Ewe ndugu yangu mpenzi muislamu, ninakuusia pamoja na kuiusia nafsi yangu tuzipe masiko ya usikivu wa kufuata, kauli hizi za Mola wetu:
“…NA SEMENI NA WATU KWA WEMA…” (2:83)
“ENYI MLIOAMINI! MUOGOPENI ALLAH NA SEMENI MANENO YA HAKI. ATAKUTENGENEZEENI VIZURI VITENDO VYENU NA ATAKUSAMEHENI MADHAMBI YENU…” (33:70-71)
Wanawazuoni wa fani ya mantwiq (logic)-Allah awarehemu– wanatuambia:
(Mambo/vitu/maneno hubainika/hujulikana kwa vinyume vyake kwa sababu kila jambo/kitu kina kinyume chake).
Hebu na tuiweke wazi kanuni hii, sote tunakubaliana bila ya shaka kwamba kinyume cha kusimama ni kukaa.
Sasa mtu anapokuambia usisimame, huwa unaelewa nini? Bila ya shaka atakuwa anakuambia utende kinyume chake, yaani ukae/uendelee kukaa.
Hali kadhalika unapoambiwa usizungumze, maana yake unatakiwa ukae kimya. Sasa kama hivi ndivyo basi ni dhahiri kwamba Allah anapotuambia:
“….NA SEMENI NA WATU KWA WEMA.” Ni kwamba anatukataza tusiseme na watu kwa ubaya, tusiwatamkie maneno machafu yatakayo wavunjia heshima zao, yatakayoumiza hisia zao, yatakayowapelekea kukata uhusiano mwema ulio baina yenu.
Maneno machafu yatakayojenga hali ya chuki na uhasama baina yenu na kuhatarisha amani. Kadhalika Allah anapotuamrisha:
“…SEMENI MANENO YA HAKI…”, ni kwamba anatuamrisha tusiseme maneno ya batili ambayo ni pamoja na kumsengenya mtu, kumtukana, kumzulia uongo, kumfitini na kadhalika.
Kumbuka ewe ndugu yangu–Allah akurehemu–kwamba kuifuata kwako amri ya Mola Muumba wako, ukasema maneno ya haki na ukaacha kusema maneno ya batili.
Kitendo chako hiki chema na cha kibinadamu, kitakuwa ni sababu ya:-
Kuendewa vizuri na mambo yako, iwe ni kazi, biashara, ukulima, uvuvi, ufugaji na kadhalika.
Je, yupo miongoni mwetu asiyetaka kutengenekewa katika mambo na shughuli zake? Bila shaka hayupo hata mmoja, basi dawa na njia pekee ni kusema maneno ya haki
Kusamehewa dhambi. Je, yupo miongoni mwetu asiyelemewa na mzigo mzito wa madhambi, kiasi cha kutokuwa ha haja ya kusamehewa dhambi?
Ikiwa unakiri kuwa mja wa dhambi, basi sema maneno ya haki kwani ni miongoni mwa vifutio dhambi.
Allah akurehemu ewe ndugu yangu, ikiwa utaamini kwamba hii ni ahadi ya Allah Mola muumba wako ambaye:
“…HAKIKA ALLAH HAVUNJI MIADI (yake).” (13:31) “…HAKIKA AHADI YA ALLAH NI HAKI…” (10:55)
Tumesema kuwa mambo hubainishwa na kinyume chake, sasa ikiwa kusema maneno ya haki ni sababu ya kutengenekewa na mambo, sambamba na kufutiwa (kusamehewa) madhambi. Basi ni ukweli usiopingika kwamba kusema maneno ya batili ni sababu ya:-
Kuharibika mambo na mipango yetu mpaka tukajiona tuna nuksi/mikosi tukaanza kutafuta wachawi, na kumbe wanga ni sisi wenyewe. Hili la kutafuta mchawi likatufikisha kuwapigia hodi waganga, tukatupa pesa na imani yetu na kusababisha mambo kuzidi kuharibika. Allah anatukumbusha:
“NA MISIBA INAYOKUPATENI NI KWA SABABU YA VITENDO VYA MIKONO YENU…” (42:30)
Kutokusamehewa dhambi ambako kama kuna maanisha jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kuangamia duniani na akhera:
“…NA ALLAH HAKUWADHULUMU, BALI WAO WENYEWE WANADHULUMU NAFSI ZAO”. (3: 117)
Jua na ufahamu ewe ndugu yangu kwamba maneno machafu hayamvunjii heshima na kumdharaulisha ila anayeyatamka na si mlengwa, hata kama yanamstahiki.
Kama ambavyo maneno mazuri hayamtukuzishi na kumpa heshima ila anayeyasema. Ni vema pia ukatambua kwamba Allah hampendi mtu mwenye maneno machafu, kama alivyosema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie:
“Hakika wa Allah hampendi mwenye maneno/matendo machafu wala mwenye kupiga makelele masokoni”. Bukhaariy
Tahadhari sana ewe ndugu yangu, usiwe mtu ambaye watu watakuogopa na kukutenga kwa sababu ya maneno/matendo yako machafu, kwani Mtume wako–Rehema na Amani zimshukie anakuambia:
“Kwa yakini mtu mwenye daraja/mahala pabaya mbele ya Allah siku ya kiyama kuliko watu wote. Ni yule ambaye watu wamemuacha/wamemuepuka kwa ajili ya kujikinga na uchafu wake (wa maneno/matendo)”. Bukhaary, Muslim, Abuu Daawoud & Tirmidhiy.
Ee ndugu yangu, ebu ona mwenyewe ubaya ulioje na maangamivu yaliyoje ya maneno/matendo machafu.
Hebu ihurumie nafsi yako na adhabu kali ya duniani na akhera inayotokana na kusema ama maneno machafu au kutenda matendo machafu.
Kwani kama hukusema maneno machafu au ikiwa hukutenda matendo machafu, utapungukiwa nini katika utu na maisha yako?!
Ninazidi kukuusia ewe ndugu yangu kwa mapenzi ya Imani bila ya kuisahau nafsi yangu. Tahadhari, tena tahadhari kabisa kuondosha au kujibu ubaya uliotendewa kwa namna/njia ambayo inayokhalifiana na kauli tukufu ya Mola wako:
“MAMBO MAZURI NA MABAYA HAYAWI SAWA ONDOSHA (ubaya unaofanyiwa) KWA MEMA, TAHAMAKI YULE AMBAYE BAINA YAKO NA BAINA YAKE KUNA UADUI ATAKUWA KAMA NI JAMAA (yako) MWENYE KUKUFIA UCHUNGU. LAKINI (jambo hili la kuondosha ubaya kwa wema) HAWATAPEWA ILA WALE WANAOSUBIRI (pindipo wanapotendewa ubaya)…” (41:34–35).
Allah anazidi kutuasa juu ya namna ya kuondosha ubaya kwa kusema:
“NA KAMA SHETANI AKIKUSHAWISHI KWA TASHWISHI (zake ili ugombane na hao wanaokufanyia ubaya) WEWE JIKINGE KWA ALLAH (kwa kusema): “AUDHU BILLAAHI MINAS-SHAYTWAANIR– RAJIYM,” BILA SHAKA YEYE (Allah) NI MWENYE KUSIKIA (mwenye kumuomba msaada), MWENYE KUJUA (namna ya kumsaidia)”. (41:36)
Naam, ni kweli kuwa hakuna anayemjua zaidi mwanadamu kuliko Allah Mola Muumba wake.
Kwa mantiki hii, hakuna ye yote anayeweza kumpa mwanadamu ushauri nasaha mwema juu ya namna ya kukabiliana na uovu/ubaya/uadui anaotendewa kuliko Allah.
Kama ndugu yangu unaniunga mkono katika ukweli huu usiokanushika, ninakuusia tushikamane na ushauri nasaha huu wa Muumba wetu.
Tuyakabili maovu/mabaya tunayotendewa na wenzetu kutokana na udhaifu wa kibinadamu kwa mema mazuri. Kwani hii ndio njia pekee ya kumgeuza adui huyu kuwa rafiki, kwa sababu ubaya hauondoshi ubaya bali ubaya huzidisha ubaya.
Ni kwa mantiki hii ndio Allah Mola Mwenyezi akamuasa Mtume wake nasi pamoja nae kwa kusema:
“SHIKAMANA NA KUSAMEHE NA AMRISHA MEMA NA WAPUZE MASAFIHI (watu wajinga, wenye maneno/matendo machafu).” (7: 199)
Elewa na ufahamu kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie–amesema:
“Ye yote atakayeizuia ghadhabu na il-hali ana uwezo wa kuipitisha. Allah Mtukufu atamuita juu ya vichwa vya viumbe siku ya kiyama ili amkhiyarishe mahurul-ayni (wanawake wa peponi) awatakao”. Abuu Daawoud & Tirmidhiy
Jitahidi ewe ndugu ndugu yangu, uwe pamoja na Allah Mola Muumba wako kama kwamba hakuna viumbe wengine.
Ni wewe tu pamoja nae na amekuumba na kukupa jukumu la kumuabudu na anaangalia namna unavyomuabudu wakati wote na mahala pote.
Fikra, mawazo na hisia zako ziwe kwamba wakati wo wote na mahala po pote jicho la Allah linakuangalia na kuyajua yote uyatendayo, uyasemayo na hata uyawazayo. Kadhalika uwe pamoja na viumbe wenzako kama mwili na nafsi moja, wao ndio wewe na wewe ndio wao.