Ewe mpenzi ndugu yangu-Allah atuwafikishe kupendana kwa ajili yake tu-Aamin.
Ninakuusia kwa mapenzi ya imani ufahamu kwamba kuna mambo mengi yenye kuokoa ambayo ni wajibu kuupamba moyo wako kwa mambo hayo.
Kwa msaada wa Allah ninakutajia baadhi ya mambo hayo yaliyo muhimu kabisa. Ewe ndugu yangu, ninakunasihi utambue kwamba mama wa mambo yenye kuokoa ni kutubia kwa Allah kutokana na madhambi yote.
Fahamu kutaka toba ni amri ya Allah kwa waja wake walio dhaifu na wasioepuka kufanya dhambi. Allah amewaraghibisha waja wake kufanya toba kutokana na madhambi wayafanyayo na akawaahidi kuwapokelea toba yao. Akasema Allah Mola Mwenyezi:
“…NA NYOTE TUBIENI KWA ALLAH, ENYI WAUMINI ILI MPATE KUFAULU”. [24:31]
Akasema tena:
“ENYI MLIOAMINI! TUBUNI KWA ALLAH TOBA ILIYO YA KWELI, HUENDA MOLA WENU AKAKUFUTIENI MAOVU YENU NA KUKUINGIZENI KATIKA PEPO ZIPITAZO MITO MBELE YAKE…” [66:8]
Akasema tena:
“…HAKIKA ALLAH HUWAPENDA WANAOTUBU NA HUWAPENDA WANAOJITAKASA” [2:222]
Akaongeza kusema:
“LAKINI MWENYE KUTUBIA BAADA YA DHULMA YAKE NA AKATENDA WEMA, BASI ALLAH ATAPOKEA TOBA YAKE. HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU” [5:39]
Akazidi kusema:
“NAYE NDIYE ANAYEPOKEA TOBA ZA WAJA WAKE NA ANASAMEHE MAKOSA NA ANAYAJUA YOTE MNAYOYATENDA” [42:25]
Naye Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema kuhusiana na suala zima la toba, tumsikilize:
“Mwenye kutubia kutokana na dhambi aliyoifanya ni kama mtu asiye na dhambi”. Ibn Maajah, Twabaraaniy & Al-Baihaqiy-Allah awarehemu.
Bwana Mtume akazidi kutuambia:
“Hakika Allah huukunjua mkono wake wakati wa mchana ili apate kutubia mkosa wa usiku. Na huukunjua mkono wake wakati wa usiku ili apate kutubia mkosa wa mchana (hufanya hivyo) mpaka litakapochomoza jua kutokea machweo (mazamio) yake”.Muslim-Allah amrehemu
Na akasema tena Bwana Mtume:
“Enyi watu! Tubieni kwa Mola wenu kabla hamjafa na harakieni kufanya amali njema kabla hamjashughulishwa. Na yaungeni mawasiliano yenu na Mola wenu kwa kukithirisha kumkumbuka kwenu”. Ibn Maajah-Allah amrehemu.
Akaongeza kusema:
“Kwa yakini Allah hukubali toba ya mja (wake) maadam roho yake haijafika kooni”. Tirmidhiy & Ibn Maajah-Allah awarehemu.
Na akatuambia: “Allah huipokea toba ya anayetubia”. Ahmad, Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
SHARTI ZA TOBA.
Ewe ndugu yangu-Allah akurehemu-fahamu kuwa kufanya toba ni ibada ambayo kusihi kwake kunaambatana na sharti kadhaa.
Kisha ni vema ukafahamu kwamba toba kamili; toba ya kweli si maneno matupu ya ulimini. Mtu akasema:
(ASTAGHFIRULLAAH WA ATUUBU ILAYHI) ulimini, bila ya majuto ya moyo wala kujivua na madhambi.
Wanazuoni wetu wema-Allah awarehemu-wametaja sharti ambazo toba ya mja haitatimia ila kwa kuzileta sharti hizo. Sharti hizo ni tatu kama zifuatazo:-
Majuto ya moyo: Mja ajute moyoni mwake kutokana na madhambi aliyoyatenda huko nyuma.
Kujivua na madhambi: Mja anapoamua kutubia, basi kumemuwajibikia kujivua na kuyaacha kabisa madhambi anayoyatakia toba. Haiingii akilini kutaka toba huku ukiendelea na maasi bila ya kuyaacha, huku ni kumdhihaki Allah.
Kuazimia kutorejea madhambini baada ya kutubia: Mja aamue kwa kutinda kuwa hatarudia tena kumuasi Mola wake kwa kufanya yale yote aliyoyakataza.
Ndugu yangu muislamu mja mwenye madhambi kama mimi, hizi ndizo sharti ambazo toba ya mja haikamiliki wala kusihi ila kwa kupatikana kwake zikiwa kamili; bila ya mapungufu yo yote.
Sharti hizi si maneno matupu tu ya wanachuoni bali zinatokana na kauli za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Toba iliyo ya kweli ni kujutia dhambi inapokupindukia, kisha ukamuomba Allah maghfira halafu usiirejee tena (dhambi hiyo)”. Ibn Abiy Haatim & Ibn Murdawayhi-Allah awarehemu.
Ewe ndugu yangu-Allah akuhidi-fahamu na ujue kwamba sharti tatu hizi ndizo sharti za kusihi toba ya madhambi baina ya mja na Mola Muumba wake tu.
Madhambi ambayo hamna ndani yake haki ya mwanadamu mithili ya mtu kuacha swala. Ama madhambi ambayo pamoja na kumuasi Allah ndani yake kuna haki ya mwanadamu, pamoja na sharti tatu hizi inaongezeka sharti ya nne.
Nayo sharti hii ni kurejesha haki ya watu aliyoidhulumu kama ni mali au ni haki ya heshima. Akishindwa kurejesha basi akamtake radhi mwenyewe ambaye atakuwa na khiari ya ama kumsamehe au kutokumsamehe.
Mja akishatubia kwa namna hii tuliyoibainisha, linaloandamia kwake ni kuwa katika hali baina ya khofu na matarajio.
Akitarajia kukubaliwa toba yake kwa fadhila na ukarimu wa Mola wake.
Huku akikhofu kuwa huenda Mola waku hakuikubali na kuipokea toba yake kwa sababu hakutubia kama Allah alivyoamrisha na kuelekeza kupitia kwa Mtume wake.
Ewe mpenzi ndugu yangu-Allah atuwafikishe kufanya toba ya kweli kweli-nakuusia uelewe kwamba ni wajibu wa muumini kujiepusha kabisa na madhambi yote.
Muumini wa kweli hujiepusha na madhambi bila ya kuangalia ukubwa au udogo wake. Anafanya hivyo kwa kutambua na kuukiri kwake ukweli kwamba ndani ya kutenda dhambi kuna ghadhabu, hasira na machukivu ya Allah Mola Muumba wake.
Allah akurehemu ikiwa utafahamu kwamba madhambi ndiyo sababu kuu ya majanga na balaa ziwapatazo waja duniani na akhera:
“FISADI (uharibifu) UMEDHIHIRI BARANI NA BAHARINI KWA SABABU YA YALE ILIYOYAFANYA MIKONO YA WATU, ILI AWAONJESHE (adhabu ya) BAADHI YA MAMBO WALIYOYAFANYA, HUENDA WAKARUDI (wakatubia kwa Allah)”. [30:41]
Muumini akiteleza akatenda dhambi, basi kunamuwajibikia kuharakia kufanya toba bila ya kuendelea nayo dhambi hiyo na wala asiiridhie.
Kunampasa muumini kutubia na kuendelea kuijadidisha toba yake kwa Mola wake kila wakati. Hii ni kwa sababu madhambi ni mengi mno; madhambi makubwa na madogo, madhambi ya dhahiri na ya siri.
Madhambi ayajuayo mja na yale asiyoyajua. Haya ndugu yangu na tutubie kabla hatujafikwa na mauti.