Kumpenda jirani, hii ni tabia ambayo Muislamu anatakiwa aijenge, aizoee na kujipamba nayo. Muislamu anapaswa kujua kuwa kumpenda jirani yake ni sehemu ya mafundisho ya dini yake ambayo Uislamu wake haukamiliki ila kwa kuyaitakidi, kuyafuata na kuyatia vitendoni. Kumpenda jirani ni pamoja na kuzijua haki zake zikupasazo na kumtekelezea.
Mafanikio, raha na furaha ya maisha ya mwadamu hutegemea kwa kiasi kikubwa sana mambo yafuatayo:-
1.Utulivu wa moyo na akili.
2.Amani na usalama wa maisha (uhai), mali na heshima (hadhi)
3.Thamani ya utu wake.
4.Mapenzi na ushirikiano wa jamii inayomzunguka.
Maeneo yote haya na mengine ambayo hatujayataja ni mazingira yanayohitaji kuandaliwa, kutayarishwa na kujengea ili mwanadamu aishi kwa amani na utulivu na kuyaonea raha na furaha maisha yake katika ulimwengu huu.
Mtu aliye karibu zaidi nawe, ukiachilia mbali wazazi wako, ndugu na jamaa na nasabu ni jirani yako.
Jirani ni mtu unayeishi naye mtaani kwako au kitongojini mwako kwa kawaida huyu ndiye mtu wa kwanza kusikia na kisha kushirikiana nawe katika machungu yaliyokusibu au furaha iliyokushukia.
Uislamu katika kulizingatia hili, umempa mtu huyu muhimu (jirani) heshima na haki za pekee bila ya kujali ni ndugu wa nasabu au la. Tulisome agizo na amri ya Mola juu ya jirani
“MWABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHOCHOTE NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI NA JAMAA NA MAYATIMA NA MASIKINI NA JIRANI YAKO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI NA RAFIKI WALIO UBAVUNI (Mwenu) NA MSAFIRI ALIYEHARIBIKIWA NA WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YENU YA KULIA????” (4:36).
Ufafanuzi mdogo aya:
JIRANI WALIO KARIBU: Huyu ni yle anayeishi karibu kabisa na wewe hata kama si Muislamu au ni yule ambaye mna udugu wa nasaba baina yenu.
JIRANI WALIO MBALI: Huyu ni yule aishiye mbali na wewe au si ndugu yako wa nasabu.
RAFIKI WALIO UBAVUNI: Huyu ni mwenzio katika kusoma (elimu) kazi, safari yaani ni mtu mnayeshirikiana au kuambatana katika jambo/suala Fulani.
Ili kuonyesha umuhimu wa jirani na haki zake Malaika Jibril – Amani imshukie – alimuusia sana Bwana Mtume juu ya jirani na kuukariri wasia wake huo mpaka Mtume akadhania ataamrishwa kumrithisha kwa kupewa fungu la mirathi kama wanavyopewa ndugu wa nasabu
“Jibril aliendelea kuniusia juu ya jirani mapaka nikadhania kuwa atamrithisha.” Bukhaariy na Muslim.
Uislamu umeifanya haki ya jirani kuwa ni haki ya kijamii inayomuhusu jirani muislamu na asiye muislamu.
Uislamu haukulitazama hili kwa mtazamo wa itikadi bali umelitazama kwa mtazamo wa amani na usalama ili watu wote waishi katika mazingira yenye amani na usalama, na jami yenye utulivu.
Taji hili la ujirani ikiwa ni pamoja haki zinazoambatana nalo anavishwa kila mtu, bila ya kujali kuwa ni muislamu au kafiri, mwema au muovu, rafiki au adui, ndugu au si ndugu, anaishi jirani kabisa na mbali na kadhalika.
Pamoja na uislamu kuwapa wote hao haki na heshima ya ujirani, umewagawa na kuwapanga katika daraja na mafungu yafuatayo.
Tuisome sote kwa pamoja hadithi hii ya Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie:
” Majirani ni watatu, Jirani mwenye haki moja nae ni Mushrikina (kafri/asiye muislamu), huyu ana haki ya ujirani (tu). Na jirani mwenye haki mbili nae ni Muislamu (mwenzio), huyu ana haki ya ujirani na haki ya Uislamu. Na jirani mwenye haki tatu, huyu ni Muislamu aliye ndugu wa nasabu, ana haki ya ujirani, haki ya Uislamu na haki ya udugu” Twabaraariy.
Hebu angalia ni namna gani Uislamu unavyomthamini hata jirani asiye muislamu kupitia mfano hai aliotupigia swahabu wa Mtume – Rehema na Amani zimshukie.
Imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Amri – Allah awawiye radhi- kwamba yeye alichinja mbuzi, akauliza, mmempelekea yule jirani Myhahudi?
Kwani mimi nimemsikia Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akisema,
“Hakuacha Jibril kuniusia juu ya jirani mpaka nikadhani atamrithisha” Bukhaariy na Abu Daawaoud.
Katika uislamu, ujirani una haki zake za pekee na haki hizi uzidi itakaposadifu kuwa na uislamu ndani yake.
Haki hizi huongezeka zaidi na zaidi iwapo ujirani huu utachangaya uislamu na udugu wa nasabu pamoja.
Mwanadamu yeyote hupitia katika mkondo wa matatizo na shida mbalimbali shida hizi huweza kutokea mchana au usiku na bila taarifa au kufanya maandalizi yoyote ya kukabiliana nayo. Maradhi ya ghafla, msiba, moto, kuingiliwa na wezi, yote haya huweza kumtokea mtu na kuhitaji msaada wa haraka.
Hakuna anayeweza kutoa msaada huu wa haraka na katika wakati muafaka ila ni jirani. Sasa kama hukuishi naye vizuri, kwa masikilizano na ushirikiano, utapataje msaada wake?
Kweli atakuwa na moyo na mapenzi ya kusaidia, ikiwa hukuyajenga mazingira mazuri mapema.?
Haki hizi za kijamii katika Uislamu zinalenga kujenga mahusiano mema baina ya jamii, kupanda moyo wa huruma, upendo na kusaidiana ili jamii ya wanadamu iishi chini ya anga la amani, utulivu, furaha na salama.
Haki hizi zikichungwa na kutekelezwa ipasavyo, natija yake ni kuwafanya watu wa mji mmoja kuwa kama mfano wa mwili mmoja, kama kwamba ni watu wa familia moja. Mipaka ya ujirani kisheria imedhibitiwa na riwaya zifuatazo:-
1. Imepokelewa kutoka kwa Imam Ally Allha amuwiye radhi amesema: Atakayesikia adhana basi huyo ni jirani yako. Yaani mtu mnayesikia pamoja adhana ya msikiti ulio jirani yeu, yeye akiwa nyumbani kwake na wewe nyumbani kwako, basi fahamu huyo ni jirani yake.
2. Riwaya nyingine inasema:- Atakayeswali swala ya sub-hi msikitini pamoja nawe, basi huyo ni jirani yako.
3. Imepokelewa kutoka kwa Bi Aysha Allah amuwiye radhi “Mpaka wa ujirani ni nyumba arobaini kwa kila upande.”
4. Imepokelewa kutoka Al-Hassan Al-Biswriy kwamba yeye aliulizwa kuhusiana na jirani, akajibu”Ni nyuma, yake arubaini kuliani mwake na arubaini kushotoni mwake (mtu)” Bukhaariy katika kitabu “AL-ADABUL MUFRAD”.
Miongoni mwa haki jumla za jirani ni kumfanyia ihsani. Ihsani, hili ni neno lenye maana pana sana, linahusisha kumtendea kila ambalo ni jema/zuri lenye kumpa faraja, furaha na matumaini, ihsani hii inakusanya vyote viwili; kauli (maneno) na amali (matendo) na hii ni amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, tusome na tuamrike.
“— NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI NA JAMAA NA MAYATIMA NA MASIKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI NA RAFIKI WALIO UBAVUNI (Mwenu)—.” [4:36]
Amri hii pia imekuja katika sunah ya Bwana Mtume (hadithi) kwa tamko la IKRAAMU na mara nyingine kwa tamko la IHSAANI kama ilivyokuja katika aya. Amesema Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie :
” Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi na amkirimu jirani yake.” Bukhaariy na akasema tena:” Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi na amfanyie Ihsaani jirani yake.” Muslim.
Tafsiri na ufafanuzi wa matamko haya mawili; ikraamu na ihsaani, umekuja katika hadithi kadhaa. Miongoni mwa hizo:
“(maswahaba) waliuliza ewe Mjumbe wa Allah ni ipi haki ya jirani kwa jirani yake? Akajibu: Akikuomba mkopo mkopeshe, akikuomba msaada msaidie, akiumwa mkague, akiwa na haja mpe (mtekelezea), akipatwa na kheri (jambo zuri) mpongeze, akipatwa na msiba umuizi (mfanyie taazia) na akifa lifuate jeneza lake (mazikoni).” Twabaraaniy
Haki nyingine za jirani, mbali na hizo ni pamoja na:-
1·Uhifadhi/utunze siri zake unazozijua.
2·Uchunge heshima na hadhi yake.
3·Ujipendekeze kwake kwa kumpa zawadi
4·Uyapupie maslahi yake kama unavyoyapupia maslahi yako.
5·Umkabili kwa bashasha na uso mkunjufu.
Amesema Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
“Ewe Abu Dhari, ukipika mchuzi basi ongeza maji yake na umuangalie jirani yako (mpelekee)” Muslim.
Mwanamke kimaumbile na kiuzoefu ndiye hugongana na kukwaruzana na jirani yake mara kwa mara.
Jambo hili huathiri kwa kiasi kubwa ujirani na kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama na kusababisha kuvunjika kwa hali ya amani na utulivu.
Njia munasibu ya kuliepusha janga hili ni kutumia njia hii ya kupeana zawadi hata zile ambazo ni duni na ndogo machoni.
Kitendo hiki cha kuzawadiana hujenga moyo wa huruma na upendo na kuifukuzilia mbali chuki. Hebu na tuuzingatie wito huu wa Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie:-
“Enyi wanawake waislamu, jirani asimdharau asimdharau jirani yake walau kwa (kumpa) makongoro (miguu) ya mbuzi” Bukhaariy na Muslim.
Kitendo cha kumpa zawadi/hadiya jirani yako humjengea hisia za kuwa unamjali, unamthamini, unampenda na kumuheshimu.
Ni hisia hizi ndizo ambazo humuondoshea chuki, husda, mafundo na fitna juu yako na mahala pake kutawaliwa na upendo, huruma na moyo wa kusaidia.
Ikiwa kumfanyia Ihsaani jirani ni jambo linalotakiwa na sheria, basi kutokumuudhi pia ni amri ya lazima. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie anatuasa juu ya hilo.
“Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi asimfanyie maudhi jirani yake.” Bukhaariy na Muslim.
Kuna matendo mengi ambayo ukiyafanya huwa ni maudhi na kero kwa jirani yako kwa mtazamo wa sheria, hayo ni pamoja na
1·kuegesha gari lako mbele ya nyumba yake na kumzibia mlango wake.
2·Kutupa takataka zako uwanjani kwake.
3·Kufungua radio yako kwa sauti kubwa
4·Kuwaacha wanao kuchezacheza na kupiga kele mbele ya nyumba yake.
Kupanga njama za kumdhuru au kumvunjia heshima yake.
Angalia namna Uislamu ulivyoyachunga hata mambo ambayo yanaweza kuleta athari mbaya kwa wakubwa na watoto. Mtegee sikio la usikivu wa kufuata na kuzingatia Mtume wako Rehema na Amani zimshukie:
“— na wala usimuudhi kwa harufu ya chungu chako ila umchotee humo, na ukinunua matunda mpe na yeye, kama hukumpa basi yaingize kwa uficho (asiyaone) na wala mwanao asitoke nalo nje na kuwakasirisha wanawe (kuwafanya waanze kulilia)”. Twabaraariy