KABILA LA KHUZAA LILITOA MCHANGO MKUBWA SANA KATIKA KUWAKATISHA TAMAA MAKURAYSHI

Katika jumla ya misaada ambayo Allah aliwapa waislamu ni kwamba kabila la “Khuzaah” lilikuwa limeandikiana mkataba wa amani na ushirikiano na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Ma’abad Mkhuzai alimpitia Bwana Mtume na kumwambia:

“Ewe Muhammad, hakika yametuhuzunisha mno yaliyokusibu wewe na maswahaba wako, tungelipendelea kwamba Allah angelikitukuza cheo chako na kwamba msiba huo ungeliwasibu mahasimu wako!”

Alipokwishaliwakilisha kabila lake katika kuelezea huzuni na masikitiko yao juu ya janga lililowapata waislamu; washirika wao. Alishika njia akaenda zake mpaka akakutana na Abuu Sufyaan akiwa pamoja na makurayshi pande za “Rauhaa”.

Hili ni eneo lililo baina ya Makkah na Madinah, liko kiasi cha umbali wa maili thelathini na sita (36) kutokea mjini Madinah.

Aliwakuta wakitupiana lawama na kujuta kwa nini hawakufyekelea mbali Bwana Mtume na maswahaba wake, wakafikia kuambizana:

“Hamkufanya lo lote, mmeupata mzizi wa watu wale (waislamu) kisha mkawaachia waende zao hivi hivi tu na wala msiukatilie mbali! Haya sasa wamebakia viongozi wao wanajikusanya kuja kupigana nanyi. Hamkumuua Muhammad na wala hamkuwachukua wanawake mateka, eeh ubaya ulioje wa mliyoyafanya!”

Baada ya kulaumiana na kushutumiana vikali kabisa wakakongamana kwa kauli moja kurejea tena Uhud kwenda kuwasagasaga waislamu waliobakia ili kuukata kabisa mzizi wa fitina.

Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema:

“Abuu Sufyaan alipomuona Ma’abad akamuuliza: Kuna khabari gani huko utokako ewe Ma’abad? Akamjibu: Khabari zilizopo ni kwamba tayari Muhammad amekwisha toka na maswahaba wake kukufuatieni katika kundi ambalo katu sijapatapo kuuona mfano wake. Wanajihisi kuungua nyoyo zao kwa shauku ya kukutana nanyi, tena wamejiunga nae wale wote waliobakia nyuma katika siku yenu (ya jana mliyowashinda) ilhali wanajuta kwa kitendo walichokifanya. Wana hasira na ghadhabu kali juu yenu sijapatapo kamwe kuuona mshabaha wake. Akasema Abuu Sufyaan: Eeh ole wako wee, unasemaje? Akasema (Ma’abad): Wallah, mimi sioni kama mtaanza kwenda zenuni kabla hamjaziona tosi za ngamia wao. Akasema (Abuu Sufyaan): Sisi tumepitisha  azimio la pamoja kufanya hujuma kali ya kuwamaliza kabisa waliobakia (jana). Akasema (Ma’abad): Kwa hakika mimi ninakuonya juu ya azimio lenu hilo. Hapo ndipo Abuu Sufyaan na watu wake wakanyong’onyea na kuishiwa nguvu”. Mwisho wa kunukuu.

Abuu Sufyaan akabadilisha mawazo, sasa badala ya kwenda kutoa pigo la kuwafagia waislamu, akatishika asijefikwa na yale ya mtu apambanaye na chui mjeruhiwa.

Badala yake akaamua kuchukua hatua mbadala, nayo ni kuwatisha waislamu na kuwakatisha tamaa kuwa hawana ubavu wa kuhimili nguvu na ukali wa jeshi lake.

Na kwamba uamuzi wa busara kwao ni kukubali kushindwa na kurudi Madinah kukusanya nguvu mpya.

Akaitumia vema fursa ya msafara wa biashara uliopita mahala walipopiga kambi ukielekea Madinah.

Akawaagiza wafanyabiashara hao wamzuie Muhammad asije na wamkhofishe dhidi ya shambulizi la kufagia na hujuma za nguvu za makurayshi dhidi yao na akawaahidi ujira kwa kuitekeleza na kuifanikisha kazi yake hiyo.

Msafara huu wa biashara ulipompitia Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-pale Hamraaul-Asad, wakamueleza yale waliyoagizwa na Abuu Sufyaan kama propaganda za kumtisha na kumvunja nguvu.

Lakini Mtume wa Allah hakuathiriwa hata kidogo na vitisho hivyo vya wafanyabiashara na akasema: “Allah anatutosha, nae ni Mlinzi bora kabisa”. Allah Taala ametusajilia tukio hili ndani ya Qur-ani ili tuwaidhike:

“WALE AMBAO WATU (waliokodiwa na Makurayshi) WALIWAAMBIA (waislamu): WATU (yaani Makurayshi) WAMEKUKU SANYIKIENI, KWA HIVYO WAOGOPENI. LAKINI (maneno hayo) YAKAWAZIDISHIA IMANI (waislamu), WAKASEMA: ALLAH ANATUTOSHA (atatukifia), NAYE NI MLINZI BORA KABISA”.[3:173]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake-Allah awaridhie-waliendelea kubakia katika kambi yao hapo Rauhaa kwa muda wa siku tatu.

Mpaka walipojua kwamba makurayshi wameondoka kuelekea Makah ndipo nao wakaamua kurudi na kuingia Madinah kwa heshima.

Wakati wa kurudi kwake, njiani Bwana Mtume alikwaana (alikutana ghafla) na Abuu Azzah Al-Jumahiy, yule mshairi aliyeivunja ahadi yake aliyoichukua kwa Mtume wa Allah. Bwana Mtume akamuweka katikati ya maswahaba, akasema khaini huyu: Ewe Mtume wa Allah! Nisamehe. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia:

Wallah, baada ya leo hutazipangusa sharafa zako mara mbili! Muumini hagongwi na nyoka mara mbili!” Kisha Bwana Mtume akaamrisha auawe kwa kukatwa shingo yake.

 

IV/. MAKABILA MENGI YALIJIKUSANYA ILI KUWASHAMBULIA WAISLAMU, BWANA MTUME AKAWA ANAWASAMBARATISHA KWA MASHAMBULIZI YA KUSHTUKIZA.

Hatua za haraka na za makusudi zilizochukuliwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa lengo la kuzima athari za Uhud.

Hazikuweza kufuta athari hizo  kwa asilimia mia moja, kwani makabila mengi yalianza kujikusanya dhidi ya waislamu.

Mabedui waliokuwa wakiishi kuzunguka mji wa Madinah walidhania kwamba sasa wanaweza kabisa kuushambulia na kuuteka mji wa Madinah bila ya upinzani wa haja kutoka kwa waislamu.

Iliwasawirikia akilini mwao kwamba baada ya kushindwa huko Uhud, waislamu sasa hawana tena uwezo  wa kujilinda dhidi ya mahasimu wao. 

Kabila la mwanzo kujikusanya kwa lengo la kuwashambulia waislamu, lilikuwa ni kabila la Baniy Asad.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoitambua azma yao hiyo ya kuishambulia Madinah, alifanya haraka kuwavamia kabla hawajajiandaa vema.

Akawapelekea Abuu Salamah akikiongoza kikosi cha maswahaba wapatao mia moja na khamsini.

Wakawashambulia kwa mbinu ya kushtukiza na wakafanikiwa kuwasambaratisha kwa kuwa walikuwa hawajajiandaa na wala hawakutarajia kabisa kushambuliwa na waislamu.

Waislamu wakawaswaga wanyama wao ngawira, kisha wakarudi Madinah baada ya kutekeleza jukumu la kujilinda walilopewa na Amirijeshi mkuu na kamanda mahiri; Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Wakarudi Madinah na ilhali hapana hata mmoja wao aliyejeruhiwa hata ukucha ila amiri wao; Abuu Salamah alitonesha jeraha lake lililompata Uhud.

Abuu Salamah hakukaa muda mrefu akaaga dunia kutokana na jeraha hilo-Allah amuwiye radhi. Baada ya tukio hili, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaletewa khabari kwamba Khalid Ibn Sufyaan Al-Hadhaliy anakusanya jeshi kuja kushambulia Madinah.

Bwana Mtume akamteua Abdullah Ibn Unays miongoni mwa maswahaba wake kwenda kumshughulikia muovu huyu.

Akamuendea kwa uficho katika sura ya mtu anayetaka kuungana nae katika kumpiga Muhammad.

Hata alipokwishayakinisha kwamba ni kweli anakusanya jeshi dhidi ya Mtume wa Allah. Akaanza kumperemba kidogo kidogo mpaka akafanikiwa kumuua na kuliacha jeshi aliloanza kulikusanya likiwa halina tena kamanda wa kuliongoza.

Kitendo hiki cha kuuawa kwa kiongozi wao kililifanya jeshi kusambaratika kwa khofu na kuwafanya waislamu kuepuka shari lao.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *