GHUSHI – UDANGANYIFU

Ghushi ni nini ?

Ifahamu ghushi kupitia hadithi hii :

Imepokelewa kwamba Mtume -Rehema na Amani zimshukie-

“alilipitia rundo la chakula (sokoni), akaingiza mkono wake ndani yake (rundo hilo) vidole vyake vikapata ubichi ubichi. (Mtume) akauliza : Nini hiki ewe muuza chakula ? Akajibu : Kimepatwa na mvua, ewe Mtume wa Allah. (Mtume) akasema : Kwa nini basi usikiweke kilicholowa juu ili watu wakione ? Atakayetughushi si katika sisi” Muslim na Tirmidhiy.

Hii ndiyo ghushi tunayokusudia, kwa mujibu wa hadithi tunaweza kuieleza ghushi kuwa ni aina fulani ya udanganyifu unaofanywa katika biashara au katika jambo jingine.

Udanganyifu huu unalenga kuficha aibu/kasoro iliyomo ndani ya bidhaa au kuchanganya bidhaa safi na ile mbovu na kuiuza kwa thamani ya bidhaa safi.

 Ghushi pia inahusisha uchanganyaji wa makusudi nafaka kama mchele na mchanga kwa lengo la kuongeza uzito au uchanganyaji wa maziwa na maji ili kuongeza ujazo. Aina hii ya ghushi inabainishwa na hadithi ifuatayo :

Imepokelewa kwamba swahaba wa Mtume, Abuu Hurayrah – Allah amuwie radhi – alipita katika kitongoji kimoja, akamuona mtu mmoja amebeba maziwa akiyauza. (Abuu Hurayrah) akayachunguza na kugundua amechanganya na maji. Abuu Hurayrah akamwambia : Utakuwaje utakapoambiwa siku ya Kiyama yatoe maji katika maziwa (utaweza) ? Al-Baihaqiy.

Muislamu ni mtu mwenye kuishi kwa kufuata sheria za Allah, hambughudhi mtu wala yeye hayuko tayari kubughudiwa.
Kama huyu ndiye muislamu basi haimpitii akilini na haimuelei kabisa kuwa na tabia ya ghushi, akipita huku na huko akiwadanganya watu na kula mali zao kwa njia za dhulma. Hii ni tabia mbaya, Allah haipendi na anaikemea vikali kabisa :

 “WALA MSILIANE MALI ZENU KWA BATILI … [2:188]

Ukijikuta umepambika na mojawapo wa mambo yafuatayo, basi jihesabu tayari umeshaathiriwa na tabia mbaya ya ghushi. Tabia hii ya ghushi inakupelekea kukanwa na Mtume na kukutoa katika kundi lake :

“Atakayechukua silaha dhidi yetu, si katika sisi, na atakayetughushi, basi si miongoni mwetu” Muslim.

Sasa hebu jikague wewe mwenyewe kupita mambo yafuatayo, utapata jibu je, ni katika sisi au si miongoni mwetu ?

1. Je, una tabia ya uhodari wa kumpambia mtu kitu kibaya mpaka akakiona kuwa ni kizuri, au shari akaiona kuwa ni wema na akatumbukia humo ? Hii ni ghushi inayokufanya uwe mtu mbaya kiasi cha kutengwa na Bwana Mtume.

2. Je, una tabia na ustadi wa kuficha aibu/kasoro ya bidhaa unayoiuza kwa mteja hali ya kuwa unajua dhahiri kuwa lau angeliiona aibu hiyo, asingenunua bidhaa hiyo kabisa au angeinunua kwa kuwa ana haja lakini si kwa bei hiyo unayomuuzia sasa. Hii nayo ni ghushi, inakuondoshea baraka katika biashara na maisha yako kwa ujumla. Jiepushe nayo.

3. Je, una tabia na mbinu za kujidhihirisha mbele za watu kinyume na ulivyo, kiasi cha kwafanya watu wakuamini kuwa ndivyo ulivyo ? Hii pia ni aina fulani ya ghushi itakayokufanya uchukiwe na kutengwa na jamii pindi ukweli utakapobainika bayana na uongo kujitenga mtengano.

4. Je, una tabia na ufundi wa kumfurahisha mtu kiasi cha kumuaminisha kuwa wewe ni mtu mwema, halafu ukaitumia fursa hiyo uliyoitengeneza kumghuri kwa lengo la kufikia maslahi yako ? Hii kama sio ghushi ni nini basi ? Hebu achana na tabia mbaya hii kwani mwisho wake ni kuumbuka na kupoteza hadhi machoni kwa jamii.

5. Je, umeaminiwa na mtu kwa mkewe au wanawe na mali yake na akakueleza siri zake ? Halafu wewe ukamzunguka na kumfanyia khiyana kwa mkewe huyo ambaye ni shemeji yako, au wanawe hao ambao wewe daraja yako mbele yao ni baba ? Au ukamkhini katika mali yake na ukafichua siri zake ? Kama uko hivyo, fahamu kwamba hiyo ni sehemu ya tabia mbaya ya ghushi, je, wewe ukitendewa hivyo kwa mkeo, wanao, mali au siri zako, utafurahi ? Kama hufurahi, basi na mwenzio naye hafurahi kama ambavyo Allah na Mtume wake wasivyolifurahia hilo.

6. Je, una maarifa ya kutengeneza fedha bandia au madini bandia na kisha kuzitumia fedha hizo au kuwauzia madini hayo wenzio ? Huko ni kula mali ya watu kwa batili na ni ghushi.

 

Hii ni sehemu tu ya sura pana ya tabia na maradhi mabaya ya ghushi. Haya ni maradhi mabaya kabisa, kwa sababu yatakufanya :

i) Upoteze hadhi na heshima yako.

ii) Udharauliwe na kupuuzwa.

iii) Usiaminiwe hata kidogo na hivyo kukosa msaada wa jamii hata katika shida.

iv) Uchukiwe na uonekane kuwa ni mtu mbaya usiyefaa kuwa karibu na jamii.

v) Upoteze baraka katika shuguli zako kutokana na manung’uniko ya watu juu yako.

vi) Ujitoe mwenyewe kwa khiyari yako katika kundi la Mtume.

vii) Ustahiki kutendewa kama unavyotendewa wenzio.

viii) Utengwe na jamii na kusababisha kukosa ushirikiano wao wa karibu.

Ili ujikinge na maradhi haya mabaya na ujiepushe kufikwa na mambo tuliyotaja hapo juu, ni wajibu wako :

a) Kama ni mfanyabiashara, kubainisha aibu/kasoro ya bidhaa yako kwa mnunuzi/mteja wako ili awe na khiyari ya kununua pamoja na aibu hiyo au kuacha kununua.

Kama hukufanya hivyo, Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie – anakuambia : “Yeyote atakayeuza kitu hali ya kuwa kina aibu (kasoro) bila ya kuibainisha (kasoro hiyo kwa mteja), ataendelea kuwa katika chuki ya Allah na malaika wataendelea kumlaani (mpaka aache)” Ibn Maajah.

b) Kama mtu kando kumfahamisha mtu anayetaka kuuziwa kitu kibaya; chenye kasoro kuwa kitu hicho kina kasoro kadha wa kadha. Kwa kufanya hivyo utajiepushia dhima mbele ya Allah ya kumuona mtu anadhulumiwa na ukaacha kumsaidia kwa kuogopa watu. Tambua :

 “…. ALLAH NDIYE MWENYE HAKI ZAIDI YA KUOGOPWA ….” 33:38.

c) Utakapomuona mtu amekuja kuposa na ukawa unajua wazi si kwa chuki binafsi kwamba mtu huyo ana kasoro katika mwenendo, tabia na dini yake.

 Si majungu wala fitina kuwaendea wazazi wa binti na kuwaeleza kwa nia njema juu ya huyo mposaye binti yao.

Ili waamue ama kumuoza pamoja na uchafu wake wa tabia kwa tamaa ya anachomiliki au waache kumuoza kwa ajili ya kuheshimu muongozo wa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – Atakapokujieni (kuposa) mnayemridhia dini na tabia zake, basi muozeni …”

d) Utakapomuona mtu anataka kushirikiana na mtu katika biashara au jambo lolote lile na ukajua  kwamba huyo anayetaka kushirikiana naye si mtu muaminifu.

Ni vema ukamueleza kwa njia ya hekima na ushauri kwani kama hukufanya hivyo nawe utahesabika kuwa ni mshirika katika madhara yote yatakayomkumba kutokana na ushirika huo wa mtu mbaya.

Kumbuka Mwenyezi Mungu anatuagiza :

“… NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA TAQ-WA, WALA MSISAIDIANE KATIKA DHAMBI NA UADUI NA MCHENI ALLAH, HAKIKA ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU” [5:2]

GHUSHI – UDANGANYIFU

Ghushi ni nini ?

Ifahamu ghushi kupitia hadithi hii :

Imepokelewa kwamba Mtume -Rehema na Amani zimshukie-

“alilipitia rundo la chakula (sokoni), akaingiza mkono wake ndani yake (rundo hilo) vidole vyake vikapata ubichi ubichi. (Mtume) akauliza : Nini hiki ewe muuza chakula ? Akajibu : Kimepatwa na mvua, ewe Mtume wa Allah. (Mtume) akasema : Kwa nini basi usikiweke kilicholowa juu ili watu wakione ? Atakayetughushi si katika sisi” Muslim na Tirmidhiy.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *