Kisheria ndoa ni mkataba wa khiari wa kuishi na kushirikiana pamoja katika matamu na machungu ya maisha baina ya mwanamume na mwanamke.
Kutimia kwa mkataba huu kwa mujibu wa sheria humgeuza mwanamume huyo kuwa mume na mwanamke aliyefunga mkataba huu kuwa mke.
Mkataba huu una athari na mabadiliko makubwa sana katika maisha ya kila mmoja wa wanandoa (mke na mume) hawa.
Mkataba huu huwaingiza wanandoa hawa katika kipindi kipya cha maisha ya ushirika baina yao; ushirika wa mwili, hisia, mawazo, machungu, matamu, na…na…..
Ushirika huu humpa kila mmoja wao haki iambatanayo na wajibu kwa mwenza wake huyo aliyemchagua katika maisha.
Atekeleze wajibu wake kwa mwenziwe ndipo astahiki kudai kutekelezewa haki yake na mwandani wake huyo.
Ushirika huu huwakumbusha wanandoa hawa kuwa (HAKUNA HAKI ISIYOKUWA NA WAJIBU). Kwa ujumla ndoa ni kiungo kinachowaunganisha pamoja mwanamume na mwanamke kuwafanya mke na mume.
Na kinampa kila mmoja wao haki sambamba na kumbebesha wajibu kwa mwenziwe, kinampa haki za kimwili, haki za kijamii na haki za kimali.
Kwa mantiki hii ni wajibu wa kila mwanandoa kuishi na mwenziwe huyu katika hali na mazingira ya wema na ampe haki zake zote anazostahiki bila ya kuchelewa au kuhisi/kuona vibaya. Hebu tuzitafakarini pamoja kauli hizi za Allah Mola aliyetuwekea utaratibu huu wa ndoa, utaratibu ambao haupatikani kwa baki ya hayawani wengine:
“…NA KAENI NAO KWA WEMA…” [4:19]
Tuzidi kutafakari:
“…NAO (wanawake) WANAYO HAKI KWA SHARIA (kufanyiwa na waume zao) KAMA ILE HAKI ILIYO JUU YAO KUWAFANYIA WAUME ZAO. NA WANAUME WANA DARAJA ZAIDI KULIKO WAO…” [2:228]
Aya inambebesha kila mwanandoa jukumu/wajibu kwa mwenziwe na wakati huo huo inampa haki ambazo kwa mwenziwe huyo zinakuwa ni wajibu.
Haki za mume ndio wajibu wa mke na kinyume chake pia, yaani haki za mke ndio wajibu wa mume.
Kila mmoja kati ya wanandoa hawa atakapoutambua wajibu wake ambao kwa janibu (upande) ya mshirika wake ni haki, baada ya kuutambua akamtekelezea bila ya kinyongo.
Bila ya shaka wawili hawa watakuwa wamejenga msingi imara wa maisha yao haya ya ndoa. Watakuwa wamejihakikishia mafaniko, ufanisi, masikilizano na furaha ya kweli katika safari hii ngumu ya maisha ya ndoa.
Ndoa iliyojengwa juu ya msingi huu wa kutambua kuwa wajibu wako ni haki ya mwenzio ina nafasi kubwa ya kudumu.
Kinyume chake, ndoa ambayo haikujengwa juu ya msingi huu mama, husheheni magomvi, mizozo na haichukui muda ila huvunjika. Na wanandoa kusambaratika na pengine kujenga chuki ya daima baina yao ambayo huzaa visasi.
Zimepokelewa “nassi”-nukuu nyingi za hadithi zinazomuusia mume kwa mkewe na kumtaka aichunge hali yake.
Na kumbainishia kuwa asitarajie ukamilifu wa moja kwa moja kwa mkewe, jambo hilo ni muhali usio ishi sambamba na mwanadamu.
Akasema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Usianeni kuwatendea wema wanawake, kwani mwanamke ameumbwa kutokana na ubavu (wa Nabii Adam-rejea Qur-ani 4:1). Na hakika eshemu iliyo kombo zaidi ya ubavu ni ile sehemu ya juu yake, ukitaka kuunyoosha utauvunja. Na ukiuacha hivyo hivyo ulivyo utaendelea kuwa kombo (kupinda), basi usianeni wema kwa wanawake”.
Bukhaariy & Muslim
Na katika riwaya nyingine Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema:
“Hakika mwanamke ameumbwa kutokana na ubavu na (ubavu) hautakunyookea kwa namna yo yote ile. Basi ukistarehe naye, utakuwa umestarehe naye na ilhali ndani yake kuna kombokombo (kupindapinda). Na ukiendelea kuunyoosha utauvunja na kuuvunja kwake ni kumtaliki”.
Muslim
Na akazidi kusema Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“ Muumini mwanamume asimbughudhi muumini mwanamke. (Mwanamume muumini) akiichukia kwake (mwanamke muumini) tabia moja, atairidhia kwake (mwanamke huyo) tabia nyingine”.
Muslim
Katika hadithi hizi za Bwana Mtume, kuna muongozo wa maisha ya ndoa kwa umati wake.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anambainishia mwanamume uhalisia wa maumbile ya mwanamke ambaye ni sehemu yake na mwenza wake katika maisha haya ya mpito na yale yajayo ya milele. Kuyajua maumbile haya ni jambo la muhimu sana kwa mwanamume.
Hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba ni rahisi mno kuishi na unayemuelewa kuliko kuishi na usiyemuelewa.
Ujuzi huu wa maumbile na hali ya mwenziwe utamsaidia mwanamume huyu kujua jinsi ya kuishi na mwenza wake huyo na kustahamiliana naye kimaisha.
Hii ndio sehemu ya falsafa ya kauli ya Bwana Mtume katika kulielezea umbile aliloumbiwa mwanamke juu yake.
Kadhalika katika hadithi hizi mwanamume anatakiwa kuwa na mizani ya kupima baina ya mema (mazuri) na maovu (mabaya) ya mwanamke.
Iwapo ataona ana tabia fulani ambayo si nzuri, basi ailinganishe tabia hii na ile nzuri impendezayo. Wala asitazame tabia hiyo mbaya kwa mtazamo wa chuki tu pekee, yaani mtazamo wa upande mmoja tu.
Wengi mingoni mwa wanamume hutazamia hali ya ukamilifu tu wake zao. Hizi ni fikra lemavu na potofu, kwani hilo ni jambo muhali lisilomkinika.
Hawa wanawake ni binadamu wenye mapungufu kwa maana ya neno lenyewe na sio malaika watakatifu. Vipi basi uwatazamie kuwa na ukamilifu usio na upungufu! Kwa nini utafute ukamilifu ambao hata wewe mwenyewe hauna?
Je, wewe mwanamume ni mkamilifu kwa hali zote hata umtazamie mwenzio huyu kuwa na ukamilifu usio na mapungufu?
Kumbuka ukamilifu ni wa Allah pekee na asiyekuwa yeye ni nyumba ya mapungufu na kunguwao (makosa ya bahati mbaya).
Fikra na mawazo haya lemavu ndio huwapelekea wanamume walio wengi kushindwa kuishi na wake na hatimaye kufikia uamuzi wa kutoa talaka kwa sababu ya kutafuta lisilokuwepo (muhali).
Inatakikana kwa wanandoa kila mmoja atambue kwamba maisha ya ndoa ni safari ndefu iliyosheheni matamu na machungu.
Ili kufika salama mwisho wa safari hii, inawabidi kustahamiliana, kuchukuliana na kuwa wepesi kusameheana wanapokoseana.
Ni kwa kufuata njia hii tu ndio wanaweza kufanikiwa kufika salama mwisho wa safari yao hiyo iliyo mithili ya bahari iliyochafuka.
Baada ya utangulizi huu juu ya ndoa, hebu sasa kwa msaada wa Allah tuanze kuzichambua haki za kila mmoja; mume na mke.
Haki ambazo kwa janibu moja zinakuwa ni haki na wakati huo huo kuwa ni wajibu kwa janibu ya pili ya ushirika huu wa ndoa.
Haki mama na ya msingi ambayo ni haki shiriki baina ya mume na mke ni UKWELI na UAMINIFU katika ndoa.
Mume ni wajibu wake kuwa mkweli na muaminifu kwa mkewe kwa maana ya maneno hayo. Naye mke atambue kuwa na yeye ana wajibu mkubwa wa kuukabili ukweli na uaminifu huo wa mumewe kwa ukweli na uaminifu wa mfano wake.
Asiwe na mwenza/mwandani mwingine zaidi ya mumewe kama ambavyo mume asimshirikishe mwanamke mwingine katika penzi la mkewe.