KUUAWA KWA KA’BU IBNUL-ASHRAF

Yahudi Ka’ab Ibn Al-Ashraf akarejea Madinah kutoka Makah alikokwenda kuchochea fitna na uadui dhidi ya Mtume na waislamu.

Akarudi hali ya kuwa uadui na chuki yake kwa Mtume wa Allah ukiwa umerudufika kuliko ilivyokuwa kabla hajaenda Makah.

Na akawa na ulimi mchafu mno usiostahamilika kwa wanawake wa Kiislamu, kiasi cha kumfanya Mtume kuwa na dhiki kubwa ya moyo na akatamani kupumzika na shari la mtu huyu muovu. Akasema Mtume–Rehema na Amani zimshukie–kuwaambia maswahaba wake:

 Nani atakaye nipumzisha na shari ya Ibn Al-shraf?” Muhammad Ibn Maslamah  Al-Answaariy akamwambia: “Mimi nitakutoshea nae, ewe Mtume wa Allah, mimi nitamuua.”

Mtume akamwambia: “Fanya hivyo ukiweza.” Akasema Ibn Maslamah: “Ewe Mtume wa Allah, hakika ya mambo yalivyo hatuna budi kusema maneno ya uongo ili tumpate.” Mtume akamwambia:

“Semeni yatakayokudhihirikieni, nyinyi mna uhalali wa kufanya hivyo.” Wakajikusanya katika jukumu la kumuua Ka’ab Ibn    Al-Ashraf, Muhammad Ibn Maslamah mwenyewe na wenzake.

 Wenzake hawa walikuwa Ubbaad Ibn Bishri, Al-Haarith Ibn Ausi, Abuu Iysa Ibn Jabri na Silkaan Ibn Salaamah, huyu alikuwa ni ndugu wa kunyonya wa Ka’ab Ibn Al-Ashraf.

Ibn Is-haaq-Allah amrehemu–anasimulia hali ilivyokuwa katika harakati za kumuuwa adui huyu wa Mtume na waumini:

“Kisha (baada ya kupata baraka za Mtume) wakamuendea adui wa Allah; Ka’ab Ibn   Al-Ashraf. 

Wakabakia nje akaingia Abuu Naailah (Silkaan Ibn Salaamah), akamjia akazungumza nae kitambo na wakiimba mashairi. Abuu Naailah ndiye aliyekuwa muimbaji wa mashairi hayo. 

Kisha akamwambia: Ole wako ewe Ibn Al-Ashfraf! Mimi nimekujilia na jambo nataka kukuambia, basi nifichie siri. Akajibu (Ibn Al-Ashraf): Nitafanya hivyo.

Akaendelea kusema: Kuja kwa mtu huyu (yaani Mtume) kwetu imekuwa ni balaa juu ya balaa! Waarabu wametufanyia uadui kwa sababu yake na wametukusanyikia  na kutupiga vita. Na wametukatia njia mpaka familia zimekosa matunzo na nafsi zimehangaika.

 Ka’ab akasema: Mimi ndiye mtoto wa Ibn Al-Ashraf ama wallah, nilikuwa nikikuambia ewe Ibn Salaamah kwamba mambo yatakuwa kama nisemavyo.

Silkaan akamwambia: Kwa yakini mimi nataka utupe ahadi nasi tukuweke rahani ili tukuamini nawe ututendee wema katika hili. Akasema (Ibn Al-Ashraf) Mtaniwekea rahani watoto wenu? Akasema (Silkaan):

Unataka kutufedhehesha, mimi ninao wenzangu wenye fikra kama zangu na ninataka nikuletee uwape ahadi na ufanye wema katika hilo.

Nasi tukuwekee rahani silaha za kutosha ili kutekeleza ahadi zetu kwako. Akasema (Ibn Al-Ashraf): Hakika katika kuweka rehani silaha ni kutekeleza ahadi.

Ibn Is-haaq anaendelea  kusimulia: Silkaan akarejea kwa wenzake (aliowaacha nje) akawapa khabari ya waliyozungumza yote.  Akawaamuru kwenda kuchukua silaha, kisha warudi wakutane nae usiku.  Wakakutana kwa Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akaenda nao mpaka sehemu iitwayo “Baqi’il-gharqad”, kisha akawaelekea na kuwaambia:

“Enendeni kwa jina la Allah, ewe Mola wa haki wasaidie”.  Kisha Mtume akarudi nyumbani kwake katika usiku wa mbalamwezi. Wakaenda mpaka wakafika katika boma la Ibn Al-Ashraf, Abuu Naailah (Silkaan) akampigia ukelele wa kumjulisha kuwa wamekuja kwa ajili ya ahadi yao.

Kusikia hivyo akalichupia guo lake la kujitanda, mkewe akashika ncha ya guo hilo na kumwambia: Hakika wewe ni mtu mshindani unayewaniwa na kukamiwa na watu wa vita huwa hawatoki nje saa hizi (usiku).

Akamjibu mkewe: Huyo ni Abuu Naailah (ndugu yangu wa kunyonya), lau angenikuta nimelala asingeliniamsha Mkewe akamwambia: Wallah, mimi naona kuna shari katika sauti yake hiyo.  Ka’ab akamwambia mkewe:

Lau kijana shujaa aitiwa mchomo wa mkuki basi angeitika tu wito huo (shujaa haogopi) Akatoka akazungumza nao kitambo, kisha wakamwambia: Waonaje ewe Ibn Al-Ashraf tukienda mpaka Shi’ibil–Ajuuz, tuzungumze hapo usiku kucha? Akajibu: Mkitaka.

Wakaenda wakitembea, wakatembea kitambo kidogo Abuu Naailah akamshika Ibn Al-Ashraf kichwani, kisha akaunusa mkono wake na kusema: Sijapata katu kunusa manukato yenye kunukia sana kama haya ya usiku wa leo.

Kisha wakaenda kitambo kidogo, akarudia kufanya vile vile kama mwanzo kwa mara ya pili. Wakaenda tene kitambo kidogo, akarudia tena mara ya tatu, sasa akamkamata barabara nywele za utosi kisha akawaambia wenzake: Mpigeni panga adui wa Allah, Panga zao zikamuangukia moja baada ya nyingine.”

Hiki ndicho kisa cha adui wa Allah; Ka’ab Ibn Al-Ashraf kama alivyokipokea mwanasira Ibn Is-Haaq, kadhalika wamekipokea wanasira wengine katika vitabu vya sira kwa riwaya inayoshabihiana na hii.

Kwa mauji haya ya Ka’ab Ibn Al-Ashraf, Allah akawa amewapumzisha waislamu na shari ya mtu muovu huyu ambayo alikuwa ameikusudia kwao.

Baada ya mauji haya wakaenda kumpa khabari Mtume aliyewatuma kuifanya kazi hii ya kuuhami Uislamu na waislamu  Mauaji haya yalikuwa katika mwezi wa Rabiul-Awwaal (Mfunguo sita) wa mwaka wa pili tangu Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alipohamia Madinah.

TANBIHI:

 Waandishi wengi wa kimashariki (Orientalists) walioandika katika uwanja wa sira ya Mtume, wanayatazama na wanayafasiri mauaji haya ya Ibn Al-Ashraf kwamba ni “Mauaji haramu ya kihaini/kisaliti.” Wakayashikia bango mauji haya na kuyafanya kuwa mada ya kumtukana na kumvunjia heshima Mtume wa Allah  Wakafikia kusema kwamba tukio hili liliitia doa jeusi historia nyeupe ya Mtume.

 Hebu na tuitumie lugha yao na tuyaite mauji haya kama wayaitavyo wao kuwa ni “Mauaji haramu”, kwa kuwa yalikuwa ni ya kushtukiza. Kadhalika tukubaliane nao kwamba yalisimama katika misingi ya kihaini na usaliti. Kisha baada ya kuzungumza lugha yao na kukubaliana nao, sasa tuwaulize:           

 Je mauaji haya haramu ya kisaliti alifanyiwa nani; adui au walii (mtu mtukufu aliye kipenzi cha Allah)? Na

Je, alikuwa adui huyu anataka vita au amani? Na

Je, ni lipi kati ya makundi mawili haya; waislamu na mayahudi lililoanza kutumia njia ya uhaini? Na

Je, ni kundi lipi kati ya mawili haya lililoanza uadui na kuuonyesha waziwazi na likavunja mkataba wa amani waliokubaliana? Na

 Je, ni kundi lipi lililomshakizia na kumchochea mwenzake maadui wamkusanyikie kuja kumpiga?

 

Mashwali haya yanahitaji jawabu linalotaka elimu ya kuwaza kwa akili halisi inayotoa hoja.

  Elimu inayotegemea na kuegemea uhalisia wa kihistoria na matukio yake ya kweli si ya kubuni ili kukidhi matakwa ya muandishi na kushibisha malengo yake. 

Ni kwa msingi wa jawabu la namna hii ndio tunaweza kulihukumu suala hili la mauji ya Ibn Al-Ashraf.

 

NI KUNDI LIPI LILILOVUNJA AHADI (MKATABA) YA AMANI?

Wamekongamana wapokezi wa sira juu ya kwamba Mtume wa Allah alifanya maagano na Mayahudi alipofika Madinah. 

Akaandikiana nao mkataba wa amani na kwamba Mtume awaache na dini yao na wao wamuache wasimbughi  na wala wasimuingilie katika dini yake. 

Wakakubaliana kwamba wasimuunge mkono wala kumsaidia adui wa Mtume na kwamba watashirikiana na waislamu dhidi ya adui atakayeivamia Madinah. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu–anatunakilia sehemu ya vipengele vya mkataba huo:

“Mayahudi waendelee kufuata dini yao na waislamu waachiwe kuabudu kwa mujibu wa imani ya dini yao.  Ila atakayefanya dhulma au dhambi, huyu hataingamiza ila nafsi yake na watu wa nyumbani kwake. Na kwamba ni juu yao kunusuriana dhidi ya ambaye atakayempiga vita mmojawapo wa wana mkataba huu (waislamu/mayahudi). Na kwamba Makurayshi na washirika wao wasipewe ushirikiano/msaada dhidi ya waislamu. Na kwamba atakayetoka Madinah kwa khiyari yake ameaminika (ana amani) a atakayebakia ameaminika pia, ila atakayefanya dhulma na dhambi. Kwa yakini Allah atamuhifadhi na kumpa amani atakayefanya wema na kumcha.”

Mkataba huu uliwadhaminia mayahudi kuishi na waislamu kwa amani na salama, kwa sababu vipengele vyake vilibainisha wazi haki na wajibu wa kila kundi kwa mwenziwe.

Na msingi wa mkataba huu ulikuwa ni kusaidiana (ushirikiano) na kila mmoja kuwa mkweli kwa mwenziwe na kunusuriana dhidi ya dhalimu au mchokozi yo yote.

Je, mayahudi walikuwa ni wakweli kwa waislamu kwa mujibu wa mkataba huu? Allah Mjuzi mno wa siri za nafsi anawashuhudia kuwa hawakuwa wakweli na akawatahadharisha waislamu kuwaamini katika kipindi hiki cha mpito. Anasema:

“ENYI MLIOAMINI! MSIWAFANYE WASIRI WENU WATU WASIOKUWA KATIKA NYINYI: HAO HAWATAACHA KUKUFANYIENI UBAYA. WANAYAPENDA YALE YANAYOKUDHURUNI. BUGHUDHA (yao juu yenu) INADHIHIRIKA KATIKA MIDOMO YAO NA YANAYOFICHWA NA VIFUA VYAO NI MAKUBWA ZAIDI. TUMEKUBAINISHIENI DALILI (zote) IKIWA NYINYI NI WATU WA KUFAHAMU. OH! NYINYI MNAWAPENDA (maadui zenu hao), HALI WAO HAWAKUPENDENI! NANYI MNAAMINI VITABU VYOTE (chenu na vyao) NA WANAPOKUTANA NANYI HUSEMA: TUMEAMINI LAKINI WANAPOKUWA PEKE YAO WANAKUUMIENI VYANDA KWA UCHUNGU (wa kukuchukieni) SEMA: KUFENI KWA UCHUNGU WENU (huo), HAKIKA ALLAH ANAYAJUA (hata) YALIYOMO VIFUANI. IKIKUPATENI KHERI HUWASIKITISHA NA IKIKUPATENI SHARI WANAIFURAHIA NA KAMA NYINYI MKISUBIRI NA MKAMCHA ALLAH, HILA ZAO HAZITAKUDHURUNI KITU HAKIKA ALLAH ANAYAJUA VIZURI YOTE WANAYOYATENDA.”  (3: 118-120)

Ndani ya aya hizi mna taswira na picha halisi ya undani wa mayahudi na uadui wao waliouficha nyoyoni mwao dhidi ya waislamu.

Matendo ya mayahudi ni ushahidi tosha juu ya haya; ni kwa nini ushindi wa waislamu dhidi ya makurayshi katika vita vya Badri uliwakera na kuwaudhi?!

Hivi ushindi huu haukustahiki kuwafurahisha, kwa sababu ni ushindi wa washirika na jirani zao na isitoshe ni ushindi wa watu wanaoshabihiana nao kiitikadi.

 Hivi tendo lao hili si kuvunja mkataba walioandikiana na waislamu na wao kuuridhia? Kwa hakika tunaweza kusema kwa majumuisho kwamba ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa Ka’ab Ibn Al-Ashraf alijiua mwenyewe kwa kujitengenezea mazingira yaliyosababisha kuuawa kwake. 

Huu ndio ukweli na haki, tumeikubali au tumeikataa bado historia itaendelea kuikiri.

 

KUUAWA KWA KA’BU IBNUL-ASHRAF

Yahudi Ka’ab Ibn Al-Ashraf akarejea Madinah kutoka Makah alikokwenda kuchochea fitna na uadui dhidi ya Mtume na waislamu.

Akarudi hali ya kuwa uadui na chuki yake kwa Mtume wa Allah ukiwa umerudufika kuliko ilivyokuwa kabla hajaenda Makah.

Na akawa na ulimi mchafu mno usiostahamilika kwa wanawake wa Kiislamu, kiasi cha kumfanya Mtume kuwa na dhiki kubwa ya moyo na akatamani kupumzika na shari la mtu huyu muovu. Akasema Mtume–Rehema na Amani zimshukie–kuwaambia maswahaba wake:

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *