Naam, ni kweli isiyo na shaka kwa kila muumini kwamba mashahidi wale waliokufa katika vita vya Uhud kwa ajili ya kuipigania dini ya Allah.
Na wale wote watakaokufa kwa ajili hiyo tu, hawafi kama walivyodhania mushrikina wa kikurayshi na wale wote wasioifahamu maana halisi ya mauti.
Wasiojua katika uhai huu ila picha na sura yake ya dhahiri tu.
Dhana na fikra zao hizi haziiondoshi hakika na ukweli kuhusu suala zima la mashahidi. Kwa yakini si suala la kupingwa kwa kila mwenye imani hai na sahihi kwamba mashahidi wako hai wanaruzukiwa mbele ya Bwana Mlezi wao waliyemsabilia maisha yao.
Wakizifurahia neema alizowapa Allah kwa fadhila zake, kutokana na maisha mazuri waliyoandaliwa huko wanatamani kurudi tena duniani. Waje kuipigania dini ya Mola wao na wauawe tena katika kuipigania dini ya Allah ili warudufishiwe neema za Mola wao.
Imamu Ahmad-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Ndugu zenu walipouliwa katika vita vya Uhud, Allah aliziweka roho zao ndani ya ndege wa kijani. Zikaenda (roho hizo) katika mito ya peponi na kula katika matunda yake na kwenda kupumzika katika kandili za dhahabu chini ya jivuli la Arshi. Walipopata uzuri wa malaji yao, manywaji yao na malazi yao, wakasema: Ee laiti ndugu zetu (walio hai) wangeliyajua aliyotufanyia Allah ili wasidhoofike katika jihadi na wala wasikimbie vitani….! ndipo Allah Mtukufu akasema: Mimi nitakufikishieni (salamu zenu hizi) kwao…ndipo Allah akateremsha aya hizi: “WALA USIWADHANI WALE WALIOUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH KUWA NI WAFU (maiti). BALI WAHAI, WANARUZUKIWA KWA MOLA WAO WANAFURAHIA ALIYOWAPA ALLAH KWA FADHILA ZAKE; NA WANAWASHANGILIA WALE AMBAO HAWAJAJIUNGA NAO, WALIO NYUMA YAO (wako ulimwenguni, bado hawajafa); YA KWAMBA HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA HAWATAHUZUNIKA. WANASHANGILIA NEEMA NA FADHILA ZA ALLAH, NA KWAMBA ALLAH HAPOTEZI UJIRA WA WANAOAMINI”. [3:169-171]
II/. ATHARI ZA VITA VYA UHUD.
MAYAHUDI NA WANAFIKI WAFURAHIKIA MSIBA MKUU ULIOWASIBU WAISLAMU KATIKA VITA HIVI NA KUITUMIA FURSA HIYO KUENEZA UVUMI MADINAH.
Ilikuwa ni sehemu ya maumbile waislamu kuhuzunika kutokana na msiba uliowapata katika vita vya Uhud na kujawa na majuto kwa kuwa yote yaliyowapata yalisababishwa na wao wenyewe.
Wakajutia yaliyowapata mashahidi wao kuuliwa na kukatwakatwa viungo vyao na wakajuta kwa majeraha mabaya yaliyompata Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.
Na pia haikuacha kuwa ni sehemu ya maumbile maadui wa waislamu Madinah na viungani mwake kuyaonea raha na furaha yaliyowasibu waislamu.
Nyoyo zao zikajawa na furaha kuu pale walipowaona waislamu wakiingia Madinah hali ya kuwa wanyonge wakitawaliwa na kimya kikuu na unyong’onyevu.
Huku wakiwa wamefunikwa na wingu la huzuni na kukimwa na kufura kwa chuki na ghadhabu kutokana na kitendo walichokifanya na kuwa wao ndio sababu ya yote yaliyowasibu na kuwapa maadui kicheko cha ushindi.
Mayahudi na wanafiki hawakuona raha kukificha kicheko na furaha yao hiyo kutokana na yaliyowapata waislamu.
Kwa hivyo wakaanza kuidhihirisha bayana furaha na kicheko chao na isitoshe wakaitumia fursa hiyo kuwatukana waislamu na Uislamu.
Wakaziachilia ndimi zao katika kumsema vibaya Mtume wa Allah, da’awa (ulingano) yake na maswahaba wake. Mayahudi wakaanza kumtilia mashaka na wasiwasi Mtume wa Allah na da’awa yake wakisema:
“Lau angelikuwa Mtume kweli, basi wasingelimshinda na wala asingepatwa na yaliyompata. Lakini yeye anatafuta ufalme tu, dola iwe yake aitawale basi”.
Wanafiki nao kwa upande wao wakaanza kuchukua juhudi za makusudi kuwatenganisha watu na Mtume wa Allah.
Na kuwakumbushia waislamu huzuni ya mashahidi wao waliokufa vitani na kuwalaumu na kuwashtumu vikali kwa kusababisha kufa kwa ndugu zao hao.
Wakijionyesha kwamba wao walichukua uamuzi wa busara pale walipoamua kurudi nyuma njiani wasiende vitani.
Na kwamba lau waislamu wangeliwatii na kuwasikiliza pale walipowatolea wito wa kurudi, basi yasingeliwapata yaliyowapata.
Kwa hivyo basi yote yaliyowapata ni matokeo ya ukaidi na upasito wao. Allah Mtukufu ametusajilia maneno ya wanafiki hawa, haya na tuyasome huku tukichukua mazingatio:
“WALE WALIOSEMA JUU YA NDUGU ZAO-NA (wao wenyewe) WAMEKATAA KWENDA VITANI: WANGALITUTII WASINGEUAWA. SEMA: JIONDOLEENI MAUTI (nyinyi wenyewe msife maisha) IKIWA MNASEMA KWELI”. [3:168]
Mayahudi na wanafiki wakakithirisha kumsema vibaya Bwana Mtume na waislamu, mpaka Madinah nzima ikachemka kwa uvumi mithili ya mchemko wa sufuria kubwa la maji.
Kiasi kwamba uvumi huo ulikurubia kulipua fitna kubwa, Bwana Mtume akachelea waislamu wasijemilikiwa na udhaifu na uvumi huu usijefikia lengo lake katika nafsi zao.
Propaganda hizi zikifanikiwa kama walivyokusudia wapikaji na wasambazaji wake zitasababisha kuporomoka kwa haiba na kitisho cha Uislamu ndani ya Madinah na nje ya mipaka yake.
Kadhalika Bwana Mtume alichelea tamaa isijewasukuma makurayshi kuwashambulia waislamu shambulizi la kumaliza nao wakiwa katika hali hii ya kizaizai.
LAZIMA ICHUKULIWE HATUA YA MAKUSUDI NA YA HARAKA ITAKAYOWAREJESHEA WAISLAMU KUJIAMINI KWAO NA KURUDISHA TISHO LAO KATIKA NAFSI ZA MAADUI ZAO. HILI LIKAZAA VITA VYA HAMRAAUL-ASADI.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaona kwamba hapana budi ichukuliwe hatua ya haraka itakayoufagilia mbali unyonge uliozalishwa na maadui katika nyoyo za waislamu.
Na lazima ipatikane tiba muafaka itakayowarejeshea waislamu kujiamini kwao na kuwarudishia tisho lao walilolipoteza katika nafsi za maadui zao.
Ndipo Bwana Mtume akaazimia kutoka na maswahaba wake kuwafuatia makurayshi bila ya kubali (kujali) wala kuyaangalia majeraha, machungu, maumivu na uchovu waliokuwa nao.
Ilikuwa ni lazima achukue hatua hiyo ya makusudi na ya haraka bila ya kungojea ili kuondosha hatari kubwa iliyokuwa inawakabili waislamu na Uislamu kwa ujumla. Katika kuchukua kwake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hatua hii alikuwa akilenga mambo mawili ya msingi:-
MOSI: Kuwakatia njia na uwanja hawa wapika na waenezaji uvumi huu
hatari kuliko silaha kali. Ahakikishe kuwa haupi uvumi huu hata
mwanya wa tundu ya sindano kufanya kazi yake katika nafsi za
maswahaba wake.
PILI: Kuwaonyesha na kuwathibitishia makurayshi na washirika wao
kwamba waislamu bado wana nguvu yao ile ile pamoja na yote
yaliyowasibu. Bado wanayo nguvu inayowawezesha kuwaogope
sha maadui wa Allah na maadui zao.
Mwanasira; Ibn Is-haaq-Allah marehemu-anasema:
“Ilipofika kesho ya siku ya Uhud ya mwezi kumi na sita Shawwal {Mfunguo mosi}. Muadhini wa Mtume wa Allah aliwaadhinia watu kumfuata adui, akatangaza: “Asitoke asitoke pamoja nasi ye yote ila yule aliyekuwa pamoja nasi jana”. Jaabir Ibn Abdillah Ibn Amrou Ibn Hiraam akamzungumza Bwana Mtume, akamwambia:
“Ewe Mtume wa Allah! Hakika baba yangu alikuwa amenipa uangalizi wa dada zangu saba na akaniambia: Ewe kijana changu wee, kwa yakini hainipasii mimi wala wewe kuwaacha watoto hawa wa kike peke yao bila ya kuwa na mwanamume wa kuwaangalia. Na sikuwa mimi ni mwenye kukufadhilishia kupigana jihadi pamoja na Mtume wa Allah kuliko nafsi yangu, basi wewe bakia uwaangalie dada zako (mimi nakwenda kupigana). Basi nikabakia kuwaangalia”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-(akaukubali udhuru wake huu uliomzuia kutoka nae ile siku ya kwanza) akampa idhini ya kutoka pamoja nae (leo). Na hakika si vinginevyo, Mtume wa Allah alitoka kwa ajili tu ya kuwaogopesha na kuwatisha maadui. Na ili iwafikilie khabari kwamba yeye ametoka kuwafuatilia ili watambue kuwa bado ana nguvu, na kwamba yaliyowasibu hayakuwadhoofisha katika kupambana na adui yao”. Mwisho wa kunukuu.
Muadhini wa Mtume wa Allah alipotoa adhana ya vita, watu wakaanza kuziendea haraka silaha zao na kuzivaa, kisha wakamiminika na kukusanyika msikitini.
Hakubakia nyuma majeruhi wala mzima bila ya kuangalia majeraha na maumivu yaliyotokana na majeraha hayo ambayo kila mmoja alikuwa ameshughulishwa na kuyaganga.
Wito wa Bwana Mtume uliwafanya wayasahu yote hayo kama kwamba halikuwepo lililotokea. Hapana ye yote miongoni mwao ila aliyasahau kabisa majeraha na maumivu yake na akajiona mzima na mwenye nguvu mpya na ari ya kusahihisha makosa aliyoyafanya.
Mpaka ikafikia wanyonge kuzibebesha nafsi zao zisiyoyaweza kwa ajili tu ya kumuitikia Mtume wa Allah kama walivyoamrishwa:
“ENYI MLIOAMINI! MUITIKIENI ALLAH NA MTUME WAKE ANAPOKUITENI KATIKA YALE YATAKAYOKUPENI UHAI MZURI (wa duniani na akhera)…” [8:24]
Imepokelewa kwamba: Abdullah Ibn Sahmi Al-Answariy na nduguye Raafii Ibn Sahmi Al-Answaariy, walikuwa wamerejea kutoka Uhud wakiwa wamejeruhiwa vibaya sana.
Wakatoka wakijikokota kwenda kuungana na Mtume wa Allah na Raafii ndiye aliyekuwa amejeruhiwa vibaya sana kuliko nduguye, akashindwa kutembea. Nduguye Abdullah akawa anambeba mgongoni kwake masaa kadhaa mpaka anapopumzika anamuacha atembee kwa kitambo kidogo.
Wakaenda hivyo hivyo mpaka wakafika kwa Mtume wa Allah, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipowaona aliwaombea dua njema.
Watu wengine ambao hawakwenda vitani jana yake walimuomba Bwana Mtume idhini ya kutoka, akawakatalia ombi lao hilo.
Kwa hivyo hakutoka ye yote miongoni mwa ambao hawakwenda vitani siku iliyotangulia ila Jaabir Ibn Abdillah-Allah amuwiye radhi-kwa sababu ya udhuru mzito aliokuwa nao na nia yake ya kweli.
Watu walipokwishakusanyika, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaswali rakaa mbili msikitini, kisha akaagiza aletewe farasi wake akampanda akiwa amevaa nguo na kofia ya chuma.
Akaagizia bendera yake ambayo ilikuwa bado haijateremshwa tangu jana, akamkabidhi Sayyidina Aliy Ibn Abiy Twaalib na kauli nyingine inasema kuwa alimpa Sayyidina Abuu Bakri. Na akampa ukhalifa wa Madinah Sayyidina Abdullah Ibn Ummu Maktuum na akamfanya Abbaad Ibn Bishri kuwa mlinzi wake.
Kisha huyoo Bwana Mtume akatoka na maswahaba wake wakaenda mpaka wakapiga kambi Hamraaul-Asad; hii ni sehemu iliyo umbali wa maili nane kutoka mjini Madinah. Akakaa hapo siku tatu; Jumatatu, Jumanne na Jumatano.
Wakati wa mchana Bwana Mtume alikuwa anawaamrisha maswahaba wake kukusanya kuni, usiku unapoingia alimuamrisha kila mmoja wao kuwasha moto. Ikawa mianga ya moto ikionekana umbali mrefu kabisa na kuzagaza pande zote.
Mng’aro wa mioto hii ukawakhadaa maadui na kuwafanya wahisi kuwa waislamu wako maelfu kwa maelfu. Ibn Is-haq-Allah amrehemu-anasema:
“Khabari za kupiga kwao kambi na mioto yao zikasambaa na kuenea kila mahala, hili likawa ndio alililowadhalilishia maadui wao”.