Zikipatikana sharti saba hizi tulizozitaja, swala ya Ijumaa itakuwa tayari ni wajibu kwa muhusika ila tu itakuwa haisihi ila kwa kupatikana sharti nne zifuatazo:-
1.Kuwa ndani ya mipaka ya mji:
Ili Ijumaa isihi kisheria ni wajibu isimamishwe ndani ya mipaka ya mji, kitongoji au kijiji chenye wakazi wasiopungua arobaini [40] ambao kwao swala ya Ijumaa ni wajibu.
Kwa mantiki hii, swala ya Ijumaa haisihi mawandani, kambini (mahala walipopiga makhema) wala katika kijiji ambacho kina watu walio chini ya idadi ya wanaopasiwa na Ijumaa. Lakini watu wa kijiji hiki wakisikia adhana ya swala ya Ijumaa inayotolewa katika kijiji kilicho jirani yao, kutawawajibikia kutoka kwenda kuswali swala ya Ijumaa katika kijiji jirani hicho.
Na kama hawaisikii adhana ya kijiji jirani, basi Ijumaa itaendelea kuwa sio wajibu kwao.
Dalili/ushahidi wa sharti hii:
Swala ya Ijumaa katika zama zake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na pia katika zama za makhalifa waongofu-Allah awawiye radhi-haikuswaliwa ila ndani ya mipaka ya mji.
Pembezoni mwa Madinah yalikuwepo makabila ya mabedui, haikuthibiti hata katika hadithi dhaifu kwamba waliswali Ijumaa au Bwana Mtume aliwaamrisha kuswali.
Kadhalika pamoja na kukithiri kwa safari za Mtume wa Allah nje ya Madinah, katu haikuthibiti kwa riwaya sahihi kwamba aliiswali swala ya Ijumaa safarini. Huu ndio ukweli, zingatia!
2.Kupatikana watu arubaini:
Idadi ya watu wanaojumuika kwa ajili ya swala ya Ijumaa na ambao kwao Ijumaa ni wajibu isipungue watu arubaini. Watu arubaini hawa wawe ni wanamume, watu wazima, wakazi wa mji husika.
Dalili ya sharti hii ya pili:
v Imepokelewa kutoka kwa Jaabir Ibn Abdillah-Allah amuwiye radhi-amesema: Suna ya Mtume imepita kwamba katika kila (idadi ya watu) arubaini na kuendelea ni Ijumaa (hiyo).
v Imepokelewa na Ka’ab Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kwamba wa mwanzo aliyewaswalisha Ijumaa ni As’ad Ibn Zaraarah-Allah amuwiye radhi-na wakati huo walikuwa ni watu arubaini.
TANBIHI:
Elewa na ufahamu ewe mpenzi ndugu msomaji wetu kwamba kuna makindano baina ya wanazuoni katika kadhia hii ya idadi ya watu inayofungamana nayo Ijumaa.
Ni arubaini, ama ni kumi na mbili au ni watu watatu, rejea vitabu vya Fiq-hi kwa ufafanuzi wa kina na rejea vema dalili za kila upande.
3. Iswaliwe katika wakati wa swala ya Adhuhuri:
Ni sharti swala ya Ijumaa iswaliwe ndani ya wakati wa Adhuhuri ndipo iweze kusihi.
Wakati wa swala ya Adhuhuri ukidhikika kiasi cha kutosalia kitambo cha kutosha kuiswali swala ya Ijumaa ndani ya kipindi hicho kabla ya kuingia kwa wakati wa swala ya Alasiri.
Katika hali kama hii kutawawajibikia hawa waliodhikiwa na wakati kuiswali Ijumaa adhuhuri rakaa nne badala ya mbili kama ambavyo ingeswaliwa ndani ya wakati.
Lau watu wataingia kuiswali swala ya Ijumaa, wakati wa Adhuhuri ukatoka na ilhali wao bado wangali ndani ya swala hiyo; hawajaimaliza.
Hapa wataigeuza swala ya Ijumaa kuwa Adhuhuri na kutimiza rakaa nne kwa nia ile ile ya Ijumaa waliyoanza nayo.
Dalili ya sharti hii:
Dalili na ushahidi huu wa sharti hii ya tatu ya kusihi kwa Ijumaa ni kitendo chake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuiswali swala ya Ijumaa ndani ya wakati huo wa Adhuhuri. Haya ni kama yanavyofahamika kupitia hadithi zifuatazo:-
I. Imepokelewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-“alikuwa akiswali swala ya Ijumaa wakati jua linapopinduka”. (Na huo ni wakati wa Adhuhuri kwani jua halipinduki ila wakati huo). Bukhaariy-Allah amrehemu.
II. Imepokelewa kutoka kwa Salamah Ibn Al-Ak-waa-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulikuwa tukiswali pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-swala ya Ijumaa. Kisha tukiondoka (kurudi majumbani) na ilhali kuta zikiwa hazina kivuli tunachoweza kujikinga nacho”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
III. Imepokelewa kutoka kwa Sahli Ibn Sa’ad-Allah amuwiye radhi-amesema: “Hatukuwa tukipata lepe la mchana (hatulali usingizi mdogo wa mchana) wala chakula cha mchana ila baada ya (kuswaliwa) swala ya Ijumaa”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
Hadithi zote hizi zinafahamisha kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa haiswali swala ya Ijumaa ila ndani ya wakati wa Adhuhuri.
Na si tu ndani ya wakati wa Adhuhuri bali ndani ya wakati wa mwanzo wa Adhuhuri, elewa na ufahamu hivi.
Kwa mantiki hii basi, hakusihi kuiswali swala ya Ijumaa kabla ya wakati huu wa Adhuhuri wala baada yake, yaani baada ya kumalizika na kuingia Alasiri.
IV. Ijumaa iwe moja tu katika mji ila kwa dharura:
Kumeshurutizwa kutoidadika (kutokuwa nyingi) swala za Ijumaa katika mji au kitongoji kimoja muda wa kumkinika hilo. Hii ni kutokana na ule wajibu wa kukutana watu wa mji mmoja mahala pamoja ili kuonyesha nembo ya swala tukufu ya Ijumaa.
Angalia:
a) Iwapo watu watakithiri (watakuwa wengi) kiasi cha kushindikana kukusanyika mahala pamoja kutokana na ufinyu wa mahala hapo. Katika hali na mazingira haya kutajuzu kuwepo na Ijumaa nyingi kwa kiasi cha kukidhi haja tu.
b) Lau swala za Ijumaa zitakuwa nyingi katika mji mmoja bila ya kuwepo na haja ya kisheria ya kufanya hivyo. Haitasihi miongoni mwa Ijumaa hizo ila ile iliyozitangulia nyingine.
Na mazingatio na marejeo katika kutangulia ni katika kuanza na sio katika kumalizika. Kwa mantiki hii basi, ile swala ya Ijumaa ambayo imamu wake ataanza kuswali kabla ya zile nyingine, hiyo ndiyo itakayokuwa sahihi.
Na nyingine zote zilizobakia zitakuwa ni batili na kutawapasa watu waliozihudhuhuria kuswali Adhuhuri mahala pa Ijumaa.
c) Ikiwa haijulikaniwi ni Ijumaa ipi iliyotangulia, basi Ijumaa zote hizo zitakuwa ni batili. Na kutawalazimu watu wa Ijumaa hizi kukusanyika mahala pamoja iwapo hilo linamkinika na wakati ukawa unaruhusu, waswali tena Ijumaa upya.
Iwapo hili halitawezekana, wote watalazimika kuswali Adhuhuri kwa ajili ya kuunga mapungufu yaliyojitokeza.
Dalili ya sharti hili:
Sharti hili la nne la kusihi kwa swala ya Ijumaa linatokana na ukweli kwamba si tu katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Bali hata katika zama za makhalifa waongofu-Allah awawiye radhi-na pia katika zama za Taabiina. Ijumaa haikuswaliwa ila mahala pamoja tu katika mji/kitongoji kizima. Zama/enzi hizo ulikuwepo katika mji/kitongoji msikiti mkubwa kushinda misikiti yote iliyopo katika mji/kitongoji husika. Msikiti huu ulijulikana kama “AL-MASJIDUL-JAAMII”-yaani “MSIKITI WA IJUMAA”, inamoswaliwa ndani yake Ijumaa ya mji/kitongoji hicho. Na misikiti mingine ilibaki ikitumiwa kwa swala tano nyingine, yaani zile za kila siku na sio Ijumaa. Hivi ndivyo tunavyoweza kufahamu kupitia hadithi zifuatazo:-
I. Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini; Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Watu walikuwa wakija mara kwa mara siku ya Ijumaa kutoka majumbani mwao na kutoka (pande) za ‘AWAALIY” (Hizi ni sehemu/vitongoji vya mashariki mwa Madinah.
Kilichokuwa karibu zaidi na Madinah kilikuwa umbali wa maili tatu au nne kutokea mjini Madinah palipokuwa pakiswaliwa hiyo Ijumaa)”.Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
II. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba amesema:
“Hakika Ijumaa ya mwanzo iliyoswaliwa baada ya ile Ijumaa (iliyoswaliwa) katika msikiti wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-(ilikuwa) katika msikiti wa Abdili-Qaysi huko Juwaathaa (hiki kilikuwa ni kimojawapo ya vitongoji vya nchi ya Bahrein enzi hizo) pande za Bahrein”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
Falsafa ya sharti hili ni kwamba kitendo cha kutosheka na mahala pamoja watu wote kinapelekea zaidi kufikiwa kwa lengo la swala hii ya Ijumaa inayowakusanya watu wengi kwa pamoja mara moja kila juma. Na lengo hili si lingine bali ni kule kuwa wamoja waislamu na kuonyesha mshikamano utakaowaogofya na kuwatisha maadui wao. Na kitendo cha kutapanyika huku na huko bila ya haja, hutengeneza na kujenga mazingira ya kugawika na kutengana na hivyo kutoa mwanya kwa adui kuingia kati yetu kirahisi na kutugonganisha wenyewe kwa wenyewe.