ADABU ZA UVAAJI

Muislamu hulichukulia suala la uvaaji kuwa ni miongoni mwa amri za Mola wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu :

“ENYI WANAADAMU! CHUKUENI MAPAMBO YENU (vaeni nguo zenu nzuri) WAKATI WA KILA SWALA; NA KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri). LAKINI MSIPITE KIASI TU. HAKIKA YEYE (Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI” [7:31]

Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa ruhusa waislamu wale, wanywe na wavae vizuri na pia waende msikitini wakiwa wamevaa nguo nzuri. Na amesema tena :

 “ENYI WANADAMU! HAKIKA TUMETEREMSHIENI NGUO ZIFICHAZO TUPU ZENU NA NGUO ZA PAMBO; NA NGUO ZA UTAWA (ucha-mungu) NDIZO BORA …” [7:26]

Mwenyezi Mungu anatubainisha kuwa amemteremshia mwanadamu mavazi/nguo za namna mbili :

  1. Vazi la pambo – hili ni kwa ajili ya kuupamba na kuusitiri utupu wake na kumtofautisha na hayawani wengine.
  2. Vazi la ucha-Mungu – hili ni kwa ajili ya kuipamba na kuisitiri nafsi yake na kumfanya binadamu kamili mkamilifu wa utu na ubinadamu. Na hili ndilo vazi bora kama alivyolisifia Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu ni vazi hili ndilo humtoa mwanadamu kutoka kwenye unyama na kumleta kwenye utu.

Mshairi wa kiarabu anaukiri ukweli huu, aliposema :

Ikiwa mtu hakuvaa vazi la ucha-mungu,
Huyo huwa utupu hata kama kavaa,
Na bora ya mambo ya mtu ni kumtii Mola wake,
Hapana kheri kwa mtu mwenye kumuasi Allah.

Na Mwenyezi Mungu anazidi kutuambia :

“…NA AMEKUFANYIENI NGUO ZINAZOKUKINGENI NA JOTO ( na baridi, na amekufanyieni) NGUO ZA CHUMA ZINAZOKUKINGENI KATIKA VITA VYENU” [16:81]

Hapa Mwenyezi Mungu Mtukufu anatubainishia aina kuu mbili za mavazi, kulingana na majira ambazo ni :

  1. Mavazi ya joto (kiangazi)
  2. Mavazi ya baridi (masika)

Na pia mavazi maalum ya vita, haya ni pamoja na BULLET PROOF tuzionazo leo. Tunasoma tena :

“NA TUKAMFUNDISHA (Daudi) MATENGENEZO YA MAVAZI YA VITA KWA AJILI YENU ILI YAKUHIFADHINI KATIKA MAPIGANO YENU – JE MTAKUWA WANAOSHUKURU ?” [21:80]

Tunafahamikiwa kwamba kumbe sanaa ya utengenezaji wa mavazi ya vita ni sanaa kongwe kabisa na mwanadamu wa kwanza kutengeneza mavazi ya vita ni Nabii Daudi – zimshukie amani-.

Naye mfasiri mkuu wa Qur-ani tukufu, Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – anatufasiria aya hizo kwa kusema :

 “Kuleni, kunyweni, vaeni na toeni sadaka bila ya israfu (kupita kiasi) wala maringo/fakhri”.

Kadhalika, Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – ametufafanulia na kutubainishia mavazi yanayojuzu/yanayofaa kuvaliwa na ambayo ni karaha. Kwa hivyo basi, imempasa na kumlazimu muislamu kuzichunga na kuzifuata adabu/taratibu zifuatazo katika suala zima la uvaaji wake :

1.      Mwanamume asivae kabisa nguo ya hariri kwa hali yeyote ile iwayo hata kama ni tai au kitambaa cha kichwa. Hii ni amri ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliposema :

“Msivae hariri, kwani atakayeivaa duniani hatoivaa akhera” Bukhaariy na Muslim. Na kauli yake Bwana Mtume il-hali akiwa ameishika hariri kwa mkono na dhahabu mkono wa kushoto :

“Hakika (vitu) viwili hivi ni haramu kwa wanamume wa umati wangu” Abu Dawoud.

2.      Nguo yake isiwe ndefu sana kiasi cha kuburuza chini. Urefu wa nguo yake usizidi kifundo cha mguu. Haya yanatokana na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :

“Mwenyezi Mungu hatomuangalia/ hatomtazama kwa jicho la rehema atakayeiburuza nguo yake kwa maringo” Bukhariy na Muslim.

3.      Apendelee zaidi kuvaa nguo nyeupe pamoja na kuwa inafaa kuvaa nguo za rangi nyingine. Hivyo ndivyo alivyotuelekeza Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :

“Vaeni nguo nyeupe kwani hizo ndizo twahara/safi na nzuri sana, na wakafinini maiti wenu kwa nguo nyeupe (yaani washoneeni sanda nyeupe)” Nisaai na Al-Haakim. Na pia imethibiti kwamba Bwana Mtume alivaa nguo ya kijani na alipiga kilemba cheusi.

4.      Mwanamke wa kiislamu avae vazi refu litakaloweza kusitiri hadi nyayo zake, aangushe ushungi kiasi cha kusitiri shingo, na kifua chake. Akifanya hivyo atakuwa ameitii kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo :

“EWE MTUME! WAAMBIE WAKE ZAKO NA WANAWAKE WA KIISLAMU WAJITEREMSHIE UZURI NGUO ZAO. KUFANYA HIVYO KUTAPELEKEA UPESI WAJULIKANE (kuwa ni watu wa heshima ili) WASIUDHIWE ..” [33:59]

Na kauli nyingine isemayo :

“…NA WAANGUSHE SHUNGI ZAO MPAKA VIFUANI MWAO NA WASIONYESHE MAPAMBO YAO ILA KWA WAUME ZAOAU BABA ZAO ….”

Na kwa kauli ya Mama Aysha – Allah amuwie radhi- :

“Mwenyezi Mungu awarehemu wanawake muhaajirati wa mwanzo, Mwenyezi Mungu alipoteremsha : “…NA WAANGUSHE SHUNGI ZAO MPAKA VIFUANI MWAO …” wakapasua maguo yao mazito na kujitanda nayo” Bukhariy.

Na kwa kauli ya Ummu Salamah – Allah amuwie radhi – :

“Ilipoteremka : “EWE MTUME! WAAMBIE WAKE ZAKO NA WANAWAKE WA KIISLAMU WAJITEREMSHIE UZURI NGUO ZAO …” Walitoka wanawake wa kiansari kama kwamba kuna kunguru vichwani mwao kutokana na maguo waliyovaa na kujitanda” Muslim.

Hivi ndivyo wanavyotakiwa kuwa waislamu wa kweli, wakiamrishwa pale pale huamrika na wakikatazwa hukatazika pasina kurudi nyuma.

5.      Mwanamume wa kiislamu asivae mavazi na mapambo ya kike na mwanamke muumini asivae mavazi mavazi na mapambo ya kike na mwanamke muumini asivae mavazi na mapambo ya kiume. Anasema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :

“Mwenyezi Mungu amemlaani mwanamume anayevaa vazi la mwanamke na mwanamke avaaye vazi la mwanamume kama alivyolaani wanamume wenye kujishabihisha na wanawake na wanawake wenye kujishabihisha na wanamume” Muslim.

6.      Aanze kuvaa upande wa kulia wa nguo yake. Kama ni kanzu, shati, koti, gauni au kizibao aanze kuvaa mkono wa kulia. Kama ni suruali basi aanze kuvaa mguu wa kulia. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mama Aysha – Allah amuwie radhi – Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –

 alikuwa akipenda kuanza kulia katika mambo yake yote; katika uvaaji wake wa viatu, uchanaji wake nywele na kujitwahirisha kwake” Bukhariy.

 

7.      Aseme anapovaa nguo mpya : Ewe Mwenyezi Mungu wewe ndio mwenye sifa zote uliyenivisha, nakuomba kheri yake na kheri iliyotengenezewa kwayo, na najilinda na shari yake na shari iliyotengenezewa kwayo.

 

8.      Asivae nguo nyepesi yenye kuonesha ndani rangi ya mwili wake (transparent). Kadhalika asivae nguo yenye kumbana sana kiasi cha kuchora ramani/finyango la mwili wake.

 

ADABU ZA UVAAJI

Muislamu hulichukulia suala la uvaaji kuwa ni miongoni mwa amri za Mola wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu :

“ENYI WANAADAMU! CHUKUENI MAPAMBO YENU (vaeni nguo zenu nzuri) WAKATI WA KILA SWALA; NA KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri). LAKINI MSIPITE KIASI TU. HAKIKA YEYE (Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI” [7:31]

Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa ruhusa waislamu wale, wanywe na wavae vizuri na pia waende msikitini wakiwa wamevaa nguo nzuri. Na amesema tena :

 “ENYI WANADAMU! HAKIKA TUMETEREMSHIENI NGUO ZIFICHAZO TUPU ZENU NA NGUO ZA PAMBO; NA NGUO ZA UTAWA (ucha-mungu) NDIZO BORA …” [7:26]

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *