Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipowasili Madinah akitokea kwenye vita vya Dhaatir-riqaa, alikaa hapo siku zilizobakia za mwezi wa Jumaada-Uula (mfunguo nane), Jumaadal-Aakhirah (Mfunguo tisa) na Rajabu (Mfunguo kumi).
Akatoka katika mwezi wa Shaaban kuelekea Badri kufuatia ile miadi ya vita aliyoiweka Abu Sufyaan wakati anaondoka na jeshi lake siku ile ya vita vya Uhud.
Badri lilikuwa ni gulio la kila mwaka ambapo watu hukusanyika hapo katika mwezi wa Shaaban, wakiuza na kubadilishana bidhaa hapo kwa muda wa siku nane.
Mwaka huo Makurayshi walikuwa wamo katika janga la ukame na njaa na bidhaa zao za kuuza nje zikawa ni chache kwa sababu ya pingamizi walizowekewa na waislamu katika biashara yao.
Kwa hali hii, hawakuwa na uwezo wa kuendesha vita kama walivyoagana na Mtume, hali hii ikamlazimisha Abuu Sufyaan kutokutoka kwenda kwenye uwanja wa mapambano; Badri.
Akachelea kwenda asije akakutana na Mtume pamoja na maswahaba wake, kisha ikawa ni zamu yao kushindwa kama wao walivyowashinda waislamu kule Uhud.
Isitoshe alichelea waislamu wasije kuitambua hali ya dhiki waliyonayo na kuitumia fursa hiyo kuwasagasaga.
Akatafuta hila na mbinu ya kuwakatisha tamaa waislamu wasitoke kuja Badri, akamkodi mtu mmoja akiitwa Nuaim Ibn Masoud.
Huyu akampa maelekezo aende Madinah kueneza khabari kuwa Makurayshi wamewakusanyia waislamu jeshi kubwa lisilo na mithali katika historia yao ya vita.
Jeshi ambalo hawatakuwa na ubavu wa kupambana nalo, kwa hivyo kwa usalama wao ni bora wasitoke kuelekea uwanja wa mapambano.
Nuaim huyoo akashika njia na kwenda zake Madinah kueneza propaganda ya Abu Sufyaan, lakini juhudi zake hizi hazikuzaa matunda yaliyolengwa na mpishi wa propaganda hizo; Abu Sufyaan.
Kwani Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakutikiswa nazo na badala yake zikamzidishia ari na hamasa ya kutoka, akaapa akisema: “Naapa kwa yule amabye nafsi yangu i mkononi mwake, mimi nitatoka hata kama hatatoka ye yote pamoja nami!”
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatoka na maswahaba wake wapatao alfu moja na mia tano.
Akamkaimisha Abdullah Ibn Abdillah Ibn Ubayyi shughuli zote za kiutawala za Madinah kwa kipindi chote cha kughibu kwake.
Walipofika Badri kama yalivyo maagano yao na Makurayshi, hawakumkuta hata Mkurayshi mmoja, kwa sababu Abuu Sufyaana alichelea kushindwa.
Akarejea njiani na watu wake huku akiwaambia:
“Enyi kusanyiko la Makurayshi! Hakika ya hali ilivyo haikufalieni nyinyi kupigana ila katika mwaka wenye neema ya chakula na maziwa. Na bila shaka mnaona mwaka wenu huu ni mwaka wa njaa na ukame, kwa hali hii mimi ninarudi siendi Badri na nyinyi rudini”.
Kwa kauli hii ya kiongozi wao, watu wote wakarejea na kwa kushindwa kwao kutekeleza miadi ya vita waliyoiweka wao wenyewe.
Makurayshi wakapatwa na fedheha ya kushindwa vita na aibu ya kumkimbia adui yao, mpaka wakafikia kuitwa na watu wa Makkah: “Jeshi la Sawiyq (aina ya kinywaji)”.
Wakiwaambia kwa njia ya dhihaka na kejeli: Hakika si vinginevyo nyinyi mlitoka kwa ajili tu ya kunywa sawiyq na wala sio kwa ajili ya vita!
Kwa kitendo chao hiki cha uoga ule ushindi na fakhri waliyoipata katika vita vya Uhud ukawa si cho chote si lo lote mbele ya makabila ya Waarabu. Heshima na haiba yao ikapomoka mbele ya macho na ndani ya nafsi zao.
