WAISLAMU WALIKUWA CHINI YA UONGOZI WA BUSARA

WAISLAMU WALIKUWA CHINI YA UONGOZI WENYE HURUMA NA BUSARA, WAKATI AMBAPO MUSHRIKINA WALIKUWA CHINI YA UONGOZI MPUMBAVU (USIO NA BUSARA) WENYE KIBURI.

Tukichukulia kwamba Abuu Jahli ndiye aliyekuwa kiongozi wa Makurayshi kwa sababu ya fikra na mawazo yake kushinda fikra zote zilizotolewa na viongozi wengine.

Na ni yeye ndiye aliyewaongoza Makurayshi katika halaki na maangamivu haya yaliyowasibu.

 Hebu sasa tuwe na mizani tupime baina ya nyongozi mbili hizi; uongozi wa waislamu kwa upande mmoja wa kitanga cha mizani na ule wa Makurayshi kwa upande mwingine.

Mizani yetu itatuonyesha kuwa waislamu walikuwa chini ya uongozi wenye huruma na busara. Na zaidi ya yote ni uongozi uliopendwa, kukubaliwa na kutiiwa na wote.

Wakati ambapo mizani yetu inatuonyesha kuwa mushrikina waliongozwa na uongozi usio na busara. Uongozi uliojaa kiburi, uongozi unaotumia nguvu zaidi katika kufikia maamuzi.

Huyu hapa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anajiweka sawa na maswahaba wake katika kila kitu na kuwafanya wahisi haki sawa baina yao.

Anawataka ushauri maswahaba wake katika mambo mengi na kuuthamini na kuuenzi ushauri wao huo. Akiupokea kwa mikono miwili ushauri bora zaidi na akiwarejesha msatarini kwa upole na hekima kila wanapoteleza na kukosea.

Akiwanyenyekea bila ya kujidhalilisha kiasi cha kumpa nafasi ya kulipa kisasi kwa ye yote aliyemdhulumu au kumkosea miongoni mwao.

Na yule Abuu Jahli akitumia udikteta katika kufikia maamuzi, hawapi watu wake nafasi ya kutoa fikra na mawazo yao.

Anamuona adui na kumpiga vita kila aliyeonyesha upinzani dhidi yake mpaka amuunge mkono na kuwa chini ya twaa yake. Kiongozi asiyemuheshimu mkubwa kwa ukubwa wake wala kumuhurumia mdogo kwa udogo wake.

Wala hafikirii natija na matokeo ya matendo yake, kwamba nikifanya au nikisema hivi itakuwaje. Katika hali na mzingira kama haya, unafikiri ni uongozi upi ulio na nafasi ya kushinda kuliko mwingine?!

 

D/. WAISLAMU WALIPIGANA KWA MIKAKATI MAALUMU WAKATI AMBAPO MUSHRIKINA WAKIPIGANA BILA YA MBINU WALA MIKAKATI.

Tukiyaangalia maandalizi na matayarisho (mobilization) ya makundi mawili haya; kundi la haki na kundi la batili katika vita vya Badri. Tutawaona waislamu wamepangwa katika safu zilizoungana mithili ya jengo imara lililokamatana barabara:

“KWA YAKINI ALLAH ANAWAPENDA WALE WANAOPIGANA KATIKA NJIA YAKE, SAFUSAFU (mkono mmoja); KAMA KWAMBA WAO NI JENGO LILILOKAMATANA BARABARA” [61:4].

Wakachagua mahala na upande munasibu wa kuelekeza mashambulizi yao dhidi ya hasimu wao, wakalipa mgongo jua na kuwafanya kutolielekea.

Kadhalika tunawaona hawamfuati adui yao pale aliposonga mbele kuwajia, bali walithibiti katika sehemu zao walizopangiwa, wakiwa wamekita magoti yao.

Wakimrushia adui yao mvua ya mishale kama alivyoamrisha kamanda wao mkuu. Waliendelea kurusha mishale mpaka pale adui alipowavaa na kukabiliana nao ana kwa ana.

Hapo ndipo kwa pamoja walichomoa panga zao na kupiga pigo la mtu mmoja wakiwa wamejenga ukuta imara bila ya kutapanyika huku na huko.

Kwa weko na mkao huu wa kivita uchache unaweza kufanya maajabu yasiyoweza kufanywa na wingi usio na mpangilio.

Hivi ndivyo walivyojipanga waislamu katika uwanja wa vita, wakiitii na kuisikiliza amri ya kamanda wao.

Ama kwa upande wa mushrikina mambo yalikuwa kinyume kwani walikuwa shaghlabaghla.

Walikuwa wengi waliotapanyika, hawana mikakati na utaratibu katika mashambulizi yao.

Wakipigana bila ya kuwa na kamanda anayekubalika na wote, kila kundi likielekeza mashambulizi yake kwa mujibu wa maelekezo na amri ya kamanda wake.

Walipigana huku jua likiwapiga nyusoni mwao na maji yakiwa katika udhibiti wa adui yao.

Pamoja na yote haya, Makurayshi wanaanza vibaya vita, kwani kabla hawajaanza kusonga mbele tayari wanawapoteza viongozi wao wanne kwa kuuawa na waislamu.

 

E/. WAISLAMU WALIKUWA NI UCHACHE UNAOMTEGEMEA MOLA WAKE NA MUSHRIKINA WALIKUWA NI WINGI ULIOGHURIKA NA NGUVU ZAKE.

Haya hebu sasa tuichunguze na kuiangalia roho na nafsi iliyokuwa ikilitawala kila kundi wakati wa mapambano.

Tunawakuta waislamu wakipigana huku wakiamini kwamba wao wanaipigania na kuitetea haki ambayo Allah na Mtume wake wanaipenda.

Walikuwa na yakini kwamba hafai kuipigania haki ila aliyeiamini na kuikubali haki hiyo. Wakisadikisha miadi na ahadi ya Allah ya kwamba atainusuru haki na kulinyanyua neno lake.

Ni imani na yakini hii ndio iliyowafanya waukatae msaada wa mushriki ye yote na uchache wao haukuwakatisha tamaa kusonga mbele.

Allah pekee walimtegemea awasaidie katika kuinusuru dini na Mtume wake.

Hii ndio roho na ari iliyowatawala waislamu katika uwanja wa mapambano.

Ama kwa upande wa mushrikina, wao walitoka majumbani mwao kwa fakhari na kujionyesha kwa watu, hivi ndivyo inavyosema Qur-ani Tukufu:

 “WALA MSIWE KAMA WALE WALIOTOKA KATIKA MAJUMBA YAO (miji yao) KWA FAKHARI NA KUJIONYEHSA KWA WATU NA KUZUILIA (watu) NJIA YA ALLAH…” [8:47].

Wakatoka wakiwa wamejawa na kiburi, majivuno na majigambo wakighuriwa na wingi wa idadi yao na nguvu yao.

Hawakusudii katika kutoka kwao huku ila kusikiwa na watu na kuzungumzwa ushujaa wao. Wakiamini kabisa kwamba ushindi unatokana na wingi, fikra hizi ndizo zilizowafanya wamwambie Iymaai Ibn Rukhswah alipotaka kuwapa msaada wake:

“Ikiwa tunapigana na watu (waislamu), basi sisi si dhaifu mbele yao na kama tunapigana na Allah kama anavyodai Muhammad, basi hakuna mwenye ubavu (nguvu) wa kupambana na Allah”.

Allah Mola Mwenyezi anaisawirisha hali yao hiyo kwa kauli yake:

“NA (kumbuka) SHETANI ALIPOWAPAMBIA VITENDO VYAO (wale makafiri) NA KUSEMA: LEO HAKUNA WATU WA KUKUSHINDENI, NA MIMI NI MLINZI WENU. LAKINI YALIPOONANA (yalipokutana) MAJESHI MAWILI (shetani) ALIRUDI NYUMA NA KUSEMA: MIMI SI PAMOJA NANYI, MIMI NAONA MSIYOYAONA, MIMI NINAMUOGOPA ALLAH NA ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU”. [8:48]

Haya hili ndilo kundi dogo lenye imani linaloipigania haki na kuutegemea msaada wa Allah pekee.

 Na lile ni kundi kubwa kafiri lenye kuhadaiwa na wingi wao, likisukumwa na jeuri, uadui na kujionyesha kwa watu.

Ukiziachilia mbali sababu hizi kuna sababu nyingine nyingi tu ambazo anaweza kuzidiriki mchunguzi wa mambo. Vyo vyote zitakavyokuwa sababu hizi, zote zitakuwa zinarejea kwenye asili moja, nayo si nyingine bali ni msaada wa Allah aliouthibitisha na kuwapa waislamu:

“…NA ALLAH ANAPENDA KUTHUBUTISHA HAKI KWA MANENO YAKE NA (anapenda) KUIKATA MIZIZI YA MAKAFIRI. ILI KUTHUBUTISHA HAKI NA KUONDOA BATILI, HATA WAKICHUKIA WATU WABAYA. (Kumbukeni) MLIPOKUWA MKIOMBA MSAADA KWA MOLA WENU, NAYE AKAKUJIBUNI KUWA: KWA YAKINI MIMI NITAKUSAIDIENI KWA MALAIKA ELFU MOJA WATAKAOFUATANA MFULULIZO (wanaongezeka tu). NA ALLAH HAKUFANYA HAYA ILA IWE BISHARA (khabari ya furaha) NA ILI NYOYO ZENU ZITUE KWAYO. NA HAKUNA MSAADA (wa kufaa) ILA UTOKAO KWA ALLAH. HAKIKA ALLAH NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE HEKIMA”. [8:7-10]

 

WAISLAMU WALIKUWA CHINI YA UONGOZI WA BUSARA

WAISLAMU WALIKUWA CHINI YA UONGOZI WENYE HURUMA NA BUSARA, WAKATI AMBAPO MUSHRIKINA WALIKUWA CHINI YA UONGOZI MPUMBAVU (USIO NA BUSARA) WENYE KIBURI.

Tukichukulia kwamba Abuu Jahli ndiye aliyekuwa kiongozi wa Makurayshi kwa sababu ya fikra na mawazo yake kushinda fikra zote zilizotolewa na viongozi wengine.

Na ni yeye ndiye aliyewaongoza Makurayshi katika halaki na maangamivu haya yaliyowasibu.

 Hebu sasa tuwe na mizani tupime baina ya nyongozi mbili hizi; uongozi wa waislamu kwa upande mmoja wa kitanga cha mizani na ule wa Makurayshi kwa upande mwingine.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *