KULINGANIA DINI KWA UFICHO

Baada ya kukatika mawasiliano baina ya mbinguni na ardhini kwa kipindi kirefu, kiasi cha kumfanya Bwana Mtume kuwa na wasiwasi wa kutopata tena mawasiliano hayo.

Ni katika kipindi hiki ndipo Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie- wakati akitembea mjini Makkah aliposikia sauti ikimwita kwa jina lake na kumsemesha.

Nabii Muhammad akainua macho yake itokeyako sauti ile, mara tahamaki akamuona yule malaika aliyemjia kule katika pango la Hiraa akiwa amekaa angani baina ya mbingu na ardhi.

 Mtume akaogopa sana kwa kukumbuka yale aliyomfanyia kule katika pango la Hiraa, hivyo akarejea haraka nyumbani kwake huku akitetemeka na kumwambia mkewe :

Nifunikeni, nifunikeni. Bwana Mtume akiwa amelala kitandani huku amejifunika gubigubi, Mwenyezi Mungu akamletea wahyi/ufunuo :

“EWE ULIYEJIFUNIKA MAGUO. SIMAMA UONYE (viumbe)” Yaani watahadhirishe watu kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa hawatoacha upotevu na itikadi potofu waliyoirithi kutoka kwa wahenga wao.

 “NA MOLA WAKO UMTUKUZE” Yaani yeye tu umtukuze na wala usimshirikishe na yeyote. “NA NGUO ZAKO UZISAFISHE” Yaani uwe umejiandaa kusimama mbele ya Mola wako, kwa sababu muumini wa kweli hawi mchafu mwenye najisi.

NA MABAYA YAPUUZE” Yaani yaepuke mambo yatakayokupelekea kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu, yaepuke kwa kumtii na kutekeleza amri zake.

NA WALA USIWAFANYIE IHSANI (viumbe) ILI UPATE KUJIKITHRISHA (wewe hapa duniani). NA KWA AJILI YA MOLA WAKO FANYA SUBIRA (kwa kila yatakayokufika)” Yaani kero na maudhi yatakayokusibu kutoka kwa jamaa zako wakati utakapowalingania kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja asiye na mshirika. [74:1-7]

Naam, Wahyi/ufunuo aliokuwa akiusubiri kwa muda mkubwa na kwa kiu kubwa ndio huu umemjia tena Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie-.

Wahyi huu unamkabidhi rasmi Nabii Muhammad jukumu na kazi nzito ya kuwalingania jamaa zake na watu wote kwa ujumla kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada.

Kazi ya kuwahamisha watu kutoka katika itikadi potofu ya ushirikina, kuwaleta kwenye nuru ya TAUHIID.

Jukumu la kuwatoa watu katika tabia na desturi mbaya zilizojaa unyama kuwaleta katika tabia murua zilizosheheni utu na ubinadamu kamili.

Mwenyezi Mungu Mtukufu akamfamisha Mtume wake tangu mapema asubuhi, kuwa kazi na jukumu alilopewa ni zito na gumu na ajiandae kukabiliana na upinzani mkali, uadui na maudhi yasiyo kifani kutoka kwa jamaa zake.

Bwana Mtume akakaa chini, akiwaza na kufikiri jinsi atakavyoitekeleza amri hii ya Mola wake, huku akitambua fika kwamba kuangamia au kuokoka kwa watu wote kunategemea sana ufanisi wake katika kazi hii ya uchungaji.

Atumie mbinu gani mpaka awakinaishe jamaa zake kuwa itikadi waliyonayo ni potofu isiyofaa na itawasababishia kupata adhabu kali ya Mwenyezi Mungu ?

Atawathibitishia vipi kwamba itikadi hii anayowaletea ndiyo itikadi sahihi itakayowaokoa na adhabu ya Mola wao ?

Je itamkinika kuwakinaisha Makurayshi kuwa miungu yao ya masanamu haidhuru na wala hainufaishi ?

Vipi hili litawezekana na il-hali wao wamezaliwa na kukulia katika itikadi hii ya kuyaabudia masanamu haya na kuyategemea katika maisha yao yote na isitoshe hii ndio dini waliyorithi kutoka kwa wahenga wao.

Je maqurayshi wataweza kuamini kuwa baada ya maisha haya ya muda mfupi ya duniani kuna maisha ya milele ya akhera, ambako huko kutakuwa na kuhisabiwa na kulipwa kila binadamu kwa mujibu wa matendo yake aliyoyatenda hapa duniani ?

 Haya ni baadhi tu ya maswali yaliyokuwa yakiisumbua na kuitesa akili ya Bwana Mtume.

