Ili adhana iweze kusihi na kuzingatiwa kisheria kuwa ni adhana kumeshurutizwa kupatikana sharti zifuatazo:-
1. UISLAMU: Kisheria haisihi adhana kwa kafiri kutokana na kutokuwa kwake na utayarifu/ustahiki wa ibada (ahliyah). Kwa mantiki hii ni lazima muadhini awe ni muislamu.
2. UPAMBANUZI (discrimination): Haisihi adhana kwa mtoto mdogo ambaye bado hajafikia umri wa upambanuzi. Kutokusihi huku kwa adhana ya mtoto kunatokana na kutokuwa kwake na utayarifu wa ibada na udhibiti wa wakati.
3. UANAMUME: Haisihi adhana ya mwanamke, kwa sababu adhana haikushariiwa wala haikusuniwa kwake bali imeharamishwa.
Hii ni kutokana na kuwepo uwezekano wa kufitinika wanaume na sauti yake.
Na hii pia ni mojawapo ya sababu nyingi zinazomnyima uimamu mbele ya mwanamume. Kama isivyosihi adhana ya mwanamke, kadhalika haisihi adhana ya “khuntha”-(Hermaphrodite) kwa sababu ya kutokujulikana uanamume au uanamke wake.
Kwa mantiki hii ni lazima muadhini awe mwanamume.
4. UTARATIBU: Ni sharti matamko ya adhana yaletwe kwa mtungo na utaratibu wake kama yalivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Hii ni kwa sababu kuacha utaratibu kunatuhumisha kufanya mchezo na kupunguza uzito wa tangazo hili la kuingia kwa wakati wa swala.
5. MFULULIZO: Ni sharti upatikane mfululizo baina ya matamko ya adhana, kiasi cha kutopatikana mwanya mkubwa baina ya tamko la kwanza na lile la linalofuatia.
6. KUINGIA WAKATI WA SWALA: Haisihi adhana na ni haramu kuadhini kabla ya kuingia wakati wa swala husika, hili linatokana na kongamano (Ijmaa) la mafaqihi.
Kongamano hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Itakapohudhuria swala, basi na akuadhinieni mmoja wenu”.
Bukhaariy & Muslim
Ni dhahiri kuwa swala haihudhurii ila kwa kuingia wakati wake.
Ikiwa adhana itatolewa nje ya wakati, kutalazimu kuadhini tena utakapoingia wakati wa swala.
Hii ni kwa sababu adhana nje ya wakati inakosa falsafa ya adhana ambayo ni kufahamisha kuingia kwa wakati wa swala.
Kwa mantiki hii ni haramu kuadhini kabla ya kuingia kwa wakati wa swala husika kutokana na kuwatatiza (kuwachanganya) watu. Na kuwaongopea kwa kungia wakati wa swala na ilhali bado haujaingia.
TANBIHI: Adhana ya swala ya Sub-hi haiguswi na sharti hii ya kuingia kwa wakati. Kwani inajuzu kuadhini baada ya kupita nusu ya usiku (usiku wa manane) kama inavyofanywa leo Makkah na Madinah.
Hili ni natija ya riwaya ya Abdallah Ibn Amrou-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema:
“Hakika Bilali huadhini usiku, basi kuleni na kunyweni mpaka muisikie adhana ya Ibn Ummu Maktuum”. Bukhaariy & Muslim
7. IWE KWA KIARABU: Ni sharti matamko yote ya adhana yaletwe kwa lugha ya Kiarabu kama yalivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allah.
Haijuzu kutolewa adhana kwa lugha nyingine yo yote isiyo Kiarabu, kwani hiyo haitakuwa adhana bali tarjamah (tafsiri ya neno kwa neno) ya adhana.
8. KUWASIKILIZISHA BAADHI YA WATU: Ni sharti adhana ya jamaa itolewe kwa sauti inayoweza kusikiwa na watu walio jirani na mahala inapotolewa.
Ama ikiwa ni adhana ya mtu anayeswali peke (Munfarid) si sharti kunyanyua sauti, bali adhana hiyo itolewe kwa sauti ya chini kiasi cha kusikia muhusika pekee.
Imepokewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia Abuu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi:
“Mimi ninakuona wewe ni mpenzi wa mifugo na kuishi mashambani. Utapokuwa pamoja na mifugo yako au kitongojini kwako na ukaadhini kwa ajili ya swala, basi inyanyue sauti yako kwa wito huo (wa swala).Kwani hausikii upeo wa sauti ya muadhini jini wala mwanadamu ila (sauti hiyo) itamshuhudia siku ya Kiyama”. Bukhaariy
TANBIHI:
Haikusuniwa adhana kwa jamaa ya wanawake, kwa sababu ya fitina inayoweza kupatikana kutokana na kusikilizika sauti zao na wanamume.
Iliyosuniwa kwao ni Iqaamah tu, kwa sababu hekima (falsafa) yake ni kuwainua waliohudhuria swala kuswali. Na haina kuinua sauti kama ilivyo kwa adhana.