Ama Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake waliendelea kubakia hapo Badri kwa muda wa siku nane zote za gulio.
Wakiuza na kununua na wakapata faida maridhawa na wakajiondoshea aibu na fedheha ya kushindwa iliyowapata katika vita vya Uhud.
Wakairejesha tena haiba na hadhi yao iliyopotea miongoni mwa makabila ya Kiarabu. Ni katika vita hii ndimo ilimoshuka kauli yake Allah Taala:
“WALE AMBAO WATU (waliokodiwa na Makurayshi) WALIWAAMBIA (waislamu): WATU (yaani Makurayshi) WAME KUKUSANYIKIENI, KWA HIVYO WAOGOPENI. LAKINI (maneno hayo) YAKAWAZIDISHIA IMANI (Waislamu), WAKASEMA: ALLAH ANATUTOSHA (atatukifia), NAYE NI MLINZI BORA KABISA. BASI WAKARUDI (vitani) NA NEEMA ZA ALLAH NA FADHILA (zake), HAKUNA UBAYA ULIOWAGUSA; NA WAKAFUATA YANAYOMRIDHISHA ALLAH. NA ALLAH NI MWENYE FADHILA KUU. HUYO (aliyekutieni khofu ile) NI SHETANI AMBAYE ANAKUOGOPESHENI MARAFIKI ZAKE, BASI MSIWAOGOPE; BALI NIOGOPENI MIMI MKIWA NI WAUMINI (kweli)”. [3:173-175]
I. KIPINDI CHA MPITO CHA AMANI NA SALAMA:
Hivyo ndivyo walivyorudi waislamu Madinah wakitokea Badri wakiwa na amani na utulivu zaidi. Wakakaa Madinah kwa amani, raha mustarehe kwa kipindi kisichopungua miezi sita.
Ni katika kipindi hiki cha amani na salama ndimo Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimuoa mama wa waumini; Ummu Salamah baada ya kufiwa na mumewe-Allah amuwiye radhi.
Mumewe huyu wa mwanzo; Abu Salamah alikuwa ni mwana wa shangazi yake Mtume na nduguye wa kunyonya na ndiye muislamu wa mwanzo kuhamia Uhabeshi.
Waislamu waliendelea kuneemeka na amani katika kipindi hiki mpaka ukamalizika mwaka wa nne na miezi miwili ya mwaka wa tano; Muharam na Swafar.
II. VITA VYA DAUMATUL-JANDAL.
Mnamo mwezi wa Rabiul-Awwal (Mfunguo sita) wa mwaka huu wa tano Hjiria (June 622), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliletewa khabari.
Kwamba kundi la mabedui (Waarabu waishio jangwani) wa “Daumatul-Jandal”-kwenye mipaka ya nchi ya Shamu-wanafanya fisadi katika ardhi.
Wanafunga njia, wanapora mali na kwamba wanajisogeza taratibu kuelekea Madinah. Mtume wa Allah akatoka na kundi la maswahaba wake alfu moja, akamtawalisha kushika hatamu za uongozi wa Madinah Subaau Ibn Arfatwah.
Akaenda kwa kujificha akipita kwenye njia zisizo zoeleka na watu, akitembea usiku na kujificha mchana mpaka akaikata njia kwa kadri ya siku kumi na tano.
Maharamia wale walipohisi majaji ya Mtume wa Allah, yakapatwa na khofu kuu na kuyapelekea kutapanyika huku na kule. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akapiga kambi katika eneo walilokuwepo na hakumkuta hata mtu mmoja miongoni mwa maharamia wale.
Akavituma vikosi na kuvitawanya kila upande kwenda kuyasaka maharamia yale, wakarejea salama wakiwa wamemkamata mmojawapo wa maharamia wale.
Wakamleta mbele ya Mtume wa Allah, akamuhubiria Uislamu nae akaridhia kusilimu, akasilimu.
Baada ya kukaa hapo kwa siku kadhaa, Bwana Mtume alirejea Madinah mwezi kumi Rabiul-Awwal akiliswaga kundi la wanyama aliowachukua baada ya maharamia kukimbia.