Mwenyezi Mungu Mtukufu ameifanya twahara kuwa ni sheria na kuwafaradhishia waja wake kwa sababu twahara humfanya muislamu aishi maisha ya unadhifu na utakasifu.
Humfanya awe mtakasifu wa mwili, nadhifu wa mavazi na mahala aishipo.
Utakasifu na unadhifu huu humjengea afya njema na mwenendo mzuri kitabia.
Usafi huu wa nje/dhahiri ni barabara na chombo cha kumfikisha katika usafi na utakasifu wa ndani/batini ambao humfanya kuwa ni mtakasifu wa moyo, mwenye kauli nzuri laini na nafsi iliyosalimika na husuda, udanganyifu na tabia mbaya zote kwa ujumla.
Muislamu wa kweli ni yule aliyetakasika nje na ndani wakati wote khasa khasa wakati wa kutekeleza ibada, hii ndio sababu Bwana Mtume akatuambia:
“Uislamu ni nadhifu, basi jinadhifisheni kwani hatoingia peponi ila aliye nadhifu”.