KUIPENDA NCHI (UZALENDO)

Uzalendo, mtu kuipenda nchi yake ni miongoni mwa tabia  njema ambazo inatakiwa ziwe ni pambo la Muislam. 

Tabia hii ina athari kubwa sana katika kuchochea maendeleo ya mtu binafsi na nchi yake kwa ujumla. 

Uzalendo humsukuma mtu kuithamini na kuionea fakhri nchi yake, vitu ambavyo ni chachu na hamira ya maendeleo.  

Uzalendo humfanya mtu kuitakia mema nchi yake kama tunavyosoma ndani ya Qu-ani:    ( Na kumbukeni khabari hii nayo); 

ALIPOSEMA IBRAHIMU ;  EE MOLA WANGU! UFANYE MJI HUU (wa Makkah) UWE WA  SALAMA NA UWAPE WAKAZI WAKE MATUNDA ……”(2:126)

Hii ni darsa ya uzalendo ndani ya Qur-ani Tukufu, huku ndiko kuipenda nchi tunakokusudia.

Nabii  Ibrahim Amani imshukie ni mfano na kigezo cha uzalendo halisi mwenye kuipenda nchi yake. 

Ushahidi wa hilo ni kule kuiombea kwake nchi  yake iwe ni nchi ya amani.  

Kwa nini basi Nabii Ibrahim asiombee nchi yake utajiri  au kitu kingine kisichokuwa amani ?   Hili ni kutokana na kuyakinisha kwake kuwa utajiri pasipo amani haina thamani (maana).

Ni chini ya anga la amani tu ndipo wananchi wa nchi yeyote ile huweza kufaidika na neema zilizomo katika nchi yao na wakapiga hatua ya maendeleo. 

Ni chini ya anga la amani na utulivu ndio huweza kuwa na makini ya kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu. 

Hapa ndipo unapojitokeza umuhimu wa sifa/tabia hii ya uzalendo katika uma/jamii ya wanadamu. 

Hebu tuzidi kuipa nafasi Qur-ani Tukufu izidi kutuonyesha uzalendo wa Nabii Ibrahim, tusome na tuwaidhike;  

MOLA WETU ! HAKIKA MIMI NIMEWAWEKA (nimewakalisha)   BAADHI YA KIZAZI CHANGU (Mwanangu Ismail na mama yake Hajara)  KATIKA BONDE (hili la Makkah) LISILOKUWA NA MIMEA YEYOTO;  KATIKA NYUMBA YAKO TAKATIFU (ya Al-Kaaba) MOLA WETU WAJAALIE WASIMAMISHE SWALA.  NA UJAALIE NYOYO ZA WATU ZIELEKEE KWAO (wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji)  NA UWARUZUKU MATUNDA ILI WAPATE  KUSHUKURU (“ 14: 37).

 Tunasema uzalendo ni mtu kupenda nchi yake hebu tujiulize nchi ni nini kwa sababu ni muhali kukipenda usichokijua na ndio maana tukawa na msemo usemao

“ ASIYEKUJUA HAKUTHAMINI”  Tunaweza kuelezea nchi kuwa ni pale mahala ambapo mtu amezaliwa katika ardhi yake na kukulia chini ya anga lake, akifunikwa nalo na kuvuta hewa yake na kulishwa na mimea ya ardhi yake na kunywa maji yake.  

Hii ndio nchi tunayokusudia mtu awe na uzalendo nayo.

 Naam, uzalendo ni kupenda nchi yako sasa kuipenda nchi ndio kufanyaje? 

Mtu afanyeje ndipo aambiwe/aonekane kuwa ni mzalendo wa nchi yake? 

Kuipenda nchi  ni kufanya kila jambo ambalo kwa namna moja au nyingine litakuwa ni sababu ya kuletea maendeleo, heshima, kuilinda dhidi ya maadui zake, kuhifadhi, rasilimali (mali asili) zake kwa faida ya kizazi hiki kilichopo na kijacho.  

Kujenga nchi katika msingi ya usawa, haki za binadamu na msingi ya ucha Mungu, watu wamtambue, wajue na kisha kumuabudu Mwenezi Mungu aliyewaumbia nchi yao na vyote vilivyomo humo. 

Hilo ndilo agizo la Mwenyezi Mungu Mtukufu wa Makureshi bali kwa watu wote kwa sababu Qur-ani ni mwongozo kwa watu wote: 

BASI NA WAMUABUDU BWANA WA NYUMBA HII (AL-KAABA)  AMBAYE ANAWALISHA (wakati Waarabu wenziwao wamo) KATIKA NJAA NA ANAWAPA AMANI (wakati wenziwao wamo) KATIKA KHOFU (102: 3 – 4).

 Ni muhali bali uongo mweupe mtu kudai kuwa anaipenda nchi yake huku anasahau kumuabudu na kumshukuru yule aliyemuumbia nchi hiyo na kujazia humo neema zake.

