MAFUNZO YA JUU WANAYOPATA WAISLAMU KUTOKA VITA VYA UHUD

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika vita hivi aliwapatia maswahaba wake bali uma mzima wa kiislamu masomo ya juu kabisa katika nyanja za:-

ü      Kuheshimu shura (ushauri na maoni ya uma).

ü      Kuwa na azma ya kweli.

ü      Kuwa na moyo thabiti, na

ü      Kustahamili maudhi na kumsamehe mkosaji.

Imekwishafahamika huko nyuma kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka kwenda katika vita hivi bila ya khiari yake, alilazimishwa.

Lakini Bwana Mtume alilazimika kutoka wakati ambapo alikuwa na mamlaka ya kupinga kwa ajili ya kuchunga na kuheshimu shura ya maswahaba wake.

Na pale maswahaba wake walipohisi kuwa wamemshurutisha walitaka kuwafikiana na rai yake ya kutokwenda vitani. Bwana Mtume akakataa kubadilisha uamuzi wa kutoka uliofikiwa na wengi baada ya kuwa amekwishafunga azma hiyo ya kutoka.

Na katika kule kuthibiti kwake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-mbele ya adui katika wakati huu wa chinjachinja na uaua.

Na katika kupambana kwake na adui katika wakati ambao waislamu waliomzunguka wanakimbia kuziokoa nafsi zao na mauti. Katika kipindi ambacho anapaaza sauti yake kuwaita waislamu wanaokimbia warudi kuthibiti pamoja nae.

Akiwashajiisha na kuzitia nguvu nyoyo zao, nao kutokana na mshindo mkuu uliowapata hawasikii na wala hawaoni.

Na katika kule kujizatiti kwake na ilhali khatari imemzunguka kila upande, hana makimbilio hata finyu, maadui wamemkusanyikia na kumzonga wakiwa na dhamira na lengo moja tu.

Nalo ni kuponya chuki zao kwa kumuua. Kwa yakini mna ndani ya yote haya kila dalili juu ya upeo wa ushujaa wa moyo aliopewa Bwana Mtume na Allah Bwana Mlezi wake.

Mna maono na ufanyajikazi haraka wa akili na nguvu ya yakini kwa Allah Mshindi Mtukuka.

Na hakika katika sura na picha hii ambayo Qur-ani imemchora Mtume na waislamu (maswahaba wake) na miongoni mwao wakiwemo mashujaa, mabwana wakubwa na mabwana wa vita. Wote hawa wakiwa katika mfadhaiko wao na kushindwa kukabiliana na hali iliyowakumba, wakikimbia mbio hawasikilizi lo lote.

Wao wakiwa katika  hali hiyo, Bwana Mtume akiwa katika uthabiti na yakini yake akiwaitia akhera yao na akiwaogofyesha na kukimbia kwao.

Hakika katika hili mna tofauti ya upeo wa mbali kabisa baina ya ushujaa wa maswahaba ukiulinganisha na ule wa Mtume wa Allah.

Na baina ya nguvu ya maswahaba ukiipima na ile ya Bwana Mtume na baina ya yakini ya maswahaba kwa Allah ukiimithilisha na ile ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Pamoja na yote yaliyomsibu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-miongoni mwa majeraha na maumivu kwa sababu ya kukimbiwa na waislamu na kumuacha akipambana peke yake na waislamu wachache tu.

Bwana Mtume hakumkaripia wala kumlaumu ye yote miongoni mwao kama ambavyo angelifanya ye yote miongoni mwetu sisi kama angekuwa katika nafasi yake.

Na pengine asingekomelea kukaripia na kulaumu tu, bali angeliadhibu vikali kabisa. Lakini je, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alifanya nini?

Hakufanya kingine cho chote zaidi ya kuwasamehe kutokana na uzembe na udhaifu wao wa kiimani waliouonyesha. Na isitoshe akawa anawaliwaza na kuziunganisha na kuzifungamanisha pamoja azma zao, akiwaambia:

“Hawatoweza kamwe kututia madhara kama haya tena mpaka tulishike hajarul-aswad”.

 Na Allah Mtukufu anamsifia Mtume wake kwa hilo pale aliposema:

“ BASI KWA SABABU YA REHEMA ITOKAYO KWA ALLAH UMEKUWA LAINI KWAO (ewe Muhammad). NA KAMA UNGEKUWA MKALI NA MWENYE MOYO MGUMU BILA SHAKA WANGALIKUKIMBIA. BASI WASAMEHE WEWE NA UWAOMBEE MSAMAHA (kwa Allah) NA USHAURIANE NAO KATIKA MAMBO…” [3:159]

 

VITA HIVI VILIKUWA NI JARIBIO GUMU LILILOTOA MAFUNZO MENGI YENYE MANUFAA MAKUBWA KWA UMA MZIMA WA KIISLAMU.

Naam, ni kweli kabisa kwamba vita hivi vilikuwa ni jaribio gumu na zito kwa waislamu. Na bila shaka vilikuwa ni mtihani wenye mshindo mkuu uliozifichua siri za nyoyo na unafiki ukapambanuka na imani.

Wakatambulika wale ambao walioipiga teke dunia  na wala hawavutwi na tamaa za kidunia na wale walioielekea dunia na tamaa zao mbaya zikaanzisha kutokana na cheche ndogo moto mkubwa (maafa) wa kutisha.

Allah Taala anabainisha sababu ya kuwapa waislamu mtihani huu mgumu:

“NA MSIBA ULIOKUFIKENI SIKU YA MKUTANO WA MAJESHI MAWILI (la waislamu na makafiri) ULIKUWA KWA IDHINI YA ALLAH, NA KUWAPAMBANUA WALIOAMINI. NA KUWAPAMBANUA WALE WALIOKUWA WANAFIKI. NAO WALIAMBIWA: NJOONI MPIGANE KATIKA NJIA YA ALLAH AU MZUIE (maadui pamoja na sisi). WAKASEMA: TUNGEJUA KUWA KUNA KUPIGANA BILA SHAKA TUNGELIKUFUATENI. WAO SIKU ILE WALIKUWA KARIBU NA UKAFIRI KULIKO NA UISLAMU (japokuwa siku zote wakidhihirisha Uislamu wa uwongo). WANASEMA KWA MIDOMO YAO YASIYOKUWA NYOYONI MWAO. NA ALLAH ANAJUA VYEMA (yote) WANAYOYAFICHA” [3:166-167]

Waislamu kwa upande mwingine walifaidika sana na vita hivi kutokana na masomo/mafunzo waliyoyapata, mafunzo ambayo yalikuwa ni dira na sukani ya maisha yao yote baada ya vita hivi.

Wakatambua maeneo ya udhaifu wao na nguvu zao na wakajifunza kwa  vitendo anavyotakiwa kuwa mpiganaji katika njia ya Allah. Ya kwamba:-

ü      Awe na imani ya kweli kuielekea akida (itikadi) anayoiamini na afanye matendo yake yote kwa ajili ya Allah pekee bila ya kuchanganya na tamaa za kidunia.

ü      Awe na ustahamilivu na uthabiti wakati apambanapo na adui na kutokuonyesha udhaifu na kukata tamaa ya kupata nusra wakati vita vinapopamba moto.

ü      Amuelekee Allah pekee na kumtegemea katika kupata msaada, nguvu na nusra.

Na Allah Taala amewapigia mithali aina hii ya Mujahidina wa kweli katika kauli yake:

“NA MANABII WANGAPI WALIPIGANA NA MAADUI, NA PAMOJA NAO KULIKUWA NA WATAKATIFU WENGI. HAWAKULEGEA KWA YALE YALIYOWASIBU KATIKA NJIA YA ALLAH, WALA HAWAKUDHOOFIKA WALA HAWAKUDHALILIKA. NA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO SUBIRA. WALA HAIKUWA KAULI YAO (watakatifu hao) ILA NI KUSEMA: MOLA WETU! TUGHUFIRIE MADHAMBI YETU NA ITHIBITISHE MIGUU YETU NA UTUSAIDIE JUU YA WATU MAKAFIRI. ALLAH AKAWAPA MALIPO YA DUNIA NA MALIPO MAZURI YA AKHERA, NA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO MEMA”. [3:146-148]  

 

AYA ZA QUR-ANI ZILIZOSHUKA KATIKA VITA VYA UHUD ZILIKUWA NI FARAJA NA FUNDISHO KWA WAUMINI.

Kama ambavyo Allah Mtukufu alivyoteremsha Suratil-Anfaal (9) katika kadhia ya vita vya Badri, akiwafundisha waislamu ndani yake misingi ya vita na adabu (taratibu) zake.

Na yawapasayo wakati wa kukutana na adui miongoni mwa uthabiti, uvumilivu na kukithirisha kumdhukuru Allah na kumtii Mtume wake.

Na wanayotakiwa kutahadhari nayo miongoni mwa kugombana, kutofautina, kufanyiana khiana, udanganyifu na kukimbia vitani.

Ndivyo hivyo hivyo Allah akashusha katika kadhia hii ya vita vya Uhud kadiri ya aya sitini katika Surat Aali Imraan (3).

Akawabainishia waumini ndani yake makosa yao katika kuitekeleza kivitendo ile misingi aliyowafundisha katika vita vya Badri. 

Na akawaonyesha natija ya makosa yao hayo muono wa macho, lakini hakuwaacha katika msiba wa kukata tamaa. Msiba ambao huziua nyoyo na kulegeza hamasa, bali akazipangusa na kuzifuta huzuni zao kwa upole na rehema.

Na akazichanganya zile lawama nyepesi na darasa lenye manufaa. Na akawabainishia kwamba kushindwa hakulichafui lile lengo wanalopigana kwa ajili yake wala utukufu wa misingi wanayoilinda na kuitetea.

Na hakukuwa kushinda na kushindwa ila ni vizuka viwili wanavyobadilishana na kupokezana watu; akishinda huyu leo huwa ameshindwa mwingine ambaye kesho anaweza kuwa mshindi vile vile. Na ni katika jumla ya kawaida (kanuni) miongoni mwa kawaida za Allah kwa viumbe wake.

Kisha akawabainishia kwamba kushindwa huku hakukuwa ni shari iliyolengwa kwao, bali kulikuwa ni mtihani.

Mtihani ambao Allah alitaka kuwadhihirishia kupitia mtihani huo waumini wakweli na kuwafichua wanafiki wafanyao khadaa.

Kwa hiyo basi, wale mashahidi (waliokufa kwa ajili ya Allah) ndio chaguo halisi alichagualo Allah miongoni mwa wenye kuipigania dini yake ili alienezee fadhila zake:

“NA MSILEGEE WALA MSIHUZUNIKE, MAANA NYINYI NDIO MTAKAOKUWA JUU IKIWA MNAAMINI KWELI. KAMA YAMEKUPATENI MAJARAHA, BASI NA WATU HAO YAMEWAPATA MAJARAHA KAMA HAYA. NA SIKU ZA NAMNA HII TUNAWALETEA WATU KWA ZAMU. (Amefanya haya) ILI ALLAH APAMBANUE WALIOAMINI (kweli, kwa hivyo hawakukimbia) NA AFANYE MIONGONI MWENU MASHAHIDI (waliouawa katika hivyo vita wapate daraja ya ushahidi). NA ALLAH HAWAPENDI MADHALIMU. NA ILI ALLAH AWASAFISHE WALIOAMINI NA KUWAFUTA (waondoke ulimwenguni wale) WALIOKUFURU. JE! MNADHANI MTAINGIA PEPONI, HALI ALLAH HAJAWAPAMBANUA WALE WALIOIPIGANIA DINI YA ALLAH MIONGONI MWENU NA KUWAPAMBANUA WALIOFANYA SUBIRA? (sharti yaonekane kwanza haya hapa ulimwenguni). NA NYINYI MLIKUWA MKITAMANI MAUTI (kuwa shahidi), KABLA HAMJAKUTANA NAYO. BASI MMEKWISHAYAONA NA HUKU MNAYATAZAMA”. [3:139-143]

Hivi ndivyo Allah Taala alivyokuwa akiwaliwaza waumini  katika mtihani wao huu mgumu na kuwafariji katika msiba huu mkuu uliowasibu.

Na akiwavumbulia pande za mazingatio katika matukio na msimamo wa vita hivi. Na akiwatahadharisha kutokuusalimisha uongozi wao kwa makafiri na wanafiki au kusikiliza uvumi uenezwao na makafiri juu ya mashahidi waliouawa katika njia ya Allah.

Kwani yawatoshea mashahidi kile alichowaandalia Allah; yaani thawabu maridhawa kabisa:

“NA KAMA MKIUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH AU MKIFA (si khasara kwenu) KWANI MSAMAHA NA REHEMA ZINAZOTOKA KWA ALLAH (kukujieni) NI BORA KULIKO VILE WANAVYOKUSANYA (hapa ulimwenguni). NA KAMA MKIFA AU MKIUAWA (ni sawasawa). (Nyote) MTAKUSANYWA KWA ALLAH”. [3:157-158]

 

MAFUNZO YA JUU WANAYOPATA WAISLAMU KUTOKA VITA VYA UHUD

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika vita hivi aliwapatia maswahaba wake bali uma mzima wa kiislamu masomo ya juu kabisa katika nyanja za:-

ü      Kuheshimu shura (ushauri na maoni ya uma).

ü      Kuwa na azma ya kweli.

ü      Kuwa na moyo thabiti, na

ü      Kustahamili maudhi na kumsamehe mkosaji.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *