KUWAHURUMIA WATU / TABIA YA HURUMA

Muislamu wa kweli ni mtu mwenye huruma. Huruma ni miongoni mwa tabia za muislamu. Chimbuko la huruma ni usafi na utakasifu wa nafsi na roho, hivyo ndiyo kusema kuwa na huruma ni nembo na alama ya kuonyesha usafi wa nafsi ya mja na utakasifu wa roho yake.

Huruma ya kweli inatokana na ulaini wa moyo ambao humpelekea mja kumsamehe aliyemkosea na kumfanyia wema aliyemtendea uovu.

Huruma ikijizatiti na kuthibiti moyoni ndipo hujitokeza nje athari yake.

Hapo ndipo utamuona mtu aliyepambika na tabia hii ya huruma anaitumia mali yake kumsaidia mwenye shida, hutumia cheo/hadhi yake kumnusuru/kumsaidia mdhulumiwa, humsamehe aliyemkosea, humpa chakula mwenye njaa na humsaidia mgonjwa.

Zote hizi ni baadhi tu ya athari za tabia ya huruma.

Huruma ni miongoni mwa sifa za watu wa peponi, Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia

“KISHA AWE MIONGONI MWA WALIOAMINI NA WAKAUSIANA KUSUBIRI NA WAKAUSIANA KUHURUMIANA. HAO NDIO WATU WA UPANDE WA KHERI (peponi)” [90:17-18]

 kuwahurumia watu ni sababu ya kupata huruma ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume isemayo:

“Hakika si vinginevyo Mwenyezi Mungu huwaonea huruma waja wake wenye huruma” – Al-Bukhaariy.

Hapana shaka mtu mwenye sifa na tabia hii ya huruma hupendwa na jamii.

Tabia hii ya kuoneana huruma pia ndio siri kubwa ya ushindi na mafanikio ya waislamu wa mwanzo, kwani kuhurumiana kwao ndiko kulikowapelekea kupendana mapenzi ya kweli, na mapenzi haya yakawapeleka katika mshikamano wa dhati ambao ukawafanya kuwa wamoja na nguvu.

Tunasoma ndani ya Qur-ani:

“MUHAMMAD NI MTUME WA ALLAH NA WALIYO PAMOJA NAYE NI WENYE NYOYO THABITI MBELE YA MAKAFIRI NA WENYE KUHURUMIANA WAO KWA WAO” (48:29)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *