BWANA MTUME ATOKA NA WAPIGANAJI ALFU MOJA

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafunga bendera tatu. Akaitoa bendera ya Ausi akampa Usaid Ibn Hudhwayri aibebe na kuipeperusha yeye.

 Bendera ya khazraj akampa Al-Hubaab Ibn Al-Mundhir na ile ya Muhaajirina akampa Musw-ab Ibn Umeir-Allah awaridhie wao na maswahaba wote  wa Mtume aliye kipenzi chake.

 Baada ya kukamilisha zoezi hili la kukabidhi bendera za vita, Bwana Mtume akaagiza aletewe farasi wake, akampanda na kutoka kuelekea uwanja wa mapambano.

Akiwaongoza maswahaba wake alfu moja, mia moja miongoni mwao wakiwa wamevaa diraya (nguo za chuma maalumu kwa ajili ya vita).

 Akaenda huku kukiwa na kundi la maswahaba kuumeni na kushotoni kwake na mbele yake kukiwa na walinzi wawili; Sa’ad Ibn Ubaadah na Sa’ad Ibn Muaadh.

Kutoka huku kwa Mtume wa Allah na jeshi lake kwenda katika vita hivi vya Badri kulikuwa ni katika siku ya Ijumaa ya tarehe sita ya mwezi wa Shawwal {mfnguo mosi} wa mwaka wa tatu wa Hijrah.

 Bwana Mtume kabla hajaondoka alimpa uamiri wa kuwaswalisha watu wa Madinah swahaba wake Abdullah Ibn Ummu Maktuum.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaenda mpaka akafika mahala panapoitwa ‘Shaykhayn’, akapiga kambi hapo.

Kisha akalikagua jeshi na kuwaamuru kurejea Madinah wale aliowaona kuwa hawajafikia umri wa kushiriki vitani (wadogo). Miongoni mwa waliorudishwa na Mtume alikuwa ni kijana mdogo Raafii Ibn Khadiij na samurah Ibn Jundub-Allah awawiye radhi.

 Bwana Mtume akaambiwa hakika huyu Raafii unayemrudisha ni mlenga shabaha mzuri sana, ndipo alipompa rukhsa ya kushiriki vitani, samurah alipoona mwenzake kapewa rukhsa na yeye amekataliwa akalia sana na kusema:

Bwana Mtume amemruhusu Raafii na kunirudisha mimi na il-hali mimi ninamuangusha katika mieleka. Bwana Mtume akayasikia maneno haya,  ndipo akaamrisha wapigane mieleka na mshindi akawa ni Samurah.

Ushindi wake huu ndio uliomshawishi Bwana Mtume amuidhinishe kushiriki vitani kama alivyomuidhinisha Raafii.

 

ABDULLAH IBN UBAYYI AMTUPA MKONO BWANA MTUME NA KUMEGA THELUTHI YA JESHI.

 

Usiku ule Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie alilala pale pale Shaykhain mahala alipopiga kambi. Akampa kazi ya kulinda jeshi (kufanya doria) Muhammad Ibn Muslimah na Dhakwaan Ibn Qaysi akamfanya kuwa ni mlinzi wake yeye. Karibu na kuchomoza kwa alfajiri  Bwana Mtume akaliamuru jeshi kuondoka, akaenda nalo mpaka akafika ‘Shautwa’, hii ni bustani iliyo baina ya Madinah na Uhud. Hapa ndipo theluthi ya jeshi ilipojitenga na Bwana Mtume, Abdullah Ibn Ubayyi akajitoa na wafuasi wake mia tatu huku akisema:

“Vijana wamemtii na kuniasi mimi, ni kwa lipi khasa tuziue nafsi zetu hapa (kwa kupigana)? Abdullah Ibn Amrou Ibn Hiraam akajaribu bila mafanikio kuwashawishi waache msimamo wao huu. Akawaomba kwa jina la Allah wasiivunje fimbo ya umoja na wasiitupe mkono kaumu yao na Mtume wao mbele ya adui. Yote haya hayakufaa kitu bali ndio yaliwachagiza kusema:

 “Tungejua kuwa kuna kupigana bila ya shaka tusingelikufuateni”. Kitendo hiki kibaya kilisababisha pengo kubwa sana katika muundo wa jeshi na mtikisiko mkubwa katika nafsi za waislamu. Kitendo hiki kilikurubia kuleta ushawishi mkubwa wa kujitenga kwa koo za Baniy Haarithah katika kabila la Khazraj na Baniy Salamah katika kabila la Ausi. Lakini Allah akawahifadhi kwa sababu ya imani yao, wakarudi katika safu za jamaa na wakaendelea kusonga mbele na jeshi.

 

BWANA MTUME ALIPANGA JESHI LAKE NA KUWAUSIA WATUPA MISHALE WASIONDOKE SEHEMU WALIYOPANGIWA KWA HALI YO YOTE IWAYO.

 

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaendelea na safari yake Mpaka akafika ‘Uhud’.

Uhud, hili ni jabali lenye vijia vingi na ambalo linakatwa kati na mabonde kadhaa. Jabali hili linazunguka duara pana luelekea tambarare finyu ambako ndiko makurayshi wamefanya kituo chao.

Pindukopinduko za ardhi katika kuporomoka kwake zilisababisha mianya katika ardhi iliyoshabihiana na mashimo.

Mashimo haya yalifaa kutumika kwa vita vya kujihami ambamo mtu aliweza kurusha mishale au mawe kutokea humo na kisha kuyafanya ngao ya kumkinga dhidi ya mashambulizi ya adui.

Hii ndio sura ya Uhud; uwanja wa mapambano ulivyokuwa. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaamua kupiga kambi katika miamba iliyokuwa upande wao.

Miamba iliyo upande wa kilima kirefu kilichoitwa ‘Jabal Aynain’. Hapa ndipo Bwana Mtume kama amiri jeshi mkuu alipoanza kuwapanga safu maswahaba wake na kuwaanda kimapambano.

Akawaelekeza kulipa migongo jabali ili liwahami na mashambulizi yanayoweza kutokea kwa nyuma yao. Huku wakizielekezea nyuso zao upande wa Madinah kwa sura itakayowawezesha kuwa mkabala na bonde la Uhud, wakilichomozea kwa juu yake.

Akawaweka watupa mishale khamsini juu ya jabali Aynayn na akamfanya Abdullah Ibn Jubeir kuwa ndio kiongozi wao, atakayeongoza mashambulizi kutokea hapo juu jabalini.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawapa watupa mishale hawa dhima na jukumu la kuwalinda wenzao wasishambuliwe kutokea nyuma wakati vita vitakapouma.

 Akawaambia wasimpe adui hata mwanya mdogo wa kuipenya ngome yao hiyo na wasiondoke mahala hapo waislamu wakishinda au wakishindwa. Kisha akawafundisha namna ya kuwashambulia wapanda farasi kwa mishale kila watakapojaribu kuwakaribia kwa lengo la kuisambaratisha ngome yao.

Kisha akawasisitizia na kuwausia tena wasiiache ngome yao hiyo hata kama wataona wenzao wakisagwasagwa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomaliza kuzipanga safu na kukipangia kila kikosi mahala pake.

 Ndipo akalikhutubia jeshi la haki, akiwahimiza maswahaba wake kupigana kwa ajili ya Allah na akiwausia kuwa na subira.

Na akawaamuru kuwa wasianze kushambulia mpaka atakapowapa idhini ya kufanya hivyo. Wakati Bwana mtume alipokuwa ameshughulika na kupanga safu za jeshi lake, wakatokeza makurayshi katika tambarare iliyotandawaa chini ya jabali lile.

Hapa majeshi mawili haya yakawa ana kwa ana, waislamu wako kwa juu na makafiri kwa chini yao. Wanawake wa kikurayshi wakaonekana baina ya safu wakipiga dufu na kuimba nyimbo za kuwahamasisha na kuwapandisha mori wa vita wanaume wao.

 

MAKURAYSHI WAJARIBU KUWASHAWISHI WAISLAMU WAACHE KUWA PAMOJA NA BWANA MTUME.

 

Yalipokutana majeshi mawili haya na kabla ya kuanza kwa mapambano, Abuu Sufyaan alianza kuchukua mkakati wa kuwashawishi Muhajirina na Answaari kujitoa katika vita hivi.

Akatoa wito akisema:

“Enyi kusanyiko la Ausi na Khazraj, tuachieni wazi njia baina yetu na binamu zetu tupambane wenyewe kwa wenyewe, nasi tutakuondokeeni (hatutakupigeni)”.

Sauti yake hii ya wito ikasambaa angani na kusikiwa na waislamu, ikasindikizwa na Abuu Aamir aliyekuwa mtawa. Akajitokeza baina ya safu akiwalingania jamaa zake Ausi:

“Enyi Ausi, njooni njooni kwangu (muacheni huyo Muhammad)”. Haikuwa jawabu ya jamaa zake ila laana, kumfukuza na kumpopoa kwa mawe mpaka akakimbia akiwa kahizika na kufedheheka, akiwaambia washirika wake; makurayshi: “Kwa yakini shari imeisibu kaumu yangu baada ya kuondoka kwangu”.

Mkakati huu wa kuwashawishi waislamu kumtupa mkono Mtume ukashindwa kama ulivyoruka patupu ule mkakati wa shambulizi la ghafla la kuparaganisha. Ikawa sasa mapambano ya ana kwa ana hayakimbiliki, ni lazima kuingia mapambanoni.

Hapa sasa makurayshi wakajaribu kuwaweka kati waislamu na kuwakusanyikia kwa pamoja kwa kutumia harakati/mbinu ya mzinge (msonge)  wa haraka.

Ikrimah Ibn Abu Jahli akaiongozea bendera yake upande wa kushoto kwa lengo la kuizunguka kambi ya jeshi la haki, lakini wapi hakuweza.

 Khalid Ibn Al-Waleed naye akajaribu kwa upande wa kulia, watupa mishale wakamuachia mvua ya mishale, farasi wakarudi nyuma haraka.

Baada ya kushindwa kwa zoezi hili, mushrikina hawa wakarejea sehemu zao ili kujipanga upya na kufikiri namna ya mashambulizi itakayowaibua washindi.

 

 

BWANA MTUME ATOKA NA WAPIGANAJI ALFU MOJA

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafunga bendera tatu. Akaitoa bendera ya Ausi akampa Usaid Ibn Hudhwayri aibebe na kuipeperusha yeye.

 Bendera ya khazraj akampa Al-Hubaab Ibn Al-Mundhir na ile ya Muhaajirina akampa Musw-ab Ibn Umeir-Allah awaridhie wao na maswahaba wote  wa Mtume aliye kipenzi chake.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *