MTUME ASHAURIANA NA MASWAHABA WAKUTANE WAPI NA ADUI

Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-akatuma wapelelezi wake kupeleleza khabari za mahasimu wake.

Wakarudi na kumpasha khabari kwamba wamepiga kambi katika bonde la Uhud, wakamkadiria idadi yao na utayarifu wao. 

Mushrikina hawa walikuwa wamewaachia farasi na ngamia wao kula katika mashamba ya watu wa Madinah yaliyokuwa nje kidogo ya mji. 

Walifanya hivyo makusudi kwa lengo la kuwadhoofisha waislamu kiuchumi kwa siku za usoni.  Mifugo hii ikafanya uharibifu mkubwa kutoka na kula mimea na miti kwa kiasi kikubwa mpaka ikakaribia kuingia Madinah. 

Khatari ikawajongelea waislamu mpaka milangoni, ikalazimu sasa zichukuliwe hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo ya hatari  bila ya kuchelewa. 

Ikawawajibikia waislamu kuchukua tahadhari na kujiandaa kupambana na adui aliye milangoni mwao. Mji wote wa Madinah ukawekwa chini ya doria kali usiku kucha, waislamu wengine wakakesha msikitini na silaha tayari kwa lo lote wakimlinda Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie. 

Kulipopambazuka Bwana Mtume akawakusanya washauri wake na kuanza kushauriana juu ya mahala pa kukutana/kupambana na adui huyu.

Al-Waaqidiy–Allah amrehemu–amepokea kwamba: “Bwana Mtume– Rehema na Amani zimshukie-aliwaambia maswahiba wake: “Nipeni ushauri”.

Abdullah Ibn Ubayyi akasimama na kusema:

“Ewe Mtume wa Allah, sisi tulikuwa katika jahilia tukipigana katika zama hizo tuliwaweka wanawake na watoto katika ngome na tukawapa mawe. Tukauunganisha mji wa Madinah kwa majengo mpaka ukawa kama ngome kwa kila upande. Kazi ya wanawake na watoto ikawa ni kuwapopoa maadui kwa mawe kutokea juu ngomeni na vilimani, nasi tukawa tunapigana kwa panga zetu katika njia zilizo wazi.  Ewe Mtume wa Allah, kwa yakini  mji wetu huu wa Madinah katu haujawahi kuingiwa na adui, nasi hatujapatapo kumtokea adui nje yake ila alitushinda.  Na hajapatapo kutuingilia humu ndani ila tulimshinda tu.  Basi ewe Mtume wa Allh achana nao, kwani wakikaa huko nje watakuwa wamejipa wenyewe kifungo kibaya.  Na kama wataamua kurudi Makah, watakuwa wamerejea patupu hali ya kushindwa bila ya kupata la manufaa.  Ewe Mtume wa Allah, nakusihi unitii katika shauri hili na utambue kwamba mimi nimeirithi rai hii kutoka kwa wazee wangu wenye busara ambao walikuwa na uoni na uzoefu wa mambo”. 

Rai ya Mtume wa Allah–Rehema na amani zimshukie–ikasadifu kuwafikiana na rai hii iliyotolewa na Ibn Ubayyi. 

Rai hii ya Mtume ilitokana na ushauri wa maswahaba wake wakubwa kutoka pande zote mbili; Muhajirina na Answaar.  Mtume wa Allah akasema:

“Kaeni/bakieni Madinah na wawekeni wanawake na watoto ngomeni, wakituingilia mjini mwetu tutapambana nao katika vijia ambavyo sisi tunavijua zaidi kuliko wao (vichochoro).  Na wapopoeni kwa mawe na mishale kutokea juu ngomeni.  Vijana barobaro ambao hawakushiriki katika vita vya Badir kutokana na umri wao kutowaruhusu. Vijana hawa walipandwa na mori na raghba ya kufa mashahidi, wakapenda kukutana na adui ana kwa ana, wakasema: “Ewe Mtume wa Allah, tutoe tukapambane na adui huyu.”

 Na watu wazima wenye dhamira njema wakasema kwa nia njema kabisa:

“Ewe Mtume wa Allah, sisi tunachelea adui yetu kudhani kuwa sisi tumeogopa kumtokea kwa uoga wa kupambana nae.  Hili litawapa moyo wa ujasiri juu yetu.  Katika vita vya Badri ulikuwa na watu mia tatu tu na bado Allah akakupa ushindi juu yao.  Leo sisi tuko wengi na tulikuwa tukiitamani siku hii na tukimuomba atufikishe, sasa leo Allah ametuletea siku hii mipakani mwetu”.

Maalik Ibn Sinaan nae akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, sisi ni watu tulio baina ya (kupata) mojawapo ya mema mawili.  Ama Allah atupe ushindi juu yao na hili ndilo tulitakalo. Na jingine ewe Mtume wa Allah, aturuzuku Allah kufa shahidi kwa sababu yao.  Wallah, ewe Mtume wa Allah, sijali lo lote litakalokuwa kati ya mawili haya, kwani kwa yakini kila moja lina kheri nasi”.

Nae Sayyidna Hamzah akasimama na kusema:

“Naapa kumuapia yule ambaye aliyekuteremshia kitabu (Qur-ani), leo sitakula chakula mpaka nipigane nao kwa upanga wangu huu nje ya Madinah”.

Huyu ndiye Nu’umaan Ibn Maalik anainuka na kusema:

“Ewe Mtume wa Allah, kwa nini unatunyima pepo? Namuapia yule ambaye hapana Mola ila yeye nitawavaa nitawavaa”. Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akamuuliza:

“Kwa nini/kivipi?” Akamjibu:

“Mimi ni mtu nimpendaye sana Allah na Mtume wake na wala sitimui mbio siku ya vita”.

Yule pale Iyaas Ibn Ausi nae anasema:

“Mimi sipendi makurayshi warudi kwao na kusema: Tumemzingira Muhammad katika ngome za Yathrib, huu utakuwa ni ujasiri wa makurayshi kwetu angalia tayari wameikanyagakanyaga mitende yetu, kama hatukuwafukuza mashamba hayalimiki”.

Abuu Sa’ad Ibn Khaythamah nae akasema:

“Nilivikosa vita vya Badir ambavyo nilivikamia, pupa yangu katika vita hivyo ilinifikisha kumtoa mwanangu ashiriki.  Akapata fungu lake kwa kufa shahidi, nami niliuwania mno ushahidi.  Jana nilimuona mwanangu usingizini akiwa katika hali nzuri sana, akivinjari katika matunda ya peponi na mito yake, nae akisema ungana nasi usuhubiane nasi peponi, kwa yakini nimeyakuta aliyoniahidi Mola wangu kuwa ni haki (kweli).  Wallah, ewe Mtume wa Allah nimepambazukiwa nikiwa na shauku ya kusuhubiana nae peponi. Umri wangu umekuwa mkubwa na mifupa yangu imelegea nami napenda kukutana na Mola wangu.  Basi ewe Mtume wa Allah, niombee kwa Allah aniruzuku kufa shahidi na kuungana na mwanangu Sa’ad peponi”.

 

BWANA MTUME ASALIMU RAI YA KUTOKA KWENDA KUPIGANA:

Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akaona kwamba kutoka ndio mapenzi na matakwa ya walio wengi.

Akawaswalisha mashwahaba wake Ijumaa, kisha akawawaidhi na kuwaamrisha kufanya jitihada na bidii na akawaambia kwamba watapata ushindi maadam watasubiri.

Watu wakafurahia mno kwenda kukabiliana na adui yao ana kwa ana.  Lakini miongoni mwao hawakupendezwa na utokaji huo kutokana na kuona kwao katika uso wa Bwana Mtume dalili ya uchukivu. 

Watu wakaanza kujiandaa kwa vita, wakavaa deraya zao na kuchukua silaha zao wakaanza kujikusanya msikitini kwa Mtume wa Allah, ulipofika wakati wa Alasiri watu walikuwa wameshajikusanya.

Mtume akawaswalisha swala ya Alasiri, baada ya kumalizika swala akaamrisha wanawake na watoto wawekwe katika ngome. 

Kisha akaingia nyumbani mwake kujitayarisha huku akiwaacha watu wakijadiliana juu ya suala la vita. 

Bado lilikuwepo kundi miongoni mwao likiona kuwa rai ya kubakia Madinah ndio ya sawa na kwamba watu wamemkalifisha Mtume kutoka wakati yeye hakutaka. Sa’ad Ibn Muaadh na Usayd Ibn Hudhwayr wakasema kuwaambia wenzao:

“Mmemwambia Mtume wa Allah mliyomwambia na kumlazimisha kutoka na il-hali yeye anashushiwa wahyi kutoka mbinguni. Basi lirudisheni suala hili kwake kwa uamuzi, atakalokuamrisheni ndilo mlifuate.  Lile mtakaloona ana mapenzi nalo, basi mtiini”.

Wakati wakiwa katika majadiliano hayo, Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-akawatokea akiwa tayari amechukua zana zake za vita. 

Wale waliokuwa wakishikilia kutoka wakasema: “Ewe Mtume wa Allah,haitufalii sisi kukukhalifu, tenda likudhihirikialo”.

Bwana Mtume akawaambia: “Nilikwisha kuitieni shauri hili la kutotoka mkalikataa.  Na wala haimpasii Mtume ye yote (sio mimi tu) aliyekwisha vaa zana zake za vita kuzivua mpaka Allah ahukumu baina yake na adui zake kwa vita. Basi kwa hivyo liangalieni nililokuamrisheni ndio mlifuate na enendeni kwa jina la Allah, ushindi ni wenu mkisubiri”.

 

MTUME ASHAURIANA NA MASWAHABA WAKUTANE WAPI NA ADUI

Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-akatuma wapelelezi wake kupeleleza khabari za mahasimu wake.

Wakarudi na kumpasha khabari kwamba wamepiga kambi katika bonde la Uhud, wakamkadiria idadi yao na utayarifu wao. 

Mushrikina hawa walikuwa wamewaachia farasi na ngamia wao kula katika mashamba ya watu wa Madinah yaliyokuwa nje kidogo ya mji. 

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *