ATHARI YA VITA VYA BADRI

VITA VYA BADRI VILIIMARISHA NGUVU YA WAISLAMU MADINAH.

Vita vya badri vilileta athari ya kina si tu kwa waislamu bali hata kwa maadui zao; mushrikina, wanafiki na watu wa kitabu (mayahudi na manaswara).

Ushindi wa waislamu katika vita hivi ulivuma na kuacha kishindo kikuu katika pande zote za bara Arabu. Ama kwa janibu (upande) ya waislamu Madinah, vita vya Badri:-

·         Viliimarisha na kuboresha nguvu yao.

·         Vilizidisha yakini yao kwamba Allah yu pamoja nao.

·         Yakini hii ya upamoja na Allah iliwaondolea kabisa khofu ya adui yao na wakawa hawamuogopi ye yote ila Allah pekee.

·         Vilileta faraja na matumaini kwa waislamu wanyonge wanaoteswa Makah na kuiona siku ya ukombozi wao iko karibu mno.

·         Viliiongezea nguvu na ithibati ya imani ya waislamu wote kwa ujumla.

·         Viliwafanya maadui kuingiwa na khofu na uoga juu ya waislamu na kuwaona kuwa si watu wa kunyanyaswa tena.

 

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliufurahia na kuuonea fakhari ushindi huu kuliko maswahaba wake wote.

Ushindi huu ulimfungulia mlango wa matumaini mema ya siku za usoni. Lakini matumaini haya mema ya siku za usoni, hayakumghafilisha kabisa na uhalisia wa mambo ya kwamba amezungukwa na maadui kila upande.

Na kwamba wanamngojelea misiba na majanga yamfike na kuitumia fursa hiyo vema dhidi yake na waislamu wote kwa ujumla.

Wako waliotaka kumuangamiza na kulipa kisasi kama ambavyo walivyokuwepo wanaotaka kuponya chuki binafsi.

Kadhalika walikuwepo waliosukumwa na mifundo ya nyoyo, dhulma na hasadi.

Hayo yote ndiyo yaliyomfanya Bwana Mtume na maswahaba wake kutobweteka na ushindi walioupata. Kinyume chake wakawa katika hali ya tahadhari na utayarifu wa kukabiliana na lo lote linaloweza kutokea.

 

WANAFIKI WALISILIMU KWA ULAGHAI ILI KUJILINDA DHIDI YA WAISLAMU.

Ama mushrikina miongoni mwa watu wa Madinah, wengi wao waliona kwamba Nabii Muhammad na maswahaba wake sasa wamekuwa na nguvu isiyofaa kupuuzwa. Na kwamba mustakbali mwema unaonekana kuwaangukia waislamu, lakini tu hawakuwa na imani ya kudumu kwa ushindi wao wala dhamana ya mustakbali huo mwema.

Wakaanza kuutazama upya msimamo wao chini ya mwangaza wa matukio huku wakijiuliza: Je, waendelee na mila yao ya ushirikina na kuufanyia uadui Uislamu?

 Au wasilimu kama walivyosilimu watu wa Madinah (Answaar), kwa kufanya hivyo watakuwa wamejikinga na uadui (shari) wa dini hii ambayo nyota yake imeanza kuchomoza.

Mushrikina hawa walichelea kuwa wakiundeleza uadui wao dhidi ya waislamu na wakabakia kuwa mushrikina, nguvu ya Uislamu itawapondaponda pindipo ikidhihiri.

 Na wakati huo huo wakawa wanachelea kuwa ushindi huu usije ukawa ni nguvu ya soda tu, kesho waislamu wakaipoteza nguvu hiyo.

Kwa hivyo waislamu wakarejea katika udhaifu na unyonge wao wa mwanzo, na wao wakawa hawakuyapata malengo ya kusilimu kwao.

 Na kusilimu kwao huku kukawazidshia uadui na jirani zao mayahudi na ndugu zao katika imani yao ya kishirikina; makurayshi na makabila mengine ya Waarabu.

Mushrikina wamehemewa, wako njia panda hawajui wafanye nini; wabakie katika ushirikina au wasilimu?

Hatimaye wakafikia uamuzi kwamba njia ya salama zaidi itakayowakinga na uadui wa makundi yale; waislamu na mayahudi ni wao kuwa wanafiki. Huku wako na kule wako:

“…WANAPOKUTANA NA WALIOAMINI HUSEMA: TUMEAMINI, NA WANAPOKUWA PEKE YAO KWA MASHETANI WAO HUSEMA: HAKIKA SISI TU PAMOJA NANYI, TUNAWACHEZA SHERE TU”. [2:14]

Wakiwa pamoja na waislamu hujitia kuwa na wao ni waislamu na hali ya kuwa batini (undani) yao wako pamoja na makafiri.

Kwa mtindo na mchezo huu wakawa wameishika fimbo katikati, haiwezi kuwapiga huku wala kule. Wakawa wanaufuata upepo kule uvumiapo, kwa mbinu yao hii wakasilimu kwa dhahiri na hivyo kupata fursa ya kuingia kundini mwa waislamu.

Na wakakufuru kwa batini yao na wakaendelea kuwa pamoja na makafiri wenzi wao.

Kwa hila na mbinu hii mbaya, wanafiki hawa wakamudu kupata siri nyingi za waislamu na kuwapelekea maadui kila walipopata upenyo. Kiongozi wa kundi hili hatari alikuwa ni Abdullah Ibn Ubayyi Ibn Saluul.

Waislamu wakajikuta wako njia panda katika suala la wanafiki hawa, kwani wao si makafiri dhahiri kwa ukafiri na uadui wao ili waislamu waamiliane nao kwa uadui. Na wala si waislamu wenye ikhlaaswi watakaopata utulivu nao:

“WANAYUMBAYUMBA BAINA YA HUKU (kwa waislamu na huko kwa makafiri). HUKU HAWAKO WALA HUKO HAWAKO…”. [4:143]

Ni kutokana na msimamo wao huu wa khadaa ndipo Allah akawashutumu kwa ukali kabisa katika aya nyingi za Qur-ani Tukufu na kuwakamia kwa adhabu kali kabisa:

“BILA SHAKA WANAFIKI WATAKUWA KATIKA TABAKA YA CHINI KABISA KATIKA MOTO. HUTAMKUTA KWA AJILI YAO MSAIDIZI (yo yote)”. [4:145]

Allah Mola Mjuzi wa dhahiri na siri akaijaalia kwake pekee adhabu ya watu hawa wabaya; wanafiki.

Hii ni kwa sababu ni YEYE ndiye ajuaye siri zao na minong’ono yao na kuzikashifu nia zao chafu na dhahiri yao yenye khadaa.

Chini ya mwavuli wao huu walijificha kiasi cha kumfanya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kutokujua mambo yao mengi, mpaka Allah alipomwambia:

“NA KATIKA MABEDUI WANAOKAA PEMBEZONI MWENU (katika vitongoji vya karibu yenu hapo Madinah) KUNA WANAFIKI. NA KATIKA WENYEJI WA MADINAH (pia kuna wengine wanafiki); WAMEBOBEA KATIKA UNAFIKI (hata) HUWAJUI (kuwa ni wanafiki). SISI TUNAWAJUA TUTAWAADHIBU MARA MBILI, KISHA WATARUDISHWA KATIKA ADHABU KUBWA”. [9:101]

Kwa ujumla wanafiki walikuwa na wanaendelea kuwa maadui wakubwa na wenye khatari na athari mbaya kwa waislamu na Uislamu.

Lengo lao kuu likiwa ni kuutokomeza na kuumaliza kabisa Uislamu na waislamu katika uso wa ardhi. Ili kulitimiza lengo lao hili, walihakikisha kuwa wanaitumia vema kila fursa waliyoipata.

 Wakatumia njia na mbinu adida (mbali mbali), walijitahidi kudhoofisha ari na moyo wa jeshi la Kiislamu kila liingiapo vitani kupambana na makundi mbali mbali ya makafiri.

 Wakifanya kila lililo katika uweza wao kuusambaratisha umoja wa waislamu ili kuipunguza nguvu yao kama si kuivunja kabisa.

Wakajaribu kuuchafua utakatifu na utukufu wa risala/ujumbe wa Allah ili upoteze heshima yake katika nyoyo za waislamu.

Msimamo wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa watu hawa, ulikuwa ni kuikubali dhahiri yao na kuiacha siri yao kwa Allah.

Akiwaonea huruma kutokana na uzito na mzigo lemea wa dhambi wanayoichuma bila ya bughdha wala maudhi yo yote yale.

 

MAYAHUDI WADHIHIRISHA UADUI KWA HASADI NA HUZUNI KUU (YA KUHAMA UTUME KWAO KWENDA KWA WAARABU).

Ushindi wa waislamu uliopelekea kuwa na nguvu kubwa Madinah, haukuwapendeza wala kuwafurahisha mayahudi wa Madinah.

Ushindi huu ulizichanachana nafsi zao kwa uchungu wa kuona sasa Uislamu unapata utukufu na kuhatarisha utukufu wa dini yao kama si kuiua kabisa.

Hili likisadifu kuwa kama wanavyodhani, basi ni dhahiri kuwa cheo na mamlaka yote yatakuwa ni ya Muhammad. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa upande wake, alikuwa na tamaa kubwa ya kukubaliwa na kuaminiwa na mayahudi kuliko mushrikina.

Tamaa hii ya Mtume ilitokana na ukweli kwamba mayahudi ni watu wa dini ambayo inayolingania ‘Tauheed’ kama unavyolingania Uislamu.

Na kwamba wao mayahudi ni watu wa kitabu ambacho Qur-ani inayasadiki mengi ndani ya kitabu hicho. Na ni watu wenye elimu wanaoamini elimu ya kuwaza kwa akili halisi (mantwiqul-ilmi)-(logic) na wanayahukumu mambo kwa kutumia elimu hiyo.

Lakini pupa yao ya utukufu/cheo cha kidini walichokuwa wakikistarehea na kwa ajili ya kulinda maslahi waliyokuwa wakiyapata chini ya mwavuli huu wa kidini.

Wanazuoni wa kiyahudi na viongozi wao wakatoa wito wa kumtia dosari na kumpaka matope Mtume na kuitukana dini ya Allah sambamba na kuupiga vita baridi Uislamu.

Nyoyo za mayahudi zikaendelea kutokota kwa uadui kisirisiri mpaka walipouona Uislamu unachomoza baada ya vita vya Badri.

Hapa sasa hawakujimudu tena, wakaudhihirisha dhahiri ubaya na uadui wao kwa Uislamu na waislamu.

Tangu wakati huo mahusiano ya ujirani mwema baina ya mayahudi na waislamu yakageuka na kuwa uadui wa wazi wazi.

Uadui huu ukipanuka na kuongezeka siku hata siku, mayahudi wakaanza kuufanyia vitimbi na kuulia njama Uislamu. Wakatumia kila njia kuungamiza na kuutokomeza Uislamu.

Uadui wa mwanzo kabisa kujitokeza ni pale walipopapatika na kufadhaika wakati ilipowafikia khabari ya kushindwa makurayshi katika vita vya Badri. Mpaka msemaji wao Ka’abu Ibn Al-Ashraf akafikia kusema:

“Hawa (makurayshi) ndio watukufu wa (makabila yote ya) waarabu na ndio wafalme wa watu. Wallah, ikiwa kweli Muhammad amewashinda watu hawa, basi kwa yakini (mtu kuingia) ndani ya tumbo la ardhi ni bora zaidi kuliko (kubakia) juu ya mgongo wake”.

 Wakauvunja mkataba wa amani walioandikiana na kukubaliana na Mtume tangu alipowasili Madinah.

Washairi wao wakaanza kuwacheza shere waislamu na kuutweza na kuubeza ushindi walioupata waislamu katika vita vya Badri. Wakisema kuwa si ushindi kitu, isitoshe wakawa wanamtaja Mtume wa Allah kwa maneno mabaya na machafu.

 

ATHARI YA VITA VYA BADRI

VITA VYA BADRI VILIIMARISHA NGUVU YA WAISLAMU MADINAH.

Vita vya badri vilileta athari ya kina si tu kwa waislamu bali hata kwa maadui zao; mushrikina, wanafiki na watu wa kitabu (mayahudi na manaswara).

Ushindi wa waislamu katika vita hivi ulivuma na kuacha kishindo kikuu katika pande zote za bara Arabu. Ama kwa janibu (upande) ya waislamu Madinah, vita vya Badri:-

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published.