WEPESI WA UISLAMU NA MAANA YA KUTAYAMAMU

Tumekwishajua kutokana na maelezo ya masomo yaliyopita kwamba udhu ni sharti ya kusihi kwa swala, tawafu (ibada ya kuizunguka Al -kaabu), kuushika na kuuchuka/kuubeba msahafu.

Kadhalika tumefahamu kuwa udhu hupatikana kwa kutumia maji katika viungo makhsusi.

Sote tunakubaliana na hakika/ukweli kuwa mwanadamu kama viumbe hai wengine ni viumbe mwenye tabia ya kubadilika kutoka hali moja kwenda katika hali nyingine iliyo tofauti na ile ya mwanzo au kutoka katika mazingira hadi mengine.

Sasa kwa kuizingatia kanuni/sheria na tabia hii ya kimazingira, inawezekana kabisa ikamtokea mwanadamu hali au mazingira ambayo atashindwa kuyatumia maji kwa ajili ya udhu au josho.

Anaweza akayakosa maji katika maeneo aliyomo wakati ule, au maji yakawa yanapatikana maeneo ya mbali sana na ikamuwia taabu kuyafikia, au akawa na maradhi ambayo yanamzuilia kutumia maji katika hali na mazingira kama haya, muislamu afanye nini na ilhali imemlazimu kuitekeleza ibada ya swala na ni maalum kuwa ibada hii haitekelezeki bila ya kuwa na udhu.

Sasa je, aache kuswali kwa sababu ya kukosa au kushindwa kuyatumia maji ?

Au ayatumie maji hata kama yanamdhuru ili apate udhu utakaomuwezesha kuswali ?

La, hasha ! Hapo sasa ndio inaonekana kazi ya msingi miongoni mwa misingi ya fiq-hi ya kiislamu usemao:

“HAPANA KUDHURU (MTU) WALA KUJIDHURU MWENYEWE.” Kutokana na msingi huu tumeelewa kuwa kumbe hakuna katika Uislamu kujitia katika madhara kwa sababu ya kuutekeleza Uislamu.

Msingi huu si dhana tu iliyosimikwa na kuwekwa na wanazuoni bali unaitegemea kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:


“…WALA MSIJITIE KWA MIKONO YENU KATIKA MAANGAMIZO …” [2:195].

Kupitia msingi huu ndipo unapojitokeza na kuonekana wepesi wa dini na mfumo huu sahihi wa maisha unaokwenda sambamba na hali, tabia na mazingira ya mwanadamu.

Katika hali na mazingira kama hayo ndio uislamu ukamuwekea mwanadamu huyu sheria ya kutayamamu kwa kutumia mchanga tahara badala ya kutumia maji katika udhu au josho.

Uislamu umetoa ruhusa hiyo ili kumpa fursa mwanadamu huyu ya kuitekeleza ibada bila ya tabu au madhara na kuziba mwanya wa kuacha kutekeleza ibada kwa kisingizio cha kukosa maji au maradhi yanayozuia utumiaji wa maji.

Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu:


“…ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI NA WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO …” [2:185]

Tusome tena ili tuzidi kuuona wepesi wa Uislamu


“….HAPENDI ALLAH KUKUTIENI KATIKA TAABU ..” [ 5:6]|
“… WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI .” [22: 78]

Baada ya kuona ni jinsi gani uislamu ulivyomuwekea muislamu mazingira mepesi katika kuutekeleza uislamu.

Hebu sasa tujaribu kuiangalia tayamamu kwa ujumla, tukianzia na maana ya kutayamamu.

Tayamamu ni neno la Kiarabu ambalo tumezoea kulitamka kama “kutayamamu”.

Neno hili lina maana mbili zifuatazo:

Maana ya kilugha: Katika lugha ya Kiarabu neno tayamamu lina maana ya kukusudia.

Maana ya kisheria: Kutayamamu ni kupakaza vumbi la mchanga twahara katika uso na mikono kwa utaratibu maalum uambatano na nia.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *