SURA YA PILI-SOMO LA KWANZA-SWALA

i) FAIDA/AINISHO/MAANA NA SWALA

Kabla hatujaingia moja kwa moja kuielezea swala na uchambuzi, ni vema kwanza tukajiuliza swala ni nini, ili tutakapokuwa tunalitaja neno swala, tujue na kuelewa tunazungumzia kitu/jambo gani.

Haya sasa, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu Mjuzi wa yote tuanze kuiangalia maana ya swala, tunasema:- Swala ni neno la Kiarabu lililobeba maana mbili, maana ya kilugha na maana ya istilahi ya fiq-hi (sheria).

Tukiipekuwa na kuiangalia Qur–ani Tukufu tutalikuta neno swala limetumika kwa maana ya dua njema na hii ndiyo maana ya swala kilugha, tusome:-“CHUKUA SADAKA KATIKA MALI ZAO UWASAFISHE NA KUWATAKASA KWA AJILI YA HIZO (sadaka zao) NA KUWATAJA KWA VIZURI (mbele yangu) NA UWAOMBEE DUA. HAKIKA KUWAOMBEA KWAKO KUTAWAPA UTULIVU (watengenekewe) NA ALLAH NDIYE ASIKIAYE NA AJUAYE” (9:103).

Ama katika Istilahi ya kifiq-hi (sheria) neno “swala” linajulikana kama ibada maalum inayokusanya kauli (maneno) na matendo maalum yanayoanzwa kwa Takbira na kukhitimishwa kwa kutoa salaamu. Hiyo ndio swala kwa mtazamo wa sheria, kwa nini basi ibada hii ikaitwa “swala” na sio jina jingine lisilo hili?

Katika kulijibu swali hili tunaweza kabisa kusema kuwa ibada hii imeitwa swala kutokana na kukusanya kwake dua/maombi maalum ya mja kwa Mola wake kitu ambacho ndio sehemu kubwa ya Ibada nzima ya Swala.

ii) NAFASI YA SWALA KATIKA UISLAMU
  • Ibada ya swala ina nafasi na daraja kubwa sana katika Uislamu, kwa sababu nyingi tu, baadhi ya sababu zinazoifanya swala iwe na nafasi ya umuhimu wa pekee ni kama zifuatavyo:-
  • Swala ndio muhimu na nguzo kubwa ya dini kama tunavyofahamishwa na kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshuke. “Swala ndio nguzo ya dini, swala ndio ufunguo wa kheri zote” Twabaraany na Al-Haakim.
  • Swala ndio ibada ya kwanza kabisa aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake katika ule usiku Mtukufu usiku wa nafasi ya Bwana Mtume ya Israa na Miraji. Na ndio ibada pekee aliyopewa Mtume Mbinguni bila ya wasita (Ukati) wa Malaika Jibrilu kwani ibada nyingine zote alipewa hapa hapa duniani kupitia kwa Malaika Jibrilu-Allah amshushie amani.
  • Swala ndio ibada ya mwanzo kabisa atakayohisabiwa na kukaguliwa mja siku ya kiyama kabla ya ibada nyinginezo.
  • Swala ndio ilikuwa wasia wa mwisho wa Bwana Mtume kwa umati wake wakati anafariki dunia hii baada ya kuikamilisha kazi aliyopewa na Mola wake.
  • Swala ndio ibada pekee iliyotajwa zaidi ya mara sabini (70) ndani ya Qur-ani, miongoni mwa sehemu ilizotajwa swala ndani ya Qur-ani Tukufu ni hizi hapa:-“SOMA ULIYOLETEWA WAHYI (uliyofunuliwa) KATIKA KITABU (hiki ulicholetewa) NA USIMAMISHE SWALA BILA SHAKA SWALA (ikisaliwa vilivyo) HUMZUILIYA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU……….” (29:45)

Tusome tena “ANGALIENI SANA SWALA (zote kuziswali, khasa jamaa) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI. NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH” (2: 238).

Hivi ni chache tu miongoni mwa aya nyingi zilizoitaja ibada hii ya swala.

Swala ndio ibada bora kuliko ibada zote kama tunavyofahamishwa na hadithi ifuatayo:
Mtu mmoja alikuja kumuuliza Mtume – Rehema na Amani zimshukie – juu ya amali iliyo bora kabisa kuliko zote, (Mtume) akamjibu “Swala “ akauliza tena Halafu ipi (amali gani inayofuata?) (Mtume) akajibu , “Halafu Swala” Akauliza tena, Halafu ipi? Akamjibu “Swala” mara tatu. Ibn Hibbaan.

Kauli ya jumla tunaweza kusema na si kusema tu bali kusema kwa kinywa kipana kabisa kwamba nafasi/umuhimu wa swala katika Uislamu ni kama umuhimu wa kichwa katika kiwiliwili. Kama kisivyokuwa na uhai kiwiliwili kilichojitenga/kutenganishwa na kichwa chake ndivyo asivyokuwa na uhai Uislamu wa mtu asiyeswali bali inawezekana asiwe na Uislamu kabisa kwa nini?

Hivyo ndivyo tunayoelewa kutokana na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshuke “Hakika baina ya mja na shiriki ni ukafiri ni kuacha swala” Muslim.

iii) DALILI YA SWALA NA TAREHE YAKE

Umethibiti ufaradhifu wa swala kwa kila muislamu ndani ya Qur-ani Tukufu, Sunnah na Ijmaa.

Ama Qur-ani imeamrisha utekelezaji wa swala katika makumi ya aya zake, miongoni mwake ni kauli tukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.”WALA HAWAKUAMRISHWA ILA KUMUABUDU ALLAH KWA KUMTAKASIA DINI (kwa ikhlaasi), WAWACHE DINI ZA UPOTOFU(upotevu), NA WASIMAMISHE SWALA NA KUTOA ZAKKAH, HIYO NDIYO DINI ILIYO SAWA (98:5)

Tuendelee kusoma:
“BASI MTUKUZENI ALLAH MNAPOINGIA KATIKA NYAKATI ZA USIKU (kwa kuswali Magharibi na Isha) NA MNAPOINGIA KATIKA ASUBUHI (kwa kuswali swala ya Alfajiri) NA SIFA ZOTE NJEMA NI ZAKE MBINGUNI NA ARDHINI NA (mtukuzeni) WAKATI WA ALASIRI NA MNAPOINGIA KATIKA WAKATI WA ADHUHURI” (30: 17-18). Maelezo yaliyo katika mabano ni ufafanuzi wa aya kama ulivyo katika kauli ya swahaba Ibni Abaan – Allah amuwiye radhi.

Tusome tena:
“KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHUSUSI” (4:103)

Ama katika sunnah, miongoni mwa hadithi za Mtume ambazo zimefunulia wazi kabisa kwamba swala ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu ni hizi zifuatazo:-

Imepokelewa hadhithi kutoka kwa Abdillah Ibn Umar-Allah awaridhe – kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – amesema, “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: Kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni Mjumbe wake (Shahada), na kusimamisha swala, kutoa Zakkah, kufunga Ramadhani na kuhiji kwa mwenye uwezo. Bukhaariy na Muslim.

Imepokelewa na Ibn Abbaas – Allah awaridhie kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alimtuma Mua’adh – Allah amridhie – kwenda katika nchi ya Yemen (kulingania dini) akamwambia “Walinganie (Waite) kutamka shahada kwamba hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba mimi Muhammad ni Mjumbe wa Allah, ikiwa wao watalitii hilo (watalikubali) basi wafahamishe kwamba Allah amefaradhisha juu yao swala tano mchana na usiku…………” Bukhaariy na Muslim.

Kauli yake Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia yule mkazi wa majangwani ambaye alimuliza swala zilizo faridhi juu yake. “Swala tano kila mchana na usiku” Yule mkazi wa majangwani akamuuliza (tena). Je, ninawiwa (ninalazimika) na swala nyingine zisizo hizo (tano) (Mtume) akamjibu “Hapana ila swala za suna” Bukhaary na Muslim.

Ama katika Ijmaa, wanazuoni wa Kiislamu wamekongamana na kuwafikiana bila ya khitilafu yoyote kwamba swala ni mojawapo ya nguzo za Uislamu. Pia wamekongamana kwamba yeyote mwenye kuiacha swala ama kwa kuifanyia mzaha au kwa kupinga anakuwa amejitoa mwenywe katika Uislamu.

Ama yule atakayeiacha kwa uvivu tu huku akikiri kuwa ni fardhi iliyomlazimu, huyu atakuwa na hatia na dhambi na atastahiki kupata adhabu ya hatia hiyo hapa hapa duniani na kule akhera.

Isitoshe kuwa ni karipio na onyo lenye kuupasua pasua moyo na mwenye kuacha swala kauli hii ya Mwenyezi Mungu Mtukufu “NI KIPI KILICHOKUPELEKENI MOTONI? WASEME “HATUKUWA MIONGONI MWA WALIOKUWA WAKISWALI”. (74:42-43).

Tunaambiwa katika aya hii kwamba siku ya kiyama Malaika watawauliza watu wa motoni. Ni kipi/jambo gani lililokufanyeni nyinyi kuwa katika mafikio na marejeo haya mabaya motoni? Hapo ndipo watu wabaya hawa, watu wa motoni watajibu kwa masikitiko na majuto makubwa, kilichotufiksha mahala hapa pabaya ni kutoihifadhi kwetu ibada ya swala duniani (hatukuwa tukiswali).

Tukiangalia na kuipekuwa tarehe ya swala tutatambua kwamba swala ni ibada kongwe kabisa kufaradhishwa kwa wanadamu Mwenyezi Mungu Mtukufu anatusimulia khabari za Mtume Ismail – Amani imshukie “NA ALIKUWA AKIWAAMRISHA WATU WAKE SWALA NA ZAKA NA ALIKUWA MRIDHIWA MBELE YA MOLA WAKE”.(19:55)

Mwenyezi Mungu anazidi kutuonyesha ukongwe na ibada hii ya swala kupitia ulimi na Nabii Issa – Amani imshukie ”……….NA AMENIUSIA SWALA NA ZAKA MAADAMU NI HAI” (19:31).

Mtume Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – alipopewa utume alikuwa akiswali rakaa mbili asubuhi na jioni. Inasemekana kuwa rakaa mbili hizo ndio makusudi na mradi wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomsemeza Mtume wake. “NA UMTUKUZE MOLA WAKO NA KUMSIFU JIONI NA ASUBUHI” (40: 55)

TUJIFUNZE NA TUKUBALI:

Kuwa swala ndio NEMBO pekee ya kumtofautisha muislamu na asiye muislamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *