KUSILIMU KWA HAMZA NA UMAR

Kwa upande mwingine adhabu, mateso, maudhi na makero ya Makurayshi kwa waislamu yaliwaletea faraja waislamu.

Mateso na makero haya ndiyo yaliyokuwa sababu na changamoto kubwa ya kusilimu mtu mkubwa, mwenye sauti na nguvu katika mji wa Makkah.

Mtu aliyekubaliwa na kutambuliwa na Makurayshi kama shujaa. Mtu huyu si mwingine bali ni ami yake Mtume Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib, mtu aliyekuwa nguzo kuwa kwa upande wa Makurayshi.

Sababu ya kusilimu kwa simba wa Allah Hamzah, jina alipewa kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kupigania dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Siku moja, Hamzah alitoka asubuhi akiwa amevaa nguo nadhifu za kifakhari, akiwa na upanga wake, akitembea kwa maringo, kifua mbele. Katika matembezi yake hayo alimpitia mjakazi mmoja aliyekuwa njiani, mjakazi yule akamwambia

” Lau Baba Amaarah (Hamzah) angeliyasikia maneno mabaya aliyoyasema Abu Jahli kumwambia mwana wa nduguye Muhammad, basi asingelitembea kwa maringo kiasi hiki”.

 Hamzah akamuuliza yule mjakazi “Kwani amesema nini?” Akamwambia

“Hakika Abu Jahli amemtukana Muhammad matusi machafu ya kufedhehesha sana”.

Hamzah akaondoka pale akiwa amepandwa na mori wa hasira, amekuwa mwekundu kutokana na hasira, akamuendea mbaya wake Abu Jahli.

Akamkuta akiwa amekaa barazani na viongozi wa Makurayshi, bila hata ya kuwaslimia kama ilivyokuwa ada na desturi yao, akamuwasha kibao cha nguvu cha uso na kumwambia kwa sauti ya ukali iliyojaa hasira zote.

“Vipi unathubutu kumtukana Muhammad na ilhali mimi nimekwishaingia katika dini yake?”

Baada ya kusema maneno hayo, Hamzah akaondoka akenda kwa Mtume na kuutangaza Uislamu wake, akasilimu.

Kusilimu kwake ikawa ni sababu ya Uislamu na Waislamu kupata nguvu na utukufu. Makurayshi wakatambua kwamba sasa Muhammad amepata ngome kuu na Hamzah hatakuwa tayari kuona mwana wa nduguye akidhulumiwa na kuonewa.

Hamzah baada ya kusilimu aliulekeza ushujaa na nguvu zake zote katika kuitetea na kuuipigania dini ya Mwenyezi Mungu, ni kwa sababu hii ndiyo Bwana mtume akamuita “Simba wa Allah” – Allah amuwiye radhi yeye na maswahaba wote wa Bwana Mtume.

Anga la Mji wa Makkah lilitanda khofu na fazaa kubwa kutokana na waislamu kuhama Uhabeshi na kusilimu kwa shujaa Hamzah.

Mambo mawili haya yaliacha pengo kubwa sana kwa upande wa Makurayshi.

Watu wenye hisia na muono wa mbali waliliona pengo hili na hatari yake ya baadaye.

Miongoni mwa watu hao alikuwa ni Umar Ibn Khatwaab, jambo hili lilimkosesha usingizi Umar, ambaye alikuwa ni kijana shujaa, bingwa wa vita na fakhari ya Makurayshi.

Alikuwa adui mkubwa wa Mtume na waislamu. Umar akaona balaa hili la jamaa zake kuhamia Uhabeshi, kutukaniwa dini yao na Makurayshi kugombana na kuzozana wao kwa wao, yote haya yamesababishwa na huyu Muhammad.

Umar akaona suluhisho na ufumbuzi pekee kwa tatizo hili ni kuukata mzizi wa fitina hiii, kwa hivyo akaazimia kumuua Mtume kwa mkono wake mwenyewe ili watu wapumzike na hicho walichokiita wao shari lake.

Ndipo siku moja akatoka nyumbani kwake akiwa na upanga wake kibindoni, anamuendea Bwana Mtume ili amkate kichwa. Mwanasira mkubwa Ibn Ishaaq – Allah amrehemu – analisimulia tukio hili, anasema :-

 “Nuaim Ibn Abdillah akakutana nae (Umar) njiani, akamuuliza : Unakwenda wapi ewe Umar ? “(Umar) akamjibu

“Ninamkusudia huyu Muhammad ambeye amewatenganisha Makurayshi, ameikosoa dini yao na kuwatukania miungu wao, naenda kumuua !” Nuaim akamwambia wallah, nafsi yako inakudanganya ewe Umar !

“Hivi unafikiri Baniy Abdi Manaaf watakuachia utembee juu ya ardhi utakapomuua Muhammad? Kwa nini basi usianze kutengeneza na kushughulikia masuala ya ndugu zako kwanza?” (Umar) akamuuliuza (Nuaim):

Ndugu zangu gani hao? Akamjibu : Shemeji yako na mwana wa ami yako Said Ibn Zayd na dada yako Fatmah Bint Khatwaab, Wallah wamekwisha silimu na kumfuata Muhammad katika dini yake, basi anza na hawa kwanza.

Ibn Ishaaq anaendelea kusema pale pale Umar akabadili njia, akamuendea dada na shemeji yake nyumbani kwao.

Akawakuta pamoja na Khabaah Ibn Arat akiwasomea Surat Twaaha katika karatasi aliyoishika.

 

 Walipomsikia Umar, Khabaab akakimbia na kwenda kujificha, Fatmah akaificha ile karatasi. Umar alipoingia akawauliza: Ni sauti gani hii niliyoisikia ? Wakamjibu: Hukusikia cho chote. Akawaambia : hapana.

Wallah nimesikia kitu na nimekwishaambiwa kwamba nyinyi mmekwisha mfuata Muhammad katika dini yake!

Umar kwisha kusema maneno hayo, akamtia kabali shemeji yake. Dada yake kuona hivyo, akamuendea Umar ili amnasue mumewe, Umar akampiga dada yake kibao cha nguvu kilichomtoa damu.

Hapo ndipo ile nguvu ya imani ilipowajia dada na shemeji yake, wakamwambia : Naam, sisi tumekwisha silimu na tumemuamini Allah na Mtume wake, sasa wewe fanya utakalo ! ama kweli damu si maji.

Umar alipoiona damu ya dada yake ikichuruzika, moyo wake ukajawa na huruma na akajuta kwa nini amefanya kitendo hicho, akamwambia dada yake.

 Hebu nipe hiyo karatasi ambayo nimekusikieni mkiisoma hivi punde, ili nipate kuona alichokuja nacho Muhammad.

Umar alikuwa ni mtu anyejua kusoma na kuandika. Dada yake akamjibu bila ya khofu wala woga;

Ewe kaka yangu, hakika wewe ni najisi kutokana/kwa sababu ya ushirikina wako na karatasi (kitabu) hii haigusi/haishiki ila aliye twahara, Umar kwa kuwa alikuwa na shauku ya kutaka kujua kilichoandikwa ndani ya ile karatasi, akainuka akaenda kukoga.

Hapo ndipo dada yake alipompa ile karatasi na ilikuwa imeandikwa Suurat – twaha (sura ya 20), akaisoma. Alipoisoma mwanzo mwanzo tu wa sura akasema :

Maneno mazuri na mtukufu yaliyoje ! Khabbaab alipoisikia kauli hiyo akatoka mafichoni alipokuwa, akamwambia Umar: Ewe Umar, Wallah mimi ninatarajia kwamba Allah ameikubali dua ya Mtume wake kwako, kwani mimi nimemsikia jana akisema:

“Ewe Mola wa haki upe nguvu (usaidie)Uislamu kwa (kusilimu) Amr Ibn Hishaam (jahl) au Umar Ibn Khatwaab” Khabab akaendelea : Ala ! ala! Ewe Umar,

Umar akamwambia Hebu nifahamishe alipo Muhammad, nikasilimu. Khabbaab akamwambia :

Yuko katika nyumba moja, jirani na kilima Swafaa pamoja na kundi la maswahaba wake.

Umar akamweka upanga wake katika ala kibindoni, akatoka na kumuendea Bwana Mtume.

 Alipofika akagonga mlango, walipoisikia sauti yake, akainuka mtu mmoja na kwenda kuchungulia, akamuona Umar akiwa na upanga wake mkononi.

Akarejea kwa Mtume akiwa amefadhaika na kumwambia : Umar huyo, yuko mlangoni na upanga wake.

Hapo ndipo (simba wa Allah) Hamzah Ibn Abdul- Mutwalib akasema kwa ushujaa: Muacheni apite, ukiwa amekuja kwa kheri ameipata na iwapo amekusudia shari, tutamuua kwa upanga wake mwenyewe. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akasema

“Muacheni apite”. Alipoingia Mtume akamuuliza : “Umejia nini? Ewe mwana wa Khatwaab?” Umar akamjibu: Ewe Mtume wa Allah, nimekuja ili nimuamini Allah na Mtume wake. Ibn Is-haaq anasema :

Mtume wa Allah akapiga takbira iliyowatambulisha maswahaba kwamba Umar amesilimu.

Ama kweli baada ya dhiki faraja, hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyowafariji waislamu wanyonge kwa kuwaleta katika Uislamu watu hawa mashuhuri.

 Kusilimu kwa Hamzah na Umar ilikuwa ni katika mwaka wa tano wa utume

KUSILIMU KWA HAMZA NA UMAR

Kwa upande mwingine adhabu, mateso, maudhi na makero ya Makurayshi kwa waislamu yaliwaletea faraja waislamu.

Mateso na makero haya ndiyo yaliyokuwa sababu na changamoto kubwa ya kusilimu mtu mkubwa, mwenye sauti na nguvu katika mji wa Makkah.

Mtu aliyekubaliwa na kutambuliwa na Makurayshi kama shujaa. Mtu huyu si mwingine bali ni ami yake Mtume Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib, mtu aliyekuwa nguzo kuwa kwa upande wa Makurayshi.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *