NAMNA YA KUTAWADHA

Ikiwa unatawadha kwa kutumia chombo kama vile birika basi ni vema kama inawezekana liwe upande wako wa kulia na kama unatumia bomba basi fungua bomba lako na

KWANZA : anza kukosha vitanga vya mikono yako huku ukisema BISMILLAHIR-RAHMANIR-RAHIYM. Osha vitanga mara tatu.

PILI: Baada ya kuosha vitanga, tia maji mdomoni na kusukutua mara tatu.

TATU: Halafu unapandisha maji puani, kusafisha tundu za pua mara tatu.

NNE: Kisha ndipo uoshe uso wako ukianzia na maoteo/mameleo ya nywele za kichwa mpaka mwisho wa kidevu kwa urefu na toka ndewe moja ya sikio hadi nyingine kwa upana.

Kuosha uso huambatana na kutia nia moyoni kuwa sasa unatawadha na si vibaya kama ukitamka nia kwa ulimi kama vile mtu kusema NAWAYTU RA-AL HADATH au NAWAYTU FARDHAL-WUDHU au maneno yenye kufanana na hayo. Vile vile uso huoshwa mara tatu.

TANO: Baada ya kukosha uso, sasa ndipo uanze kuosha mikono ukianzia na mkono wa kulia.

Ukoshe mkono huo tangu juu ya kifupa panya mpaka vidoleni au kinyume chake na utafanya hivyo hivyo kwa mkono wa kushoto. Ikumbukwe kuwa mikono nayo huoshwa mara tatu.

SITA: Kisha tena ndipo upake maji sehemu ya kichwa mara tatu.

SABA: Kisha osha masikio yako, ndani na nje mara tatu.

NANE: Halafu ndio umailizie kutawadha kwa kuosha miguu yako, huku ukianzia na mguu wa kulia toka kifundoni mwa mguu mpaka nyayoni, na utafanya hivyo hivyo kwa mguu wa kushoto ambao nao utaosha mara tatu.

Kwa utaratibu huu udhu wako utakuwa umekamilika na hivyo kumaanisha kuwa sasa unayo rukhsa ya kusimama na kuzungumza na Mola wako ndani ya swala.

Utaratibu/mpango huu wa udhu unatokana na riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Imaam Ally -Allah amuwie Radhi – kwamba yeye alitawadha na (akaanza) kuosha vitanga vyake mpaka akavitakasa, kisha akasukutua mara tatu na akauosha uso wake mara tatu na (akaosha) mikono yake mara tatu na akapaka maji kichwa chake mara moja kisha (ndipo) akaosha miguu yake mpaka vifundoni, kisha akasema :

“Nilipendelea kukuonyesheni jinsi ilivyokuwa twahara (udhu) wa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie -“ At-Tirmidhi.

Hadithi inayofanana na hii tuliyoitaja hapa imetajwa pia na Imaam Bukhariy katika SAHIHI yake {kitabu cha hadithi} akiipokea kutoka kwa Sayyidna Uthmaan- Allah amuwie Radhi-. 

UDHU NA NAMNA YA KUTAWADHA

i) MAANA YA UDHU :

Tamko/Neno udhu linafasirika katika lugha ya kiarabu kama wema, uzuri na ung’avu.

Ama maana ya udhu katika istilahi ya wanazuoni wa fani ya Fiq-hi;

udhu ni twahara inayotumia maji, twahara hii inahusisha viungo maalum vya mwili, baadhi yake hukoshwa kama mikono, uso na miguu na vingine hupakwa maji kama vile kichwa.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published.