Ni kupitia maswali haya yasiyojibika kirahisi, ndipo Bwana Mtume akapanga mikakati imara na madhubuti ili kuhakikisha kuwa anaitekeleza kwa ufanisi mkubwa kazi aliyopewa na Mola wake.

Kwa kuzingatia kuwa jambo hili analowaletea watu ni jambo geni masikioni mwao, Bwana Mtume akaonelea ni vema aianze kazi hii kwa kulingania watu kwa uficho.

Akaanza kumuendea kila aliyekuwa akimuamini na kumuona kuwa ana busara za kuweza kuelewa ujumbe atakaompelekea miongoni mwa ndugu, jamaa na rafiki zake.

 Kuianza kazi hii kwa kuwalingania jamaa zake, hakumaanishi kuwa Nabii Muhammad aliwapa upendeleo maalum jamaa zake, bali hili linatokana na amri ya Mwenyezi Mungu alipomwambia:

 “NA UWAONYE JAMAA ZAKO WALIO KARIBU (nawe)” [26:215]

Nini falsafa na hekima hii ya amri ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake, amri ambayo inamtaka kabla hajaufikisha ujumbe wake kwa watu wote, aanze kuufikisha kwanza kwa jamaa zake tena wale wa karibu ?

Hii ni kwa sababu ili mtu aweze kukubaliwa na jamii nzima ni lazima kwanza akubalike na familia na jamaa zake mwenyewe, Ikiwa mtu/kiongozi anakataliwa na jamaa zake mwenyewe ambao ndio watu wa mwanzo kumjua, vipi unatazamia akubaliwe na jamii isiyomjua ?!

Bila shaka watu watasema : Ndugu zake mwenyewe hawamtaki, tumkubali sisi ? Bila shaka atakuwa na matatizo, kwa nini akataliwe na jamaa zake?

Nabii Muhammad akaandaa hafla na kuwaalika jamaa zake katika karamu.

Kutokana na sifa alizojijengea kwa jamaa zake bali kwa jamii nzima, wito wake uliitikiwa kwa nguvu kubwa.

Wakiwa wanaendelea kula walichoandaliwa, Bwana Mtume akaitumia fursa hii kuwafikishia ujumbe wa Mola wake na kuwaambia :

“Shukrani zote njema zinamstahiki Allah, ninamshukuru na kumuomba msaada na ninamuamini yeye pekee na ninamtegemea kwa kila jambo langu. Ninashuhudia kuwa hapa Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH peke yake asiye na mshirika. Amma baad, bila shaka mchungaji huwa hawaongopei jamaa zake, Lau mimi nitajasiri kuwaongopea watu wote, sitathubutu kukuongopeeni nyinyi. Ninaapa kwa ALLAH ambaye hakuna Mola wa haki ila YEYE, hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyie khasa na kwa watu wote kwa ujumla. Na Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikulinganieni kumpwekesha yeye, akaniambia “NA UWAONYE JAMAA ZAKO WALIO KARIBU (nawe)” kwa hiyo mimi ninakutakeni mseme maneno mawili tu yaliyo mepesi ulimini lakini mazito sana katika mizani ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama.

Shuhudieni kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH (neno la kwanza) na kwamba mimi ni Mtume wa ALLAH (neno la pili).

Wallah mtakufa kama mlalavyo na mtafufuliwa kama muamkavyo, na mtahisabiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa yote muyatendayo hapa duniani.

Mtalipwa wema kwa wema na uovu kwa uovu na huko pepo ya daima au moto wa milele. Enyi watoto wa Abdul-Mutwalib.

 Wallah simjui kijana aliyewaletea jamaa zake jambo zuri kuliko hili nilikoluteneeni mimi, mimi nimekuleteeni kheri za dunia na akhera.

Basi ni nani atakayeniitika katika jambo hili na kuniunga katika kulisimamia ?”

Hivi ndivyo Nabii Muhammad alivyoanza kulitekeleza jukumu alilopewa na Mola wake.

 

KULINGANIA DINI KWA UFICHO

Baada ya kukatika mawasiliano baina ya mbinguni na ardhini kwa kipindi kirefu, kiasi cha kumfanya Bwana Mtume kuwa na wasiwasi wa kutopata tena mawasiliano hayo.

Ni katika kipindi hiki ndipo Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie- wakati akitembea mjini Makkah aliposikia sauti ikimwita kwa jina lake na kumsemesha.

Nabii Muhammad akainua macho yake itokeyako sauti ile, mara tahamaki akamuona yule malaika aliyemjia kule katika pango la Hiraa akiwa amekaa angani baina ya mbingu na ardhi.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *