SWALA YA JAMAA

I.      MAANA YA SWALA YA JAMAA:

Muradi na mapendeleo ya swala ya jamaa ni ile swala ya fardhi au ya suna iliyosuniwa kuswaliwa jamaa. Inayoswaliwa kwa pamoja na zaidi ya mtu mmoja ndani ya msikiti au nje ya msikiti. Hii ndio swala ya jamaa tutakayohusika nayo katika somo hili.

 

  II.      HISTORIA FUPI YA SWALA YA JAMAA:

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alianza kusimamisha swala ya jamaa Madinah baada ya Hijrah. Katika kipindi chote cha utume alichokaa Makah, kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu hakupata kuswali jamaa.

Hili lilitokana na unyonge waliokuwa nao maswahaba wakati huo na hivyo kusababisha kila mmoja wao kuswali pekee nyumbani kwake. Mtume alipohamia Madinah na Uislamu ukawa na nguvu ndipo swala ya jamaa ikaanza na akaidumisha mpaka anaondoka duniani.

 

 III.      HUKUMU YA SWALA YA JAMAA:

Ilivyo sahihi ni kwamba jamaa isiyokuwa ya swala ya Ijumaa ni FARDHI KIFAAYAH. Hauwapomokei/hauwaondokei ufaradhi wake watu wa mji ila pale mahala ambapo inapodhihiri nembo/alama yake.

Iwapo swala ya jamaa haikuswaliwa kabisa katika mji au ikaswaliwa kwa uficho, watu wote wa mji husika watapata dhambi na kutamuwajibikia Imamu (kiongozi) kuwapiga vita mpaka waisimamishe jamaa.

Asili na chimbuko la swala hii ya jamaa ni kauli yake Allah Mola Mtukufu:

“NA UNAPOKUWA PAMOJA NAO (waislamu katika vita) UKAWASWALISHA (jamaa), BASI KUNDI MOJA MIONGONI MWAO WASIMAME PAMOJA NAWE (waswali)…”. [4:102]

 

 IV.      FADHILA/UBORA WA JAMAA:

Swala ya jamaa ina fadhila kubwa na ujira adhimu. Zimepokewa hadithi nyingi sahihi katika kutaja na kueleza fadhila na ubora wa swala ya jamaa.

Mbali na kutaja fadhila za jamaa, hadithi hizo kwa upande mwingine pia ni ushahidi wa swala ya jamaa. Miongoni mwa hadithi hizo ni hizi zifuatazo, amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:-

1)    “Swala ya jamaa inaizidi swala ya mtu pweke (munfaridi) kwa daraja ishirini na saba”. Bukhaariy & Muslim

2)    “Hapana watu watatu kijijini au kitongojini haisimamishwi miongoni mwao swala ya jamaa ila shetani huwatawala na kuwageuzia kwake. Hakika si vinginevyo mbwa mwitu humla kondoo aliye mbali na kundi”. Abuu Daawoud & Ibn hibbaan.

3)    “Ninamuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, kwa yakini niliazimia kuamrisha zikusanywe kuni, kisha niamrishe swala iadhiniwe. Halafu nimuamrishe mtu awaswalishe watu, kisha mimi niwaendee watu wasiohudhuria swala ya jamaa nikawachomee nyumba zao”. Bukhaariy & Muslim

 

 V.      FALSAFA/HEKIMA YA SWALA YA JAMAA:

Hakika si vinginevyo nguzo hii ya Uislamu husimama juu ya msingi wa kufahamiana waislamu na kuwa ndugu wenye kusaidiana katika kuithubutisha haki na kuiondosha batili.

 Kufahamiana na kuunga udugu huku hakutimii katika kumbi zilizo bora zaidi kuliko kumbi za misikiti ambamo waislamu hukutana humo mara tano kila siku kwa ajili ya kutekeleza fardhi ya swala.

Misikitini ndimo mahala ambamo tofauti za watu kimaslahi, chuki binafsi na mifundo huondoshwa  kutokana na  kukutana kwao mara tano kila siku katika swala ya jamaa.

 

  VI.      UCHACHE WA JAMAA:

Jamaa hufungamana kwa watu wawili; imamu na maamuma na kuendelea. Hivyo ndivyo ilivyokuja katika hadithi kadhaa za Bwana Mtume. Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Watu wawili na kuendelea ni jamaa hiyo”. Katika hadithi nyingine Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia Maalik Ibn al-Huwayrith na mwenziwe:

“Na aadhini mmoja wenu (wawili nyie) na akuswalisheni aliye mkubwa kati yenu”.

Imepokelewa na Abuu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-kwamba mtu mmoja aliingia msikitini wakati ambapo tayari Mtume alikuwa ameshawaswalisha maswahaba wake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:

“Nani atampa sadaka huyu, akaswali pamoja nae? Akasimama mtu mmoja akaswali pamoja nae (jamaa)”. Ahmad, Abuu Daawoud & Tirmidhiy

Na kila idadi ya watu inapozidi ndio hupendeza zaidi kwa Allah, haya ni kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:

“Swala ya mtu pamoja na mtu hupendeza zaidi (nzuri zaidi) kuliko swala yake pekee. Na swala yake pamoja na watu wawili hupendeza zaidi kuliko swala yake na mtu mmoja. Na swala yenye idadi kubwa (ya watu) hupendeza mno kwa Allah”. Ahmad, Abuu Daawoud, Nasaai & Ibn Hibbaan.

Na kuwa swala ya jamaa msikitini ni bora zaidi kuliko kuswaliwa nyumbani. Na jamaa ya msikiti wa mbali ni bora zaidi kuliko ile ya msikiti wa karibu.

Hili linatokana na kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hakika mtu mwenye ujira mkubwa katika swala kuliko wote ni yule wa mbali wao zaidi kuiendea swala”. Muslim

 

TANBIHI:

Kunajuzu kwa wanawake kuhudhuria swala ya jamaa misikitini kwa sharti ya kujiepusha na mambo/vitu vinavyoweza kuamsha matamanio na kupelekea kuzuka kwa fitna.

Yaani watoke kwenda huko misikitini hali ya kuwa wamejistiri kwa mujibu wa sheria, hawakujipamba wala kujitia manukato.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Msiwazuilie vijakazi wa Allah na misikiti ya Allah na watoke (kwenda huko) bila ya kujitia manukato”. Ahmad & Abuu Daawoud.

Akasema tena Bwana Mtume: “Mwanamke ye yote aliyejifukiza udi asihudhurie pamoja nasi swala ya Ishaa”. Muslim, Abuu Daawoud & Nasaai.

Pamoja na wanawake kuruhusiwa kuswali jamaa misikitini lakini ilivyo bora kwao ni kuswali majumbani mwao. Imepokewa kutoka kwa Ummu Humayd As-saaidiyah-kwamba yeye alimuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia:

Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi ninapenda kuswali pamoja nawe (jamaa). Bwana Mtume akamwambia:

“Kwa yakini ninalitambua hilo, (lakini) na swala yako chumbani kwako ni bora kwako wewe (swala hiyo) kuliko swala yako katika msikiti wa jamaa zako (kitongojini mwako).  Na swala yako katika msikiti wa jamaa zako ni bora kwako kuliko swala yako katika msikiti wa jamaa”. Ahmad & Twabaraaniy

 

VII.   NAMNA YA KUTOKA KWENDA MSIKITINI KUHUDHURIA SWALA YA JAMAA:

Kumesuniwa kwa mtu mwenye kutoka nyumbani kwake kwenda msikitini kuhudhuria swala ya jamaa, atangulize mguu wake wa kulia na aseme wakati wa kutoka:

“BISMILLLAAHI TAWAKKALTU ‘ALAL-LAAH, WALAA HAULA WALAA QUWWATA ILLA BILLAAH, ALLAAHUMMA INNIY ‘AUDHUBIKA AN ADHWILLA AU UDHWALLA, AU AZILLA AU UZALLA, AU ADHWLIMA AU UDHWLAMA, AU AJ-HALA AU UJ-HALA ‘ALAYYA. ALLAAHUMMA INNIY AS-ALUKA BIHAQQIS-SAAILIYNA ‘ALAYKA WA BIHAQQI MAMSHAAYA HAADHA, FAINNIY LAM AKHRUJ ASHARA WALAA BATWARAA, WALAA RIYAA WALAA SUM’AH, KHARAJTUT-TIQAA SUKHTWIKA WABTIGHAA MARDHWAATIKA. AS-ALUKA AN TAHGFIRA LIY DHUNUUBIY JAMIY’AN, FAINNAHU LAA YAGHFIRUD-DHUNUUBA ILLA ANTA. ALLAAHUMMAJ-‘AL FIY QALBIY NUURA, WA FIY LISAANIY NUURA, WA FIY SAM’IY NUURA, WA FIY BASWARIY NUURA, WA ‘AN YAMIYNIY NUURA, WA ‘AN SHIMAALIY NUURA, WA MIN FAUQIY NUURA, ALLAAHUMMA A’ADHWIM FIYYA NUURA”.

Dua hii ni mkusanyiko wa matamko ya riwaya tofauti zilizopokewa na maimamu Tirmidhiy, Bukhaariy & Muslim

Kisha aanze kupiga khatua kuelekea huko msikitini kwa ushwari, utulivu, heshima na staha. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Qataadah-Allah amuwiye radhi-amesema:

Wakati ambapo sisi tukiswali pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mara akasikia ghasia za watu. Alipomaliza kuswali akauliza: “Mna nini nyinyi”.

Wakajibu tulikuwa tunaikimbilizia swala. Mtume akawaambia:

“Msifanye hivyo, mnapoiendea swala basi umekulazimuni utulivu (ushwari). Popote mtapoidiriki swalini na kilichokufutuni (katika hiyo swala) basi kitimizeni (baada ya imamu kutoa salamu)”. Bukhaariy, Muslim & wengineo.

Akishafika msikitini, autangulize mguu wake wa kulia wakati wa kuingia na aseme:

“BISMILLAAH, ‘AUDHUBILLAAHIL-‘ADHWIYM, WABIWAJIHIHIL-KARIYM WASULTWAANIHIL-QADIYM MINAS-SHAYTWAANIR-RAJIYM, ALLAAHUMMA SWALLI ‘ALAA NABIYYINAA MUHAMMADIN WA AALIHI WASALLAM, ALLAAHUMMMAGH-FIRLIY DHUNUUBIY, WAFTAH LIY ABWAABA RAHAMATIKA”.

Dua hii ya kuingia msikitini imepokewa na Imamu Ahmad & Ibn Maajah

Akishaingia msikitini basi asikae kitako mpaka aswali rakaa mbili za suna ijulikanayo kama ‘Tahiyyatul-Masjid’.

Haya ndio maelekezo ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika kauli yake: “Atapoingia mmoja wenu msikitini basi na asikae kitako mpaka aswali (kwanza) rakaa mbili”. Muslim

Ila kama ataingia msikitini wakati wa kuchomoza au kuzama kwa jua, wakati huo atakaa bila ya kuswali, kwa sababu Bwana Mtume amekataza kuswali ndani ya nyakati mbili hizo. Na wakati wa kutoka msikitini kurudi nyumbani, atoke kwa kutanguliza mguu wa kushoto na aisome dua hii tuliyoitaja hapo juu. Ila badala ya kusema: WAFTAH LIY ABWAABA RAHMATIKA, atasema: WAFTAH LIY ABWAABA FADHWLIKA.

 

SWALA YA JAMAA

I.      MAANA YA SWALA YA JAMAA:

Muradi na mapendeleo ya swala ya jamaa ni ile swala ya fardhi au ya suna iliyosuniwa kuswaliwa jamaa. Inayoswaliwa kwa pamoja na zaidi ya mtu mmoja ndani ya msikiti au nje ya msikiti. Hii ndio swala ya jamaa tutakayohusika nayo katika somo hili.

 II.      HISTORIA FUPI YA SWALA YA JAMAA:

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alianza kusimamisha swala ya jamaa Madinah baada ya Hijrah. Katika kipindi chote cha utume alichokaa Makah, kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu hakupata kuswali jamaa.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *