UADILIFU

Tangu zama na zama kumekuwepo na kelele za wanadamu juu ya kiu yao ya kuitaka kuiona jamii ya wanadamu ulimwenguni kote ikiishi katika amani na utulivu.

Chimbuko na msingi wa amani na utulivu huu uwe ni uadilifu, uadilifu ambao utamuaminisha mtu na dhuluma na kumuhakikishia haki zake zote.

Ustaarabu na mifumo mbalimbali ya maisha iliyobuniwa na kufumwa na wanadamu wenyewe katika nchi zao.

Walioibuni mifumo hiyo wamejaribu kuzitekeleza ndoto za jamii zao katika kuzihakikishia maisha mazuri na hduma bora za kijamii hiyo imeweza kutimiza ndoto hizo lakini imeshindwa vibaya kabisa kusimamisha uadilifu utakaoleta amani na utulivu.

Kwani ni chini ya mwavuli wa amani na utulivu ndio mwanadamu anaweza kuiona ladha na tamu ya maisha mazuri na huduma bora za kijamii.

Itoshe kuwa ni ushahidi dhahiri kwamba mifumo hiyo imeshindwa kuleta uadilifu namna mataifa mbalimbali yalivyotumbukia katika maafa na majanga kutokana  na uadui, dhuluma na kiburi.

 Yote haya ni ushahidi usipoingika kwamba “mifumo binadamu” haiwezi kusimamisha uadilifu duniani. Uadilifu ambao utakuwa ndio chemchem itakayotoa maji safi na salama {amani na utulivu}

 Historia imetuthibitishia kwamba hakuna “mfumo” binadamu” wo wote ule, si wa magharibi wala wa mashariki unaoweza kusimamisha udilifu zaidi ya “Mfumo sahihi wa maisha ulioweka nguzo madhubuti za uadilifu zinazomuhakikishia kila mtu haki zake za:-

§        Kuishi, kuabudu, kusema, kushauri, kukosoa

§        Kijamii {kupata elimu, kufanya kazi, kupata mahitaji ya msingi, kusikilizwa}

§        Usalama wa maisha, mali na hadhi/heshima yake

§        Kuchagua mfumo wa maisha kwa mujibu wa itikadi yake, na kudalika

 Ni kutokana na umuhimu na nafasi hii ya uadilifu katika maisha ya mwanadamu, ndipo muislamu anauona uadilifu kwa maana yake pana kama ni wajibu ulio juu ya wajibati zote. Mtazamo na uoni huu wa muislamu unatokana na amri/agizo la Allah:

“KWA HAKIKA ALLAH ANAAMRISHA UADILIFU NA KUFANYA HISANI, NA KUWAPA JAMAA (na wengineo) NA ANAKATAZA UCHAFU NA UOVU NA DHULMA —.” [16:90]

Na Allah akatangaza wazi ya kwamba anawapenda watu waadhilifu, kinyume cha tangazo hili pia chafanya kazi ya kwamba madhalimu hawana nafasi ya kupendwa.

” — HAKIKA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO UADILIFU.” [60:8]

 Allah ameamrisha uadilifu katika kusema na kutenda (hukumu).

” — NA MSEMAPO (katika shahada na penginepo) SEMENI KWA UADILIFU (insafu) HATA KAMA NI JAMAA (usimpendelee kwa ajili ya ujamaa ulio baina yenu au kwa ajili ya mrungura na mambo kama haya) —.” [6:152]

 Huo ni uadilifu wa maneno (katika kusema) na huu ni uadilifu katika kutenda (hukumu):

 HAKIKA ALLAH ANAKUAMRISHENI KUZIRUDISHA AMANA KWA WENYEWE (wanaozistahiki). NA MNAPOHUKUMU BAINA YA WATU MUHUKUMU KWA UADILIFU (haki) —“ [4:58]

 Ni kutokana na agizo na muongozo huu kutoka kwa Mola wake, muongozo ambao akiufuata utamuhakikishia amani na utulivu.

Ndio muislamu anafanya uadilifu katika kauli na matendo (hukumu) yake. Anautanguliza uadilifu mbele katika mambo yake sehemu ya tabia yake isiyotengeka nae.

Uadilifu unakuwa ni pambo linalomfanya apendeze na kukubalika na wapenda haki po pote pale. Kwa uadilifu kutoka katika chuo kikuu cha uadilifu {Uislamu}.

Shahada hii inamfanya kuwa muadilifu asiyeyumbishwa na mapenzi, ujamaa au rushwa katika kutenda haki.

Shahada hii inamlazimisha kumtendea uadilifu na haki hata yule ambaye ni adui yake mkubwa, inamfanya avitofautishe vitu viwili hivi, uadui na uadilifu/haki kwa kutarajia kuvuna mapenzi na radhi ya Mola wake.

“ENYI MLIOAMINI! KUWENI WASIMAMIZI (Wa kupitisha haki)  KWA AJILI YA ALLAH, MUWE MKITOA SHAHADA (ushahidi) KWA UADILIFU. WALA KUCHUKIANA NA WATU KUSIKUPELEKEENI KUTOWAFANYIA UADILIFU (insafu). FANYENI UADILIFU, HUKO NDIKO KUNAKOMKURUBISHA MTU NA UCHA MUNGU NA MCHENI ALLAH, HAKIKA ALLAH ANAZO HABARI ZA (yote) MNAYOYATENDA.”[5:8] Tunaweza kuigawa tabia hii ya uadilifu katika mafungu yafuatayo:-

 i/.        Uadilifu kwa Allah:

Huu haumaanishi kingine zaidi ya kutomshirikisha Allah katika ibada na sifa zake. Kumtii bila ya kumuasi, atajwe na akumbukwe bila ya kusahauliwa.

Ashukuriwe kwa neema zake zisizodhibitika bilA ya kukufuriwa.

Mja akiyatenda haya atahesabika kuwa ameonyesha uadilifu wake mbele ya Mola Muumba wake. Uadilifu huu utamvisha vazi la ucha Mungu na kumfanya kipenzi cha Mola wake.

 ii/.       Uadilifu kwa wanadamu:

Huu unamtaka mwanadamu awe muadilifu kwa wanadamu wenziwe kwa kumpa haki kila anayeistahiki kwa mujibu wa sheria.

 Katika kulitekeleza hili asiuweke mbele ya macho yake ujamaa, urafiki, rushwa, uadui na kadhalika.

Huu unahusisha pia kuwafanyia uadilifu na kuwapa haki wanazozistahiki wake kwa kila aliye na zaidi ya mke mmoja. Katika hili watoto pia hawaachwi nyuma, asiwapendelee hawa zaidi kuliko wale.

 iii/.      Uadilifu katika itikadi:

Huu unamtaka mtu asiitakidi ila kweli na haki na ayaone mambo kwa uhakika wake kama yalivyo. Aithibitishe itikadi yake hiyo kupitia nafsi yake mwenyewe na ulimwengu unaomzunguka huku akiamini kuwa anaifanyia kazi kauli ya Mola wake:

“TUTAWAONYESHA (ukweli wa) MANENO YETU HAYA KATIKA NCHI ZA MBALI NA KATIKA NAFSI ZAO WENYEWE MPAKA IWABAINIKIE KWAMBA HAYA NI KWELI —.” [41 : 58]

 Sura/Picha ya uadilifu katika uislamu:

Hebu uone uadilifu unavyofanya kazi katika uislamu. Huyu hapa Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anatupigia mfano usio na mfano katika kutekeleza kimatendo misingi ya uadilifu na usawa katia uislamu.

 Anatekeleza uadilifu katika haki bila ya ubaguzi wala upendeleo baina ya mwenye nguvu na mnyonge, baina ya mkubwa na mdogo wala baina ya mtukufu na aliye duni.

Anawaangalia wote hawa kwa jicho la usawa mbele ya sheria. Hampendelii tajiri kwa sababu ya utajiri wake kama asivyompendelea mtukufu/mwenye hadhi kwa sababu tu ya utukufu/hadhi na daraja yake machoni mwa jamii sawasawa kama yalivyo meno ya chanuo.

Huyu hapa mwanamke mtukufu anapatikana na hatia ya wizi katika zama zake Mtume. Jamaa zake wanahangaika kutoka kulificha suala hili ili lisimfikie Bwana Mtume kwani wwanatambua fika kwama hukumu ya mwizi ni ile aiyoitoa Allah:

“NA MWIZI MWANAMUME NA MWIZI MWANAMKE, IKATENI MIKONO YAO (ikiwa ni) MALIPO YA YALE WALIYOYACHUMA (Hii) NDIYO ADHABU ITOKAYO KWA ALLAH NA ALLAH NI MWENYE NGUVU NA MWENYE HAKIMA.” [5 : 38].

 Habari hizi za kuiba kwa mwanamke mtukufu huyu zikimfikia Mtume ni lazima atapandishwa kizimbani na hatimaye hukumu hii ya Allah kupitishwa dhidi yake.

Kwa kuiona hatari hii wakamtafuta mtu atakayemuombea mwanamke huyu kwa Mtume asikatwe mkono.

Ni nani basi atakayeifanya kazi hii, hakuna mwingine ila mtu aliye karibu zaidi na Mtume aliamua nini na hatima ya mwanamke yule ilikuwaje, huyu hapa mama wa waumini, Bi Aysha (mkewe Mtume) Allah amuwiye radhi anasimulia kwamba liliwahangaisha Makurayshi suala la mwanamke wa kabila la Makhzuum aliyeiba.

Wakasema. Ni nani atayezungumza na Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kuhusiana na suala lake?! wakasema:

Hakuna atakayethubutu ila usaamah Ibn Zayd, kipenzi cha Mtume wa Allah usaamah (akaenda) akamzungumza Mtume, Mtume akamuuliza huku akiwa amebadilika kwa ghadhabu kama asiyemjua: Unaomba msamaha katika hukumu miongoni mwa hukumu za Allah (isitekelezwe)? Kisha Mtume akainuka na kutoa khutba kisha akasema:

“Hakika waliangamia waliokuwa kabla ya yenu kwa sababu alipokuwa akiiba mtukufu miongoni mwao walimauchia (bila ya kumuhukumu). Na anapoiba mnyonge miongoni mwao humsimamishia hukumu. Ninaapa kwa jina la  Allah, lau kama Fatmah Binti Muhammad (mwanangu) angeiba, basi ningemkata mkono wake. Bukhaariy na Muslim.

 Maneno haya ya Mtume wa Allah yanabainisha sababu ya kuangamizwa kwa nyumati zilizopita kuwa ni kukosekana uadilifu na usawa miongoni mwao na kutawaliwa na adui wa haki ubaguzi na upendeleo katika jamii hizo.

Pia yanathibitisha kwamba Uislamu ni dini inayolingania kulinda na kuheshimu haki, usawa na uadilifu na inawatizama watu wote kwa jicho la usawa mbele ya sheria.

 Matunda ya uadilifu katika utawala.

Miongoni mwa matunda mazuri ya uadilifu katika utawala ni kuenea kwa amani ya nafsi. Mtawala kama ni muadilifu hana sababu ya kuwakhofu na kuwaogopa raia wake.

Ukweli wa hili linathibitishwa na kisa kichopokewa kwamba kaisari (mfalme wa urumi wa wakati huo) alimpeleka mjumbe wake kwa Umar Ibn Khatwab (kiongozi wa dola ya Kiislamu) akamchunguze na kumpeleleza kiongozi huyu shujaa anayeheshimwa na kuogopewa na madola mengine na anayependwa na raia wake, Ajue ni nini siri ya mafanikio yake, kisha amletee ripoti. mpelelezi huyu alipofika Madinah (makao Makuu ya dola ya kiislamu wakati huo) aliwauliza wenyeji: Mfalme wenu yuko wapi?

Wakamjibu: Sisi hatuna mfalme bali tunaye Amiri (kiongozi) naye ametoka amekwenda nje ya mji. Akatoka kwenda kumfuata huko aliko, akamkuta amelala mchangani na kuifanya mto fimboyake ndogo aliyokuwa akitembea nayo.

Alipomuona katika hali hii (akiwa hana ulinzi wowote) moyo wkae ukaingiwa na  unyenyekevu akaseema: Mtu ambaye wafalme wote hawapati usingizi kwa kumuogopa hii ndio hali yake: Ewe umar umefanya uadilifu, ukalala kwa amani bila ya walinzi na mfalme wetu anafanya dhuluma, anakesha kwa khofu hapato usingizi.!

 Huu ndio uadilifu na matunda yake, waliotumwa Mitume kuja kuutangaza na kuusimamisha ulimwenguni kote ili dunia iwe ni kisiwa cha amani,

“KWA HAKIKA TULIWAPELEKA MITUME WETU KWA DALILI WAZIWAZI NA TUKAVITEREMSHA VITABU NA UADILIFU PAMOJA NAO, ILI WATU WASIMAMIE UADILIFU……………….(57: 25)

 

UADILIFU

Tangu zama na zama kumekuwepo na kelele za wanadamu juu ya kiu yao ya kuitaka kuiona jamii ya wanadamu ulimwenguni kote ikiishi katika amani na utulivu.

Chimbuko na msingi wa amani na utulivu huu uwe ni uadilifu, uadilifu ambao utamuaminisha mtu na dhuluma na kumuhakikishia haki zake zote.

Ustaarabu na mifumo mbalimbali ya maisha iliyobuniwa na kufumwa na wanadamu wenyewe katika nchi zao.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *