwana Mtume- Allah amshushie Rehema na Amani- mara baada ya kuzaliwa alinyonyeshwa na mama yake Bi Amina Bint Wahab kwa siku kadhaa.
Kisha akanyonyeshwa na Bibi Thuwaybatul Aslamiyyah ambaye alikuwa ni mjakazi wa wa Ammi yake Mtume Abuu Lahab.
Baada ya hapo ndipo waliamua kumtafutia mlezi na mnyonyeshaji kama ilivyokuwa ada na desturi ya Waarabu wakati huo.
Wakampata Bibi Haliymah Assaadiyyah, Bibi huyu alimchukua Bwana Mtume na kwenda kuishi naye katika kitongoji cha Baniy Saad kwa muda wa miaka miwili akimnyonyesha.
Akamuachisha ziwa baada ya miaka miwili, na hili liliashiria kuisha kwa mkataba na kulazimika kumrudisha mtoto kwa mama yake.
Kutokana na jinsi mama huyu mlezi alivyompenda mwanawe huyu wa kumlea kwa sababu ya baraka walizozipata tangu kuanza kumlea mtoto huyu alimsihi sana mama yake Mtume amruhusu aendelee kuishi na kumlea mtoto huyu mwenye baraka.
Kitongoji cha Baniy Saad kilikuwa ni ardhi iliyo na upungufu mkubwa wa mvua, lakini mara tu baada ya kufika Bwana Mtume katika kitongoji kile, hali ilibadilika kabisa, ukame ukatoweka, ardhi ikaotesha mimea, mazao yakakithiri, wanyama wakapata malisho mengi na hivyo kutoa maziwa ya kutosha.
Hali na afya za watu wa kitongoji kile zikaboreka kutokana na baraka za mtoto huyu yatima. Kwa kuyazingatia yote haya mama yake Mtume alimkubalia Bibi Haliymah aendelee kumlea Mtume kwa kipindi kingine cha miaka miwili.
Ada na desturi hii ya waarabu kuwapeleka watoto kulelewa mashambani ilijengeka juu ya sababu mbili kuu :
MOSI Mashambani ndiko kuna mazingira safi yaliyosheheni hewa safi yenye afya. Kutokana na hewa hii safi na chakula freshi watoto huwa na afya njema.
PILI Wakazi wa mashambani ndio waliokuwa wakizungumza lugha fasaha. Hivyo mtoto alipata fursa ya kujifunza na hatimaye kuzungumza lugha fasaha.
Bibi Haliymah alikuwa akiishi na mumewe Bwana Abuu Kabshah. Bibi huyu anasimulia ukuaji na tabia za mtoto huyu wa ajabu, anasema :
“Mtoto huyu alikuwa akikuwa haraka haraka kuliko kawaida ya watoto, alikuwa akizungumza maneno fasaha ilhali yungali mtoto bado, kila aliyemuona alimpenda na kuvutiwa naye. Alikuwa halii na kupiga makelele kama wafanyavyo watoto wengine ila akiachwa bila ya nguo. Akipatwa na mshtuko ghafla wakati wa usiku nilikuwa nikitoka naye nje ya nyumba, naye huziangalia nyota mbinguni kwa muda mrefu mpaka akalala”.
Haya ni machache tu miongoni mwa mengi aliyoyaeleza Bibi Haliymah juu ya mtoto huyu yatima.