Mwaka wa huzuni ambamo Mtume aliipoteza mihimili yake miwili; muhimili wa ndani, mkewe Bi Khadijah na Muhimili wa nje Ami yake Mzee Abuu Twaalib;
Upasito wa watu wa Makkah na mapokezi mabaya ya watu wa Twaif. Matukio yote haya yalimtia Mtume katika hali ya huzuni kuu, na kumkatisha tamaa na watu wake kwa kiasi kikubwa sana .
Ni katika hali na mazingira haya ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomkirimu Mtume wake safari ya Israa na Miiraji kabla ya Hijrah ya Madinah.
Israa ni ile safari ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kutoka mji mtukufu wa Makkah usiku mpaka Baaytul-Maqdisi Jerusalem, Katika nchi ya Palestine.
Ama Miiraji ni ile safari iliyoanzia hapo katika Baytil-Muqaddas kuelekea ulimwengu na anga za juu kabisa (mbinguni) kuonana na Mola wake na hatimaye kupewa zawadi ya swala tano yeye na umati wake .
Safari ya Israa imetajwa ndani ya Qur – ani Tukufu:
UTUKUFU NI WAKE YEYE AMBAYE ALIMPELEKA MJA WAKE USIKU (mmoja tu) KUTOKA MSIKITI MTUKUFU (wa makkah) mpaka MSIKITI WA MBALI (wa Baytul-Muqaddas – Palestine) AMBAO (tumeubariki na) TUMEVIBARIKI VILIVYOKO PEMBEZONI MWAKE. (Tulimpeleka Hivyo) ILI TUMUONYESHE BAADHI YA ALAMA ZETU. .HAKIKA YEYE ( Allah) M MWENYE KUSIKIA ( na ) mwenye kuona” ( 17:1).
Ama Safari ya Miraji imepokelewa katika vitabu sahihi vya hadithi .
Hadithi sahihi zaidi katika kuitaja safari hii ni ile iliyopokelewa na kuitaja safari hii ni ile iliyopokelewa na Maimamu Bukhaariy na Muslim na Kunakiliwa na Kadhi Iyaadh katika kitabu chake kiitwacho “Shifaa”.
Imepokelewa riwaya kutoka kwa swahaba wa Mtume : Anasi Ibn Maalik – Allah amuwiye radhi – amesema :
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie ; aliletwa buraqu, naye ni mnyama mkubwa kuliko punda na ni mdogo chini ya nyumbu.
(Spidi yake anapokimbia) huweka kwato zake ukomo wa macho yake” Mtume akasema :
Nikampanda mpaka nikafika Baytul – Muqaddasi , Hapo nikamfunga kwenye kikuku ambacho walikuwa wakimfungia Mitume (kabla yangu).
Kisha nikaingia msikitini na kuswali humo nakaa mbili halafu nikatoka ndipo Jibril aliponiletea chombo chenye pombe na kingine kina maziwa (nichague) nikachagua (na kunywa) maziwa. Jibril akasema umechagua jumbile (umbo).
Halafu tukapandishwaa mbinguni, Jibril akabisha hodi akaulizwa U nani wewe ?
Akajibu Jibril, akaulizwa (tena) U pamoja na nani wewe ? Akajibu Muhammad . Akaulizwa (tena) : Je ameitwa kuja huku ? Akajibu , naam ameitwa .
Tukafunguliwa , Kutahamaki huyu ndiye Adam, akanikaribisha na kuniombea dua njema. Kisha tukapandishwa mpaka uwingu wa pili, Jibril akabisha hodi akaulizwa : U nani wewe?
Akajibu Jibril, akaulizwa (tena) U pamoja na nani wewe ? Akajibu Muhammad. Akaulizwa ( tena ) ;Je ameitwa kuja huku ? akajibu naam ameitwa.
Tukafunguliwa tahamaki niko uso kwa uso na ndugu wawili wa mama mkubwa na mama mdogo ; Yahyah na Issa mwana wa Mariam Wakanikaribisha na kuniombea dua njema.
Halafu Tukapandishwa uwingu wa tatu ( Jibril) akataja ( maneno ) kama yale ya mwanzo basi tukafunguliwa .
Kutahamaki huyu ndiye Yusuf naye akiwa kapewa nusu ya uzuri akanikaribisha na kuniombea dua njema .
Kisha tukapandishwa mpaka uwingu wa nne , ( Jibril ) akataja ( maneno ) yale yale, Tahamaki niko ana kwa ana na Idrisa, akanikaribisha na kuniombea dua njema. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suurati Maryam.
“NA TULIMUINUA DARAJA YA JUU KABISA’ (19:57).
Kisha tukapandishwa mpaka uwingu wa tano akataja maneno yale yale.
Tahamaki niko mbele ya Haruni akanikaribisha na kuniombea dua njema .
Halafu tukapandishwa mpaka uwingu wa sita akataja maneno yale yale Tahamaki huyu ndiye Musa akanikaribisha na kuniombea dua njema.
Kisha tukapandishwa mpaka uwingu wa saba akataja maneno yale yale.
Tahamaki niko ana kwa ana na Ibrahim akiwa ameegemeza mgogo wake kwenye (Msikiti wa) Baytul – Maamuri.
Msikiti huo huingiwa na malaika sabini alfu (70,000) kila siku (wapya wasio wale waliopata kuingia).
Kisha ( Jibril) akanipeleka mpaka penye Mkunazi wa kumalizikia ( mambo yote ) . Majani ya Mkunazi huo ni kama (Ukubwa wa) masikio ya tembo na matunda yake ni kama magurudumu. Mkunazi ule ulipofunikwa kwa amri ya Mola wangu , Ulibadilika.
Basi hakuna yeyote katika viumbe wa Mwenyezi Mungu anayeweza kuusifia mkunazi huo kutokana na uzuri wake. Mwenyezi Mungu akanifunulia hapo aliyonifunulia yaani wahyi na akanifaradhisha mimi na umati wangu swala khamsini mchana na usiku.
Nikateremka mpaka kwa Musa akaniuliza Mola wako ameufaradhishia nini umati wako ? Nikamwambia swala Khamsini akaniambia rejea kwa Mola ukamuombe akupunguzie kwa sababu umati wako hawataliweza hilo kwani mimi nimewajaribu Baniy Israil na kuwa na uzoefu nao. Akasema (Mtume) Nikarudi kwa mola wangu na kumwambia ewe Mola wangu Wapunguzie umati wangu, akanipunguzia Swala Tano (zikabakia arobaini na tano).
Nikarejea kwa Musa nikamwambia amenipunguzia tano. Akaniambia umati wako hawataziweza hizo, rudi tena kwa Mola wake ukamuombe akupunguzie; Akasema (Mtume)
“Nikawa nikienda na kurudi baina ya Mola wangu Mtukufu na Musa mpaka akasema utakatifu ni wake; Ewe Muhammad hizo ni swala tano kila mchana na usiku. Kila swala moja kwa swala kumi basi hizo ni swala khamsini. Na yeyote atakayekusudia kufanya jambo jema na asilitende, ataandikiwa jema moja, Na atakayekusudia kutenda jema na akalitenda ataandikiwa mema kumi, Na atakayekusudia kutenda na asilitende hataandikiwa chochote. Na atakayekusudia kufanya ovu na akalifanya ataandikiwa dhambi/baya moja”
Akasema Nikashuka mpaka kwa Mussa, nikampa khabari ya huko.
Akasema rudi tena kwa Mola wako umuombe takhfifu nikamwambia nimerejea kwa Mola wangu mpaka nimeomuonea haya kisha Bwana Mtume – rehema na Amani zimshukie akarejea usiku ule ule kulipopambazuka akadamkia kwenye baraza ya Makurayshi.
Abu Jahli Ibn Hishaam akamjia nae akamuhadithia khabari yote iliyotokea Abu Jahli akaita Enyi Bany Ka’abi Ibn Luayyi njooni makafiri wa kikurayshi wakamjia, Bwana Mtume anaelezea khabari ile baada ya kuusikia wakawa wako miongoni mwao waliopiga makofi na wengine wakawa wameshika vichwa vyao kwa kustaajabu na kupinga.
Baadhi ya watu waliokuwa wamemuamini Mtume waliritadi na kurudi ukafirini, hawa walikuwa ni wale madhaifu na Imani.
Baadhi ya watu wakamuendea rafiki mkubwa wa Mtume Bwana Abi Bakri na kumpasha khabari ile. Akamwambia ikiwa amesema hivyo basi amesema kweli wakamwuliza Unamsadiki kwa khabari hizi? Akajaribu, Mimi ninamsadiki kwa khabari za mbali zaidi kuliko hizo (za kwenda Baytul-Muqaddasi usiku na kurudi hapa usiku huohuo).
Tangu siku hiyo ndipo alipoitwa Abu bakari Sidiyk (Abu Bakri Msadikrishaji). Kisha makafiri wale wakaanza kumtahini Mtume kwa kumuuliza sifa za msikiti wa Baytul–muqaddasi na miongoni mwao walikuwepo walioujua.
Ama Bwana mtume alikuwa hapata kuuona kabla ya safari hiyo.
Mwenyezi Mungu akamletea Mtume wake msikiti ukawa mbele ya macho yake akawa anawasifia mlango baada ya mlango na sehemu baada ya sehemu.
Wakasema ama kwa upande wa sifa tu amepatia kweli. Sasa tuelezee khabari ya msafara yetu. Walikuwa na misafara yao ya biashara ikitokea shamu.
Bwana Mtume akawaeleza idadi ya ngamia waliomo katika misafara hiyo na hali yake na akawaambia itakufikieni siku fulani mchana ikiongozwa na ngamia wa kijivu.
Wakaondola wakiingojea siku hiyo kwa hamu, akasema mmoja wao siku hiyo wallah Jua hilo limechomoza, Na mwingine akasema Wallah na msafara huo umeingia na unaongozwa na ngamia wa kijivu kama alivyosema Muhammad.
Utabiri na ukweli huu wa bwana Mtume haukuwazidishia Mukurayshi ila kibri na upinzani mpaka wakasema huu ni uchawi wa dhahiri.
Asubuhi ya usiku ule wa safari ua Israaa na Miiraji, Jibril alikuja na akamfundisha Mtume jinsi ya kuswali na nyakati za swala. Aswali rakaa mbili alfajiri, rakaa nne adhuhuri na nyingine lasiri na rakaa tatu magharibi na nne ishaa.
Bwana Mtume kabla ya kufaradhiwa suala alikuwa akiswali rakaa mbili asubuhi na jioni kama alivyokuwa akiswali Nabii Ibrahimu – Rehema na Amani ziwashukie wote.