USALITI NA UVUNJAJI WA AHADI WA BANIY QURAYDHWAH NDIO UPENYO WALIOPITIA WAISLAMU (NDIO SABABU YA VITA VYA AHZAAB)

Hapana shaka kwamba msaada wa ki-Mungu ndio uliowaokoa waislamu katika vita hivi vya Ahzaab na kwamba lau si kuja kwa msaada huu, kumalizwa kwa waislamu lingekuwa ni jambo lisilozuilika.

Na da’awah ya Kiislamu ingelifikia ukomo bila ya shaka na hili ndilo alilokuwa akilichelea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akawa anamuomba Mola wake pale aliposema:

“Ewe Mola wa haki wee! Ukitaka hutoabudiwa”.Naam, lau Allah angetaka waislamu washindwe katika vita hivi, Uislamu ungekuwa ni kitu kisichotajikana tena.

Na kingeliangamia kikundi hiki kidogo kilichokuwa kinampwekesha Allah kwa kumuabudu yeye peke yake bila ya kumshirikisha na ye yote/cho chote sambamba na kuisimamisha dini yake katika ardhi.

Na ni jambo lisilokubali mabishano kwamba usaliti na uvunjaji ahadi wa Baniy Quraydhwah ndio upenyo waliopitia waislamu.

Yaani ndio sababu pekee iliyowahalalishia waislamu kuingia vitani na Mayahudi hawa wa Kibaniy-Quraydhwah.

Lau si usaliti wao huu, mushrikina wasingeliweza kupata njia ya kuwafikia waislamu, kwani walisimama mbele ya handaki kwa muda mrefu.

Wakalizunguka mara nyingi na wakajaribu mara kadhaa kupata upenyo watakaopenyea kuwafikia waislamu. Lakini wapi, waislamu walikuwa macho na makini katika ulinzi kiasi cha kuweza kuziba mianya yote na kuzima majaribio yote ya kupenyea upande wao.

 Lilikuwa ni jambo jaizi kwa mushrikina hawa kukimwa na hali hii na kuchoshwa kusimama mbele ya handaki.

 Na kukata tamaa ya kuifikia kambi ya waislamu baada ya kushindwa kwa majaribio yao kadhaa. Uchovu huu na kukimwa huku ilikuwa ni sababu tosha ya kuwarejesha makwao bila ya kuyafikia matakwa yao dhidi ya waislamu kama ilivyokuwa shabaha yao.

Lakini kujiingiza kwa Baniy Quraydhwah upande wa majeshi shirika (Ahzaab) na uvunjaji wao wa ahadi walioahidiana na waislamu.

 Hapana shaka ndio sababu iliyowarejeshea mushrikina matumaini mapya baada ya kukata tamaa, kuamsha mori, kuzidisha ari yao na mbinyo upande wa kambi ya waislamu kiasi cha kuwaendesha mbio.

Hii ndio ikawa sababu kuu ya mtetemesho na khofu iliyowasibu waislamu na kizaizai kilichotokea katika safu zao.

Na ndio iliyowafanya wanafiki na wenye maradhi mioyoni mwao kuitumia fursa hiyo kuwakatisha tamaa waumini, wakisema kama walivyonukuliwa na Allah:

“…ENYI WENYEJI WA YATHRIBU (Madinah)! HAMNA MAHALI PA KUKAA NYINYI, BASI RUDINI (makwenu msiingie katika jeshi pamoja na Muhammad). NA KUNDI JINGINE MIONGONI MWAO LIKAOMBA RUHUSA KWA MTUME KWA KUSEMA: HAKIKA NYUMBA ZETU NI TUPU (hapana watu, tunakwenda zetu), LAKINI HAZIKUWA TUPU, HAWAKUTAKA ILA KUKIMBIA TU”. [33:13]

Hakika wasifu uliotolewa na Qur-ani Tukufu katika kuielezea hali ya waumini katika mazingira haya magumu, unasawirisha kwa uwazi kabisa nguvu ya hujuma malizi iliyoelekezwa na mushrikina upande wa waumini.

Pale walipowajia kuwashambulia kutokea juu na chini yao na inaonyesha wazi kiwango cha khofu iliyowapata waislamu hata macho yakakodoka na nyoyo zikapanda kooni na wakamdhania Allah dhana mbalimbali:

“HAPO WAUMINI WALITIWA MTIHANI (kweli kweli) NA WAKATETEMESHWA KWA MATETEMESHO MAKALI”. [33:11]

 

Ulikuwa ni usaliti na khiana pamoja:

Usaliti huu uliokurubia kuifagilia mbali dola ya Kiislamu, haukuwa na sababu yo yote zaidi ya chuki na mfundo vilivyo kuwemo nafsini mwa Mayahudi dhidi ya Waislamu.

Waislamu waliendelea kuwa wakweli na watekelezaji wa ahadi yao waliofunga na Baniy Quraydhwah. Utekelezaji na ukweli huu kwa ahadi yao ukawa ndio hoja kuu aliyoitumia Ka’ab Ibn Asad kwa Huyay Ibn Akhtwab pale alipokuwa akijaribu kumshawishi kuvunja ahadi na Mtume, alipomwambia:

“Ole wako ewe Huyay, achana na mimi kwani sitafanya unaloniitia, hakika mimi sijaona kwa Muhammad ila utekelezaji na ukweli”.

Lau ingelikuwepo upande wa waislamu sababu yo yote iliyowapelekea Baniy Quraydhwah kuwafanyia usaliti huu, ingeliwastahikia kufanya hivyo.

F    Fakaifa na huu ni usaliti unaoulipa ukweli na utekelezaji?

F    Fakaifa na huu ni usaliti uliokusudia kuufyekelea mbali na kuitokomeza kabisa dola ya Kiislamu?

F    Fakaifa usaliti huu ulikusudia kuingamiza dini ya haki ambayo kwayo Allah amemtumiliza Mtume wake wa mwisho ili kuzishinda dini zote?

F    Fakaifa na ahadi iliyokuwa baina yao na Mtume wa Allah iliwataka kuwalinda waislamu na sio kuwafanyia uhaini na usaliti katika kipindi hiki kigumu kuwahi kuwapitia?

Ukweli khasa ni kwamba kitendo hiki cha Baniy Quraydhwah hakikuwa ni uvunjaji wa ahadi tu bali wakati huo huo kilikuwa ni usaliti na uhaini pamoja.

Kiasi cha kuonwa ni kibaya mno hata na watu wao wenyewe walipokuwa wakiujadili ujumbe ulioletwa kwao na Huyay Ibn Akhtwab, wakasema:

“Ikiwa hamtamnusuru Muhammad, basi muacheni na adui yake”.

Zaidi ya yote hayo huo ulikuwa ni usaliti duni na uhaini wa kipuuzi, kwa sababu huko ni kumchoma kwa nyuma mtu aliyekupa mgongo huku akikuamini.

 

         II.          Jazaa maumbile juu ya usaliti huu muovu:

Hebu tujiulize nini huwa malipo ya usaliti na uhaini kama huu katika kanuni/sheria za kimataifa? Na nini huwa malipo na jazaa ya wahaini na wasaliti hawa katika kivuli cha dini, haki na uadilifu?

Je, ni dhulma kuwapa jazaa inayolingana na uzito wa matendo yao na kufanyiwa kama walivyokuwa wakitaka kuwafanyia wenziwao?

Hapana shaka kwamba hii ndio jazaa maumbile inayokubaliwa na dini zote, inakubaliwa na sheria za vita zile za kale na za sasa na inakubaliwa na kila sauti ya haki, uadilifu na murua.

Basi je, baada ya kutendewa yote hayo bado waislamu watakuwa na hatia wakiwazingira wasaliti hawa mpaka wakajisalimisha mikononi mwao?

Kisha wakawafagia kama wao walivyotaka kuwafagia? Je, bado ilimkinika waislamu kupata amani kwa upande huu wa Mayahudi baada ya usaliti huu?

Je, waislamu wawaache wasaliti hawa kuendelea kuwa miongoni mwao wakizichuka siri zao na kuwapelekea maadui zao?

Je, ilikuwa ni lazima waislamu kuwafukuza Madinah wasaliti hawa kama walivyowafukuza Banin- Nadhwiyr hapo kabla?

Wawaachie wakiwa huru katika ardhi wayakusanye makabila na makundi dhidi yao?

Yalikuwa ni maumbile khasa waislamu kujisafisha na wasaliti na wahaini hawa na wawatendee kama wao walivyotaka kuwatendea.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *