SOMO LA SITA-KUPAKAZA MAJI JUU YA KHOFU

(i) KHOFU NI NINI?

Khofu ni neno la Kiarabu ambalo hutumika kwa maana ya aina maalumu ya kiatu chenye umbo la soksi. Viatu hivi vinaweza kuwa ni vya ngozi au malighafi nyingine ifananayo na ngozi kama vile kitambaa kigumu.

(ii) HUKUMU NA DALILI YA KUPAKAZA MAJI JUU YA KHOFU.

Mojawapo ya misingi iliyojengewa sheria ya Kiislamu ni WEPESI. Siku zote uislamu huwatakia wepesi na urahisi wafuasi wake katika utendaji na utekelezaji wao wa ibada na matendo yao ya maisha ya kila siku.

Ni kwa kuuzingatia msingi huu ndipo hutaweza kukuta hata mara moja uislamu umeweka sheria isiyotelelezeka. Hii ni kwa sababu sheria zote za uislamu zimechunga sana udhaifu wa mtekelezaji wa sheria hizo (binadamu) na mazingira aishimo na bila kusahau hali mbalimbali anazozipitia au kumpitia.

Sasa basi ili kuuthibitishana kuudhihirisha ukweli huu uislamu umemjuzishia na kumruhusu muislamu kupakaza maji juu ya khofu badala ya kuosha miguu wakati wa kutawadha kwa masharti makhususi tutakayoyaona hapo baadae.

Ruhusa hii ni kwa wanamume na wanawake pamoja na itatumika mtu awapo safarini au mjini (hayumo safarini).

Kupakaza maji juu ya khofu kumethibiti katika suna tukufu ya Bwana Mtume. Miongoni mwa hadithi zilizothibiti katika mas-ala ya upakaji maji juu ya khofu ni hizi zifuatazo:
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie: “Atakapotawadha mmoja wenu (udhu kamili), kasha akavaa khofu. (Atakapotawadha tena) basi na apakaze maji juu yake (hizo khofu) na wala asizivue akitaka (kufanya hivyo) ila akipatwa na janaba.” Daaruqutwiy na Al-Haakim.

Imepokelewa na Mughyrah Ibn Shu’ubah – Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – kwamba – Mtume alitoka kwa ajili ya kukidhi haja (kujisaidia), Mughiyrah akamfuata kumpelekea maji, alipokwisha kukidhi haja yake, (Mughirah akawa anammwagia maji naye Mtume akitawadha na (mwisho) akapakaza maji juu ya khofu zake. Bukhaariy.

Na katika riwaya nyingine ya Mughiyrah Allah amuwiye radhi-amesema: Nilikuwa safarini pamoja na Mtume – Rehema na Amani zimshukie – nikaporomoka (nikainama) ili nimvue khofu zake, mtume akasema: “Ziache, kwani mimi nimezivaa il hali (miguu) ikiwa twahara.”

(iii) HEKIMA/FALSAFA YA KUWEKWA SHERIA YA KUPAKAZA KHOFU

Falsafa ya sheria hii ni kama tulivyotanguia kueleza mwanzoni mwa somo letu hili kuwa ni kuwawepesishia na kuwarahisishia waislamu utekelezaji wao wa ibada zinazowalazimu kila siku, hasa hasa majira/wakati wa kipindi cha baridi kali.

Uislamu umeileta na kuweka sheria hii ili mtu asipate udhuru na upenyo wa kuacha kutekeleza ibada ya swala kwa hoja ya baridi kali. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia: “….. WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI ……” (22:78)

(iv) SHARTI ZA KUPAKAZA KHOFU

Ili upakazaji juu ya khofu usihi kisheria ni budi zipatikane sharti kadhaa kama zilivyotajwa na Mafaqihi (Wataalamu wa fani ya fiq-hi).

Miongoni mwa sharti muhimu kabisa ni hizi zifuatazo:-

 • Uwepo uwezekano wa kuweza kuzitembelea. (Hizo khofu mbili). Sharti hili litapatikana ikiwa khofu ni madhubuti na imara.
 • Zinastahimili mwendo
 • Zinatosha sawasawa miguuni.
 • Ziweze kusitiri miguu mpaka vifundoni yaani zisitiri mahala ambapo ni fardhi/wajibu kuoshwa katika udhu.
 • Khofu ziwe ni twahara, yaani azivae zikiwa ni twahara kwani haisihi kupakaza maji juu ya khofu yenye najisi isiyosameheka kisheria. Sharti hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia swahaba wake Mughiyrah Ibn Shu’ubah alipotaka kumvua Mtume khofu zake ili apate kuosha miguu katika kutawadha: “Ziache (usizivue) kwa sababu nimezivaa zikiwa twahara.” Daaruqutwniy na Al-haakim.
 • Zivaliwe baada ya twahara kamili. Mtu haruhusiwi kupakaza juu ya khofu mpaka kwanza atawadhe udhu kamili ikiwa ni pamoja na kuiosha miguu kama kawaida. Baada ya udhu ndipo anaweza kuzivaa, udhu ukitenguka na akataka kutawadha tena, hapa sasa ndio atapata ruhusa ya kupakaza maji juu ya khofu badala ya kuzivua na kuosha miguu.
 • Zisiwe zimetoboka au kubenuka kiasi cha kuonyesha sehemu ya mguu.

TANBIHI

(a) Inajuzu kisheria kupakaza maji juu ya kilemba/kofia kwa dharura ya baridi kali au safari badala ya kupakaza kichwa. Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa na Imamu Muslim: “Kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alitawadha akiwa safarini, akapakaza maji utosini kwake na juu ya kilemba.” Pamoja na kupakaza kilemba., alipakaza pia baadhi ya sehemu za utosi kama hadithi inavyojieleza.

(v) NAMNA YA UPAKAZAJI WA KHOFU

Sheria haikumuachia kila mtu aitekeleze ruhusa hii ya upakazaji maji juu ya khofu kwa namna aitakayo mwenyewe, bali imeelekeza namna maalumu ya upakaji ambayo kila mtu hana budi kuifuata.

Haya sasa tufuatane pamoja tuone ni jinsi gani tunaweza kuzipakaza khofu maji:-

 • Mpakaji aanze kwa kuilowesha maji mikono yake (vitanga). Halafu aweke tumbo la kitanga cha mkono wake wa kushoto chini ya kisigino cha khofu na tumbo la kitanga cha mkono wa kulia aweke kwenye ncha ya vidole (sehemu ya mbele ya khofu).
 • Baada ya uwekaji huo wa vitanga ndipo akipitishe kitanga cha kulia kuelekea muundini na kile cha kushoto kuelekea ncha za vidole. Mpakaji apakaze khofu kwa mfuo.
 • Yaani avitawanye vidole vyake wakati wa kupaka, asivifumbe pamoja. Kadhalika upakaji uwe ni baada ya kumaliza kutawadha viungo vingine visivyo miguu na apakaze akiwa amezivaa tayari.
(vi) MAS-ALA:

Lau mtu atapakaza maji juu ya khofu bila ya kupakaza chini yake, itajuzu. Hii ni kutokana na kauli ya Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi: “Ingelikuwa dini hufuata rai (ya mtu) kupakaza chini ya khofu ingekuwa ni bora zaidi kupakaza chini kuliko kupakaza juu yake.” Abu Daawoud.

(vii) MUDA WA UPAKAZAJI:

Ruhusa ya upakazaji maji juu ya khofu imewekewa muda maalumu na sheria. Baada ya kumalizika muda huo, ruhusa hii inabadilika.

Muda wa upakazaji unagawanyika sehemu mbili kwa kumzingatia mpakaji:-

 • Mpakazaji mkazi yaani asiye msafiri atapakaza siku moja (masaa ishirini na nne )
 • Mpakazaji msafiri atapakaza siku tatu (masaa sabini na mbili (72) )

Utaratibu huu wa muda unatokana na hadithi iliyopokelewa na Swaf-waan Ibn ‘Assaal – Allah amuwiye radhi – amesema: Alituamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – kupakaza maji juu ya khofu tutakapozivaa baada ya twahara (udhu) siku tatu tuwapo safarini na mchana na usiku (siku moja) tuwapo makazi (hatumo safarini) na janaba.”

Kadhalika tunayapata maelekezo ya muda wa upakazaji katika hadithi ya Shurayhi Ibn Haaniy – Allah amuwiye radhi – amesema:- Nilimuuliza Bi Aysha (mkewe Mtume) – Allah amuwiye radhi – kuhusiana na upakazaji maji juu ya khofu, akasema: (Nenda) kamuulize Aliy Ibn Twaalib, kwnai yeye ni mjuzi mno wa (mas-ala) haya kuliko mimi, kwa sababu yeye alikuwa akisafiri pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie. (Nikaenda) nikamuuliza akaniambia: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie: “Inamjuzia msafiri kupakaza siku tatu (mchana na usiku) na mkazi siku moja (mchana na usiku). Muslim

TUJIFUNZE NA TUKUBALI:
Kuwa watu huzidiana kielimu. Anapokuwepo mwenye elimu zaidi kuliko wewe, basi ni vema ufafanuzi wa mas-ala utolewe na yeye kama alivyotupigia mfano mama wa waumini Bi. Aysha – radhi za Allah ziwe pamoja nae.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *