SUBIRI KWA MITIHANI INAYOKUSIBU

Ndugu yangu katika imani-Allah Taala atupe imani ya kweli itakayotupa kheri za duniani na akhera-Aamiyn!

Tunaendelea kuusiana katika mapenzi ya Allah, ufahamu na uelewe kwamba miongoni mwa mambo makubwa yenye kuokoa ni kusubiri kwa mitihani unayotahiniwa na Allah.

Subira yako hii iende sambamba na kuzishukuru neema za Allah alizokuneemesha na kuipa mgongo dunia imshughulishayo mja kiasi cha kumsahau Allah Mola Muumba wake.

Elewa kuwa subira ni miongoni mwa ibada ngumu lakini zenye fadhila kubwa kabisa. Subira ni hitajio muhimu la kila muumini katika hali zake zote na katika kipindi chake chote cha kuishi katika ardhi hii ya Maulana.

Subira ni siri na ufunguo wa fanaka, furaha, amani, salama na mafanikio yote katika ulimwengu huu wa mpito na ule wa milele.

Qur-ani Tukufu imesheheni aya kathiri zinazotaja fadhila za subira, aya hizi zinashereheshwa na hadithi adida (nyingi) za Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Hebu tuzitafakari kwa pamoja aya zifuatazo tuone namna gani Allah anavyotuita katika biashara ya subira; biashara isiyododa wala kukhasirika, tusome:

 “ENYI MLIOAMINI! JISAIDIENI (katika mambo yenu) KWA SUBIRA NA SWALA; BILA SHAKA ALLAH YU PAMOJA NA WANAOSUBIRI” [2:153]   

Haya mpenzi ndugu yangu-Allah atupe fahamu-tunaelewa nini katika aya hii tukufu? Bila shaka utakubaliana nami ndugu yako kuwa aya hii inaeleza kuwa muumini ndiye mlengwa na shabaha ya mitihani na misukosuko kama inavyotuwazikia kupitia aya hii:

“NA TUTAKUTIENI KATIKA MSUKOSUKO WA (baadhi ya mambo haya); KHOFU NA NJAA NA UPUNGUFU WA MALI NA WA WATU NA WA MATUNDA. NA WAPASHE KHABARI NJEMA WANAOSUBIRI”. [2:155]

Tayari imetuthibitikia kuwa muumini ni lazima ataonjwa na Mola wake kwa kumtahini kwa mitihani mbalimbali, hana pa kukimbilia.

Sasa la msingi la kujiuliza ni je, akisibiwa na masaibu na mitihani hii ya Mola wake afanye nini? Aya ikatoa dawa na kuonyesha kuwa tegemeo na kimbilio pekee la muumini wakati wa masaibu na misukosuko ni SUBIRA na SWALA.

 Kwa maneno mengine tunaweza kusema subira na swala ni silaha kali inayompa ushindi mnono muumini katika vita ngumu ya masaibu na misukosuko ya maisha ya kila siku.

Aya ikamalizia kwa kueleza daraja na cheo cha wanaosubiri na kuswali pindi waonjwapo na Mola wao kuwa watakuwa pamoja na Allah.

Yaani msaada wa Allah utakuwa pamoja nao katika dhiki na masaibu yote ya leo hapa duniani na ya kesho kule akhera.

Mpenzi ndugu yangu, je unapenda kupendwa na Allah? Kama unapenda na bila shaka hakuna asiyependa, basi subiri unaposibiwa na masaibu yatokayo kwa Allah, kwani subira hiyo ndio thamani ya kuyanunulia mapenzi ya Allah, tusome pamoja na tuamini:

“…NA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO SUBIRA”. [3:146]

Ndugu yangu-Allah atuwafikishe kusubiri-tuendelee kutafakari pamoja kwa maslahi na manufaa ya nafsi zetu wenyewe. Allah Mola Mwenyezi anamkhutubu Mtume  wake-Rehema na Amani zimshukie-kwa kumwambia:

“NA SUBIRI NA KUSUBIRI KWAKO KUSIWE ILA KWA AJILI YA ALLAH TU…” [16:127]

Sote tunatambua kuwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipewa na Mola wake jukumu gumu na zito la kuufikisha ujumbe wake kwa waja wake.

Katika kulitekeleza jukumu hili Bwana Mtume alikumbwa na misukosuko mikubwa ambayo ilikuwa ni kikwazo kikubwa katika kufikisha ujumbe wa Allah kwa waja wa Allah.

Ndipo Allah aliyemtuma mja wake kwa waja wake akamuagiza Mtume wake kusubiri. Kwa kuwa kusubiri tu hakutoshi anamwambia subira yake yote iwe ni kwa ajili yake yeye tu Allah ambaye ndiye atakayewalipa wote wanaosubiri:

“…NA BILA SHAKA WAFANYAO SUBIRA (wakajizuilia na maasia na wakaendelea kufanya ya twaa) WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO HESABU”. [39:10]

Bwana Mtume akanyenyekea na akajisalimisha kwa Mola wake, akasubiri kwa ajili ya Allah mpaka nusura ya Allah na ushindi ukapatikana na watu wakaingia katika dini ya Allah makundi kwa makundi.

Nasi basi ewe ndugu yangu katika Uislamu tumuige na kumgeza Mtume wa Allah katika kusubiri kwa ajili ya Allah ili itufikie nusra na ushindi kutoka kwa Allah.

Ewe ndugu yangu, nakusihi tukiri kuwa muumini ana haja kubwa kuelekea subira wakati wa kufikwa na mabalaa mbalimbali yasiyo na hodi wala taarifa.

 Asubiri na wala asipapatike anapofikwa na mabalaa hayo, anachotakiwa kufanya ni kutulia, kunyenyekea, asione dhiki wala uchungu.

Asiwashitakie viumbe mtihani wake huo, bali arejee kwa Allah kwa unyenyekevu na kujisalimishia kwake amuombe faraja na awe na dhana njema kwa Allah Mola awaonjaye waja wake. 

Na ajue kwa yakini kwamba Allah hakumshushia balaa hilo ila anazo yeye ndani yake kheri nyingi.

Ikiwa ni pamoja na kuinuliwa daraja, kuzidishiwa mema yake na kufutiwa madhambi kwa ushahidi wa hadithi za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Lakini yote haya hayapatikani ila kwa gharama ya subira, tena kusubiri kwenyewe kuwe ni kwa ajili ya Allah tu.

Muumini anahitajia sana subira katika kufanya mambo ya twaa; mambo ambayo ndani yake inapatikana radhi ya Allah, ambayo ndio matakwa na lengo mama la kuazimiwa na kufikiwa na kila muislamu.

Asubiri mja kwa kutokuona uvivu kufanya mambo ya twaa, ayatekeleze kama alivyoamrishwa na Allah kwa ukamilifu na unyenyekevu mkubwa.

Na ayafanye kwa ajili tu ya Allah (Ikhlaaswi) na waka asikusudie kuwaonyesha watu cho chote katika mambo ya twaa anayoyafanya.

Ni muhimu kila muislamu akatambua kuwa hali na tabia ya nafsi ni kuona uzito na uvivu katika kufanya mambo ya twaa.

Kwa hali hii basi, inambidi mja ajitahidi upeo wa jitihada yake kuilazimisha nafsi yake kuzoea kutenda mambo ya twaa kwa subira njema.

Ndugu yangu mpenzi-Allah aturehemu-elewa na ufahamu kwamba eneo jingine ambalo mja anahitajia sana subira ni katika bahari tamu na kipenzi cha nafsi; bahari maasi. Allah Mola Mtukufu anatufahamisha juu ya tabia ya nafsi:

“…KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA WANGU AMEIREHEMU…” [12:53]

Kwa hali hii basi, kumempasa na kumuwajibikia mja kuizuilia nafsi yake na mambo ya maasi na haramu.

Hii ni kwa sababu nafsi huyapenda mno na kuyaonea tamu mambo hayo kwa hivyo humkokota na kumvutia mja katika mambo hayo.

Aizuie kwa subira njema kufanya maasi kwa dhahiri, kuyazungumzia na kuyaelekea kwa batini.

Naam, muumini anahitajia subira kubwa katika matamanio yake halali.

Haya ni yale yote ambayo raghba ya nafsi ndani ya matamanio hayo hukomelea katika kuionea ladha na starehe dunia bila ya kuwa na athari katika maisha yake ya milele kule akhera.

Hii ni kwa sababu kuzama na kujiachia katika matamanio halali humburuzia mja katika mambo ya shubuha na haramu.

Hukithirisha raghba ya dunia na kumchochea mja kuipupia, jambo ambalo hupelekea kuyapenda zaidi maisha ya dunia yenye kupita kuliko yale ya nyumba ya milele (akhera).

Mpaka hapa natumai ndugu yangu-Allah akurehemu-kwa msaada wa Allah utakuwa umejua thamani ya subira na haja ya muumini kuwa na subira katika hali na maisha yake yote.

Basi ninakuusia bila ya kujisahau mwenyewe tulazimikiane na subira tutafuzu kwa kupata kheri na mafanikio yote ya dunia na akhera.

 

SUBIRI KWA MITIHANI INAYOKUSIBU

Ndugu yangu katika imani-Allah Taala atupe imani ya kweli itakayotupa kheri za duniani na akhera-Aamiyn!

Tunaendelea kuusiana katika mapenzi ya Allah, ufahamu na uelewe kwamba miongoni mwa mambo makubwa yenye kuokoa ni kusubiri kwa mitihani unayotahiniwa na Allah.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *