Katika mwaka uliofuatia kundi la watu wasiopungua kumi na mbili kutoka (Madinah) lilikuwa ni miongoni ma uma uliohudhuria msimu wa Hijjah kutoka pande mbalimbali za bara Arabu.
Kundi hili lilikusanya watu kumi kutoka katika kabila la Khazraji na wawili wakiwa ni wa kabila la Ausi.
Ausi na Khazraji ndio makabila makubwa yaliyounda wazalendo wa Yathrib wakati huo.
Historia imetusajili majina ya watu hawa muhimu katika historia nzima ya uislamu, watu ambao mchango wao umekuwa ni sababu ya kuifikisha uislamu hapa ulipo leo. Kwa upande wa Khazraji walikuwa ni mabwana:-
1. As’ad Ibn Zaraarah.
2. Auf Ibn Al-Haarith
3. Muaadh Ibn Al-Harith
4. Raajiri Ibn Maalik
5. Dhakawaan Ibn Swaamti
6. Ubaadah Ibn Swaamit
7. Yaziyd Ibn Tha’alabah
8. Abbaas Ibn Ubaadah
9. Uqbah Ibn Aamir, na
10. Qutwabah Ibn Aamir
ama kwa upande wa Ausi walikuwa
1. Abul-Haytham Ibn Tiyhaani
2. Uwaym Ibn Saa’idah
Kundi hili lilikutana na Bwana Mtume usiku katika sehemu ijulikanayo kama “Aqabah”.
Hapa ni mahala ambapo shetani hupigwa mawe wakati wa kutekeleza ibada ya Hijjah tangu zama hizo hadi leo hi.
Bwana Mtume katika mkutano wake huu wa siri na uficho mkubwa na watu hawa kumi na mbili, aliitumia fursa hii ya pekee kuwapasha zaidi habari za uislamu.
Katika kuhitimisha kwake mkutano huu Mtume aliwataka watu hawa wapeane nae ahadi ya utii na uaminifu.
Nao kutokana na mafundisho ya uislamu yaliyokwishaana kuziathiri nyoyo zao, bila kusita walikubali.
Wakafunga maagano ya utii na uaminifu kwa mtume wa Allah na maagano haya yakaitwa “Maagano ya kwanza Aqabah” maagano haya kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria yalikuwa ni katika mwaka wa kumi na mbili (12) wa utume.
Qur-ani tukufu imetusajilia na kutuwekea kumbukumbu za tukio hili lililoleta mapinduzi makubwa katika historia ya uislamu, tusome pamoja
“BILA SHAKA WALE WANAOFUNGAMANA NAWE KWA HAKIKA WANAFUNGAMANA NA ALLAH, MKONO WA ALLAH UKOO JUU YA MIKONO YAO. BASI AVUNJAE AHADI (hizi) ANAVUNJA KWA KUIDHURU NAFSI YAKE NA ATEKELEZAYE ALIYOMUAHIDI ALLAHA (Allaha) ATAMLIPA UJIRA MKUBWA,”(48:10)
Ni yapi yaliyokuwamo ndani ya maagano/mafungamano haya? Ibn Ishaaq mtaalamu mashuhuri wa fani ya sira na historia kwa ujumla amepokea ikiwa nai riwaya itokanayao na Bwna Ubaadah Ibn Swaamit (mmoja wapo wa wanafungamanao) Amesema:
“Tuliagana na Mjumbe wa Allah Rehema na Amani zimshukie ya kwamba:-
Hatutamshirikisha Allah na chochote, wala
1. Hatutoiba, wala
2. Hatutozini, na wala
3. Hatutawauwas watoto wetu, wala
4. Hatutaleta uzushi tunaouzua tu wenyewe, na wala
5. Hatutamuasi katika jambo jema.
Mtume akasema kutuambia
“Mkiyatekeleza mtapata pepo, na ikiwa mtaghushi (mtafanya udanganyifu mkavunja) lolote katika (ahadi) hizo (mlizozitoa). Mtaadhibiwa kwa kupata adabu/adhabu yake (kosa hilo) hapa duniani na hiyo ndio kafara yake. Ama (mtakapuvunja ahadi) na mkasitiriwa (msijulikane) mpaka siku ya Qiyamah, basi suala lenu hilo litakuwa katika mikono ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, akitaka ama atakuadhibuni au atakusameheni.”
Watu wote hawa walisilimu mbelle ya Mtume na kuwa waislamu wema, watiifu na waaminifu kwa Allha na Mtume wake Ibn Is-haaq Allah amrehemu anazidi kusema
“Walipoondoka watu hawa, Mtume wa Allah Reheme na Amani zimshukie aliwapa (Swahaba wake) Musw-ab Ibn Umayr na akamuamrisha akawasomesha Qur-ani, awafundishe uislamu na Fiq-hi ya kiislamu. Akawa Musw-ab akiitwa (Msomeshaji/mwalimu) katika mji wa madina’
Madinah mwalimu Musw-ab Ibn Umayr alifikia katika nyumba ya Bwana As-ad Ibn Zuraarah wa ukoo wa Baniy Najjaar.
Huyu ndiye aliyekuwa ukoo wa mwenyeji wake. Ni vema tukakumbuka kwamba bwana huyu alikuwa ni miongoni mwa watu wa kabila la Khazraji waliosilimu mbele ya mtume na kuhudhruia maagano yote mawili.
Lile la kwanza la Aqabah na la pili lililofanyika hapo hapo Aqabah ndugu wawili hawa katika dini wakashirikiana pamoja katika kuutangaza uislamu Madinah. Walitumia njia ya nasaha na upole katika kuwakinaisha na kuwashawishi wenyeji wa madinah kuingia katika uislamu.
Ibn Ishaaq na Ibn Al-athiyr wanasimulia baadhi ya yaliyotukia madinah wakati alipoingia katika mji huo mwalimu Musw-ab wanasema siku moja Asad Ibn Zuraarah alitoka na mgeni wake Mwalimu Musw-ab Ibn Umayr, wakingia katika bustani ya Baniy Dhwafar, watu waliokwishasilimu wakakaa kuwazunguka Sa’ad Ibn Muaadh na Usayd Ibn Hudhwayr wakasikia juu ya mkutano huu hawa wakati huo walikuwa ni viongozi wa koo zao na walikuwa ni makafiri, bado hawajasilimu.
Saa’ad akamwambia mwenziwe Usayd
“waendee watu wawili hawa waliokuja majumbani mwetu uwakemee na uwakataze. Kwani lau si As’ad Ibn Zuraarah ambaye ni mwana wa mama yangu mdogo, ningekutoshea kazi hii.
“baada ya kuambiwa hivyo tu, Usayd akatwaa mkuki wake na kuwaendea alipofika akawauliza. Ni lipi lililokuleteni, kuwatukana wanyonge wetu?
Tuondokeeni! Mwalimu Musw-ab akamwambia: Hukai kidogo ukasikiliza? Ukiliridhia tulisemalo likubali, na ukilichukia tutaacha likuchukizalo.
Usayd akasema “Umefanya uadilifu,” akakaa Musw-ab kama mwalimu mzoefu bila kuchelewa akanza kumpasha juu ya Uislamu, nae akisikiliza kwa makini.
Alipokoma, Usayd akasema:
“Habari nzuri na njema zilioje hizi! Hivi mnafanyaje mnapotaka kuingia katika dini hii? Wakamwambia {Musw-ab na As-ad}: unakoga na kuzitwaharisha nguo zako, kasha unatoa shahada ya haki, halafu unaswali rakaa mbili Usayd akayafanya yote hayo na akasilimu kasha akawaambia hakika nyumba yangu kuna mtu mmoja, huyo akikufuateni hatobakia nyuma yeyote katika watu wake ila atakufuateni, mtu huyu ni Sa’ad Ibn Mu’aadh, nami nitamtuma kwenu.
Kisha akashika njia kumuendea Bwana Sa’ad na watu wake. Sa’ad alipomuangalia akasema:
Namuapia Mwenyezi Mungu, hakika Usayd amekujieni na uso mwingine, sio ule aliotoka nao hapa! Halafu akamuuliza rafiki yake Usayd Hebu niambie kweli, umefanya nini?
Akamjibu Nimezungumza na watu wawili wale, basi wallah! Sikuona ubaya wowote kwo. Nae yaani Sa’ad akawaendea kama alivyowaendea rafiki yake akiwa mkali kweli kweli.
Akapozwa kwa maneno mazuri kama aliyoambiwa mtangulizi wake, akalainika na kukaa chini kusikiliza, akasomewa Qurani.
Akaukubali uislamu na kusilimu kasha akarudi kwa jamaa zake akiwa na rafikiye Usayd Ibn Zuraarah, alipofika akawauliza:
Enyi kizazi cha kukoo wa Abdil ash-hal, mnanitambuaje mimi kwenu? Wakamjibu kwetu wewe ni Bwana na mbora wetu. Akawaambia Basi ikiwa msemayo ndiyo ni haramu kuanzia sasa nyinyi kuzungumza na mimi, nyote waume kwa wake mpaka mumuamini Allah na Mtume wake!
Basi baada ya kumaliza kusema hivyo tu hakubakia mwnaamume wala mwanamke katika jamaa zake ila alisilimu.
Mwalimu Musw-ab na As’ad wakaendelea kuulingania uislamu Madinah mpaka haikusalia nyumba yoyote ila walikuwemo humo waislamu wake kwa waume.
Kukawa hakuna kinachozungumzwa Madinah ila ni juu ya Uislamu tu.
Hivi ndivyo yalivyokuwa maagano ya kwanza ya “Aqabah” yaliyokuwa kati ya Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie na kundi la watu kumi na mbili kutoka Madinah {Yathrib} Allah awawiye radhi.