Maji kwa kuzingatia sifa na hukumu zake yanagawanyika sehemu/mafungu matatu:-
1: MAJI TWAHUUR au MAJI MUTLAQ hili ndilo fungu la kwanza la maji. Haya ni maji yenye sifa mbili kuu:-
a/ Yenyewe ni twahara.
b/ Yana uwezo wa kutwaharisha.
Maji yenye sifa hizi ni kama vile maji ya mvua, bahari, maziwa, mito, chemchem na visima.
Maji haya yatafaa kutumika katika twahara muda wa kubakia katika jumbile lake la asili bila ya kubadilika mojawapo ya sifa zake tatu ambazo ni:-
i/rangi
ii/Tamu (ladha)
iii/ Harufu (riha)
Hukumu ya maji haya ni kwamba yanaondosha hadathi zote mbili; kubwa na ndogo, na najisi. Maji haya pia hutumika kwa kunywa, kufulia, kupikia, na shughuli nyingine za maisha ya kila siku ya mwanadamu.
2: MAJI TWAHARA: Haya ni maji ambayo yana sifa moja tu ya kuwa yenyewe ni twahara lakini hayana uwezo wa kutwaharisha.
Haya ni maji twahara ambayo yamechanganyika na kitu kilicho twahara kama vile sabuni, sukari, zafarani, unga, asali au maziwa na kitu hiki kikaharibu moja wapo ya sifa zile tatu za maji yaani rangi, ladha au harufu.
Kuharibika huku kwa mojawapo ya sifa za maji ndiko kunakoyanyang’anya maji vile uwezo na nguvu yake ya kutwaharisha.
Hukumu ya maji haya: yenyewe ni twahara na yanaweza kutumika katika matumizi mengine yote ya mwanadamu kama vile kunywa, kuoshea vyombo na kadhalika ila hayawezi kutumiwa katika suala zima la twahara kama vile kuondosha hadathi ndogo (kutawadha),hadathi kubwa (kukoga) na kuondosha najisi.
3: MAJI NAJISI: Haya ni maji yaliyonajisika kwa kuingia ndani yake najisi itakayoharibu mojawapo ya zile sifa tatu za maji.
Hukumu ya maji haya ni kutokufaa kutumika katika twahara na matumizi mengine ya kila siku ya mwanadamu.