Najisi kwa mtazamo wa sheria zimegawanywa katika aina tatu zifuatazo :
1.NAJISI NZITO: Hii ni najisi ya mbwa na nguruwe na mnyama aliyezaliwa kutokana nao au mmoja wao (mbwa na nguruwe). Najisi hii imeitwa najisi nzito kutokana na uzito unaompata mtu katika kuiondosha
2.NAJISI KHAFIFU: Hii ni mkojo wa mtoto mchanga wa kiume aliye chini ya miaka miwili na hali ila maziwa ya mama tu. Najisi hii imeitwa Najisi khafifu kwa sababu ya wepesi unaopatikana katika uiondosha.
3.NAJISI YA KATI NA KATI: Hii imekusanya baki ya najisi nyingine ukiondoa najisi ya mbwa na nguruwe na mkojo wa mtoto mchanga wa kiume. Najisi hii imeitwa Najisi ya kati na kati kwa kuwa haiko kwenye uzito na wala haikufika kwenye ukhafifu.
JINSI/NAMNA YA KUZIONDOSHA NAJISI HIZI:
Ni muhimu tukakumbuka kuwa ni haramu kujipakaza najisi na ni wajibu kuiondosha mara tu inapoingia mwilini, nguoni au mahala pake mtu.
Hutwahirishwa mahala palipoingiwa na najisi ya mbwa na nguruwe kwa kupaosha mahala hapo paliponajisika kwa kupaosha mara saba na mojawapo wa mara saba hizo iwe kwa kusugua na mchanga. Bwana Mtume -Allah amrehemu na amshushie amani- amesema :
“Twahara ya chombo cha mmoja wenu atakapokiramba mbwa ni kukiosha mara saba, ya kwanza yake ( hizo mara saba) iwe ni kwa mchanga” Muslim
Najisi khafifu hutwahirishwa mahala paliponajisika kwa kuingiwa/kupatwa na najisi khafifu kwa kuimwagia maji sehemu hiyo, maji yaenee.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ummu Qays Bint Mihswan-Allah amridhie- kwamba
“alimpeleka Mtume wa Allah mtoto wake mdogo wa kiume ambaye hajala chakula (ananyonya) akamkojolea (mtume) nguoni, akaagizia maji na kuyamiminia palipokojolewa na hakuifua (nguo)”. Bukhaariy na Muslim.
Najisi ya kati na kati, mahala paliponajisika kwa kuingiwa na najisi hii hutwaharishwa kwa kupaosha na maji twahara mpaka iondoke rangi, utamu na harufu ya najisi hiyo.
Haidhuru kubakia kimojawapo rangi au harufu ziloshindikana kuondoka.
TANBIHI: Usiitumbukize nguo iliyonajisika ndani ya maji machache kama vile ndoo ukadhani kuwa umeitwahirisha bali itakuwa bado imenajisika na kunajisisha maji yote na hivyo kuyafanya yasifae tena kutwahirishia.
Unachopaswa kufanya ni kutumia kata au kilicho mfano wa kata, uteke maji na kuitwahirishia nguo hiyo pembeni ambapo maji yanayochuruzika kutoka katika nguo iliyonajisika hayaingii tena chomboni.
TWAHARA YA ARDHI:
Ardhi ikipatwa na najisi, hutwahirishwa kwa kumwagiwa maji juu yake mpaka najisi iondoke, hivyo ndivyo alivyoagiza Bwana Mtume. Imepokelewa riwaya kutoka kwa Abuu Hurayra-Allah amridhie- kwamba amesema :
Alikuja bedui mmoja akakojoa msikitini, watu (maswahaba) wakamuinukia ili wamuadhibu, Mtume akawaambia :
“Mwacheni (amalize haja yake) na (kisha) mumwagie mkojo wake ndoo ya maji” Bukhaariy na Muslim.
Msikiti wa Bwana Mtume –Allah amshushie rehma na amani- ulikuwa haukusakafiwa kama ilivyo misikiti yetu ya leo bali ulikuwa na sakafu ya udongo/mchanga kama zilivyo nyumba zetu za vijijini.
Ardhi pia hutwahirika kwa kukauka yenyewe kutokana na kupigwa kwa jua au kunyeshewa mvua na kuondoka athari ya najisi.
TWAHARA YA SAMLI, JIBINI, SIAGI NA MFANO WA VITU HIVYO
Samli, jibini siagi na vitu vinavyofanana navyo vikiingiwa na najisi na vikiwa katika hali ya ugumu na vimeganda na si hali ya kumiminika, hutwahirika kwa kuitoa najisi iliyoingia pamoja na sehemu zinazozunguka/zilizojiranikiana na najisi ile.
Bwana Mtume-Allah amshushie rehema na amani- aliulizwa kuhusiana na (hukmu ya) panya aliyetumbukia (na kufia) ndani ya samli, akajibu
“Mtupeni na sehemu inayomzunguka na kuleni samli yenu”. Al-Bukhariy.
Ama itakapokuwa samli, siagi, jibini na chochote chenye kufanana navyo katika hali ya kumiminika/maji maji na ikaingiwa na najisi itanajisika yote na haitofaa tena kwa matumizi ya binadamu.
TWAHARA YA NGOZI
Ngozi ya mnyama hutwahirishwa kwa kudabighiwa.
Dabghu ni kuondosha damu, mafuta na mabaki ya nyama zilizosalia katika ngozi baada ya mnyama kuchunwa.
Uondoshaji huu hufanyika ka kutumia vitu vikali vyenye muonjo wa asidi, baada ya hapo ndipo ngozi hutwahirishwa na maji na kufaa kutumika kwa matumizi mbali mbali ya binadamu.
Imepokelewa na Ibn Abbas – Allah amridhie- kwa Bwana Mtume-Allah amshushie rehema na amani- amesema
“Ngozi itakapodabighiwa imetwahirika” Bukhaariy na Muslim.