Bi Khadijah binti Khuwaylid, Bibi mkureshi alikuwa ni mwanamke mwenye tabia njema, anayekubalika na kuheshimika katika jamii ya watu wa Makkah.
Mbali na sifa hizi, Bibi huyu alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa wa mji wa Makkah, alipenda sana kufanya biashara.
Kutokana na kuona mbali na upevu wa akili yake alikuwa akiizalisha mali yake kwa kuwaajiri watu. Aliwapa mali wakaiuze kwa mkataba na kuwapa sehemu ya faida iliyopatikana.
Habari za tabia murua, uaminifu na ukweli wa Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie – zilipoyagonga masikio ya Bi Khadija; akajawa na raghba ya kutaka kumuhusisha mtu huyu mwaminifu na mkweli katika biashara yake.
Akamtumia salamu za kumuita naye Bwana Mtume akaitikia mwito. Bi Khadijah akamueleza alilomuitia ya kwamba amfanyie biashara naye atampa sehemu kubwa ya faida itakayopatikana.
Bwana Mtume akakubali na mara moja akaianza kazi yake hii mpya ya biashara badala ya ya ile kazi yake ya kwanza ya uchungaji.
Ikumbukwe wakati huo Mtume alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano. Akatoka kuelekea Shamu katika msafara wa biashara akiambatana na Bwana Maysarah, msaidizi aliyepewa na Bi Khadijah.
Wakafika Shamu, wakafanya biashara wa kuuza na kununua, wakapata faida kubwa sana kuliko iliyokuwa ikipatikana huko nyuma.
Bwana Maysarah alishuhudia katika safari yake na Bwana Mtume tabia njema, ukweli na uaminifu wa Mtume na hivi ndivyo vilivyokuwa vigezo vya ufanisi katika biashara yao.
Kadhalika aliona miujiza mingi iliyoonyesha kwamba Muhammad ndiye Mtume mtarajiwa aliyebashiriwa katika vitabu vitakatifu.
Miongoni mwa miujiza hiyo ni pale Bwana Mtume alipopumzika chini ya mti uliokuwa karibu na kibanda cha Padri Nestori.
Padri huyu baada ya kumuona Mtume amepumzika chini ya mti ule akamuendea Maysarah na kumuuliza khabari za Mtume.
Bwana Maysara akamueleza Padri Nestori kila alilolijua juu ya Mtume kwa kulisikia ama kulishuhudia yeye mwenyewe.
Hapo ndipo Padri Nestori akamwambia Bwana Maysara :
“Hajapumzika chini ya mti huu ila ni Mtume (Kwani huu ni mti wa mitume) basi (nakuusia) uhiifadhi siri hii (ili mayahudi wasimdhuru)”. Pia Maysarah alikuona wakati wa jua kali la utosi kiwingu kikimfunika Bwana Mtume kumkinga na jua.