Yale ambayo swala huyatekeleza mara tano kila siku, swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani huyatakeleza mara moja kila mwaka.
Katika kipindi chote cha swaumu yaani tokea kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua magharibi, hatuli hata chembe moja ya chakula na wala hatunywi walau tone moja tu la maji.
Tunajizuia hivyo il-hali tunavyo vya kuvila na kunywa. Ni lipi basi litufanyalo hata tukavumilia kwa hiari zetu machungu haya ya njaa na joto la kiu ?
Tukijiuliza swali hili hatutapata jawabu zaidi ya kuvimilia kwetu taklifu zote hizi kunatokana na imani yetu thabiti kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumcha yeye na kuiogopa siku ya Kiyama ambayo Mwenyezi Mungu ametuasa tuiogope :
“NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA NA HAWATADHULUMIWA” [2:281]
Kwa hivyo basi itabainika kwamba funga ni suala linalofungamana na imani na ndio maana Mwenyezi Mungu alipotuamrisha kufunga katika aya ya swaumu, akatuita kwa jina la imani, akasema :
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH” [2:183]
Jua na ufahamu ndugu yangu Muislamu kwamba saumu ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, ambazo Uislamu haukamiliki ila kwa kupatikana zote.
Kwa mantiki hii, yeyote atakayeikanusha na kuipinga nguzo hii ya swaumu na kusema si wajibu, huyo atakuwa amekufuru, Tunasoma katika hadithi ya Bwana Mtume :
“Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano; kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH na kwamba Muhammad ni mjumbe wake, na kusimamisha swala na kutoa zaka na kufunga Ramadhani na kuhiji nyumba ya Mwenyezi Mungu” Bukhariy na Muslim kutoka kwa Ibn Umar.
Ibada hii ya funga ni ibada kongwe sana, haikuanzia kwa umma huu wa Nabii Muhammad bali ni ibada iliyokuwa ikifanywa na nyumati zingine zilizopita kabla yetu. Ushahidi wa hili ni kauli yake Mola Mtukufu :
“ENYI MLIOAMINI MMELAZIMISHWA KUFUNGA KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU …” [2:183]
Tukivipekua vitabu vya historia tutakuta vinatuambia kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu ameufaradhishia ummah huu ibada ya funga katika mwezi wa Shaaban {mwezi wa nane kwa mpangilio wa miezi ya kiislamu} mwaka wa pili wa Hijra {yaani tangu bwana Mtume kuhamia Madinah} kabla ya vita vya Badri. Mwenyezi Mungu anatuambia
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) ….”
Hebu tujiulize, kufunga swaumu ni nini ? Kwani tukijua swaumu ndio tutaweza kufunga kama alivyotuamrishwa na funga hiyo kutupelekea kwenye ucha Mungu (taq-wa) ambalo ndio lengo la swaumu.
Neno SWAUMU/FUNGA linatafsirika kwa maana mbili;maana ya kilugha na ile ya kisheria. Tukilitizama neno SWAUMU/FUNGA kwa darubini ya lugha, tutalikuta linatoa maana ya KUJIZUIA na chochote kile.
Mtu akijizuia kula anaambiwa kafunga, akijizuia kuzungumza anaambia kafunga na …. na ….. Maana hii ya funga katika lugha mafaqihi hawakulitoa kichwani bali wameichukua ndani ya Qur-ani Tukufu :
“HAKIKA MIMI NIMEWEKA NADHIRI KWA (ALLAH) MWINGI WA REHEMA YA KUFUNGA, KWA HIVYO LEO SITASEMA NA MTU” [19:26]
Bibi Maryam, mama yake Nabii Isa –Amani ya Allah ziwashukie wote – alipokwishajifungua mwanawe kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu bila ya baba, ilimpata tabu kuu ya kufikiri atawaambia nini jamaa zake hata wamsadiki na kuamini kuwa ujauzito ule unatokana na uweza wa Mola Mtukufu na hautokani na uchafu wa zinaa.
Ni katika hali hii ya kutafakari jawabu la kuwajibu jamaa zake watakapomuuliza habari za mtoto wake, hapo ndipo Mwenyezi Mungu aliyetawalia suala lile akamwambia :
“…NA KAMA UKIMUONA MTU YEYOTE (akauliza habari ya mtoto huyu) SEMA HAKIKA MIMI NIMEWEKA NADHIRI KWA (ALLAH) MWINGI WA REHEMA YA KUFUNGA, KWA HIVYO LEO SITASEMA NA MTU”
Bi Maryam aliposema kuwa kaweka nadhiri ya kufunga, hakuwa na maana ya kufunga Ramadhani bali neno “funga” hapa limetumika kwa maana ya kujizuia kusema/kuzungumza na jamaa zake.
Hapa ndipo imepatikana maana ya funga kilugha kuwa ni kujizuia na lolote lile.
Swaumu/Funga katika sheria ina maana ya kujizuiliya kula, kunywa na mambo yote yanayofunguza swaumu kwa namna maalum na muda maalum.
Muda huu ni tangu kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua. Kujizuiliya huku ni lazima kuambatane na nia.
Hii ndio maana ya funga kwa ujumla. Je, hii ndio khasa aliyokusudia Mwenyezi Mungu katika aya ya swaumu.
Ni nini ukweli/uhakika wa swaumu ? Swaumu ya kweli mbali na kujizuia kula na kunywa, inampasa muislamu ajizuiliye viungo vyake kama vile masikio, macho, ulimi, mkono, mguu na utupu na yale yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu. Ayazuiliye masikio yake kuyasikiliza yale yote yaliyokatazwa kuyasikiliza kama vile kusikiliza maneno ya watu bila ya ridhaa yao, kusikiliza utesi na useng’enyi, ayahifadhi macho yake kuwaangalia wanawake/wanaume wasio maharimu zake, asiangalie ndani ya nyumba ya mtu bila ya idhini yake, asiangalie nyuchi, asimtazame mtu kwa jicho la dharau na kadhalika.
Hali kadhalika avizuiliye viungo vyake vingine vilivyosalia na kila ambalo limekatazwa na sheria kulitenda.
Muislamu atakapoweza kulizuia tumbo lake kula na kunywa na akavizuia viungo vyake vingine na yale yote ya haramu, hapo ndipo atakuwa amefunga kama alivyoagiza na kuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na hiyo ndio funga itakayotoa natija ya ucha-Mungu ambalo ndilo lengo mama la swaumu/funga.
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – amesema: Amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –
“Haikuwa swaumu ni kujizuiliya kula na kunywa (tu) bali ni swaumu ni kujiepusha na upuzi na mambo machafu. Basi yeyote atakayekutukana au kukufanyia upuuzi, basi mwambie hakika mimi nimefunga” Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan.
Na akasema tena Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“Asiyeacha maneno ya urongo/uzushi na kuyafanyia kazi, Mwenyezi Mungu hana haja na kuacha kwake chakula na kinywaji chake” Al-Bukhariy.
Itakuwazikia na kukubainikia kutokana na hadithi hizi kuwa funga ya kweli haikomelei katika kula na kunywa tu.
Pia ni vema ikafahamika kuwa funga ndio ibada pekee isiyoweza kuchezewa na shetani, ndio ibada pekee isiyoingiwa na riyaa, ndio ibada pekee isiyoandikwa thawabu zake na Malaika, hii ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema : “Funga ni yangu na ni mimi ambaye nitakayeilipiza”
HEKIMA/FALSAFA YA FUNGA :
Baada ya kuona funga ya kweli, hebu sasa tujiulize ni kwa nini Mwenyezi Mungu ametulazimisha kufunga na kutuacha tuteseke na machungu ya njaa na joto la kiu ?
Je, funga ni adhabu kwetu ? Bila ya shaka Mwenyezi Mungu hawezi kutuamrisha jambo ila huwa mna ndani ya jambo lile manufaa, maslahi, na faida kwetu sisi waja tulioamrishwa.
Elewa ewe Muislamu kuwa funga ina faida nyingi sana; faida za kiroho, kijamii na kiafya. Funga hukibomoa na kukivunjilia mbali kibri cha mwanadamu na humfanya auone unyonge na udhaifu wake.
Yeye kama kiumbe anahitajia chakula, maji na hewa ili aweze kuishi, kwa mantiki hii binadamu hawezi kujitegemea mwenyewe bali daima anamuhitajia Mwenyezi Mungu Muumba ambaye ndiye humpa hiba ya chakula, maji na hewa. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu :
“ENYI WATU! NYINYI NDIO WENYE HAJA KWA ALLAH; ALLAH NI MKWASI (na nyinyi hakuhitajieni) ASIFIWAYE (kwa neema zake juu ya viumbe wake vyote)” [35:25]
Funga ni mwalimu wa subira. Funga humfinyanga na kumuandaa binadamu kuwa na subira katika kukabiliana na majanga mbali mbali ya maisha.
Humfanya azoee machungu ya njaa na joto la kiu wakati wa ukame, vita, awapo gerezani, aunguapo na kushindwa kula.
Kwa kuwa binadamu huyu atakuwa ameipata shahada ya uvimilivu/subira kutoka chuo kikuu cha subira; Ramadhani, na ni dhahiri kuwa atakuwa thabiti na imara katika kukabiliana na matatizo mbali mbali maishani mwake. Na Mola Mtukufu amewaahidi wenye kusubiri ujira/malipo makubwa aliposema :
“ …NA BILA SHAKA WENYE KUSUBIRI WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO HESABU” [39:10]
Funga ya Ramadhani ni chuo cha uaminifu. Funga inamfundisha Muislamu kuwa mkweli katika mahusiano yake na waja wenzake.
Inamfundisha kuidhibiti na kuichunga nafsi yake, inamfanya amuone Mola wake kuwa yu naye kila wakati na kila mahala na hivyo kuipanda khofu ya Mwenyezi Mungu ndani ya moyo wake.
Natija ya kumuogopa Mwenyezi Mungu ni nafsi kujiepusha na yote yaliyoharamishwa na kutenda yale iliyoamrishwa.
Funga humfanya Muislamu kuwa na huruma kwa wenziwe na ni huruma hii ndio impelekeayo kumsaidia masikini, mgonjwa, yatima, mjane na baki ya wanyonge wengine waliomo katika jamii zetu.
Funga ina athari kubwa, kwa mfungaji, na athari hizi hudhihiri katika tabia na nafsi, funga ni silaha ya ajabu sana ambayo Mwenyezi Mungu ameileta ili kuuvunja unyama wa binadamu, ambao huu ndio humfanya binadamu akawa mbaya kuliko hata mnyama wa mwitu kiasi cha kuona ni jambo dogo tu kuitoa roho ya mwanadamu mwenziwe.
Funga humtoa huku na kumpeleka katika ubinadamu na utu na hapo ndipo utamuona mfungaji namna alivyo mnyenyekevu, mpole, mnyonge na mwenye huruma.
Funga huyavunja matamanio mabaya ya nafsi. Kwani hapana kiwezacho kuivunjavunja nafsi ya mwanadamu kama njaa.
Kwa ujumla, funga humpamba muislamu na sifa njema kwa sababu humkalifisha kuvizuia viungo vyake na mambo ya haramu na kumfanya kuwa kuwa mkweli, muaminifu, mnyenyekevu, mpole, mkarimu na baki ya sifa nyinginezo nzuri, tukufu.
Kwa hivyo funga ni chuo kinachotoa mafunzo juu ya kuidhibiti na kuimiliki nafsi na kumpamba muislamu na sifa njema na kumuepusha na tabia mbaya.
Mwenyezi Mungu, Mtenegenezaji, Mpangaji, na Mpitishaji wa mambo yote, Mwenye hekima na busara, Mtunga sheria aliye mjuzi ameiwajibisha funga kwa hekima/falsafa za juu sana kama tulivyoona.
TUNDA LA RAMADHANI :
Karibu tena ewe ndugu yangu uburudike na tunda la Ramadhani.
- Imepokelewa (hadithi) kutoka kwa Ya’alaa Ibn Murrah –Allah amuwie Radhi- amesema: Amesema Mjumbe wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – :
“Allah anayapenda mambo matatu; kuharakia kufuturu, kuchelewa (kula) daku na kufumbatanisha mikono miwili mmoja juu ya mwingine katika swala” Twabraaniy.
MAELEZO:
Haya muislamu, hayo ndiyo mambo matatu ayapendayo Mola wako na yote yamo ndani ya uweza wako na bila shaka kama Allah anayapenda pia atakuwa anawapenda wayafanyayo mambo hayo. Je, wewe ndugu yangu, hutaki kupendwa na Mola wako ? haya shime “!
- Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik – Allah amuwie Radhi – amesema : Amesema mjumbe wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – :
“Kuleni daku, kwani hakika mna baraka katika daku” Ibn Hibban.
MAELEZO :
Kula daku ni suna na mwenendo wa Bwana Mtume, alikuwa hafungi bila ya kula daku. Hii haimaanishi kuwa kama mtu hakula daku, funga yake haikubaliwi, la hasha bali atakosa fadhila kwa kuiwacha Sunna ya Nabii Muhammad.
Wakati wa kula daku huanzia nusu ya usiku (saa sita) mpaka kabla kabla ya kuchomoza alfajiri kwa muda mchache.
Haya ni kwa mujibu wa kauli ya swahaba wa Mtume : Zayd bin Thaabit –Allah amuwie Radhi – :
“Tulikula daku pamoja na Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie – kisha akainuka kwenda kuswali (Alfajiri) nikamuuliza : kilikuwepo kitambo gani baina ya adhan ya alfajiri na huko kula daku ? Akasema : Kiasi cha kusoma aya khamsini” Bukhaariy na Muslim.