KUJITOA MHANGA

Kimaumbile mwanadamu ni kiumbe mwenye tabia ya ubinafsi, tabia ya kujifikiria yeye mwenyewe. Tabia ya kujipendelea na kutanguliza mbele maslahi yake. Haya ndiyo maumbile ya mwanadamu:

“…NA NAFSI ZIMEWEKEWA UBAKHILI MBELE (ya macho yake) …” [4:128]

Mwanadamu ni mchoyo apendaye kupokea bila kutoa, kufaidi bila kufidisha na husema mimi mimi na wala hasemi uma uma.

Ni maafa na janga kubwa uma/jamii kuwa na wananchi wenye mioyo/roho za ubinafsi, hawa hawana nafasi ya kuangalia maslahi ya uma.

Hawawezi kujitolea muhanga kwa ajili ya maendeleo ya uma, uma wenye watu wenye roho hii ya ubinafsi hauwezi kupiga hatua ya maendeleo.

Muumini wa kweli hawi mbinafsi bali huyatanguliza mbele maslahi ya uma kabla ya maslahi yake binafsi.

Hii inatokana na kule kuamini kwake kwamba kila alicho nacho ni neema aliyopewa na Mola wake na ni mtihani kwake. Imani hii ndiyo humfikisha kusema:

“…HAYA NI KWA FADHILA ZA MOLA WANGU, ILI ANIJARIBU NITASHUKURU AU NITAKUWA MWIZI WA FADHILA…” [27:40]

Muumini analikubali agizo na wito wa Mola wake katika kutoa kile alichomneemesha katika njia za kheri na kuyatanguliza mbele maslahi ya uma.

Anafanya yote haya huku akiwa na imani isiyo na shaka kwamba atakuta jazaa ya kutoa huku mbele ya Mola wake na ziada na kwamba Allah atampa badali ya anachokitoa:

“…NA CHO CHOTE MTAKACHOTOA, BASI YEYE ATAKILIPA, NAYE NI MBORA WA WANAORUZUKU…” [34:39]

Muumini wa kweli hana chembe ya shaka moyoni mwake kwamba baya lo lote litakalomsibu katika njia ya kujitoa muhanga kwa ajili ya maslahi ya uma, Allah atamjaza jazaa iliyo bora kabisa:

“NA KAMA MKIUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH AU MKIFA (si khasara kwenu) KWANI MSAMAHA NA REHEMA ZINAZOTOKA KWA ALLAH (kukujieni) NI BORA KULIKO VILE WANAVYOKUSANYA (hapa ulimwenguni)”. [3:157]

Imani ya kweli humtoa mja katika ubinafsi na kumjaza moyo wa kuupenda na kuutanguliza uma.

Answaar; wenyeji wa Madinah wamepiga mfano ambao historia ya wanadamu haijapatapo kuusajili katika kuwapendelea na kuwatanguliza mbele ndugu zao wa imani kuliko nafsi zao. Mapokezi mema yaliyosheheni mapenzi (upendo), moyo wa kutoa na ukarimu ulioonyeshwa na Answaar kwa ndugu zao Muhaajirina ni mfano hai unaotoa taswira ya maisha ya jamii ya kiislamu yanavyopaswa kuwa.

Answaar walifikia hatua ya kuwagombea wageni wao,kila mmoja akitaka mgeni afikie kwake mpaka kiasi cha kuamua kupiga kura na aliyeshinda ndiye aliyemchukua mgeni.

Hili lilitokana na idadi ya wenyeji kuwa kubwa kuliko idadi ya wageni wao na upeo wao katika kufahamu fadhila za udugu huu wa imani na kutoa kwa ajili ya Allah.

Huu ni upeo na daraja ya juu ya imani, huu ni ushindi wa Answaar dhidi ya ubinafsi na ubakhili ambao ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu.

Hivi ndivyo Allah anavyolisajili tukio hili la utu ndani ya Qur-ani Tukufu, tusome na tuzingatie:

“NA WALE WALIOFANYA MASKANI YAO HAPA (yaani Madinah) NA WAKAUTAKASA UISLAMU (wao bara bara) KABLA YA (kuja) HAO (Muhajiri huko Madinah) NA WAKAWAPENDA HAO WALIOHAMIA KWAO, WALA HAWAPATI, HAWAONI DHIKI NYOYONI MWAO KWA HAYO WALIYOPEWA (hao Muhajiri) NA WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI NDOGO. NA WAEPUSHWAO NA UBAKHILI WA NAFSI ZAO HAO NDIO WENYE KUFAULU KWELI KWELI”. [59:9]

Na aangalie mtu hali na imani ya jamii hii ya mwanzo ya kiislamu ailinganishe na jamii yetu ya leo, bila ya shaka ataona kuna tofauti kubwa kabisa.

Kwa nini basi iwepo tofauti na sio tofauti tu bali tofauti kubwa, kubwa sana. Ikiwa wale walikuwa ni waislamu na sisi leo ni waislamu, kwa nini tunashindwa kuwa kama wao?!

Ni dhahiri kuwa wenzetu wale imani iliwakolea na kujaa katika nyoyo zao na hivyo kusababisha watawaliwe na moyo wa kutoa, kuweka mbele maslahi ya uma na kujitoa muhanga.

Ama sisi leo, ninajasiri kusema kuwa bado nyoyo zetu hazijatawaliwa na imani ya kweli na hivyo kutoa mwanya wa ubinafsi, upendeleo na ubakhili kuzikalia kiurahisi kabisa nyoyo zetu.

Ndio ikawa leo hakuna muislamu anayemjali muislamu mwenziwe bali mwanadamu mwenziwe. Kila mmoja wetu ameyaweka mbele ya macho yake maslahi binafsi.

Hakika uislamu kama mfumo sahihi wa maisha umemsawirishia muislamu taswira maalumu ya maisha, iwe ni maisha binafsi au maisha jamii.

Uislamu unamlea muislamu kuwa na upendo, huruma na kuitendea wema jamii yake bali jamii nzima ya wanadamu.

Unawataka watu wa tabaka la juu kimaisha (matajiri) kuwasaida ndugu zao wa tabaka la chini (maskini), kuwaangalia kimalezi mayatima na kuwakomboa mateka wa kivita.

Huu ni moyo wa huruma ambao uislamu unaujenga ndani ya moyo wa muumini kiasi cha kumfanya ayatende yote hayo bila ya kutarajia jazaa, sifa wala shukrani kutoka kwa hao anaowasaidia. Bali anachotaraji kwa kufanya hivyo ni radhi ya Mola wake tu:

“NA HUWALISHA CHAKULA MAYATIMA NA MASKINI NA WAFUNGWA, NA HALI YA KUWA WENYEWE WANAKIPENDA (chakula hicho). (Husema wenyewe katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho): TUNAKULISHENI KWA AJILI YA KUTAKA RADHI YA ALLAH (tu) HATUTAKI KWENU MALIPO WALA SHUKRANI”. [76:8-9]

Hii ni huruma inayotokana na imani ya kweli ambayo ni miongoni mwa matunda ya malezi ya Uislamu.

Malezi ambayo yanamfanya mtu atoe kwa radhi yake mwenyewe katika kuisadia jamii yake bila ya kulazimishwa, kama zinavyofanya serikali mbali mbali kuwatenza nguvu wananchi kulipa kodi.

Kila ambaye amejisalimisha chini ya bendera ya Uislamu ana dhima shingoni mwake ya kujitoa muhanga kwa nafsi (roho) na mali yake kama anavyomtaka Mola wake.

Afanye tijara (biashara) isiyododa wala kumtia khasarani na Mola Muumba wake. Nafsi na mali yake ambavyo vyote hivyo ni hiba na milki ya Allah ndio bidhaa na mnunuzi wa bidhaa hiyo ni Mola wake.

Na thamani ya bidhaa zake hizo ni pepo ya Allah na njia ya kufika huko ni jihadi kwa maana zake zote. Mwisho wa njia hii ni nusra (ushindi) au kufa shahidi na jazaa ya kufa huko inatoka kwa yule ambaye yeye ndiye mbora wa kutoa jazaa:

“ALLAH AMENUNUA KWA WAUMINI NAFSI ZAO NA MALI ZAO (watoe nafsi zao na mali zao katika kupigania dini) ILI NA YEYE AWAPE PEPO. WANAPIGANA KATIKA NJIA YA ALLAH,WANAUWA NA WANAUWAWA. HII NDIO AHADI ALIYOJILAZIMISHA (Allah) KATIKA TAURATI NA INJILI NA QUR-ANI. NA NI NANI ATEKELEZAYE ZAIDI AHADI YAKE KULIKO ALLAH? BASI FURAHINI KWA BIASHARA YENU MLIYOFANYA NAYE (Allah) NA HUKO NDIKO KUFUZU KULIKO KUKUBWA”. [9:111]

Aya hii tukufu ilikuwa na taathira kubwa katika imani ya waislamu wale wa mwanzo. Waliuitikia vema wito huu wa kufanya biashara na Mola wao.

Muhammad Ibn Ka`ab Al-quradhwiy anasema: Alisema Abdullah Ibn Rawaahah-Allah amuwiye radhi-kumwambia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika ule usiku wa Aqabah: Shurutiza kwa ajili ya Mola wako na kwa ajili yako mwenyewe masharti uyatakayo. Mtume akasema: “Ninashurutiza kwa ajili ya Mola wangu

Mumuabudu yeye pekee na wala msimshirikishe na kitu cho chote.

Na ninashurutiza kwa ajili ya nafsi yangu

Mnihami kama mnavyozihami nafsi zenu na mali zenu”.

Abdullah akauliza: Sisi tukiyafanya yote hayo tutapata nini? Mtume akamjibu: “Pepo”. Wakasema (wote kwa pamoja): Ina faida biashara hii wala hatutaivunja.

Hisia hizi za kiimani zikamea na kustawi katika nyoyo za waumini hawa wa mwanzo.

Hisia zao katika kutoa, kuweka mbele maslahi ya uma na kujitoa muhanga kwa ajili ya dini ya Allah zikawa ni hisia za kweli.

Hisia zenye kusadikishwa na kauli na amali zao, kila mmoja wao akikimbilia kutoa na kukufanya kwa mashindano.

Ukarimu na utoaji huu ukazifutilia mbali fikra potofu za shetani mpotoshaji ya kwamba kutoa ni kujitia ufakirini:

“SHETANI ANAKUOGOPESHENI UFUKARA NA ANAKUAMRISHENI UBAKHILI NA ALLAH ANAKUAHIDINI MSAMAHA UTOKAO KWAKE NA IHSANI ( kubwa pindi mkitoa)…” [2:268]

Imepokelewa kutoka kwa Jariyr Ibn Abdillah-Allah awawiye radhi-amesema:

Tulikuwa mbele ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mapema mchana. Basi wakamjia watu wakiwa pekupeku, watupu (hawana nguo), wametoboa katikati maguo ya sufi na kuyavaa,wamebeba mapanga.

Karibu wote walikuwa wanatoka katika kabila la Mudhwar. Uso wa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ukabadilika kutokana na hali ya shida/haja ya watu wale aliyoiona.

Mtume akaingia ndani, akamuamrisha Bilali kuadhini,nae akaadhini na kukimu swala. Mtume akaswalisha, kisha akakhutubu baada ya swala, akasema:

“ENYI WATU! MCHENI MOLA WENU AMBAYE AMEKUUMBENI KATIKA NAFSI (asili) MOJA. NA AKAMUUMBA MKEWE KATIKA NAFSI ILE ILE. NA AKAENEZA WANAUME WENGI NA WANAWAKE KUTOKA KATIKA WAWILI HAO. NA MCHENI ALLAH AMBAYE KWAYE MNAOMBANA. NA (muwatazame) JAMAA, HAKIKA ALLAH NI MLINZI JUU YENU”. [4:1]

“ENYI MLIOAMINI! MCHENI ALLAH, NA KILA MTU AANGALIE ANAYOYATANGULIZA KWA AJILI YA KESHO (Akhera) NA MCHENI ALLAH; HAKIKA ALLAH ANAZO KHABARI ZA MNAYOYATENDA (yote)”. [59:18]

Baada ya Mtume kumaliza tu kuzisoma aya hizo, akaondoka mtu akataswadaki dinari au dirham yake. Mwingine akatoa nguo yake, pishi yake ya ngano,pishi yake ya tende, mpaka Mtume akasema: “…Walau nusu ya kokwa ya tende”.

Anasema Abdillah:(Mtume kwisha kusema hivyo) akaja mtu katika Maanswar na rundo la chakula, kisha wakafuatana watu katika kutoa mpaka nikaona marundo mawili makubwa ya chakula na nguo.

Mpaka nikauona uso wa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-uking`ara kama kwamba ni fedha iliyochovywa dhahabu, Mtume akasema:

“Atakayeanzisha katika Uislamu suna (mwenendo) njema, atapata ujira wake (suna hiyo) na ujira wa watakaoifuata suna hiyo baada yake bila ya kupungua cho chote katika ujira wao. Na atakayeanzisha katika Uislamu suna mbaya, atapata dhambi zake (suna hiyo) na dhambi za watakaoifuata suna hiyo baada yake bila ya kupungua cho chote katika dhambi zao”. Muslim

Maisha ya maswahaba wa Mtume-Allah awawiye radhi-mara nyingi yalitoa sura ya familia moja katika wakati wa dhiki na faraja.

Kila mmoja akikitoa anachokimiliki kwa ndugu zake wa imani. Wakigawana na kula chakula kama watu wa familia/kaya moja, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anaisawirisha familia hii kwa kauli yake:

“Hakika Waashiari wanapokwenda jaramba vitani au kinapopungua chakula cha familia zao Madinah. Hukikusanya pamoja chakula walichonacho katika nguo moja, kisha wakagawana baina yao kwa usawa. Mimi (Mtume) ni katika wao na wao ni katika mimi”. Bukhaariy & Muslim

Ukarimu wa mtu kuitoa nafsi yake huambatana na ukarimu wa kutoa mali, vitu viwili hivi ndivyo nguzo kuu ya kujitoa muhanga kwa mtu.

Vita vya kiislamu ni ushahidi wa wazi unaoonyesha msimamo thabiti na imani isiyotetereka ya maswahaba wa Mtume.

Ambao walipenda kufa katika kuitetea na kuipigania dini ya Allah kama watu wengine wanavyopenda kuishi.

Ni chini ya kivuli hiki cha kutoa, kuweka mbele maslahi ya uma na kujitoa muhanga katika kuipigania dini ya Allah hujengeka tabia tukufu.

Tabia ambazo huifanya jamii kusimama katika misingi ya utu, huruma, upendo na mshikamano. Misingi hii huiepusha jamii na migongano ya kijamii na mmomonyoko wa kimaadili na kuifanya amani na utulivu uitawale jamii hiyo.

 

KUJITOA MHANGA

Kimaumbile mwanadamu ni kiumbe mwenye tabia ya ubinafsi, tabia ya kujifikiria yeye mwenyewe. Tabia ya kujipendelea na kutanguliza mbele maslahi yake. Haya ndiyo maumbile ya mwanadamu:

“…NA NAFSI ZIMEWEKEWA UBAKHILI MBELE (ya macho yake) …” [4:128]

Mwanadamu ni mchoyo apendaye kupokea bila kutoa, kufaidi bila kufidisha na husema mimi mimi na wala hasemi uma uma.

Ni maafa na janga kubwa uma/jamii kuwa na wananchi wenye mioyo/roho za ubinafsi, hawa hawana nafasi ya kuangalia maslahi ya uma.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *