HADITHI YA UZUSHI

Ama tukio la pili ni lile tukio la uzushi na uwongo dhidi ya Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwa jambo ambalo Allah alimtakasa nalo.

Tukio hili linaanzia pale ambapo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa njiani kurejea Madinah akitokea kwenye vita vya Banil-Muswtwalaq.

Mtume alipiga kambi njiani usiku ili watu wapumzike na kisha kuendelea na safari baada ya mapumziko hayo mafupi. Bi. Aysha akatoka nje ya kambi kwenda kukidhi haja yake akiwa peke yake, njiani kikamuanguka kidani chake.

Akarudi tena kule alikotoka kukitafuta, akakitafuta mpaka akachelewa kurudi kambini. Ikumbukwe kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa na haraka ya kufika Madinah, kwa ajili hii akaamuru kambi ivunjwe na safari iendelee. 

Alitoa amri hii bila ya yeye wala ye yote miongoni mwa maswahaba kujua kuwa Bi. Aysha  hayupo.

Wakakibeba kibanda chake na kukipakia juu ya ngamia wake wakidhania kuwa yumo ndani yake na haraka haraka wakaondoka, huku wakimuacha nyuma bila ya kujua.

Bi. Aysha baada ya kukitafuta kidani chake kwa kitambo na kukipata, akarejea kambini na hapo hakumkuta hata mtu mmoja.

Basi akaamua kubakia hapo hapo akiwa na yakini kwamba hapana budi watamrudia tu pale watakapotambua kuwa hayupo.

Akakaa hapo mpaka usingizi ukamshinda, akalala. Nyuma kabisa ya msafara alikuwepo mtu mmoja aitwaye Swafwaan Ibn Muatwali, huyu alikuwa akiufuatia msafara kwa nyuma kwa ajili ya kuokota kitu/mzigo uliosahauliwa  na msafara.

Akiwa katika harakati zake hizi akamuona Bi. Aysha na kusema: “Innaa Lillaahi wa Inna Ilayhi Raajiuun”hakika sisi sote ni milki ya Allah na kwake yeye tutarejea”.

Akaendelea kusema maneno hayo mpaka Bi. Aysha akazinduka kutoka usingizini, alipoamka akampelekea ngamia wake nae akampanda.

Akaondoka Swafwaan akimvuta ngamia aliyembeba Bi. Aysha mpaka akaingia nae Madinah majira ya mchana wa jua kali.

Abdullah Ibn Ubayyi alipomuona akauliza: “Huyo ni nani?”, akaambiwa:

“Ni Bi. Aysha huyo”. Kusikia hivyo akasema:

“Loh! Mke wa Mtume wenu amelala na mwanaume mpaka asubuhi, halafu tena hawara yake huyo akaja akimkokota juu ya ngamia wake!”

Hapo tena midomo ya wanafiki ikapata la kubwabwaja, wakawa hawana la kuzungumza ila suala lile la uzushi dhidi ya Bi. Aysha mkewe Mtume kwa upande mmoja na Swafwaan kwa upande wa pili. 

Mji mzima wa Madinah ukazizima kwa khabari hii ya uongo na uzushi mtupu mpaka pale wahyi uliposhuka kumtakasa na uchafu aliosingiziwa.

Wahyi ukawakadhibisha hawa waliouzua uzushi huu, ukawafedhehesha na kuwakamia kupata adhabu kali kama jazaa ya uovu wao huo.

 

III.          MAZINGIRA YA TUKIO HILI LA UZUSHI.

Kwa kweli, tukio hili kwa dhati yake lilikuwa ni suala/jambo la kawaida tu ambalo halikustahili kuamsha hisia za tuhuma au shaka.

Kwani halikuzidi katika mazingira yake juu ya kwamba mwanamke mwenye heshima ameachwa na msafara bila yeye wala wao kujua.

Akakutwa njiani na mtu anayeufuatia msafara kwa nyuma kama ilivyokuwa ada, huyu akamuweka katika hifadhi yake mpaka akamrejesha kwake. 

Kitendo hiki alichomtendea mwanamke huyu ni kitendo cha mtu anayetekeleza wajibu wake kwa kutambua kuwa ni wajibu wake kufanya hivyo.

Na kama haikuwa ni wajibu basi haipungui kuwa ni murua unaomsukuma mtu karimu kutoka ndani ya uvungu wa moyo wake kuutenda.

Na katika hali zote mbili hizi, hakukustahiki kuwepo na ukumbi/jukwaa la shaka katika kadhia hii ya mwanamume karimu mwenye murua na mwanamke mtukufu mwenye staha.

Kwa sababu hili ni suala la kimaumbile linalosukumwa na mazingira ya utu wa kibinadamu katika suala zima la kusaidiana katika shida.

Tukirudi nyuma tunamkuta Bibi huyu mtukufu wakati anahama Makah kwenda zake Madinah, hakuambatana na ye yote zaidi ya mwanawe mchanga wa kiume.

Uthman Ibn Twalhah  – ambaye hakuwa muislamu bali mushriki – murua haukumpa hata kidogo kumuacha mwanamke na mtoto mchanga peke yao jangwani.

 Akasuhubiana nae katika kipando (mnyama) chake mpaka akamfikisha Madinah, halafu ndipo akageuza na kuelekea Makkah alikokuwa akienda wakati anakutana na Bibi huyu.

Katika hili hapana hata mtu mmoja katika wakazi wa Madinah aliyethubutu kufungua kinywa chake kusema pamoja na ukweli kwamba Uthman bado alikuwa ni mushriki na adui wa waislamu.

Na pia pamoja na ukweli kwamba safari hii ilikuwa ni ya masafa marefu na hivyo kutoa mwanya na fursa ya kutosha kwa  mwenye kutaka kuutumia mwanya/fursa hiyo kufanya alitakalo.

Kwa hakika na ukweli haya yote yalijiri kutokana na ule ukarimu na silka ya Kiarabu ambayo inamuwajibishia mwanamume ye yote kumuhami, kumuhifadhi na kumlinda mwanamke anapokuwa hana wa kumuhami hata kama mwanamke huyo ni katika watu duni madhalili.

Haya ni vipi basi itakuwa na ilhali Bi. Aysha ni mke wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na isitoshe ni mzawa wa nyumba ya Abu Bakri yule msadikishaji!

Hiyo ni nyumba ambayo haikujulikana kwa machafu katika zama za Jahilia, vipi unafikiri ndugu msomaji itakuwa nyumba hiyo katika kipindi hiki cha nuru ya Uislamu!

Ni vipi utafanyika uchafu na ilhali Swafwaan ni mtu mwenye imani thabiti kwa Allah na Mtume wake na anaifuata kikamilifu misingi ya Uislamu ambayo inakataza maovu na machafu?!

Na vipi itakuwa na ilhali zaidi ya yote hayo, yeye ni Muarabu mwenye damu ya silka na ukarimu wa Kiarabu na murua wao?!

Na je, haikutoshi kuwa yeye ni muumini anayeamini kwa mujibu wa imani yake kuwa wake za Mtume wake ni mama zake?!

 

IV.          MFUNDO WA IBN UBAYYI NDIO ULIOKUWA SABABU KHASA YA UZUSHI NA URONGO HUU.

Lakini hali ilivyo, ni mfundo, hasadi na chuki vilivyoula moyo wa Abdillah Ibn Ubayyi na kuujaza ghadhabu dhidi ya Uislamu na Mtume wake ndivyo vilivyomsukuma kutunga  na kuzua uzushi na uongo huu duni.

Ibn Ubayyi alirudi katika safari hii akiwa ameghadhibika na kuungua moyo kwa sababu ya kuruka patupu vitimbi vyake na kumpelekea kupatwa na udhalili na unyonge.

Akaingia Madinah na ilhali nafsi yake ikichemka na kutokota ghadhabu na chuki dhidi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akawa anaizengea fursa itakayomtua mzigo thakili (mzito) wa chuki na ghadhabu iliyomo nafsini mwake.

Alipowaona Bi. Aysha na Swafwaan wakirejea peke yao Madinah, akaona hakuna fursa nzuri zaidi ya kuzusha uzushi na uvumi kuliko hiyo.

Na kuwasha moto wa fitna ambao alishindwa kuuwasha baina ya Muhajirina na Answari katika lile tukio la kibarua na mshirika wa Khazraji.

Akaanza kuuachilia ulimi wake katika kumsingizia Bi. Aysha machafu ili kutia chuki baina ya Mtume na mtu wake wa karibu zaidi; Abu Bakri.

Au pengine atafanikiwa kuwatia shaka waislamu kuelekea utukufu wa Mtume wao au kuzusha ghasia na magomvi baina ya jamaa zake Khazraji na waislamu wengine.

Kwa kweli matukio na mazingira ya msafara huu yalikuwa yakihitajia haraka na ndio maana mwendo wa jeshi hili wakati wa kurudi ulikuwa una mshindo mkuu.

Kwa sababu ya kuenea na kutangaa fitna baina ya waislamu na wafuasi wa Abdillah Ibn Ubayyi. Na Mtume alifanya haraka ili awashughulishe watu na suala la fitna hii mpaka Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawa anamchapa mnyama wake na mjeledi ili ampeleke mbio.

Kwa hali hii, si ajabu kwa msafara kumacha Bi. Aysha  katika safari hii ya haraka ya kurejea bila ya mtu ye yote kujua kuwa hayumo ndani ya msafara.

Lakini lengo duni na uhasama mtwefu vilimpomosha Ibn Ubayyi mpaka daraja ya chini kabisa, ndipo akaufyatua uzushi huu ambao mbele za watu wenye uzingativu yakinifu si lo lote ila ni upuuzi mtupu tu usio na maana hata chembe.

Wakaunyakua na kuupokea uzushi na uongo huu watu wa sampuli yake; wanafiki wenziwe na wakautapanya na kuueneza kila mahala.

Mpaka masikio yakashehenezwa nao, ndimi zikayapokea na akayazungumza asiyejua kilichojificha nyuma ya uzushi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *