Sharti za kusihi kutayamamu, haya ni mambo ambayo sheria imelazimisha na kuwajibisha yapatikane kwanza kabla mtu hajaanza kutayamamu.
Kusihi kwa tayamamu sambamba na ibada itayofanywa kwa tayamamu hiyo, kutategemea sana upatikanaji wa mambo yafuatayo:
1. Kujua kuingia wakati wa swala anayoitayamamu. Tayamamu hisihi kabla ya kuingia wakati wa swala.
2. Kutafuta maji baada ya kuingia wakati wa swala. Sharti hili ni iwapo anatayamamu kwa sababu ya kukosa maji.
3. Mchanga twahara usio na vumbi la mkaa, unga, (wa nafaka kama vile mahindi) au vumbi la chokaa na kadhalika.
4. Aondoe najisi kabla ya kuanza kutayamamu
5. Ajitahidi kuelekea Qibla kabla ya kuanza kutayamamu.
FAIDA: SHARTI ZA KUWAJIBISHA KUTAYAMAMU
Ili mtu apate ruhusa na kibali cha kutayamamu ni lazima yapatikane mambo/sifa zifuatazo:
1. Uislamu: Tayamamu ni sheria inayomuhusu muislamu peke yake. Kwa mantiki hii asiye muislamu hana tayamamu.
2. Baleghe: Hana tayamamu na wala haisihi kwa mtoto mdogo.
3. akili timamu: hana tayamamu mwendawazimu kwa sababu ya kutokulitambua alitendalo, jambo ambalo ni sharti kubwa katika kusihi na kukubalika utendaji na utekelezaji wa ihada zote za mja katika uislamu.