Vitu vitumikavyo katika twahara ni hivi vinne vifuatavyo:
i.Maji
ii.Mchanga
iii.Dab-ghu na
iv. Mawe.
i/ MAJI: Maji yakiwa miongoni mwa vitu vinne hivi ndiyo yatumikayo sana katika suala zima la twahara.
Maji yanayofaa kutumika katika twahara kwa mtazamo wa fiq-hi hujulikana kama MAJI MUTLAQ ambayo haya yana sifa ya kuwa yenyewe ni twahara na yanaweza kutwaharisha kitu kingine.
Maji haya ni :-
1:MAJI YA MVUA – haya ni yale yateremkayo kutoka mawinguni. Mwenyezi Mungu anatuambia juu ya maji haya:.
“NA TUNAYATEREMSHA KUTOKA MAWINGUNI MAJI SAFI (kabisa) (25:48)
Na akasema tena:
“NA AKAKUTEREMSHIENI MAJI KUTOKA MAWINGUNI ILI KUKUTWAHIRISHENI KWAYO…”(8:11)
2: MAJI YA THELUJI – haya ni yale yateremkayo kutoka mawinguni yakiwa katika hali ya kumiminika kisha yakaganda.
3: MAJI YA UMANDI – haya ni yale yateremkayo kutoka mawinguni yakiwa katika hali ya kuganda kisha yakayeyuka yanapofika ardhini. Mtume anatuambia katika kuonyesha utwahara wa aina hizi za maji:
“Ewe Mola wa haki nikoshe kutokana na makosa yangu kwa theluji, maji na (maji ya) umandi”
4:MAJI YA BAHARI – Yaani maji chumvi
5:MAJI YA MAZIWA NA MITO – Yaani maji tamu yasiyo ya chumvi.
Imepokelewa na Abu- Hurayrah- Allah amridhie- amesema:
Mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu – Allah amrehemu na kumshushia amani – akasema:
Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu sisi tunasafiri, na tunachukua maji kidogo tu, tukiyatumia kutawadhia tutashikwa na kiu, je, tutawadhe kwa maji ya bahari? Mtume akamjibu:
“Hiyo (bahari) ni twahara maji yake, halali mfu wake” Bukhaariy na Muslim.
6:MAJI YA CHEMCHEM:Haya ni yale yachimbukayo yenyewe kutoka ndani ya ardhi bila ya kutumia zana kuyatoa.
7:MAJI YAVISIMA: Hayo ni yale yachimbuliwayo kutoka ardhini.
Aina zote hizi za maji tulizozitaja na ambazo zinazofanana na hizi inafaa kuyatumia katika twahara yakiwa peke yake au yakichanganywa pamoja baina aina moja na nyingine.
ii/ MCHANGA: Mchanga hutumika katika twahara badala ya maji ikiwa mtu amekosa maji au maji yapo lakini hawezi kuyatumia kwa sababu ya maradhi ambayo akitumia maji yatazidi au yatachelewa kupona.
Twahara hii ya kutumia mchanga badala ya maji ndio hujulikana katika sheria kama TAYAMMAMU.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:-
“NA KAMA MKIWA WAGONJWA (mmekatazwa kutumia maji) AU MMO SAFARINI AU MMOJA WENU AMETOKA MSALANI (chooni) AU MMEWAGUSA WANAWAKE NA MSIPATE MAJI BASI UKUSUDIENI (tayamamuni) UDONGO SAFI, MPAKE NYUSO ZENU NA MIKONO YENU…” (4:43)
iii/ DAB-GHU: Dab-ghu ni njia/utaratibu utumikao katika kuitwaharisha ngozi ya mnyama ili iweze kufaa kutumika katika matumizi mbalimbali ya binadamu.
Hutumika vitu vikali kabisa vyenye muonjo wa tindikali kuondoa taka zilizo juu ya ngozi kama vile damu, mafuta na vipande vya nyama vilivyosalia wakati wa kuchuna.
Baada ya hatua zote hizi ndipo ngozi hutiwa maji ikawa ni twahara inayoweza kutumiwa.
iv/ MAWE: Mawe au chochote chenye kufanana na mawe kama vile karatasi (toilet paper), na vinginevyo vinavyoweza kuondosha najisi hutumika katika kuchamba (kustanji) wakati yanapokosekana maji.
Aina hizi za vitu vitumikavyo katika twahara zinaonyesha wepesi wa dini hii ya kiislamu katika kuweka sheria na hukumu zake ambazo zinakwenda sambamba na tabia na mazingira ya mwanadamu.
Haya yanathibitishwa na ruhusa tuliyopewa na sheria ya kujitwaharisha kwa kutumia aina zote za maji tulizozitaja na tukiyakosa maji au yakiwa yanatudhuru tumeruhusiwa kutumia mchanga.