Suala la kuwapenda wazazi na kuwafanyia wema ni amri na agizo la MwenyeziMungu; na kwenda kinyume na agizo hilo ni uasi na dhambi :-
“NA MOLA WAKO AMEHUKUMU KUWA MSIMUABUDU YOYOTE ILA YEYE TU. NA (ameagiza) KUWAFANYIA WEMA (mkubwa) WAZAZI. KAMA MMOJA WAO AKIFIKIA UZEE, (naye yuko) PAMOJA NAWE, AU WOTE WAWILI, BASI USIWAAMBIE HATA AH! WALA USIWAKEMEE NA USEME NAO KWA MSEMO WA HESHIMA (kabisa) NA UWAINAMISHIE BAWA LA UNYENYEKEVU KWA (njia ya kuwaonea) HURUMA (kwa kuwa wamekuwa wazee) NA USEME : MOLA WANGU WAREHEMU (wazee wangu) KAMA WALIVYONILEA KATIKA UTOTO” [17:23-24]
Wazazi wako ndio sababu ya kuwepo kwako katika uso wa dunia hii baada ya IRAADA na QADARI ya Mola Mtukufu.
Wazazi wako wamepata taabu na shida nyingi sana katika kukulea tangu ulipokuwa mtoto mdogo usiyejijua wala kujiweza kwa lolote mpaka leo umekuwa baba au mama mzima unayeweza kusimamia mambo yako mwenyewe.
Mama yako amekubeba kwa shida kubwa tumboni mwake miezi tisa, kisha akakuzaa kwa uchungu mkubwa, halafu akakunyonyesha na kukulea kwa huruma na mapenzi makubwa yasiyo na kifani wala mfano na hii ndiyo maana ya maneno ya waswahili waliposema :
“NANI KAMA MAMA”.
Baba yako naye kwa upande wake alikuwa akihangaika mchana na kutwa kufanya kazi ili kuhakikisha kuwa unakula, unakunywa, unavaa, unalala mahala pazuri, unapata elimu na unatibiwa unapoumwa.
Kwa kuzingatia wema na ihsani hii isiyolipika tuliyotendewa na wazazi wetu ndipo MwenyeziMungu akatuwajibishia kuwapenda, kuwafanyia wema na kuwatii.
Bwana Mtume-Allah Amrehemu na amshushie amani- anatuambia :
“Mtoto mwema (kwa wazazi wake) haingii motoni, na mtoto asi (mwovu, asiyetii wazazi) haingii peponi”
Daima haki huambatana na wajibu, sasa kama hivi ndivyo basi kama mtoto alivyo na haki kwa wazazi wake ndivyo alivyo na wajibu pia.
Ni wajibu wa kila mtoto :
Kuwapenda na kuwaheshimu wazazi wake.
Kuwatii na kuwasikiliza katika wanayomuamrsiha na kumkataza muda wa kuwa si katika kumuasi Mola Mtukufu
Kutokuwaudhi kwa maneno au matendo. Asizungumze nao kwa dharau na maneno makali, asiwakemee wala kuwakaripia.
Watembeapo pamoja, asiwe mbele yao wao wakawa nyuma.
Kuwahudumia kwa chakula, mavazi, makazi na matibabu hasa wanapokuwa hawana uwezo.
Kuwatengea muda wa kukaa nao na kuwasikiliza matatizo yao.
Kuwaombea msamaha wa mwisho mwema kwa MwenyeziMungu.
Kuwaamrisha kutenda mema na kuwakataza kutenda maovu kwa kutumia lugha laini yenye heshima na adabu.
Wajibu wa kuwapenda na kuwatenda wema haukomi kwa kufa kwao bali unaendelea hata baada ya kuondoka kwao katika ulimwengu huu na kwenda za akhera.
Mtu mmoja alimjia Bwana Mtume – Allah amrehemu na kumshushia amani- akamuuliza
“Ewe Mtume wa MwenyeziMungu, Je, baada ya kufa wazazi wangu kuna wema ninaowajibika kuwatendea ? Mtume akamjibu : ” Ndio, waombee dua na maghufira (msamaha), tekeleza ahadi zao (walizotoa wakati wa uhai wao), uunge udugu wao na wakirimu/waheshimu marafiki zao” Abu Daawuud na Ibn Majah.
Ni muhimu mtoto akumbuke kwamba vyovyote vile atakavyowatendea wema wazazi wake hawezi kuwalipa kwa huruma, mapenzi, wema na ihsani waliyomtendea wao bali ni wajibu wake kujitahidi mwisho wa jitihada zake katika kuwatendea wema huku akitambua kuwa hilo ni agizo na amri ya Mola Mtukufu.
Hebu mtoto mwenzangu tuyatafakari pamoja maneno haya ya Bwana Mtume :
“Radhi za Allah zi katika radhi za wazazi na ghadhabu za Allah zi katika ghadhabu za wazazi”
Uchaguzi ni wako uwaridhishe wazazi wako kama ulivyoelekezwa na Mola Muumba wako upate radhi zake ambazo ndio tiketi yako ya kuingilia peponi na uwaghadhibishe kwa kuenda kinyume na amri na agizo la Mola uvune ghadhabu zake ambazo ndizo tiketi ya kuingilia motoni.
TANBIIH:
Kuwaasi na kuwatupa wazazi ni katika madhambi makubwa yenye kuangamiza.