Kilelezo na nembo kuu ya kuonyesha taswira ya uzalendo wa mja kwa nchi yake kiwe ni kumshukuru Mola Muumba wake na Muumba wa mbingu na ardhi ambamo humo ndimo nchi yake imo; 

Shukrani za kweli ni zile ziambatanazo na ibada ambayo nayo inaangukia katika matapo/mapote mawili makuu;  maamrisho na makatazo. 

Hii ni sawa na kusema ibada ni kutenda tu liloamrishwa na Mola wako na kuacha kutenda ulilokatazwa na Mola wako. 

Tunatarajia kutokana na maelezo yetu hayo kuwa kumbe kuipenda nchi yako ni katika jumla ya ibada na ni sehemu miongoni mwa sehemu zinazoiunda dini. 

Ni wajibu na jukumu la kila mmoja wetu kuipenda nchi yake. 

Mwanafunzi mwenye uzalendo na nchi yake ni yule anayesoma kwa hima juhudi na bidii huku akizingatia  miiko na taratibu za elimu ambazo ni pamoja na kwaheshimu waalimu wake na kanuni zote za shule sambamba  na kushirikiana na wenzake. 

Mwanafunzi mzalendo huyu huyafanya yote haya kwa lengo la kupata stadi, maarifa, na ujuzi ili aweze kuitumikia nchi yake.  

Mfanya biashara mpenda nchi yalke ni yule aliye muaminifu katika biashara yake, hafanyi udanganyifu katika biashara yake kwa kuwauzia wananchi wenzake bidhaa zilizo chini ya kiwango cha ubora, hawapunji katika mizani, hawauzii kwa bei ya juu kupita kiasi.

 Huitoa haki ya Mungu Mnemeshaji wake (Zakah) kuwapa wananchi wenzake wenye hali duni.  Mfanyakazi Mzalendo ni yule afikaye kazini mapema kwa muda utakiwao na kufanya kazi kikamilifu kwa mujibu wa taratibu za kazi,  Ni yule atokaye kazini kwenda nyumbani  kwa muda uliopangwa . 

Ni yule asiyedai rushwa kwa kuteekeleza wajibu wake.  Ni yule mwenye mashirikiano mema na wafanyakazi wenziwe hata wale walio chini yake kikazi. 

Kauli ya jumla, mzalendo halisi ni yule ayatangulizae maslahi ya nchi yake mbele ya maslahi yake binafsi. 

Ni yule anayeshirikiana na wananchi wenzake katika kuijenga na kuendelkeza nchi yao kwa kuifanyia kazi kauli tukufu ya Mola wake Mtukufu.

“…………….NASAIDIANENI  KATI KA WEMA NA TAQWA”  WALA MSUSASAIDIANNE KATIKA DHAMBI NA UADUI” (5:2).

Hakuna  hata mmoja anayeweza kuthubutu kusema kuwa kushirikiana katika kuijenga nchi si katika mema na Taqwa, ikiwa yupo  basi Qur-ani inasema

“…………………HAYO NI KWA SABABU WAO NI WATU WASIO NA AKILI” (5: 58)

 Rejea historia umuangalie mzalendo mkweli mwenye uchungu na nchi yake, Bwana Mtume  Rehema na Amani zimshukie – namna alivyoshirikiana na Makurayshi wenziwe, waumini na makafiri wao katika kujenga nchi yao ya Hijaazi (Makkah) yakutoshe kuuona uzalendo na Mtume kwa nchi yake maneno yake aliyoyasema wakati anatoka Makkah kwenda madinah akiwakimbia jamaa zake waliokula njama kumuua kwa sababu tu ya Uislamu aliowaletea Mtume alipompanda ngamia wake tayari kwa safari ya Madinah, aliutazama mji wa Makkah kwa kitambo kwa macho ya kuuaga kisha kasema 

“ WALLAH “ HAKIKA  wewe (Makkah) ndio ardhi ya Mwnyezi Mungu iliyo kipenzi mno kwangu (nipendavyo zaidi kuliko zote hata huko Madinnah niendako)  Nawe ndiwe ardhi ya Mwenyezi Mungu aipendayo kuliko zote.  Lau si kwa sababu ya watu wako (Makurayshi) kunitoa (kunifukuza) ndani yako kwa nguvu (kwa hukata kuniua kwao) basi msingelitoka (ninsingehamia Madinah).

Naam, wamesma kweli waliosema Mtu kwao.

Ukishindwa kuiona picha ya uzalendo wa Mtume kupitia meneno yako haya, itakuwa ni moja kati ya mambo mawili ima hutaki tu au  akili yako haiakilishi (haifanyi kazi iliyoambiwa ) sasa kama huo si uzalendo na kuupenda nchi ni nini basi tuambie. 

 

KUIPENDA NCHI (UZALENDO)

Uzalendo, mtu kuipenda nchi yake ni miongoni mwa tabia  njema ambazo inatakiwa ziwe ni pambo la Muislam. 

Tabia hii ina athari kubwa sana katika kuchochea maendeleo ya mtu binafsi na nchi yake kwa ujumla. 

Uzalendo humsukuma mtu kuithamini na kuionea fakhri nchi yake, vitu ambavyo ni chachu na hamira ya maendeleo.  

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *