BINADAMU NA KAZI

Kazi ni sehemu isiyotengeka ya maisha ya mwanadamu. Allah Mtukufu ameifanya kazi kuwa ndio wasila wa mwanadamu katika kupata maisha (riziki) yake ulimwenguni hapa. Tusome huku tukitafakari.

“YEYE NDIYE ALIYEFANYA ARDHI IWE INAWEZA KUTUMIKA (Kwa kila myatakayo) KWA AJILI YENU. BASI NENDENI KATIKA PANDE ZAKE ZOTE NA KULENI  KATIKA RIZIKI YAKE, NA KWAKE YEYE NDIO MAREJEO (yenu nyote)” (67: 65)

Kwenda katika pande (sehemu/nchi) za ardhi hili ni suala la kushughulika na kuhangaika kwa ajili ya kutafuta maisha.

Mitume wa Allah-Rehema na Amani ya Allah iwashukie – ambao ndio Waalimu wateule wa Allah kwa waja wake, pia nao walishiriki katika kufanya kazi.

Hawa Allah asingeshindwa kuwaruzuku bila ya kufanya kazi. Lakini aliwataka wafanye kazi ili wawe ni mfano mwema wa kuigwa na sisi wafuasi wao.

Pia ili kuonyesha kwamba kila mmoja. Hana budi kula kupitia jasho lake.

Huyu hjapa Nabii Daudi mfanyakazi:

”….NA TUKAMLAINISHA CHUMA. (Tukamwambia). TENGENEZA (nguo za chuma) PANA NA UPIME VIZURI KATIKA KIUNGANISHA, NA FANYENI VITENDO VIZURI…….” (34:10-12)

Aya inatubainishia kwamba Nabiii Daudi – Amani ya Allah imshukie – alikuwa ni fundi muhunzi akitengeneza na kuuza mavazi ya chuma ambayo yalikuwa yakitumika vitani.

Tena Allah, anamuagiza aifanya kazi yake hiyo kwa ufanisi mkubwa. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie analisisitiza suala hili la ufanisi kazini katika kauli yake:

Hakika Allah anapenda mmoja wenu afanyapo kazi, basi aifanya kwa ukamilifu/uzuri (ufanisi) Al-baihaqiy). Ione nafasi ya kazi katika uislamu kupitia aya hii, tusome na tutafakari pamoja.

“NA ITAKAPOKWISHA SWALA (kuswaliwa) TAWANYIKENI KATIKA ARDHI MTAFUTE FADHILA ZA ALLAH……….” (62:10).

Nae Bwana Mtume Rehema na Amani zimminikie – anasema katika hadithi – Qudsi:

“ Hakika Allah anasema: Ewe mja wangu wee! Utikise mkono wako nikuteremshie riziki”

Tutafahamikiwa kutokana na rukuu hizi za aya na hadithi kwamba ni wajibu tufanye kazi ili iwe ni sababu ya kupatia riziki na baki ya mahitaji yetu mengine katika maisha haya.

Ni lazima tujishughulishe na kuhangaika kufanya kila shughuli halali tuiwezayo ili tuweze kujipatia riziki zetu huku tukiamini kuwa bado tumo ndani ya ibada tuliyoumbwa kwa ajili yake.

 Tufahamu na tuelewe kwamba Allah Mtukufu hakutuumba na kutuleta hapa duniani bure bure tu

“JE MLIDHANI YA KWAMBA TUMEKUUMBENI BURE NA YA KWAMBA NYINYI KWETU HAMTARUDISHWA?” (23: 115).

Hapana tena hapana Allah hakutuumba bure, bali ametuumba kwa hekima na busara nyingi. Ametuumba tufanye kazi tupate riziki zetu, tumuabudu bila ya kumshirikisha na chochote, tumtukuze na tumshukuru kwa neema zake zisizodhibitika na akili zetu.

“KULENI KATIKA VILE ALIVYOKUPENI ALLAH, VILIVYO HALALI NA VIZURI. NA SHUKURUNI NEEMA ZA ALLAH, IKIWA KWELI MNAMUABUDU YEYE.” (16: 114).

Tufanye kazi ili iwe ndio sababu ya mafanikio yetu hapa duniani tulipo hivi sasa na huko akhera tuelekeako. Tufanye kazi huku tukiamini kuwa hiyo ni amri ya Mola wetu na ndio utaratibu aliotupangia katika kupata riziki zetu: ……..

”BASI NENDENI KATIKA PANDE ZAKE ZOTE NA KULENI KATIKA RIZIKI ZAKE……” (67:15).

Katika aya hii Allah Mtukufu anatuagiza na kutuamrisha waja wake tuziendee pande za ardhi, tujishughulishe/tufanye kazi.

Tusome elimu mbalimbali zitakazotuwezesha kuitumia kwa manufaa yetu rasimali aliyoijaza tele angani, ardhini,  na majini.

Kutokana na rasimali hizo tufanye uhunzi, biashara, kilimo, ufugaji na ……na……ili tuweze kupata raha na mafanikio katika maisha haya ya majaribio na iwe pia ndio sababu ya fanaka katika maisha hayo ya milele yajayo.

Pia tutakuwa tumelitekeleza agizo na amri ya Mola wetu ya kufanya kazi na hivyo kujihakikishia fursa ya kupata radhi zake ambazo hazitamaanisha kingine zaidi ya raha na amani ya milele duniani, kaburini na kule peponi.

Ni muhimu tukaelewa na kufahamu kwamba Allah Mtukufu kwa hekima zake zilizotukuka ameviumba vitu vyote na kuviwekea faida yake.

Tukiangalia mathalani faida ya mimea ni nafaka na makapi yake, nafaka tunazitumia kama chakula chetu na wanyama na makapi/pumba kama chakula cha wanyama tu.

 “NA ALAMA (ya kuonyesha moja ya rehema za Allah) JUU YAO NI ARDHI ILIYOKUFA. TUNAIFUFUA NA TUKATOA NDANI YAKE NAFAKA. WAKAWA WANAZILA” (36; 33).

Faida ya miti ni yale matunda, vivuli na mazao yake mengine kama vile mbao ambazo tunazitumia  katika manufaa/maslahi yetu mbalimbali.

“NA TUKAFANYA NDANI YAKE MABUSTANI YA MITENDE NA MIZABIBU NA KUPITISHA CHEM CHEM NDANI YAKE. ILI WALE KATIKA MATUNDA  YAKE, NA HAIKUYAFANYA (matunda) HAYO MIKONO YAO, JE, HAWASHUKURU”.(36: 34-35).

Faida ya wanyama ni pamoja na maziwa, suti, manyoa, nyama, mifupa yake na mazao yake mengine kama vile ngozi na pembe zake. Pia tunawatumia wanyama  kama chombo cha usafiri wetu na mizigo yetu, kadhalika tunawatumia katika shughuli zetu za kilimo.

“ NA (pia) AMEWAUMBA WANYAMA. KATIKA HAO MNAPATA (vifaa vitiavyo) JOTO NA MANUFAA (mengine) NA WENGINE MNAWALA NA MNAONA RAHA MNAPOWARUDISHA JIONI NA MNAPOWAPELEKA MALISHONI ASUBUHI. NA (wanyama hao pia) HUBEBA MIZIGO YENU KUPELEKA KATIKA MIJI MSIYOWEZA KUIFIKA ISIPOKUWA KWA MASHAKA NA TAABU. HAKIKA MOLA WENU NI MPOLE SANA (na) MWENYE REHEMA NYINGI. NA (amewaumba) FARASI NA NYUMBU NA PUNDA ILI MUWAPANDE NA (wawe) MAPAMBO……” (16: 5-8)

Ndugu yangu muislamu hatuwezi kutaja faida ya neema za Allah zilizo juu yetu tukasesha bali hata hizo neema zenyewe

“……….NA KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA KUZIHISABU………” (14: 34)

Na faida ya mwanadamu ni kujishughulisha na kufanya kazi ili aweze kuzitumia neema hizi alizopewa bure na Mola wake kwa ajili ya ustawi wake katika ardhi hii na akhera.

Kisha amuabudu na  kumshukuru  Mola wake juu ya neema zake hizo ili ampe ziada ya neema.

(NA (kumbukeni) ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa) “ KAMA MKISHUKURU, NITAKUZIDISHIENI NA KAMA MKIKUFURU (jueni) KUWA ADHABU YANGU NI KALI SANA” (14:7)

Ewe ndugu muislamu, Allah Mtukufu ametuelekeza na kutuongoza tufanye kazi na tusifanye uvivu pale alipomuamrisha mdudu mdogo nyuki kufanya kazi na  kujijenga nyumba majabalini na mitini.

Ale katika anuwai za matunda ili aweze kuutekeleza wajibu alioumbiwa ambao ni kutengeneza asali, chakula na dawa kwa binadamu. Tusome na tuchukue mfano mzuri wa mdudu nyuki katika kufanya kazi.

(NA MOLA WAKO AKAMFAHAMISHA NYUKI YA KWAMA “ JITENGENEZEE MAJUMBA (yako) KATIKA MILIMA NA KATIKA MITI NA KATIKA YAKE (majumba) WANAYOJENGA (watu)” KISHA  “KULA KATIKA KILA MATUNDA, NA UPITE KATIKA NJIA ZA MOLA WAKO ZILIZOFANYWA NYEPESI  (kuzipita).” KINATOKA KATIKA MATUMBO YAKO KINYWAJI (asali) CHENYE RANGI MBALIMBALI, NDANI YAKE KINA PONYO (pozo) KWA WANADAMU. HAKIKA KATIKA HAYO MUNA MAZINGATIO KWA WATU WENYE FIKRA”. (16: 68-69).

Ni vema ukafahamu na kuelewa kwamba kazi ndio kipimo cha utu.

Fakhri na utukufu wa mtu hujidhihirisha kupitia kazi, huoni kuwa ombaomba ni mtu duni asiye na  thamani machoni mwa jamii?

Huoni kuwa wale waliochukua taabu katika kusoma na kufanya kazi ndio watu maarufu na wenye maisha  mazuri katika jamii” Hawa wana nafasi kubwa zaidi ya kuirithi pepo ya Allah kupitia neema zake alizowapa kutokana na juhudi yao katika kufanya kazi. 

“ NA UTAFUTE KWA YALE ALIYOKUPA ALLAH- MAKAZI MAZURI YA AKHERA. WALA USISAHAU SEHEMU YAKO YA DUNIA NA UFANYE WEMA KAMA ALLAH ALIVYOKUFANYIA…….”  (28:77).

Hao matajiri, wavumbuzi, wataalamu na mabingwa.

Katika fani mbalimbali tuwaonao leo, hawakuzifikia daraja/nafasi hizo kwa kubahatika tu. La  hasha!.

Bali imewagharimu taabu, muda na juhudi kubwa za makusudi mpaka kufika hapo walipo leo na kuanza kufaidi matunda ya  taabu na juhudi zao za jana.

Mafanikio na fanaka yako wewe leo hapa  duniani na kesho kule akhera yatategemea kwa kiasi kikubwa.

i)                   Juhudi na bidii yako  katika kufanya kazi.

ii)                 Kufanya kazi kwa ufanisi.

iii)               Kuifanya kila kazi ikupasayo katika wakati wake muafaka bila ya kuichelewesha .

KUMBUKA

Kufanya kazi ni agizo na amri ya Allah.

Kufanya kazi na kula kutokana na kazi hiyo ni ibada kama ibada nyingine.

Kuacha kufanya kazi bila ya udhuru ni dhambi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *